Jibu lipo katika madaraka ya Bunge yaliyoaainishwa na Ibara ya 63 ya Katiba. Ibara hii inatuambia wazi kuwa Rais ni sehemu moja ya Bunge. Si busara kwa demokrasia kwa sehemu ya pili ya bunge kudai jibu linalolikubali. Sio lazima Bunge liridhike na majibu yote yaliyotolewa. Ushauri wangu ni kuwa sehemu ya pili ya Bunge ingeendelea na shughuli nyingine muhimu kwa kwa taifa letu. Shughuli kama kuangalia uwezekano wa nguvu umeme wa nuklea [kwa matumizi ya amani]. Wananchi wanapenda kupata nishati na sio malumbano kuhusu maamuzi yaliyopita na pengine kukosewa.
Je sehemu ya pili ya Bunge inaweza kuchukua hatua gani ? Ibara ya 63 inatoa upeo wa hatua zinaoweza kuchukuliwa :
63-(2) Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.
(3) Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza–
(a) kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;
(b) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti;
(c) kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;
(d) kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria;
(e) kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.