Salum 'Ndege Mwema' Abdallah na kigoma cha daku

Salum 'Ndege Mwema' Abdallah na kigoma cha daku

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
BABU YANGU SALUM ''NDEGE MWEMA'' ABDALLAH NA KIGOMA CHA DAKU

Naiaga Ramadhani kwa kutabaruku na babu yangu Salum Abdallah (Allah amrehemu yeye na wazee wetu wote waliotangulia mbele ya haki) na kigoma chake cha daku na nyimbo iliyokuwa haipigwi ila pale wapigaji watakapofika nyumbani kwetu.

Inaelekea nyimbo hii alitungiwa yeye makhsusi.

Ramadhani ya mwaka wa 1965 nikiwa na umri wa miaka 13 ikanikuta Tabora nilipokwenda kumtembelea babu alipotoka jela.

Maghrib ikikaribia uwanja mbele ya nyumba yetu unafagiliwa na majamvi yanatandikwa adhana ikipigwa futari zinaanza kutolewa na kufunikwa na makawa makubwa.

Baada ya kushuka msikitini watu wanakaa kufuturu.

Watu wengi walikuwa wanakuja kufuturu pale nyumbani.

Sikumbuki katika miaka ile kuona watu wakila chapati, sambusa, na mapochopocho mengine kama futari katika miaka ile.

Siku zile futari ni mihogo, maharage, kunde, ndizi mzuzu na ndizi mbivu na uji wa pilipili manga, chai ilikuwa si sana labda kama sikui ile kuna kuja wageni kufuturu.

Tabora ndiko nilikojifunza kula mihogo iliyoungwa kwa karanga badala ya nazi vyakula vyote hivi vilikuwa vinatoka shambani kwetu.

Unywaji wa chai katika kufuturu ulikuwa nadra.

Wala hapakuwa na unywaji wa juisi.
Hivi vitu vimekuja miaka hii ya hivi karibuni.

Sielewi kwa nini ilikuwa vile ni hali za watu au ndivyo ilivyotakiwa iwe?

Sasa nakuja kwa babu.

Baada ya sala ya tarweh watu hukaa wakazungumza kuvuta muda wa daku na pale nyumbani kwa babu ndipo ilikuwa barza kubwa ya mtaa watu wakikutana hapo.

Niliambiwa miaka ile ya kupigania uhuru miaka ya 1950 hapo ndipo taarifa zote za Nyerere zilipokuwa zikipatikana na watu kutiana moyo kuwa Muingereza siku zake zinahesabika uhuru unanukia.

Baada ya uhuru ghafla ndiyo balaa likamkumba babu yangu kwa kukamatwa na kuwekwa kuzuizini kwa tuhuma kuwa alikuwa katika njama za kupindua serikali ya Nyerere babu na viongozi wengine wa vyama vya wafanyakazi akihusishwa na maasi yale.

Barza ile ya babu ilipooza alipokuwa kifungoni kwani marafiki zake wengi walikata mguu kufika pale na hata alipotoka Jela ya Uyui ile ingia toka kama ya zamani haikuwapo.

Hakuna aliyetaka kunasibishwa na mtu ''haini.''

Lakini juu ya haya kuna watu hawakumtupa mkono babu walikuja kila siku ya mwezi wa Ramadhani kumuimbia nyimbo ambayo ilikuwa haimbiwi yeyeyote mji mzima isipokuwa yeye babu yangu.

Nyimbo hii ilikuwa inaitwa ‘’Ndege Mwema.’’

Mashairi yake yalikuwa yakimsifia babu kwa ubinadamu na ukarimu wake.

Tabora kigoma cha daku ni tofauti na vigoma vya dafu kwengineko ambako yanapigwa matari peke yake.

Tabora kigoma cha daku kina ngoma nyingi kigoma cha daku kinapigwa kwa staili ya mchanganyika wa ngoma za Kimanyema na Waswezi na nyimbo zake zina ‘’melody,’’ za kuvutia.

Kigoma cha daku wakishamuona huko wanakotoka babu kakaa nje sasa watakuwa wanakuja nyumba baada ya nyuma wanasimama na kupiga kwa dakika moja mbili wanazima wanaendelea hadi wanakaribia nyumba yetu.

Kabla ya kufika mapigo yanabadilika na lile goma kubwa utalisikia sasa likirindima na sauti za waimbaji utazisikia zikiimba kwa masikitiko.

Wanafika mbele ya babu hapo ndipo utazisikia ala zinazungumza.

Babu kakaa kajiinamia kama vile ngoma zile zinampeleka mbali sana.

Baada ya muda atanyanyuka atawafata huku anafungua pochi yake kuwatunza.

Watazima muziki kisha watapiga mwimbo mwingine kwa mdundo wa kuondoka na kwa mdundo huo watamuaga babu.

Babu hapo na yeye ataondoka kuingia ndani.

Maisha yake yote babu yangu aliishi na tuhuma ya kutaka kupindua serikali lau kama ilikua ni uongo.

Alipofariki dunia mwaka wa 1974 TANU ilifika katika mazishi yake na walisoma risala nzuri sana ya kumsifia kwa mchango wake wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika akiwa mwanachama wa TANU na akiwa kiongozi wa TRAU wakamsifia kwa ukarimu wakasema kuwa mkono wake siku zote ulikuwa wazi akitoa kwa ajili ya nchi yake.

Huyu ndiye babu yangu na kigoma cha daku na mwimbo wake, ‘’Ndege Mwema.’’

PICHA: Salum Abdallah (mshale) kuliani kwake ni Kassanga Tumbo.

20210513_194556.jpg
 
Back
Top Bottom