beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,880
- 6,368
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema serikali haitaongeza muda wa kusajili laini za simu kwa alama za vidole, huku akitahadharisha kuwa katika siku zilizosalia, kasi ya wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi umeongezeka.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu siku zilizobaki kabla ukomo wa siku 20 alizotoa Rais John Magufuli, haujawadia. Mwisho wa usajili ni Januari 20 mwaka huu.
“Kumejitokeza wizi wa kimtandao; wananchi tuwe macho sana tunapomalizia hizi siku zilizosalia kabla laini ambazo hazijasaliwa hazijazimwa. Watu wanatumia siku chache zilizosalia kuibia watu kwa kiwango cha juu; bila kuwa makini, watu tutaibiwa sana,” alihadharisha Waziri Kamwelwe.
Waandishi wa habari walipotaka kujua kama siku za usajili huo kwa alama za vidole zitaongezwa, waziri alisema: “Aa! Aaa! Hakuna siku kuongezwa; siku za usajili hazitaongezwa.”
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi mwanzoni mwa wiki, takribani laini za simu 22,839,867 zilikuwa hazijasajiliwa kwa alama za vidole kupitia kampuni mbalimbali watoa huduma. Mintarafu wizi Waziri Kamwelwe alisema:
Kuna wizi wa mtandao; watu wanatumia simu ya ndugu yako kwenye namba ya mtu mnayejuana; anamtumia ujumbe rafiki yako kwa namba yako; anajua unamfahamu, Mfano, mtu anasema ndugu yangu Isack, nina shida naomba unisaidia Sh milioni moja au milioni mbili. Hao mara nyingi wanasingizia wanaumwa koo au wako kwenye kikao hawawezi kuzungumza. Kabla hujamtumia mtu pesa, mpigie kwanza ujiridhishe kuwa ndiye hasa mtu unayemkusudia.
Aliwahimiza wananchi kuwa makini dhidi ya watu wanaowatumia ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi wakiwataka wawatumie pesa wakijdai ni ndugu au rafiki zao. Uchunguzi umebaini kuwa njia nyingine wanazotumia matapeli kuibia watu fedha kwa njia ya mtandao ni kutuma ujumbe unaosema:
“Mtoto wako ameanguka ghafla shuleni hivyo mzazi tuwasiliane haraka.” Kupitia ujumbe huo, aliyetumiwa ujumbe huo anapotaka kujua kulikoni, mmoja wa matapeli hao hujidai ni daktari huku wengine wakijifanya ni walimu na humwambiwa mhusika kuwa, mtoto wake yupo hospitali anahudumiwa, lakini wakimtaka atume pesa haraka kusaidia mahitaji ya haraka kama dawa au damu au maji (drip). Njia nyingine iliyoshika kasi kipindi hiki ni ile ya kumwambia mtu: “Tuma kwa namba hii. Litakuja jina….”
Na ile inayokwambia kuwa umeshinda katika bahati nasibu hivyo, matapeli kukutaka utume kiasi fulani cha fedha ili atumiwe zawadi yako.
Zimesalia siku nne kumalizika kwa nyongeza ya siku 20 za usajili wa laini za simu kwa alama za vidole alizozitoa Rais John Magufuli. Awali, mwisho wa kusajili laini hizo ulikuwa Desemba 31, mwaka jana.
Desemba 27, 2019 Rais Magufuli alifanya usajili wa laini yake ya simu kwa kutumia alama za vidole na kuwasisitiza Watanzania wote wahakikishe laini zao za simu zinasajiliwa kwa alama za vidole kama ilivyoelekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akiwa wilayani Chato katika Mkoa wa Geita, Rais Magufuli aliongeza siku 20 kuanzia Januari Mosi mwaka huu ili wananchi ambao wasingeweza kuwa wamesajili laini zao Desemba 31, mwaka jana, waweze kukamilisha usajili na kuiagiza TCRA kuzima laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa baada ya januari 20, mwaka huu.
Rais alisema miongoni mwa faida za kusajili laini za simu ni usalama sambamba na kudhibiti uhalifu ukiwamo utapeli. Mwanzoni mwa juma, gazeti hili liliripoti takwimu zinazoonesha kuwa, usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama za umefikia asilimia 52.42.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Frederick Ntobi, alinukuliwa akisema idadi ya laini za simu zilizosajiliwa kwa alama za vidole kuanzia Machi 2018 hadi Januari 7, 2020 ni 25,160,147 sawa na asilimia 52.42, huku idadi ya laini zote za simu zilizoko sokoni ambazo zimesajiliwa ni 48,000,014.
Kukwama kwa watu wengi kusajili simu zao, kunaelezwa kuwa kunatokana na watu wengi kushindwa kupata namba za utambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu hizo uchunguzi umebaini kuwa ni pamoja na watu wengi kutokamilisha viambatanisho na taarifa muhimu zinazohitajika kikiwemo cheti cha kuzaliwa huku wengine wakisema idadi ya wato huduma wa Nida katika mchakato huo ni ndogo.
Chanzo: Habari Leo