SoC04 Serikali ikomeshe matukio ya utekaji, ni doa kwa uhuru, amani, usalama na demokrasia ya nchi yetu

SoC04 Serikali ikomeshe matukio ya utekaji, ni doa kwa uhuru, amani, usalama na demokrasia ya nchi yetu

Tanzania Tuitakayo competition threads

Xpertz

Member
Joined
May 3, 2024
Posts
13
Reaction score
10
UTANGULIZI

Kwa takribani kipindi cha miaka 8 mfululizo nchini Tanzania (2016-2024) matukio ya watu kutekwa nyara, kupotezwa na hata kushambuliwa au kuuawa na watu wasiojulikana huku wahusika wa matukio hayo wakiwa hawapatikani yamekua matukio ya mfuatano na ya kawaida kabisa. Yalishamiri sana katika Serikali ya awamu ya tano ila sasa yameanza kurejea kwa kasi chini ya serikali ya awamu ya sita, haya sio matukio yenye nia njema na taswira ya taifa letu na mustakabali wa amani yetu na demokrasia ya nchi. Picha mbaya zaidi ya matukio haya ni kwamba yamekua yakiwakumba wakosoaji wa serikali pamoja na wanaharakati.

Mmoja wa wahanga wa matukio hayo ya kinyama ni aliyekua mkosoaji mkubwa wa Serikali na mbunge wa singida mashariki Tindu Anthipasi Lissu aliyeshambuliwa na watu wasiojulikana jijini Dodoma makao makuu ya nchi eneo lenye ulinzi mkali ila hadi leo wahusika hawajakamatwa. Hii inatoa picha gani? Kwamba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeshindwa kabisa kuwajua wahusika? Haiwezekani. Lazima SERIKALI ichukue hatua za dhati kuyamaliza matukio haya, hayana tija wala picha nzuri kwa taifa letu yanaichafua nchi mno.

Hakuna mwananchi wa kawaida mwenye uhakika na usalama wake kwa sasa, raia wanaishi kama digidigi au swala kwenye taifa lao, wanawindwa kila kukicha na majangili, cha kusikitisha wawindaji hao haramu(watekaji) hawakamatwi wala hawajulikani wamepewa tu jina maarufu wanaitwa WATU WASIOJULIKANA. Inasikitisha sana kwamba hakuna anayejivunia amani na uhuru, raia unaweza kutekwa mda wowote na kufanywa chochote na wahusika wasijulikane, INATISHA MNO

Nashauri yafuatayo yafanyike kukomesha tabia hii isiyo ya kiungwana ya watu kutekwa na kupotezwa

1. IUNDWE TUME HURU NJE YA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUFANYA UCHUNGUZI HURU
Kwa kiasi kikubwa matukio hayo ambayo yameacha majeruhi, wajane na yatima wengi yamekua yakihusishwa na uhusika wa vyombo hivyo, kwa muktadha huo ni vyema vyombo hivyo visipewe kazi ya kujichunguza hii itasaidia upatikanaji wa haki jinai nchini ambapo inaonekana wenye madaraka au nguvu ya fedha bado wana upenyo wa kuwafanya wakosoaji wao vyovyote watakavyo na vyombo vyetu vishindwe kuwabaini na kuwachukulia hatua.

2. IUNDWE SHERIA VIONGOZI WA KISIASA WAWEKEWE MIPAKA KWENYE VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA
Kumekuwepo malalamiko ya viongozi wengi wa vyama vya siasa na wanaharakati kwamba kuna baadhi ya viongozi wamekua wakitumia mamlaka yao vibaya kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Rais Dr. Samia Suluhu Hassan pia aliwahi kukiri kwamba kuna baadhi ya wateule wake wamekua wakitumia ubabe na kuwaumiza wananchi na kuwataka waache tabia hiyo. Hii inaonesha dhahiri kama ndivyo basi huenda wakawa na mkono hata kwenye matukio haya ya watu kutekwa,kupotezwa na kuumizwa, huenda ni matokeo ya matumizi mabaya ya madaraka. Lazima tuweke mipaka ya kimaagizo kwa viongozi wa kisiasa wasiweze kutumia mamlaka hizo kushughulikia maadui zao wa kisiasa nk

3. JESHI LA POLISI LIWE NA MFUMO WA UWAJIBIKAJI
Kwa miaka kadhaa sasa jeshi la polisi limekua likikumbwa na matukio mengi ya uzembe, mahabusu kufia vituo vya polisi pamoja na jeshi hilo kushindwa kuwapata na kuwadhibiti watu wanaotekeleza matukio ya utekaji nchini hususani yanayowakumba wakosoaji wa Serikali, hii ina maana jeshi la polisi nchini linapaswa kujisafisha dhidi ya matukio hayo kwa kuwa na mifumo imara ya uwajibikaji. Haiwezekani watu wanatekwa na kufanyiwa unyama mpaka kwenye vituo vya polisi (mfano kijana Edgar maarufu kama Sativa kwenye karakana ya polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam) na kutupwa hadi kwenye mbuga za wanyama halafu jeshi la polisi lipo lipo tu hakuna hatua za dhati kukomesha matukio hayo.

4. SHERIA YA UKAMATAJI WA RAIA IREKEBISHWE
Matukio mengi ya utekaji nchini yamekua yakiripotiwa kwamba watekaji wamekua wakija wamevaa kiraia na magari ambayo mengine hayana hata namba za utambulisho(Plate number) au namba feki za utambulisho na kujitambulisha kama maafisa usalama au askari mwishowe ndio wamegeuka wauaji na watekaji, wakiondoka na raia ndio unakua mwisho wake kuonekana au kuwa hai. Nashauri utaratibu uwe watu wakija kumkamata mtu lazima wakamchukulie ofisini kwa mtendaji au mwenyekiti wa eneo husika kwa maandishi na utambulisho rasmi vinginevyo raia anayekamatwa atumie kila mbinu kukataa ukamatwaji wa kihuni na iwe mwisho wa matukio haya ya kidhalimu nchini yanayoacha wengi na ulemavu, misiba, wajane na watoto wasio na msaada sambamba na kuichafua nchi vibaya mno kimataifa kama eneo lisilo salama sana kuishi kutokana na kuwepo watekaji maarufu kama watu wasiojulikana ambao wamejitwalia utukufu kwa kufanikiwa kuendesha matukio hayo mikoa hadi mikoa bila vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria. Ni mtalii gani atakua na furaha kuendelea kuja kutalii nchi ambayo mtu anaweza kupotezwa kama mdudu na vyombo vya ulinzi na usalama visiwabaini wahalifu?

5. MATUKIO YOTE YALIYOTOKEA(YALIYOPITA) YAPATIWE MAJIBU
Lazima Serikali ili kurejesha heshima ya taifa matukio yote yaliyotokea yapatiwe ufumbuzi wa haraka na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria wafikishwe mahakamani ili iwe fundisho. Kitendo cha matukio yaliyopita kuachwa huku waovu waliofanya matukio hayo wakiendelea kuwa uraiani ni ishara kwamba Serikali imeridhika na matukio hayo na huenda hata yanayoendelea kutokea wahusika ni wale wale, je nani anayewalea wahalifu hao, nani mwenye maslahi nayo kama Serikali haitafuti muarobaini wa matukio hayo kwa kuwakamata wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria?

MATOKEO YA KUPUUZWA MATUKIO YA UTEKAJI
Nchi inachafuka kimataifa pia tunaunda kizazi sugu kinachoamini kwamba uhuru uliopo ni kwa baadhi ya watu wenye mamlaka na fedha ila wananchi wa kawaida wanaweza kupotezwa na kufanywa chochote wakati wowote na wahusika wasijulikane wala kuchukuliwa hatua za kisheria. Matokeo yake kundi la wahanga ambao ni yatima, wajane na walemavu waliotokana na matukio hayo sambamba na wadau wa demokrasia na uhuru watatafuta njia mbadala ya kutetea haki ya uhuru wao katika taifa lao kwa namna nyingine sababu vyombo vyenye dhamana ya kuwalinda (serikali/dola) vimeshindwa. Hii huweza kuja kupelekea machafuko nchini au hata mapinduzi kwani sio wote wanaofurahishwa na matukio ya namna hiyo. Ni matukio yanayojenga kizazi hatari

Kwa Upande mwingine matukio hayo yamekua yakiua ari na morali ya wananchi kushiriki mambo mbalimbali ya kidemokrasia ikiwemo uhuru wa kutoa maoni kutokana na hofu ya kupotezwa. Uhuru wa vyombo vya habari pia unaendelea kudhoofika kila kukicha kutokana na wanahabari hususan wa habari za kisiasa na kiuchunguzi kuwa moja kati ya wahanga wa uhalifu huo wa UTEKAJI

Inatosha

Ifike mwisho, huu sio utamaduni wetu, nchi imekua kama ya magenge ya kimafia kwamba kuna watu wanaweza kuteka watu na kuwapoteza na hakuna wa kuwapata wala kuwafanya chochote HII HAIKUBALIKI HATA KIDOGO

Kama taifa tunapata wapi nguvu ya kujiita nchi huru? Tunapata wapi nguvu ya kujiita taifa lenye amani, usalama na demokrasia kama wenzetu wanapotezwa wanatekwa na kufanyiwa unyama kila siku na wahusika hawakamatwi?

FB_IMG_1719664793973.jpg
FB_IMG_1719664813470.jpg

Picha kwa hisani ya JamiiForums.com
 
Upvote 1
Back
Top Bottom