Serikali: Tutaendelea kutengeneza mazingira ya kuwezesha ustawi wa vyombo vya habari

Serikali: Tutaendelea kutengeneza mazingira ya kuwezesha ustawi wa vyombo vya habari

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Serikali itaendelea kutengeneza Mazingira
Akishiriki Mkutano wa 14 wa Chama cha Mawasiliano cha Afrika Mashariki (EACA), Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba amesema Serikali itaendelea kutengeneza Mazingira yanayowezesha vyombo vya habari kustawi

Amesema hiyo inajumuisha kushughulikia masuala muhimu kama vile kuanzisha na kutumia kwa ufanisi Mfuko wa Mafunzo ya Vyombo vya Habari, ambao utakuwa muhimu katika kusaidia maendeleo ya kitaaluma ya waandishi wa habari nchini

Makoba.PNG

Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, akitoa neno katika Mkutano wa 14 wa Chama cha Mawasiliano cha Afrika Mashariki (EACA) uliofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Wadau wa vyombo vya Habari kuhakikisha kuwa maudhui yanayotolewa kwa Umma ni ya ubora wa juu na yanaendana na maslahi ya Kitaifa.

DASTAN KAMANZI, MKURUGENZI TANZANIA MEDIA FOUNDATION
Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Dastan Kamanzi amesema Maendeleo Endelevu ndani ya Sekta ya Vyombo vya Habari na Mawasiliano hayawezi kufikiwa bila ushirikishwaji wa kweli wa Jamii

Amesema Wananchi wanapohusishwa kikamilifu katika utengenezaji, usambazaji na majadiliano ya maudhui ya Vyombo vya Habari, inajenga hisia ya Umiliki na Uwajibikaji

Kamanzi.PNG

Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Dastan Kamanzi.

Ameongeza "Ubunifu unaolenga Wananchi unatoa uwezo wa kutengeneza Vyombo vya Habari ambavyo siyo tu kwaajili ya Watu, bali pia vinavyotokana na Watu wenyewe. Majukwaa ya mtandaoni, mitandao ya kijamii au mikutano ya kuhamasisha mazungumzo na maoni, yakisaidia Vyombo vya Habari kuelewa vyema mahitaji ya hadhira yao"

JAN AJWANG, AFISA PROGRAMU - MEDIA FOCUS ON AFRICA (UGANDA)
Afisa Programu wa Media Focus on Afrika (Uganda), Jan Ajwang amesema Vyombo vingi vya Habari havifanyi utafiti kuwa Wasikilizaji au Wafuatiliaji wao wanataka kusikia au kutazama nini

Amesema, "Wanadhani kwamba kwa sababu 'X' inafanya tunachopaswa kufanya, basi ni sawa lakini data zinasemaje? Wananchi wanasemaje? Hadhira inasema nini? Je, tumewauliza? Na hatufanyi hivyo. Tunapokosa kuwekeza katika utafiti wa hadhira, tunajipiga risasi mguuni wenyewe"

Ajwang.PNG

Afisa Programu wa Media Focus on Afrika (Uganda), Jan Ajwang.
Ameongeza "Unawasha redio, unakuta kila Chombo cha habari kinazungumzia ni nani atakayeshika madaraka katika kipindi kijacho na mambo mengine kama hayo. Je, wananchi wanataka nini? Je, wanawasikiliza? Je, ni kitu wanachoweza kuzungumzia? Je, vipi kama wanavutiwa na masuala ya afya? Au wanataka kujua kuhusu elimu? Je, tumewauliza?

MAXENCE MELO, MKURUGENZI MTENDAJI - JAMIIFORUMS
Akizungumza katika Mkutano wa 14 wa Chama cha Mawasiliano cha Afrika Mashariki (EACA), Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo amesema JamiiForums inatengeneza Majukwaa salama na yenye ulinzi, yanayoweza kusaidia Wananchi kutumia Haki yao ya Uhuru wa Kujieleza lakini pia kufanya Mazungumzo yenye Tija

Amezungumzia Jukwaa la Fichua Uovu ndani ya JamiiForums.com linalomwezesha mtu kutoa taarifa ya za Matukio mbalimbali Nchini hasa Taarifa za Ufisadi

Max 1.PNG

Mkurugenzi wa JamiiForums, Maxence Melo (aliyevaa suti ya bluu), akichangia hoja katika Mkutano wa 14 wa Chama cha Mawasiliano cha Afrika Mashariki (EACA) uliofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ameongeza "Kwa hivyo, tuliamua kutengeneza na kuanzisha Jukwaa hilo ili kuhakikisha kuwa watu wanaweza kufichua mambo kwa siri zaidi"

Pia, Maxence amesema Matumzi ya Teknolojia ya Akili Mnemba yameongeza uzalishwaji wa Taarifa Potofu kwenye Jamii

Amebainisha kuwa JamiiForums iliamua kuanzisha Jukwaa mahsusi la Uhakiki wa taarifa zinazopatikana ndani na nje ya Mtandao linaloitwa JamiiCheck.com ili kutoa suluhisho la ndani katika kupambana na Taarifa Potofu

Jukwaa hili lilianzishwa mwaka 2022 ambapo hadi sasa limehakiki zaidi ya taarifa 600 zinazogusa maeneo mbalimbali ikiwemo Siasa, Afya, Uchumi na Michezo

DAVID OMWOYO, AFISA MTENDAJI MKUU - MEDIA COUNCIL OF KENYA
Afisa Mtendaji Mkuu wa Media Council Kenya, David Omwoyo amesema kuwawezesha Wananchi kutambua habari zinazofaa, kufichua upotoshaji, na kuwaelimisha juu ya athari za kushiriki katika upotoshaji wa habari na kusambaza habari potofu ni muhimu zaidi kuliko kuwafuata watu mitandaoni na kuwashughulikia kwa nguvu

Amesema "Teknolojia inabadilika kwa kasi zaidi kuliko uwezo wa wasimamizi kuweka Sheria hivyo ni muhimu kuwapa Wananchi ujuzi wa habari ili waweze kutambua habari za uongo, upotoshaji na teknolojia za uundaji wa video za kughushi"

Ameongeza "Tunahitaji kupunguza udhibiti na badala yake kuwawezesha Watu kuchambua ukweli na kujielewa wenyewe"

DKT. DARIUS MUKIZA, MHADHIRI - UDSM
Dkt. Darius Mukiza Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema wadau na mashirika ya habari wamekuwa wakijadiliana kila wakati namna ya kuja na mifumo itakayochanganua habari za ukweli na uongo.

“Wakati huo tukihimiza wale wote wanaotumia teknolojia na programu za habari kuhakikisha wanakuwa na sehemu ya kuangalia ukweli katika habari ‘(Fact Check), na sisi waandishi tujikite kwenye ukweli”

‘Hata sheria za nchi zinasema ni kosambaza habari za uongo. Ni kweli changamoto hii hipo hivyo ni jukumu letu kupambana nayo kitaalamu na kisayansi zaidi pamoja na kutoa elimu, ”

DKT. DAVID MRISHO, MHADHIRI - SAUT
Dkt. David Mrisho Mhadhiri Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza, amesema tatizo ni elimu inayohusu habari na matumizi ya habari. Kuna uhusiano wa ukuaji wa teknolojia na usahihi wa habari zinazotolewa. Amesema suala lililopo ni namna gani waandishi wanapika habari hizo lakini pia na uwezo wa kifikra kwa walaji na kama wanafahamu aina ya habari wanazotaka.

Amesema “Vyuo vikuu, taasisi za elimu na wadau wanapaswa kuendelea kutoa elimu sahihi ya namna ya habari inavyopaswa kuliwa, kupelekwa na zenye manufaa kwa watu,”

Pia, ameshauri kufanya aina za habari zenye saikolojia chanya na si habari za vifo, magonjwa pamoja na habari za usuluhishaji. Amesema kwa upande mwingine lazima vyuo vianze kufundisha uelewa wa vyombo vya habari kama somo ili kuamsha uelewa wa kutengeneza maudhui.

“Mfano kunapokuwa na taarifa nyingi kwa pamoja lazima walaji wajue wanachukua habari gani na wanahabari wajue wanawapa habari za aina gani walaji wao suala hili lifundishwe kuanzia awali,” amesema.

EACA ni nini?
Chama cha Mawasiliano cha Afrika Mashariki (EACA) kilianzishwa mwaka 2011 na kundi la wanazuoni wa Uandishi wa Habari, Vyombo vya Habari, na Mawasiliano wanaofanya kazi Afrika Mashariki.

EACA inawakutanisha pamoja wanazuoni, watafiti, na wadau wengine wanaohusika na masomo ya mawasiliano na vyombo vya habari ili kushirikiana katika utafiti kuhusu vyombo vya habari katika kanda hii.

Wanachama wa EACA wanatoka hasa kwenye vyuo vikuu vya Afrika Mashariki, lakini chama hiki kiko wazi kwa ushirikiano na wanazuoni na wataalamu wa uandishi wa habari na vyombo vya habari kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kimekuwa na wanachama kutoka Ujerumani, Afrika Kusini, Afrika Magharibi, Norway, na Marekani miongoni mwa wengine. Tangu kuanzishwa kwake, EACA imefanya mikutano ya kila mwaka nchini Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania, na Uganda.
 
Back
Top Bottom