Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
KWA UFUPI
1.Ushuzi hujumuisha asilimia 59 ya gesi ya naitrojeni, asilimia 21 ya haidrojen, ammonia, asilimia 9 ya ukaa au kabonidayoksaidi, asilimia 7 ya methane na asilimia 4 ya oksijeni.
2.Kila binadamu hutoa hewa chafu kulingana na wingi wa gesi tumboni
3.Hata ukiubana ushuzi, lazima ukutoke uwapo usingizini
Unapokuwa mtoto unajiuliza maswali mengi, iwapo mwalimu, mzazi au watu wazima wanatoa hewa chafu hudhani labda ni kosa au jambo la aibu.
Dar es Salaam. Kwa wengine, kutoa hewa chafu huenda kukawa ni jambo la aibu na pia la kufadhaisha.
Tendo hilo pengine limeshawahi kumfanya mtu akakosa kujiamini kiasi cha kubadili njia, lakini hata hivyo ni la kawaida ambalo kila binadamu mwenye uhai hulifanya.
Kitendo hiki kina majina mengi kulingana na mazingira au utamaduni wa sehemu husika.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu huita tendo hili kuwa ni, kujamba, sura au ushuzi, lakini kwa lugha isiyo na makali, huitwa kutoa hewa chafu.
Pamoja na jamii kuchukulia tendo hilo la kutoa hewa chafu kama la aibu na unapolifanya mbele ya watu huweza kumfanya mtu asijisikie vizuri, lakini yapo mengi ya kibaolojia yanayofanyika hadi binadamu akatoa hewa chafu mwilini.
Kwa kifupi huu ni mfumo halisi na wa kila siku wa utendaji kazi wa miili yetu ndiyo husababisha hali hii.
Kutoa hewa chafu ni nini?
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili, Meshack Shimwela anasema kutoa hewa chafu kunasababishwa na kubanwa kwa hewa ambayo tunaipata au kuimeza wakati wa kula au kunywa.
Pia, hewa chafu huweza kuingia kutokana na gesi kuingia kwenye utumbo kutoka kwenye damu. Gesi hizi huweza kuzalishwa na kemikali katika utumbo au bakteria.
Dk. Shimwela anasema bakteria wanaoishi tumboni, humengenya chakula na kuzalisha gesi ya ammonia, sulfur dioxide ambazo huwa na harufu mithili ya choo au mkojo. Harufu hutegemea aina ya chakula. Tumbo lenyewe, likipata maradhi au maambukizi huongeza kasi ya gesi, anasema
Anaongeza kuwa bakteria wabaya wanaweza kutengeneza gesi na kuwa hewa chafu ikizidi sana ni tatizo na inaashiria tatizo.
Nini hujumuisha hewa chafu tumboni?
Dk James Roth, mwandishi wa kitabu cha aina za gesi ya tumboni (gastrointestinal) kutoka Uingereza, anasema kwa kawaida ushuzi hujumuisha asilimia 59 ya gesi ya naitrojeni, asilimia 21 ya haidrojen na ammonia, asilimia 9 ya ukaa au kabonidayoksaidi, asilimia 7 ya methane na asilimia 4 ya oksijeni.
Mtaalamu wa Chakula na Lishe, Pazi Mwinymvua anachanganua mfumo wa utoaji wa hewa chafu na kusema: Unapokula chakula, usagaji hufanyika tumboni na baadaye mambo mawili hutokea, la kwanza ni mabaki na viini lishe.
Anasema baada ya mmengenyo mabaki ya aina tatu hutengenezwa nayo ni majimaji, haja kubwa na gesi.
Pazi anaonya kuwa endapo mtu atakosa kupata ushuzi na choo, basi huenda ikawa ni hali ya hatari wakati mwingine pengine utumbo umejikunja. Hivyo, kutoa hewa chafu ni afya.
Kwa baadhi ya watu, hewa chafu husababishwa na kuoza au kuchacha kwa vyakula ambavyo havijamengenywa katika mfumo wa usagaji wa chakula. Baada ya kipindi fulani gesi hii huwa sumu na huweza kusababisha matatizo kama kuvimbiwa, kiungulia,
Kwa nini ushuzi hutoa harufu mbaya?
Kile tunachokula ndicho kinachotathmini aina ya hewa chafu tunayotoa.
Hewa chafu kwa kawaida ina asilimia moja tu ya Hydrogen Sulfide na Mercaptan ambayo ina sulfur dioxide ndani yake.
Salfur ndiyo huufanya ushuzi utoe hewa chafu. Mifano ni vyakula kama kabichi, maharage, mayai, mahindi au vyakula vyenye hamira nyingi.
Dk Anorld Kaaya, wa Hospitali ya Seliani Arusha, anasema, maharage husababisha kwa kiasi kikubwa mtu kutoa hewa chafu kwa sababu ya sukari iliyomo ndani yake ambayo ni vigumu kumengenywa mwilini. Hii sukari inapowafikia bakteria wema walioko tumboni, hufurahia kwa kupata mlo mkubwa na mzuri na huzalisha gesi nyingi anasema
Kwa nini sauti hutoka wakati wa kutoa hewa chafu? Hewa chafu ina sauti. Kisayansi, sauti hii hutokana na mitetemo katika njia ya haja kubwa ambao pia hutegemea presha inayosukuma gesi itoke na pia hutegemea ugumu wa misuli ya njia ya haja kubwa.
Hewa chafu ya binadamu na bomu la atomiki
Gazeti la habari za Sayansi la nchini Washington DC la Machi 30, 2002 linachanganua na kusema kuwa binadamu mwenye afya njema, huweza kutoa nusu lita ya hewa chafu kwa siku.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa mtu akijamba kwa kipindi cha miaka sita na miezi tisa mfululizo huweza kuzalisha nishati ya kutosha kutengeneza bomu la atomiki.
Wanawake hutoa hewa chafu zaidi?
Baadhi ya tafiti zimethibitisha kuwa, mwanamke na mwanaume wanapokula chakula cha aina moja, wanawake huzalisha gesi zaidi kuliko wanaume. Hata hivyo, wengine wanadai kuwa wanawake huzalisha hewa chafu yenye harufu zaidi kuliko wanaume.
Hewa chafu inawasha moto
Kama ilivyoandikwa hapo juu, wataalamu wanasema gesi ya methane na haidrojeni inayozalishwa na ushuzi inaweza kusababisha moto endapo utaamua kuiwasha kwa njia maalumu.
Dk. Shimwela anasema, gesi ya methane inaweza kuwasha moto na ndiyo maana mara kadhaa moshi huonekana unafuka katika majalala na kumbe moshi ule husababishwa na wingi wa gesi ya methane.
Mchwa hutoa hewa chafu
Ni ngumu kuamini kuwa mchwa ndiye huongoza kwa kujamba kwa wanyama, na hivyo huzalisha gesi ya methane. Wana uwezo wa kuzalisha gesi kama kiwanda cha binadamu kinavyoweza kutengeneza gesi hiyo.
Ukijibana kutoa hewa chafu, utakutoka usingizini Hata ujitahidi kiasi gani kujibana usitoe hewa chafu, itatoka wakati utapokuwa umepumzika, hasa ukiwa umelala usingizi.
Hewa chafu kwa maiti
Maiti huendelea kutoa gesi hadi saa tatu baada ya mtu kufariki dunia. Hii huambatana na milio ya hewa chafu.
Hali hii husababishwa na misuli kusinyaa.
Safari ya ushuzi kwa sekunde
Wataalamu wanasema harufu ya hewa chafu huanza kusikika sekunde 10-15 baada ya mtu kutoa hewa chafu. Hii ni kwa sababu inachukua muda mrefu kwa harufu kuifikia pua.
Muda wa kutoa hewa chafu
Kwa kawaida, binadamu mwenye afya njema hutoa hewa chafu kwa wingi pengine na kupata haja kubwa nyakati za asubuhi kwa lugha ya Kiingereza huitwa morning thunder.
Wengi hudhani kuwa unapozuia hewa chafu, hewa hiyo hupotea, lakini madaktari wamekubali kuwa, gesi hiyo haitoki au kupotea bali hurudi ndani ya utumbo na hutoka tena baadaye. Hewa chafu haipotei, bali hubadili tu muda wa kutoka.
Mbwa hufurahia hewa chafu
Kwa kawaida, harufu yeyote mbaya kwa binadamu, mbwa huiona kama sisi tunavyonusa harufu ya marashi mazuri.
Mbwa huiona harufu ya hewa chafu kama binadamu wanavyofurahia harufu ya nyama choma au chakula kizuri. Kwa kawaida, mbwa hunusa makalio ya mtu aliyetoa hewa chafu zaidi ili avute harufu mbaya.
Hewa chafu mbele ya umma
Mtandao wa Wikipedia unachanganua kuwa baadhi ya tamaduni huchukulia tendo la kutoa hewa chafu lifanywe kistaarabu na baadhi ya tamaduni hawaoni haya kupumua hadharani na pia hufurahia tendo hilo.
Mfano ni kabila la Yanomami huko America Kusini, kwao husalimiana kwa kutoa hewa chafu na China unaweza kupata kazi ya kunusa harufu hiyo!
Katika Roma ya zamani, Mfalme Claudius akihofia kwamba kujizuia kutoa hewa chafu kunaweza kuwa hatari kiafya, alipitisha sheria kwamba ni ruhusa kutoa hewa chafu kwenye karamu. chanzo. Sayansi yabaini: Siri ya utoaji wa hewa chafu mwilini - mwanzo - mwananchi.co.tz