SoC02 Sayari: Tafadhali okoa nafsi zetu

SoC02 Sayari: Tafadhali okoa nafsi zetu

Stories of Change - 2022 Competition

qachira

New Member
Joined
Sep 13, 2022
Posts
1
Reaction score
1
“Baba, usiniache, tafadhali!?” nilikumbuka maneno yangu siku ile baba alipofariki. Kifo chake kilikua cha kusikitisha, ngozi yake dhaifu ili babuka kwa joto, siku zile za jua kali. Sikua na jinsi ya kumuokoa, hali yake ya ualbino ilifanya yeye ndio awe dhaifu zaidi kwenye lile joto kali.

“Maskini baba” nilijisemea huku nikitikisa kichwa.

“Mzee Zungu alikuwa na busara, lakini mimi sikuwa kwa maana ningekua nayo huenda angekua hai” niliwaza zaidi.

“Mpawe, karibu chakula” sauti ya Sonia ilinishitua. Nilimgeukia huku nikijaribu kuachia tabasamu, “Asante mke wangu”.

“Pole mke wangu” Nilisema huku nikilishika tumbo lake, alikua mjamzito wa miezi sita. Jasho lilikua likimtiririka, joto lilikua kali sana majira yale.

“Asante baba” alinijibu huku akinishika mkono. Tulienda nje ya nyumba yetu, ambapo tulipendelea kukaa wakati wa chakula, chini ya mti wa maembe uliokwisha kauka kawa kukosa maji

“Nawa mume wangu” alisema huku akikung’uta mikono yake pembeni baada ya kunawa.

“Leo pia hakuna mboga za majani Mume wangu,yani hazipatikani kabisa” Sonia alisema baada ya kumeza tonge la kwanza.

“Nadhani soko la nchi za nje limepatikana, ndiko wakulima wanaziuza” Alisema huku akinitazama.

“Hapana, hii ni kwasababu ya mabadiliko ya hali ya hewa, mazao yanakauka kupigwa na jua kali, na hata mvua zikinyesha zinaleta majanga kama mafuriko” nilisema kwa msisitizo. Baada ya kuongelea kuhusu jua, mawazo ya kifo cha baba yangu yakanirudia tena.

“Mwanangu, tunza mazingira yako, nayo yatakukutunza” Maneno yake yalikuja tena akilini mwangu, sauti yake ile ya upole iliyojaa busara haikua rahisi kusahaulika.

“Mpawe baba,…” Sonia alinitikisa kidogo baada ya kugundua sikuwa pale. Nilimtazama kwa huzuni, uchungu ulinijaa tena, kumpoteza baba kwa uzembe wangu lilikua ni jambo lisoweza kusameheka kirahisi.

“Unatatizo gani baba?” alisema huku akinitazama.

“Nipo sawa, hebu tumalize kula ili tuingie ndani, jua ni kali” nilisema huku nikiongeza kasi ya kula..

Tulimaliza kula. Niliosha vyombo, kisha tukapumzika.

Jioni ilipofika, Sonia aliandaa chakula cha jioni na baada ya kula alikwenda kupumzika. Nilibaki sebuleni nikisikiliza redio.

“Barani Afrika!.. Nchi ya Tanzania imeonywa kuhusu baa la njaa linaloweza kuiwakumba kutokana na ukame..” Nilibadilisha stesheni kutafuta habari za michezo.

“Ligi za ulaya zimesimama kutokana na joto kali..”.

“Kila kona habari za mabadiliko ya tabia nchi ziliongelewa, hali ilizidi kuwa mbaya”

“Mpawe, kuiponya dunia ndiyo jinsi ya kumuokoa mwanao na mimi” nilikumbuka maneneo ya baba. Siku ya mwisho mwili wake ulikua umeungua sana baada ya joto kuwa kali. Marashi ya kulinda ngozi hayakuweza kumsaidia. Machozi yalitoka, huzuni ilinijaa tena, kifo cha Mzee Zungu baba yangu kingezuilika kama tu ningekua msikivu.

“Hujachelewa mwanangu!, fanya hima umuokoe mwanao” Nilisikia sauti yake, “Baba” niliita huku nikipepesa macho pande zote za sebule. Sauti ya upepo makali ilisikia na kuongeza uwoga wangu, na ghafla, picha ya Mzee Zungu ilidondoka kutoka ukutani baada ya upepo kuisukuma. Moyo wangu ulipasuka kama kile kioo cha picha kilivo pasuka.

“Mume wangu” sauti ya Sonia ilinishitua kutoka usingizini. Nilitonoa macho huku nikimtazama yeye, na kasha kuitazama ile picha ya Mzee Zungu ilikuwa pale pale ukutani. Nilivuta pumzi kwa nguvu.

“Mke wangu, ninaomba kalamu na karatasi” Nilisema huku nikimtizama usoni mwake. Alikua amejaa hofu juu yangu. Aliondoka haraka na kuniletea kaalmu na karatasi. Alinipatina na gazeti iliniandikie juu yake, ukurasa wake wa juu ulikua umeandikwa “Misitu ya ufaransa yateketea kwa moto”.

“Unaandika nini baba?” Sonial aliniuliza.

“Sawa baba, harakisha uje kumpumzika” alisema huku akielekea chumbani. Hakujua kuwa ile ndio ilikua mara ya mwisho kuniona. Nilikaza moyo na kuanza kuandika barua, baada ya kumaliza niliikunja na kuondoka pale nyumbani, nisirudi tena.

Baada ya Miaka Kumi
“Chungu, leo nitakuambia kuhusu baba yako” Sonia alimwambia mwanae walipokuwa wamekaa kwenye mkeka chini ya mti wa maembe. Mti ule ulikua umechipua na kupendeza.

“Kwani yupo wapi Mama?” Chungu aliuliza kwa shauku.

“Soma hii barua kwa sauti Mwanangu ” Sonia alisema huku akimkabidhi Chungu karatasi.

“Baba kanitumia?” Chungu aliuliza huku akiipokea. “Soma mwanangu” Sonia alisema huku akimvika vizuri kofia iliyokua inamzuia asichomwe na jua moja kwa moja. Ngozi yake ilikua laini na ya kupendeza. Jua halikumuathiri kwa maana miale yake ilikua umepungua ukali.

Chungu alianza kuisoma.

“Mwanangu,

Ule usemi wa dunia ni tambala bovu sio sahihi. Dunia iko hai, inaroho na kazi ya hio roho ni kutoa maisha kwa viumbe hai viishivyo juu yake. Najua ninakuchanganya kwa maneno yangu, lakini naomba nikuelezee zaidi.

Babu yako alikua sope, miale ya jua na joto vilimdhuru, na kwa bahati mbaya joto na jua kali viliongezeka kila mwaka. Ila kabla ya kifo chake, alinishauri nitunze mazingira. Lakini kwa ukosefu wa busara sikufuata ushauri wake. Niliendelea kukata miti na kuchoma misitu, niliendelea kuharibu na kuchafua vyanzo vya maji, nilitumia bidhaa zenye kuharibu mazingira na mwishowe niliweza kutoboa anga ya ozone, moyo wa dunia. Hivyo joto kali, miale hatari, mafuriko na njaa ndiyo majanga yaliyofuata. Haikuishia hapo mwanangu, mazao na vyanzo vya maji yalikauka, mifugo ilikufa na vilio vilitawala, kilio hicho kilikua change pale babu yako alipo fariki. Mwanangu, wewe pia umezaliwa na ulemavu wa ngozi, ninajua hili kwa sababu ya historia ya mama yako na yangu.

Niliumia sana nilipojua kua ungezaliwa kwenye dunia isiyo rafiki kwako. Hivyo nimekata shauri, ninakwenda kumtafuta sayari dunia. Nimeamua kumtafuta kwa kutunza mazingira, nikitambua na yeye angetuokoa kwa kututunza sisi.

Nimeamua kufanya kazi ya kuitunza dunia kwa kupanda miti, kusafisha vyanzo vya maji, kuelimisha watu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Nimeamua kupunguza shughuli za kibanadamu ambazo zina haribu mazingira. Ninatumaini matunda ya kazi yangu yatakunufaisha wewe na kizazi chako.

Mwisho wa yote, mwanangu, ninaomba radhi kwa yote uliyo pitia kwa kuukosa uwepo wangu katika maisha yako.

Ipo siku tutaonana mwanangu.

Wako, Mpawe Zungu”.

Chungu alimaliza kusoma ile barua, uso wake ulijawa furaha na amani.

“Mbona unafuraha mwanangu?” Sonia alimuuliza mwanae baada ya kuona furaha yake.

“Mama, baba hayupo ili mimi niwepo” alisema akitabasamu.

“Kweli mwanangu” Sonia alipata faraja kutoka kwenye maneno ya mwanae

“Mama, twende tukazime ule moto pale jalalani, tuitunze dunia” Chungu alisema huku akiinuka na kukimbilia jalalani.

“Twende mwanangu” Sonia alijibu huku akitazama angani, alijua mume wako kokote alipo alifurahia kuona mwanae akiitunza dunia.
1663070107562.png

Mwisho.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom