Kuwa na serikali moja ni vizuri zaidi na jambo jema kuliko serikali mbili au tatu ikiwezekana nchi igawanywe kimajimbo na zanzibar iwe kama jimbo ikiwezekana na wawe na sheria zao za kijimbo na wafanye shughuli zao kijimbo ila mwisho wa siku wote tuwe na katiba moja ya nchi ya watu wa tanzania kama MAREKANI rais awe mmoja na kuwa na wakuu wa majimbo.
mfn:
Kila mikoa mitatu kufuatana na kanda iungane iwe jimbo moja na zanzibar pia iwe kama jimbo la visiwan shughuli zao za kiuchumi ziendeshwe kijimbo na kuwezesha makusanyo ya mapato yafanyike kijimbo baada ya hapo tujitahidi kuwekeza kwny biashara za kijimbo maana itasaidia kwa mikoa tegemez hasa ya kusini mwa tanzania kusaidiwa. Wakuu wa mikoa waondolewe wakuu wa mikoa waondolewe, wakuu wa wilaya pia tuwe na viongoz wa kata ambao watakuwa wana jumuika moja kwa moja na wananch kwny maamuzi.
Hii itasaidia kupunguza ukubwa wa serikali kuu na idadi ya wabunge maana wakuu wa majimbo ndo watakuwa wawakilishi wetu kwny baraza la mashauri ila tuwe na mawaziri wa sekta muhimu tu ambazo inabidi zifanane kama elimu, afya, fedha na ulinzi basi na kila jimbo liwe na wizara ndogondogo kutokana shughuli zao kuu za kiuchumi na maendeleo.
Mkuu,
Umeongelea suala la serikali moja kuu (federal government) kama mfano wa USA na kutaka kuwa na serikali za majimbo. Mfano huo unaweza kutekelezeka kwenye nchi kama USA kwa kuwa nchi zote (majimbo yote) yanakubaliana na dhana hiyo. Wenzetu wa Zanzibar tayari wanayo serikali yao, inaitwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na wanadai mamlaka zaidi kama kutambulika kimatatifa; yaani wawe na uwakilishi UN, bendera yao itambulike kimataifa, na Rais wa Zanzibar apewe heshima kimataifa kama Rais wa Zanzibar, siyo kama ilivyo sasa. Kwa maoni yao wazanzibar wanaona hofu ya 'kumezwa' katika huu Muungano kwa jinsi ulivyo sasa hivi na wanahofu ya kuwa kukiwa na serikali moja ndiyo watakuwa wamemalizika kabisa. Kumbuka wazanzibar walipigania nchi yao kwa visu, majambia, mapanga na hata mawe na kumng'oa mwarabu katika Mapinduzi ya 12 Januari 1964. Kwa mantiki hiyo suala la serikali moja litakuwa gumu sana kukubalika huko Zanzibar.
Suala lingine wanalolipigia sana debe ccm ni serikali mbili, kama ilivyo sasa, uwepo wa serikali ya Zanzibar na serikali ya Muungano. Hili nalo linakuwa gumu kumeza kwa sisi watu wa Tanzania Bara (Tanganyika), ambao tunaona mashaka vilevile ya kuwa tumemezwa kwa miaka 49. Wazazi wetu pia walipigania uhuru wa nchi iliyoitwa Tanganyika na ikapata uhuru 9 Desemba 1961. Baada ya kuungana na Zanzibar, wenzetu pamoja na uchache wao, waliruhusiwa kubaki na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hata kama imenyang'anywa meno, ilhali watanganyika tukalazimishwa kukubali kuipoteza nchi yetu. Pengine hali ya dunia ya wakati ule 1964 ilikubali mfumo huu, lakini umefika wakati tunajitafakari na kujiuliza sisi ni kina nani, kwa nini hatuna serikali yetu, na tunataka kufanya maamuzi ya kutupeleka mbele miaka mingine 50 ama zaidi. Hii ndiyo mantiki inayofanya watanganyika (ama kama wanavyopenda kutuita wanasiasa watanzania Bara) tuone ugumu kukubali uwepo wa serikali mbili.
Kwa mtazamo wangu bado nafikiri serikali tatu ndiyo njia pekee itakayoweza kuwapa watu wa pande zote mbili nafasi ya kujiona ya kuwa ni sehemu ya Muungano huu. Suala la gharama za uendeshaji linaweza kutafutiwa ufumbuzi kwa kuwa na serikali ndogo yenye watendaji makini. Hapo sasa mfano wa USA unakuwa mzuri ya kwamba tuwe na Serikali Kuu yenye Rais wa Tanzania, na Serikali ya Zanzibar inayoongozwa na mtu mwenye Cheo kama cha 'Governor', na Serikali ya Tanganyika pia iwe na 'Governor'. Masuala yasiyokuwa ya Muungano yasishughulikiwe na Serikali Kuu, bali 'Governor' wa Tanganyika apewe mamlaka kamili ya kusimamia shughuli za kila siku za Tanganyika. Vilevile 'Governor' wa Zanzibar apewe mamlaka ya kusimamia shughuli za kila siku za nchini mwake bila bugudha kutoka kwa serikali kuu.
Hilo jina la 'Governor' si lazima liwe hilo, hata ikiamuliwa aitwe Rais wa Zanzibar au wa tanganyika, ukweli utabaki pale pale ya kwamba ni kiongozi wa serikali yenye madaraka kamili. Jambo linalopaswa kufikiriwa hapa ni namna gani serikali hiyo/hizo zitaendeshwa kwa gharama nafuu. Hili libakie zoezi ambalo kila serikali ijipange kubeba msalaba wake kwa kiasi kikubwa. Serikali itakayoamua kutoa misamaha ya kodi na kuwakumbatia mafisadi itafilisika... Kwa mtazamo wangu hata ufanisi utaongezeka zaidi tukiwa na muundo huu. Serikali kuu ibakie na Wizara chache tu za Muungano mfano Ulinzi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani na Fedha. Wizara zingine zote zirudi kwenye serikali za Tanganyika na Zanzibar, ambazo zitaamua zina uwezo wa kuwa na Wizara ngapi, mawaziri wangapi n.k. Na hizo serikali ziwe na uwezo wa kutunga sheria na kuwa na wasimamizi wa sheria zao wenyewe, kama mfano wa USA kuwa na Sheriff's Department na Federal Police Department. Kama makosa madogo madogo ya jinai yashughulikiwe na Polisi na mahakama ndani ya serikali 'ndogo' bila kuihusisha serikali kuu.