mkiluvya
JF-Expert Member
- May 23, 2019
- 809
- 729
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali kupitia mpango wa maboresho ya mazingira ya biashara nchini (Blue Print) imeweza kufuta tozo 163 kati ya 173 zilizokuwa zikisababisha kero na usumbufu kwa wafanyabiashara nchini. Akizungumza katika ufunguzi wa Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DIFT) jana Ijumaa (Julai 3, 2020), Waziri Mkuu Majaliwa alisema jitihada hizo za Serikali zinalenga kukuza mchango wa sekta ya biashara katika pato la taifa nchini.
Alisema kupitia maboresho ya Blue Print, kati ya tozo hizo tozo 114 ni za sekta ya kilimo na mifugo, tozo 5 kutoka Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) na tozo 44 kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambazo zililalamikiwa na wafanyabiashara kutokana na kutoza gharama kubwa wakati wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
‘’Kufutwa kwa tozo hizo kumewezesha ongezeko la usajili wa taasisi ya OSHA kwa nafasi 16657 mwaka 2019 ikilinganishwa na nafasi 11663 mwaka 2018, hivyo Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara nchini kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutunga Sheria za Uwezeshaji Biashara’’
Kwa mujibu wa Majaliwa alisema Serikali pia inaendelea kupitia majukumu ya mamlaka mbalimbali za udhibiti ili kuhakikisha zinawawiana kimajukumu hatua inayolenga kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara pindi wanapohitaji huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hizo.
Aidha alisema kuwa Serikali pia itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara kwa kuweka mazingira bora na rafiki ili kuziwezesha sekta za viwanda na biashara kuendelea kuvutia wawekezaji na kuchangia katika ukuzaji wa uchumi wa nchi.
Aliongeza kuwa maonesho ya mwaka ya 2020, yamewekwa kimkakati ili kuwezesha shughuli za mazao, biashara pamoja na huduma kuweza kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuziwesha sekta za kilimo, biashara kuweza kujitosheleza na mahitaji ya bidhaa muhimu ikiwemo chakula.
Akizungumzia taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Benki ya Dunia, kuitangaza Tanzania kuingia katika nchi ya kipato cha kati, Majaliwa alisema juhudi hizo zimetokana na msukumo uliowekwa na Rais Dkt. John Magufuli wa kujenga sera imara za uchumi usio na utegemezi.
‘Mafanikio haya yanaiweka Tanzania katika ramani ya dunia, jambo kubwa ni kuwa tumeingia katika nchi ya kipato cha kati miaka 5 kabla ya malengo tuliyojiwekea katika kuifikia hatua hiyo mwaka 2025’’