Seneta mmoja nchini Kenya ameeleza kuunga mkono hatua ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwapiga marufuku wanaharakati kutoka Kenya.
Samson Cherargei, seneta wa kaunti ya Nandi, anasema ni haki ya Rais Samia kuzuia watu wanaoingilia masuala ya nchi yake kutoka nje.
"Namuunga mkono kikamilifu Rais Suluhu kwa kuwapiga marufuku wanaharakati wa Kenya kutaka kuingilia masuala ya nchi yake. Uhusiano wa Kimataifa unataka kuwepo kwa heshima miongoni mwa Mataifa rafiki." Amesema
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024) Jana Jumatatu Mei 19, 2025, Rais Samia alisema kuna mwenendo unaoibuka wa baadhi ya wanaharakati kuvuka mipaka na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.
“Tusuiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region (kanda) yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku,” alisema Rais Samia.
"Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu, aliongeza Rais Samia.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wasimamizi wa sera za nje, wanapaswa kuhakikisha kuwa hakuna “watovu wa adabu” kutoka mataifa mengine wanaovuka mipaka ya Tanzania na kuingilia masuala ya kitaifa.
“Niombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na ninyi wasimamizi wa sera zetu za nje, msitoe nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kuvuka hapa kwetu,” alisisitiza.
Kesi ya Tundu Lissu inaendelea huku mashinikizo kutoka ndani na nje ya nchi yakiongezeka, yakihusisha madai ya ukandamizaji wa haki za kiraia na kisiasa, jambo ambalo Serikali ya Tanzania inakanusha.
Source: Jambo TV
Soma pia