SoC01 Salum na teknolojia ya simu

SoC01 Salum na teknolojia ya simu

Stories of Change - 2021 Competition

Ahmad bin Adam

New Member
Joined
Sep 18, 2021
Posts
1
Reaction score
1
Nawasalimu ndugu pamoja na wadau wote wa JF. Natumai ni wazima. Hili ni andiko langu lililojikita katika nyanja ya teknolojia. Tunatarajia kupatikana mambo yasiyopungua matatu kutoka katika andiko hili. Elimika, burudika, badilika. Tutaanza simulizi yetu inayomzungumzia kijana Salum kama ifuatavyo:

SALUM NA TEKNOLOJIA YA SIMU

UTANGULIZI MFUPI KUHUSU SALUM

“Mamaa…!” sauti iliyojaa woga na huzuni ilitoka kwenye kinywa cha Salum wakati akiwa anakimbia. Watu waliokuwa wakimfukuza Salum walikua ni vipande vya wanaadamu walioshiba kimiili. Hawakuonesha dalili yoyote ya kukata tamaa katika kumkimbiza kwao licha ya kuwa ni kijana mwenye mbio nyingi. Kila mmoja kati ya watu hao alikuwa na bunduki refu na wote hasira zao ni kumkamata kijana Salum. Mmoja wao aliwazidi wenziwe kwa urefu na alikuwa na macho yaliyopiga wekundu na makali. Ghafla sauti kali ya mifyetuko ya risasi ilisikika na kuushtua moyo wake. Alifungua macho yake na kugeuza uso wake kushoto na kulia na hakuona kitu chochote. Tahamaki ilikuwa ni ndoto aliyokuwa anaota usingizini. Hata dakika haikutimia Salum alisikia sauti ikitokea upande wa mlangoni chumbani kwake “ngo!, ngo!, ngo!”. Akagundua ile mifyetuko ya risasi aliyoisikia ilikuwa ni sauti ya kugongwa kwa mlango wake. “Mmmmhh!!!” alisikika Salum na Bi Asha ikiwa ni ishara kuwa yeye ameshaamka. Hivyo ndivyo Bi Asha alivyokuwa akimuamsha mwanawe Salum pindi anapogundua kuwa hakuamka kwa ajili ya sala ya alfajiri. Alifungua simu yake na kuperuzi kwa dakika kadhaa kisha akaiwacha kwenye chaji. Ilikuwa ni 12:30 za asubuhi na Salum alijing’atua kutoka kwenye kitanda chake akiwa amejawa na uchofu. Alihisi maumivu makali kichwani mwake kuliko yale aliyokuwa anahisi siku zote. Alitembea kwa kujizoazoa na kutoka chumbani kwake kwa ajili ya kujiandaa na siku ile.

SALUM NI NANI? KUTAMBULISHWA KWA BAADHI YA WAHUSIKA

Wazazi wake Salum (21) walimgomba mara kwa mara kwa sifa yake ya uvivu. Ule mwili wake ulio tuna kwa misuli na kifua kilichopanda juu, havikumsaidia chochote kwani uwajubikaji na ukakamavu wa mtu hupimwa kwa umaridadi wake unaotokana na uthabati wa nafsi yake. Salum ni kijana mwenye kimo cha wastani, hivyo ni mtu aliyebahatika kuepuka na kupachikwa majina kama “magondi” na “mbilikimo” na kundi rika wenzake wakati alipokua anasoma skuli. Ni mweupe na mwenye sura ya kiarabu, pua yake ni nyembamba na iliyorefuka na hata hivyo hakuwa ni mwenye kuelewa chochote katika lugha ya kiarabu isipokua kile kijulikanacho kama “cha kuombea maji”. Nywele zake zilikuwa na weusi uliokoza, huwezi kusema ni za kiswahili na wala huwezi kusema ni singa, kwani vijana walioishi mtaani kwao walibishana sana juu ya hilo. Salum ni mtoto wa 4 kati ya watoto 7 wa familia ya Bwana Seif na Bi Asha. Familia hiyo inaishi Mtaa wa Kiponda uliopo ndani ya mji mkongwe katika Kisiwa cha Unguja. Baba yake Bw. Seif ni mfanyabiashara na anamiliki gari tatu aina ya ‘dyna’ anazozitumia kwa kazi ya kusafirishia michanga. Ni mtu makini na asiyependa mchezo kwenye kazi. Wafanyakazi wake wamekua wakipeana moyo mara kwa mara katika hali ya kutaniana juu ya ukali wake kwa kuambiana pasipo na uwepo wake “boss hanuniwi!”. Mama yake ni mama wa nyumbani. Ni mtu maridadi, mwenye kupangilia mambo vilivyo na ni mwenye jitihada. Bw. Seif amekua akimsifia sana na kustaajabishwa na jitihada zake katika kuhakikisha mipangilio ya nyumba inakwenda vizuri katika familia hiyo inayohudumia watoto saba licha ya kutokuwepo kwa msaidizi wa kazi.

MAISHA YA SALUM NA SIMU

Ni mwezi mmoja na nusu sasa tokea Salum kuhitimu kidato cha sita. Hivi sasa anasubiri kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya chuo ili aanze hatua yake ya kwanza katika kujiendeleza na elimu ya juu. Kwa kitambo sasa, amekua akitumia muda wake mwingi akiwa nyumbani kwani hakuamua kujishughulisha na chochote tangu amalize skuli. Na sana huutumia akiwa chumbani kwake faragha na simu yake. Alikuwa ni kama mtu ambae anaishi dunia mbili. Dunia hii tunayoishi na ile ya mitandaoni. Hutembelea tovuti hii na ile, pamoja na kuzama ndani ya mitandao ya kijamii kwa muda mrefu. Ni kama vile ambavyo hutembea baina ya majumba ya mji mkongwe, chochoro hadi chochoro, na ni mithili ya vile anavyokwenda Forodhani kupiga mbizi ndani ya bahari. Kukaa kwake faragha kulimfanya yeye kutojichanganyisha sana na watu na hivyo kuwa na marafiki wachache. Hali hiyo alianza kujizoesha nayo tokea apate simu yake ya kwanza aliyonunuliwa na baba yake.

SALUM ADUKULIWA ACCOUNT YAKE

Ni 7:30 za usiku, akiwa kitandani na simu yake akiperuzi katika mtandao wa instagram, Salum aliona post yenye muundo wa tangazo lililomvutia machoni mwake. Alianza kulisoma kwa umakini na kustaajabishwa mno na lile tangazo. Tangazo hilo lilimhakikishia yeye njia rahisi ya kuongeza ‘followers’ kwenye akaunti yake na kwa muda mfupi kabisa. Akaunti aliyokuwa anaitumia ilikuwa ina ‘followers’ 1180, na aliipata kwa mmoja wa wauzaji account za Instagram mitandaoni. Licha ya hivyo, hakuridhishwa na idadi hiyo na alitamani iongezeke hadi kupatikane kijialama cha buluu mbele ya jina lake. Hivyo basi, kwa ujasiri alibofya lile tangazo na lilimtaka yeye kujaza jina lake, barua pepe na nywila ili apate kujisajili kwenye ukurasa ule. Kwenye ule ukurasa, Salum alikua na hiari ya kuchagua akaunti yenye idadi ya ‘followers’ anaowataka kwa masharti ya kutuma kiunganishi cha tangazo hilo kwa idadi maalumu ya watu. Kwa akaunti aliyoichagua, ilimbidi yeye awatumie watu 25 wengine lile tangazo ili kutunikiwa akaunti anayoitaka. Salum hakurudi nyuma na alijaribu kufanya hivyo kadri iwezekanavyo. Je alifanikiwa?

TABIA ZA AJABU KWENYE SIMU YAKE

Wakati mmoja Salum alipokua anarudi nyumbani kutoka dukani alisikia sauti ya mlio wa simu yenye kuashiria kuingia kwa ujumbe mpya. Pamoja na kwamba haukua ni mlio wa simu yake, aligeuka kutafuta sehemu ilipotokea sauti kwani ilitokea sehemu ya karibu. Na pale alipojaribu kuangalia simu yake alikuta ujumbe mpya aliotumiwa na kaka yake. Aliusoma na akamjibu kisha akaendelea na mambo yake. Jambo hilo halikumshtua na wala hakulitilia maanani kwa muda ule.

Mchana mmoja Salum alikua anajaribu kutafuta video fupi ya mpira aliyowahi kuiangalia wiki iliyopita huko YouTube ambayo aliisahau jina lake, ila hakuipata. Hatimaye akaamua kubofya sehemu ya kumbukumbu za video (history) na kuitafutia huko akitarajia kuiona. Jambo lililomstaajabisha kwa siku ile ni kuwa, pamoja na kwamba yeye aliiona ile video aliyokuwa akiitafuta, alikuta idadi ya video kadhaa zilizotizamwa katika kumbukumbu ya video zake. Kilichomstaajabisha zaidi ni kwamba video hizo zilikuwa ni za kihindi na hakuna dalili ya kuwepo mtu yoyote anayeweza kufungua simu yake na kuangalia video hizo. "Hamdiya yeye kutwa yupo na wakorea, sasa nani awe kaangalia hizi video za kihindi!?". Alisema kimoyomoyo wakati alipomshuku dada yake kuwa ndiye aliyehusika.

Siku zilikwenda, na Salum, kila kukicha hakuacha kuona tabia za ajabu ambazo zinajitokeza kwenye simu yake. Muito wa simu yake pamoja na wa ujumbe ulibadilika mara kwa mara na ilimbidi arudi kwenye mipangilio ya simu na kupangilia tena upya miito aliyotaka kuitumia. Tokea kipindi kile cha mwanzo alipokua anashtuka na kujiuliza maswali ambayo hakupata majibu yake katu, mpaka ameshakua ni mwenye kuzoeana na hiyo hali hvi sasa

NAMNA ALIVYOKUJA KUTAMBUA

Ni wiki tatu sasa tokea Salum kuanza masomo yake akiwa chuoni. Wakati mmoja alipokua katika mazungumzo na baadhi ya wanafunzi wenzake aliamua kuwasimulia hali ambayo anaiona kwenye simu yake kwani ilishaanza kuwa ni kero kwake. Wapo waliostaajabishwa, waliochukulia kama ni kichekesho na utani, na mmoja wao alimwambia kuwa simu yake ina virus. Jambo ambalo lilimuingia akilini na akalipokea kwa mikono miwili kwamba ndio sababu kuu.

Ilipofika jumamosi, Salum alitoka nyumbani mapema asubuhi kuelekea nje ya ofisi za Zanlink hapo mtaa wa majestic. Kusudio lake ni kwenda kutumia mtandao kupitia WiFi iliyopo hapo kwa lengo la kufanya ‘backup’ ya vitu vyote vilivyomo ndani ya simu yake. Aliamini kuwa simu yake ina kirusi na njia pekee ni kwamba yeye aifanyie ‘reset’ kisha aanze upya kufanya ‘restore’ ya mafaili yake pindi atakapomaliza kuifuta. Ingawa ni jambo la ajabu kusikia kuwa simu eti inaingia kirusi, kuwepo kwa faili ambalo lilianziwa na alama ya kidoto ambalo halikuweza kufutika, kulimfanya kuamini sana uwepo wa kirusi kwenye simu yake.

Alifanikiwa kuhifadhi vitu vyake vyote mtandaoni kupitia akaunti yake ya Gmail. Alihisi kupata faraja hivi sasa, kwani muda mfupi tu ataanza kuipangilia upya simu yake na kurejesha vitu vyake kwa mara nyengine. Haukupita muda mrefu, Salum alisikika kwa sauti ya mshangao na walio karibu naye “Aka!”. Ni baada ya kujaribu zaidi ya mara moja kuandika nywila ya akaunti yake pale alipokusudia kuirejesha hiyo akaunti na kushindwa. Kila alipojaribu kuandika nywila yake, mtandao ulimuelekeza kuwa nywila ile sio sahihi. Alielekezwa kuweka nywila ya mwisho aliyowahi kuitumia hapo kabla, pia hakufanikiwa katika hilo. Salum alitumia nywila moja tu kwenye account zake zote. Hakutaka kutumia nywila tofauti kwa kuwa alihofia kuzisahau. Alipojaribu tena kwa njia nyengine kuipata akaunti yake, mtandao ulimueleza athibitishe nambari aliyoihusisha kwenye mipangilio ya akaunti yake ambayo ilimalizikiwa na “* * **49”. Salum alipigwa na butwaa. Namba ile iliyojionesha haikuwa ni nambari yake wala ya mtu yeyote katika watu wa nyumbani kwao. Alithubutu kuandika nambari yake katika ile sehemu aliyowekewa kujaza nambari ila ilishindikana. Alipohitaji msaada kwa kijana aliyekuwepo karibu, alielezwa kuwa akaunti yake imeshadukuliwa na haitokua rahisi kwake kuipata tena. Sallaale! Ingawa hakuonesha kushtushwa sana na ile hali kupitia uso wake, lakini moyo ulishituka na kichwa kilimuuma. Hakuwahi kufikiria kuwa jambo kama lile linaweza kutokezea na kwa hali kama ile. “Imewezaje kudukuliwa akaunti yangu ilihali sikumpa yeyote taarifa zangu?”. Alijiuliza mfano wa maswali hayo na hakufanikiwa kupata majibu.

Salum alianza maisha mapya akiwa na akaunti mpya ya gmail ilihali hapo nyuma ameshapoteza pamoja na akaunti ya gmail, akaunti yake ya instagram. Wingi ulioje wa watu katika zama hizi wanaopaswa kumchukulia Salum kama ni mfano hai? TAFAKARI!!

Matarajio yangu ni kwamba umeelimika, umeburudika na umeazimia kubadilika. Ahsante sana kwa kusoma andiko hili. Napokea maoni na nakuomba kwa moyo wa dhati kwamba usisahau kunipigia kura.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom