Uchaguzi 2020 Seif Maalim Seif: Tunataka kujenga nyumba moja, kwanini tugombanie fito?

Uchaguzi 2020 Seif Maalim Seif: Tunataka kujenga nyumba moja, kwanini tugombanie fito?

Sam Gidori

Senior Member
Joined
Sep 7, 2020
Posts
165
Reaction score
417
Tutaunganisha sera za vyama vyote vya siasa ndani ya siku 100 za kwanza madarakani
Mgombea Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima Tanzania, AAFP, Seif Maalim Seif amesema kuwa ndani ya siku 100 za kwanza atakapokuwa madarakani atafanya mabadiliko katika mfumo wa Vyama vingi ili kuwezesha kuwa na sera ya pamoja ya Vyama vyote.

Seif amefanya mazungumzo maalum na Jamii Forums ambapo amesema kuwa mfumo wa sasa wa Vyama vingi ulioanzishwa mwaka 1992 unasababisha kuundwa kwa Serikali inayotokana na Chama kilichopata kura nyingi zaidi, ambapo Sera za Chama hicho ndiyo hutumika kupanga dira ya maendeleo kwa miaka mitano ambayo Serikali hiyo itakuwa madarakani.

"Hii dhana ya kuwa Chama kitakachoshinda kinachukua kila kitu ni kama ulaghai. Watanzania wamegawanyika katika itikadi na nadharia tofauti. Lengo letu ni kuunda Serikali yenye Sera jumuishi. Tutakusanya Ilani za vyama vyote, tutakaa na Wagombea wa Vyama vyote, na ndani ya siku 100 za mwanzo, tutakachozingatia ni kwamba maendeleo hayahitaji tofauti ya Vyama wala itikadi. Tunataka kujenga nyumba moja, kwanini tugombanie fito?" alisema Seif.

Maendeleo hayahitaji tofauti ya Vyama wala itikadi. Tunataka kujenga nyumba moja, kwanini tugombanie fito?
Seif Maalim Seif

Mfumo uendeshaji wa kampeni unadhihaki Demokrasia
Seif amesema kuwa Vyama vilivyojitoa kusimamia maslahi ya Watanzania havikuundwa kwa lengo la kusimamia maslahi binafsi, lakini kutokana na tofauti za kiuchumi kati ya vyama hivyo, kuviweka katika uwanja mmoja wa mapambano ni kudhihaki Demokrasia na si kulea Demokrasia.

"Huwezi kuangalia Chama kimoja kinatumia helikopta, Chama kingine kinatumia magari mawili, matatu tu; hauwezi kuzunguka nchi nzima hivyo. Tunahitaji kuwa makini katika kutengeneza mazingira ambayo vyama vyote vinaweza kushiriki katika kuwahudumia Watanzania. Demokrasia ni gharama, na gharama imeongezeka zaidi kutokana na ukiritimba na Sera mbovu za Chama kilichopo madarakani sasa," amesema Seif.

Kukosekana kwa elimu ya uraia kunaongeza ugumu wa kampeni
Seif anasema kuwa changamoto ya jamii kutokuwa na uelewa kuhusu elimu ya uraia imesababisha watu wengi kushindwa kuelewa Sera za Vyama vya Siasa, kutokana na kile alichokishuhudia wakati wa mikutano ya ana kwa ana na wapiga kura, kwamba watu wengi wanashindwa kufanya mlinganyo wa Sera za Vyama vya Siasa na uhalisia wa maisha yao na kuishia kufuata mkumbo.

"Unakwenda eneo ambalo tayari kumekuwa na wafuasi wengi wa Chama fulani ambao wametokana na mgawanyiko wa ushabiki, mathalani kwenye ngome ya Chama tawala, watakuona kana kwamba wewe unatumika na Chama kikubwa cha upinzani. Tatizo ni upokeaji wa maana kamili ya Demokrasia, kwamba tunatakiwa kutofautiana bila kuumizana," amesema Seif.

Amewataka wananchi kutoshawishiwa na wingi wa watu walio katika mrengo wa Chama fulani, au idadi ya watu wanaojitokeza katika kampeni za Uchaguzi, badala yake wampigie kura mgombea mwenye nia ya dhati ya kutatua changamoto zao.

"Unajaza uwanja, unaleta matamasha, unakwenda kuzungumza na watu kwa kuwahutubia badala ya kusikiliza kero zao. Unakwenda pahala, unawaambia watu utawajengea barabara kumbe shida yao ni maji. Kuna tija katika kuwakusanya watu katika viwanja vya mpira na kuhatarisha maisha yao na kuacha shughuli zao kwenda kusikiliza sera kwa dakika mbili, tatu, baada ya hapo kunakuwa na vurugu au usalama mdogo? Tujaribu kuliangalia hili, ili miaka mitano, mikutano ya kampeni ifanyike katika kumbi za mikutano, kuwe na idadi ndogo ya watu, tutapunguza kadhia kwa jeshi la polisi, tutasaidia kwa shughuli za kiuchumi kutokusimama, na Vyombo vya Habari vitatumika kuwasilisha Sera za wagombea majumbani mwao [wananchi]."

Uwezeshaji wa Wanawake kimadaraka ni ulaghai
Seif anasema kuwa Chama chake hakitoi kipaumbele katika kumpa nafasi ya Uongozi Mwanamke kutokana na uhalisia wa changamoto zinazomkabili Mwanamke katika jamii ya Kiafrika iliyotawaliwa na mfumo dume, badala yake Chama cha Wakulima Tanzania kinatanguliza kutoa suluhu ya matatizo ya msingi yanayomkabili Mwanamke kama vile kuboresha huduma za afya kwa Mwanamke, kuwapatia ruzuku, kuwamilikisha ardhi nk.

"Huu ulaghai wa kusema kuwa tunampa Mwanamke nafasi ya Uongozi si wa kweli. Ndio maana sisi tukaja na mkakati wa kumwezesha Mwanamke kwa kumpa mikopo nafuu na isiyo riba, mradi awe Mtanzania, tumpe elimu ya mikopo na ujasiriamali na kumtafutia masoko yake, huku ndiko kumwezesha Mwanamke. Lakini sio ulaghai wa kumpa asilimia 50 kwa 50. Jiulize, ni Viongozi Wanawake wangapi walioingia majimboni wanaowasaidia Wanawake wenzao? Utakuta kwamba wamejitajirisha wao wenyewe na kutengeneza mgawanyiko mkubwa zaidi katika jamii," alisema Seif.

Vyama vinavyopiga sana kelele havina ufumbuzi wa changamoto za wananchi
Seif amesema kuwa anazifahamu changamoto zinazowakabili waandishi wa habari na vyombo vya habari, hivyo atakapoingia madarakani atafanya mabadiliko katika mfumo wa Vyombo vya Habari ili kuviwezesha kutoa habari kwa uhuru na usawa kiasi cha kumshawishi mwananchi kufanya maamuzi bila kuwa na ushawishi wa kukusanywa na malori ama matamasha ya muziki.

"Kwa kuwa mazingira ya Vyombo vya Habari hayakuwa rafiki, waandishi wa habari wanalazimika kuchagua upande. Kumekuwa na mgawanyiko mkubwa ndani ya vyombo vya habari, wale wanaounga mkono Serikali na wale wenye mtazamo tofauti na Serikali. Ukiwa kwenye mambo ya kupinga Serikali, unatazamwa kwa jicho la wasiwasi, ukiwa upande wa Serikali unatazamwa kwa jicho la mashaka. Ningependa kuwaomba waandishi wa habari waache kukuza habari za hivi Vyama vinavyopiga sana kelele, kusema ukweli, ukiangalia, havina ufumbuzi wa changamoto za wananchi, isipokuwa labda mazingira au uwezo mkubwa."

Seif Maalim Seif.png
 
Hii ni kweli. Mawazo haya yanafaa kwa taifa.

Tanzania stand up.
 
Nilikua namtafuta maalim kwenye picha simuoni
Kumbeeeeeeee kuna original na sio original
 
Back
Top Bottom