Halmashauri zetu zote zina idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambayo inatekeeleza majukumu yake chini ya Sehemu mbili yaani Sehemu ya Maendeleo ya Viwanda na Uwekezaji, na Sehemu ya Biashara na Masoko.
Idara hii ikiwezeshwa ipasavyo inaweza kuwa roho na msingi wa Halmashauri zetu kujitegemea, kwa kupunguza au hata kuondoa utegemezi kwa Serikali Kuu.
Hata hivyo, kwa sasa mara nyingi utakuta maafisa wa idara hii badala ya kubuni na kuendeleza miradi ya uwekezaji, wanajikita katika kufuatilia mapato yatokanayo na leseni za biashara ambazo wafanyabiashara hulipa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.
Msingi wa hoja ni kwamba idara hii iwezeshwe hasa kwa upande wa rasilimali watu na Tafiti zenye miradi. Serikali inapaswa kuajiri maafisa viwanda, maafisa biashara na maafisa uwekezaji (wachumi) kulingana na taaluma zao. Sio sahihi kwa Afisa Biashara mwenye ujuzi wa masoko na wateja kupewa jukumu la kubuni miradi ya viwanda au uwekezaji, hali hii lazima itapunguza ufanisi.
Bila mpangilio huu sahihi, Halmashauri zitaendelea kutegemea mgao kutoka Serikali Kuu na kuwakamua wajasiriamali wenye mitaji midogo na yenye mikopo ndani yake kwa ushuru na tozo kibao badala ya kubuni na kutekeleza miradi ya kibiashara na uwekezaji yenye tija kwa uchumi wa ndani.
Ni wakati sasa wa Serikali kupanga upya idara hii kwa mantiki na utaalamu ili iwe injini halisi ya maendeleo ya kiuchumi katika ngazi za Halmashauri.