Serikali iiunde upya LATRA na madereva, ushuru wa magari na mitihani na vyeti viwe na idara zake tofauti

Richard

Platinum Member
Joined
Oct 23, 2006
Posts
16,890
Reaction score
26,440
Katika malalamiko ambayo madereva wameyatoa leo ni kuhusu kutozwa zaidi ya tozo 20 wakiwa mabarabarani, pia kuna haja ya kuangalia namna ya muundo na uendeshaji wa LATRA unavyofanya kazi.

Hata polisi kutumia mwanya wa kuwabana madereva na kuwachomoa chochote huko barabarani pia hakuleti tija kwa madereva, abiria na wadau wengine wa usafiri na khasa wenye mabasi.

Udereva ni ujuzi (skill) ambayo si kila mtu aweza kuitumia khasa kwa mamagari makubwa kama mabasi na malori ya mizigo. Pia umiliki wa vyombo hivyo nao ni uwezo wa kifedha na ujuzi wa namna ya kuendesha biashara ya usafirishaji ama wa abiria au mizigo.

Napenda kuishauri serikali kupitia wizara ya usafirishaji kuiangalia LATRA na kuifumua ili kuijenga upya na pia kuunda taasisi zingine tofauti lakini zenye kuwasiliana kuhusu madereva, leseni na ukusanyaji wa kodi kama ushuru wa barabara na makosa ya barabarani.

Serikali iunde mfumo tokea chini kabisa (from scratch)ambao utazingatia sheria za bunge, uendeshaji wa kisasa na utaalam ambao utajumuisha watu wenye uelewa na masuala ya usafirishaji wa abiria, udereva na usimamizi wa barabara (TANROAD)

Kwa mfano mmoja wa madereva leo kasema kwamba meneja wa TANROAD pale Kibaha alemamua kujenga uzio wa chini katikati ya barabara ili kuweza kudhibiti msongamano lakini kumbe bila kufahamu ameongeza msongamano huo ambao usingekuwepo kama barabara kubwa ya kwenda Morogoro ingekuwa na upana uleule tokea Dar-es-Salaam.

Sasa ni namna gani serikali itaweza kuunda mfumo huo mpya na wenye ufanisi katika kudhibiti madereva na kuhakikisha usafirishaji abiria hauna usumbufu kwao wala madereva na wamiliki wa vyombo hivyo.

1. Hatua ya kutunga sheria na kuwa tiyari kuitumia sheria hiyo. Hiyo ni pamoja na kuunda taasisi itayokusanya taarifa, kutoa adhabu na kusimamia sheria hizo.

Hapa nazungumzia sheria ya usalama barabarani ambayo itamtaka dereva yoyote kuwa na leseni ya udereva, isokwisha muda wake na kwamba kila gari lazima lisajiliwe na lijulikane nani ni mmiliki wake au mtunzaji (keeper).

Kukusanya mapato itakuwa ni jukumu la taasisi hiyo khasa ushuru wa barabara, na tozo zingine kama zipo pamoja na kuhakikisha tozo hizo au ushuru huo walipwa pale inapotakiwa.

Sheria na miongozo ya kulinda faragha za madereva na raia kwamba ni kwa kiasi gani taarifa hizo zatumika kusambazwa baina ya vyombo kama mahakama, polisi na makampuni ya bima.

2. Mfumo wa kiufundi Technical Architecture

Kuunda kanzidata mbili zinoingiliana ya taarifa za dereva ambayo itawasiliana na NIDA na ingine ambayo itahusiana na namba maalum ya injini ya gari au VIN.

Kuunda mfumo wa APIs ambao polisi, mahakama, madaktari na kampuni za bima zitaweza kuusoma na kuona taarifa za dereva na gari ili kubaini kama kuna mapungufu.

Mwisho kuunda mfumo salama wa utambulisho (secure digital identity) ambao itafanya mifumo hii mitatu iwasiliane yaani NIDA, Uhamiaji ili kuthibitisha uraia wa mtu anapoomba leseni ya udereva.

3. Uendeshaji wa mifumo hiyo- Operational Core Modules.

Mfumo huu utawezesha raia khasa madereva kuitumia kila siku katika simu zao kufanya masuala mbalimbali yahusuyo uderava kama mfumo wa dereva au driver module ambao utafatilia mitihani ya madereva, kutoa leseni za awali kabla ya leseni kamili, na pia kutoa points pale polisi wanapoweka points.

Pia kuna mfumo wa vehicle module ambao waangalia gari lilipotoka, log yake na anaelimiliki pamoja na namna ya gari au plate number. Sijaelewa polisi anakuwa atumia sheria ipi kuondoa plate number kutoka kwenye gari ambapo lina mmiliki wake.

Mfumo wa malipo ambapo dereva mwenyewe akiona adaiwa faini ataingia kwenye tovuti na kulipa iwe tozo au faini ya barabarani bila kumpatia fedha hizo polisi.

4. Usalama na kulinda mfumo dhidi ya wizi.

Mfumo huu ni moja ya mifumo muhimu sana kwa serikali kwa sababu wauingizia serikali mapato hivyo kuwa mashakani na shughuli za wizi na watu waso waaminifu.

Mfumo huu utatoa vitu viwili.

1. Uwezo wa kutoa kadi za leseni na vyeti vyenye alama za usalama ambazo zitakuwa ngumu kuzichakachua.

2. Kulinda mapato na dhidi ya vitendo vya rushwa- Anti- Corruption Automation.

Mfumo huu utaondoa watu kukutana uso kwa uso kuombana rushwa iwe TRA au polisi barabarani.

Ukiwasikiliza madereva wao madai yao ni kutumia pesa sana kulipa tozo mabarabarani tangia mwanzo wa safari hadi mwisho jambo ambao si la afya na lasababisha "anxiety" na kutokuelewana na wamiliki wa mabasi hayo.

Jambo jingine ambao halitaweza kuwafrahisha wataosoma mada hii ni kwamba stendi ya Magufuli yatakiwa iwe ni kwa ajili abiria tu na kama ikiwezekana ijengwe sehemu ingine kwa ajili ya maduka, kupumzika na pia kwa ajili ya wapokeaji na wasindikizaji.

Sehemu ambayo mabasi yapaki panatakiwa pasiwe na mtu yoyote yule ambaye ama afanya udalali wa tiketi au yupo kwenye harakati za wizi, hivyo eneo lote lenye sehemu za kupaki mabasi (Parking Bays) latakiwa kuwa ni kwa ajili yamabasi tu na si vinginevyo na hata madereva wanapopaki mabasi yao watakiwa wafunge milango na kuzima injini ili kwenda kupumzika katika vyumba maalum vya madereva (driver resting rooms).

Kuundwe mfumo wa PA na ule wa mabango ya matangazo ambayo itaongoza namna ya kuwataarifu abiria kuhusu utayari wa basi kabla ya safari na mabango hayo yaonyeshe ratiba ya mabasi, na safari zake huku wahusika wakitangaza kila hatua ya safari za mabasi hayo.

Serikali ijenge eneo jingine maalum kwa ajili ya maduka, mapunziko, maegesho ya magari na sehemu maalum kwa ajili ya taxis na vibajaji na eneo hili litaungana na kituo hicho cha mabasi kwa njia maalum iwe madaraja maalum au vivuko kutoka eneo hilo na kituo cha mabasi.

Serikali ione kwamba hii ni fursa kwake kwa kuweka kutengeneza miundombimu ambayo itaisaidia serikali yenyewe kuweka kupata mapato na kuwezesha watu kupata ajira kimasihara.

Lakipi pia kama nchi tukiwa twaelekea kushereheka miaka 65 ya uhuru serikali yapaswa kuangalia namna ya mfumo wake wa uongozi katika mikoa yake kama waendana na mahitaji ya mabadiliko ya lazima katika kuboresha miji na makazi ya raia wake.

Ni jambo la muhimu serikali ikachunguza kuwepo kwa migongano ya kiutendaji kati ya viongozi wake wa kimkoa khasa mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya.

Ningeshauri meya wa jiji la Da-es-Salaam kupewa madaraka ya kuamua ni aina gani ya vipaumbele kama suala la usafiri na maboresho ya miundombonu katika miji. NI hivi majuzi raisi kalalamikia sual ala uchafu katika miji yetu jambo ambao mameya wa manispaa waweza kabisa kusimamia na kuhakikisha miji yetu ni misafi kila wakati.

Waafrika wenzetu kama Rwanda wameweza kuweka miji yao katika hali ya usafi, madereva wa kinyarwanda watambua kuwepo sheria khasa kwa wenye vibajaji ambao ni lazima wavae zile kofia ngumu, tuige huko tuchukue mazuri.

Narudia tena tarehe 9 Disemba 2026 Tanganyika itatimiza miaka 65 ya Uhuru wake na kama taifa tutumie fursa hiyo kujitafakari katika mengi kuanzia kutatua matatizo madogomadogo kama ya madereva wa mabasi na pia namna ya kutunza miji yetu kwa kujenga miundombinu inoeleweka.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…