SoC02 Sayansi na teknolojia nchini

Stories of Change - 2022 Competition

Valence chacha

New Member
Joined
Jul 30, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Tanzania imebarikiwa watu wengi wenye vipaji mbalimbali vya ubunifu ila tumekuwa tukiwadharau na kuwashusha pale wanapojaribu kuziendeleza ndoto zao kwa dhana ya kusema "hiyo akili kubwa ya Teknolojia kabarikiwa Mzungu pekee" kitu ambacho kinakatisha tamaa.

Ila baadhi ya wazalendo wamekuwa wakiwashika mkono walau waweze kutambulika na Serikali, ila mbaya zaidi baadhi ya viongozi nao wamekuwa katika kundi la wanao katisha tamaa.

Tunapata picha kwamba Serikali haiwaamini watu wake na wananchi hatuwaamini watoto/vijana wetu tulionao uraiani kwamba wanaweza kufanya jambo fulani la Kisayansi.

Mfano wa kuigwa Mh. Hayati John Pombe Magufuli, yeye alijenga imani kwa vijana aliowapa kazi ya kufanya ukarabati wa ndege hapa nchini na kuokoa kiwango kikubwa cha pesa ambapo ndege ilitakiwa ikafanyiwe matengenezo South Africa.

Hivyo pia Rais wetu wa sasa Mh. Samia Suluhu Hassan angejenga imani kwa vijana wa Tanzania kwa kutengeneza filamu yake ya Royal Tour, kwani tuna waongozaji wazuri wa Filamu (film directors) kwa mfano; Leah Mwendamseke (Lamata) na Seko Shamte hawa ni mfano wa waongozaji wazuri wa filamu hapa nchini hivyo nina imani kuwa wangeweza kutengeneza filamu bora na kwa gharama naafuu zaidi pia wangekuza tasnia zao kimataifa zaidi.

WITO KWA SERIKALI
Wazo langu ni kwamba uandaliwe mkakati maalum wa kuwasaidia watu wenye uwezo wa kisayansi waliopo mitaani (bila kujali vyeti kwa maana kuna watu wana ujuzi mkubwa kuzidi watu waliosoma na wenye vyeti vyao) na wapewe bajeti yao na Serikali kwa maana kupitia taaluma zao wanaweza kuliingizia Taifa pesa nyingi na pia wataokoa gharama nyingi zaidi ambazo labda wangeletwa wataalamu kutoka nje ya nchi kuja kufanya shughuli ambayo wao binafsi wanaimudu, lakini pia inapaswa Serikali na wananchi tujenge imani juu ya vijana wetu na kuwapa vipaumbele katika kuhakikisha wanayafikia malengo ya ndoto zao.

Nchi ya China ni moja ya nchi zilizoendelea zaidi duniani na sababu kubwa ya maendeleo yake ni Sayansi na Teknolojia, Tanzania pia tuna ndoto ya kuufikia uchumi wa viwanda, ila hivyo viwanda bila Sayansi na Teknolojia hatuwezi kufikia malengo.

Kuna maneno mitaani vijana wanapenda kusema "baada ya Mungu Mzungu" kwamba eti Mwafrika hawezi lolote linalohusu Sayansi na Teknolojia, ila kwa muujibu wa Historia ni kwamba mtu wa kwanza kufua chuma na kuyeyusha hapa barani Afrika ni Jamii ya Wahaya kutokea hapa nchini Tanzania, na hiyo ni kabla ya ujio wa Wazungu kufika barani Afrika.

Hivyo basi kuendelea kujishusha hadhi sisi wenyewe ndivyo kadri tunadhoofu kifikra, hata mtoto anayekua akilisikia hilo neno basi litamjengea aamini kuwa yeye ni wa kushindwa daima, na aamini kuwa Mzungu pekee ndio mwenye uelewa juu ya mambo ya Sayansi na Teknolojia, kumbe hata sisi pia maarifa tunayo.

Pia mashuleni ingefundishwa Sayansi na Teknolojia ile inayoendana na ulimwengu wa sasa, ni huzuni kuona hadi leo hii simu ya maandishi bado inafundishwa mashuleni na wakati yupo zama za simu janja (Smart phone) hiyo simu ya maandishi wanayoisoma wataitumia wapi? (pendekezo labda ikae kwenye somo la Historia) lakini pia linafundishwa somo la kuandika barua pepe kwa njia ya Posta, ningependekeza kwamba wafundishwe pia kuandika kwa njia ya kidijitali (Email) kwa maana ni taasisi na mashirika mengi kwa sasa wanatumia mfumo huu wa kidijitali (Email) kupokea maombi ya kazi na mawasiliano mengineyo, sasa inasikitisha kuona kijana aliyemaliza kidato cha nne hawezi kuandika aina hii ya barua pepe ya kimtandao (Email) anaweza barua ya sanduku la Posta pekee , hivyo itolewe elimu inayoendana na wakati tuliopo.

Kwa vijana wenye uelewa mkubwa wa Sayansi na Teknolojia Serikali ijitolee kuwasomesha nje ya nchi, wasome mambo ambayo ni uhitaji kwa Taifa letu ili tuweze kufikia lengo la uchumi wa viwanda.

Pia Serikali itoe mchango mkubwa kwa watu wenye uwezo huu ikibidi waweke mashindano nchini (kama ilivyo kwenye michezo) baada ya hapo washiriki kimataifa zaidi, hii itawapa nia na juhudi zaidi na kuwafungulia mwangaza wa kutimiza ndoto zao.

Mwisho tuifute dhana hii katika jamii kwamba mambo ya Sayansi na Teknolojia anaweza Mzungu pekee na Mwafrika hawezi (huo ni utumwa wa kifikra) hii itatujengea akili kufikiri kwa mapana zaidi bila kujidharau, ni jukumu letu sote raia pamoja na Serikali kujenga Taifa letu.
 
Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…