mraniwene
New Member
- Apr 23, 2022
- 2
- 1
(Mwanzo) Hadithi Fupi
“Mamu, Mamu, we Mariamu si nakuita ina maana hunisikii?”, ilisikika sauti ya Mama Ibra kama ilivyo kila siku mida ya saa kumi na moja na nusu akiwa anamuamsha mwanaye. “Amka haraka jamani tutakosa wateja, na wateja ndio pesa. Au unafikiri hivi vitumbua vitajipeleka vyenyewe sokoni? Mamu nikikufuata humo ndani”, Mama Ibra aliendelea huku akigeuza vitumbua. “Mama nimeamka jamani, nimefungua macho kabisa hapa nilikua naswali tu kabla sijatoka kwenye godoro”, Mariamu alisikika akijibu kwa sauti iliyoshiba zengwe la usingizi. “Unaswali? Unaswali umelala? Embu amka huko jiandae ukatembeze vitumbua sokoni. Alafu mgongee hapo kaka yako ajiandae kwenda shule, kila siku anachelewa tu,” mama Ibra aliongezea huku amesimama anaangalia ndani ya sebule ambapo ndio huwa wanajilaza wakati wa usiku. “Sawa mama”, Mariamu alimjibu kwa upole huku akiinuka na kujinyosha.
Mama Ibra (Ashura) ni mfano wa wanawake wengi wanaoishi Tanzania. Nyumba yake ya vyumba viwili ndio mali pekee yenye thamani zaidi maishani mwake. Chumba kikubwa hutumika kama sebule pamoja na chumba cha kulala wanawake (yeye na Mariamu) na chumba kidogo ndimo ambapo wanaume hulala (mumewe na mwanaye wa kiume aitwae Ibra). Ashura, ndiye mtafutaji pekee na mwenye kipato katika familia yake. Mumewe hushinda kwenye magenge ya kahawa na wazee wenzake akicheza kamali wakati wa mchana, usiku hupitia kilabuni kunywa pombe na kujiliwaza. Japokua Ashura ndiye mtafutaji, bado mumewe hufanya maamuzi yote ya familia na pia hupewa karibia hela yote ya mauzo anayopata mke wake. Mariamu ni msichana mdogo wa miaka kumi na mbili na ndio anamalizia elimu yake ya msingi akiwa darasa la saba.
“Yani Mamu hujatoka tu?”, Ashura aliuliza huku akiingiza vitumbua kwenye beseni. “Nakuja mama”, Mariamu alijibu kwa upole. “Ibra, Ibra, Ibraaaaa, Amka upesi baba anakuja, si unajua akifika hapa kila mtu ni kupigwa kama ngoma”. “kulugulugulugulu”, sauti ilisikika kutoka chumbani kwa Ibra ikiashiria anaamka kwa upesi. “We Mamu, maji ya moto hayo hapo oga upige mswaki haraka upeleke vitumbua pale sokoni.”, Ashura aliagiza huku akiingiza maji ya moto kwenye ndoo.
Ndani ya muda mfupi Mariamu alikua ameshajiandaa kwa ajili ya Kwenda kupeleka vitumbua sokoni. “We Ibra uwahi umsindikize dada yako sokoni, kila siku anatembea mwenyewe.
Hili giza si unaliona lakini?”, Ashura alisema huku akimwekea Ibra maji ya kuoga. “Mama bwana we ni twishe tu niende, kaka mwenyewe unajua anavyooga masaa mawili, ntachelewa shule”, Mariamu alimwambia mama yake. “Haya mwanangu, uende ila angalia uwe salama, ile filimbi si unayo? Ukipata tatizo tu ipige. Mungu akusaidie usikutane tu na baba yako huko njiani maana wanangu ye anawaona kama ngoma tu za kupiga”, Ashura alijibu kwa uchungu huku akimtwisha beseni Mariamu.
Ndani ya sekunde chache Mariamu alianza safari kuelekea sokoni huku akitembea kwa haraka ili kuwahi wateja. Alijua akichelewa watakosa hela, na baba yake hatamuelewa. Huku akiwa na mawazo mazito na akitembea kwa haraka Mariamu alijikwaa na kudondosha vitumbua vyote. “Mamaaaa, mtumeeeeee, uwi leo nimeisha”, alisema huku aking’ata kidole. Kunyanua macho vizuri, alimuona baba yake kwa mbali akipepesuka huku anaelekea nyumbani. Mariamu aliangalia vile vitumbua, kisha akanyanyua macho kuangalia baba yake kwa mbali ambaye alikua bado hajamtambua. Kwa haraka akabeba lile beseni na kuingia kichakani kujificha ili baba yake asimuone. Ndani ya dakika tatu Mariamu alijibanza kimya bila kutoa sauti kwa kumuogopa baba yake. Alichungulia kwa makini huku akiwaza suluhisho la janga lililomkuta. Baada ya baba yake kupita Mariamu alijaribu kutoka kichakani bila kufanikiwa. Haikuchukua muda kugundua kuwa alikua amejiingiza kwenye kichaka ambapo teja walikua wakilala. Japo alihangaika sana, kila alichofanya kilisababisha kuumia zaidi. Teja aliyekua amemshika aliashiria wenzake kuamka. “Jamani nyama amkeni nyama”, alisema huku akicheka. “Babaa, babaa”, Mariamu alilia kwa sauti ili baba yake aje kumsaidia kwa kuwa hakua amefika mbali sana.
(Kati) Makala Fupi
Je, nini unafikiri kilitokea?
Mila na desturi zetu Tanzania zinatuelekeza jinsi ya kuishi;
Mila na desturi ni mambo muhimu kwenye jamii zetu na yatazidi kuwa msingi muhimu wa kuimarisha Maisha yetu kama waafrika. Kuna umuhimu mkubwa kuwa na mila na desturi zinazotambulika na kuheshimika kwa umoja na jamii zote za Tanzania. Ni kweli kwamba makabila tofauti huwa na mila na desturi zinazotofuatiana kulingana na asili zao. Hii ina uzuri wake na ubaya pia. Uzuri ni kwamba tunapata ladha mbali mbali ya tabia na mienendo ya makabila kulingana na tofauti zao. Ubaya ni kwamba, makabila haya yanapokutana na kuunganishwa kupitia ndoa, mara nyingi Watoto huwa ndio waathirika wakubwa wa tofauti hizo.
Yapo makabila ambayo mwanaume hupewa mamlaka yote juu ya familia bila kujali jinsi anavyoipeleka na kuendesha familia hiyo. Hii husababisha familia nyingine kuumia na kupoteza muelekeo wa maisha, haswa watoto. Watoto wamekua kama wafungwa katika familia zao, wakiishi roho juu na kuwa na wasiwasi muda wote. Tumeona mfano mzuri wa mtoto “Mariamu” hapo juu ambaye kutokana na kumuogopa baba yake maisha yake yamewekwa hatarini. Tunaona pia jinsi baba wa familia asivyowajibika ila kutegemea wanae na mkewe kufanya kazi na kumletea pesa.
Mambo haya yanaweza kurekebishwa mashuleni. Wahenga wanasema “Samaki mkunje angali mbichi”. Msemo huu unatuonesha kuwa ili kubadilisha mambo katika ngazi ya familia au nchi ni lazima tuweke nguvu zaidi kuwasaidia watoto kwa malezi bora tangu wanapokua wadogo. Malezi haya kwa kiasi kikubwa lazima yafanyike shuleni, kupitia elimu na walimu wanaokua na mda mwingi zaidi na watoto.
Pamoja tunaweza kuleta mabadiliko chanya nchini kwetu.
(Mwisho) Ushauri
Kuna umuhimu masomo ya mila na desturi kuingizwa kwenye mitaala ya elimu ya msingi. Katika mitaala hiyo mila na desturi zaweza kugawanywa katika nafasi mbili. Moja ikiwa ni kuzielewa mila na desturi za makabila nyingine, na upande wa pili ukiwa ni kuelewa misimamo ya serikali na jamii kwa ujumla juu ya mila na desturi Fulani. Kwa mfano; mila na desturi ya makabila mengi inaagiza familia kuongozwa na baba, lakini sheria hairuhusu baba huyo kuchukua nafasi hiyo na kuitumia vibaya kwa kuikandamiza familia yake.
Kwa mantiki hii, masomo haya yanatakiwa yapewe kipaumbele sio tu kwa Watoto wa kike ila wakiume pia. Kuwafundisha mila na desturi zinazokubalika Tanzania nzima, kutawasaidia Watoto wa kiume makabila mbalimbali kuwaheshimu Watoto wa kike na wanawake kwenye Maisha yao.
Kutawasaidia pia kujua jukumu lao la kufanya kazi ili kuilinda na kuhudumia familia zao kama sheria inavowataka.
Upvote
0