VIONGOZI wawili wa Pwani Jumamosi walionekana kulitetea Kundi la Mombasa Republican Council (MRC), huku mmoja wao akisema yuko tayari kulifadhili iwapo litamfuata.
Mbunge Maalum wa ODM Sheikh Mohamed Dor, alisema MRC wanaweza kufadhiliwa na nchi yoyote ya kigeni ulimwenguni iwapo mienendo yake inafuata sheria.
Mimi sijaanza. Lakini wakija kwangu, wakiniomba, nitawafadhili, alisema Sheikh Dor alipokuwa akizindua rasmi chama chake katika jumba la mikutano la Chandaria mjini Mombasa.
Sheikh Dor alisema kundi hilo linafaa kufadhiliwa na mtu yeyote, hata mataifa ya Ulaya.
Mkenya yeyote, Mganda yeyote na Mtanzania yeyote ana haki ya kuisaidia MRC kwa sababu haijavunja Katiba. Ikiwa pesa zinatoka Italia, Ufaransa, zatoka Ujerumani, zije. Bora MRC hawajakiuka Katiba, akasema.
Alieleza kuwa MRC wanataka haki za Wapwani. Wanataka masuala ya ardhi, wanataka nafasi za kazi na kadhalika.
Mimi nawambia MRC waendelee kutafuta pesa wafadhili shughuli zao, akasema.
Mbunge huyo wa chama cha Waziri Mkuu Raila Odinga alizindua chama kipya cha Unity Party of Kenya (UPK) na kusema kitawaunganisha Wakenya wote.
Vile vile alikashifu hatua ya polisi ya kuwaandama viongozi wa MRC na kuwatia mbaroni bila ya kuwa na hatia yoyote.
Mahakama
Hakika ni hatua mbaya kuwaandama viongozi wa MRC. Tungoje wakati kiongozi wa MRC amevunja katiba au sheria ndipo tumfuate. Kuna mahakama. Wacha korti iamue, akasema.
Mwenzake wa Mvita Najib Balala alikanusha madai ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID), Ndegwa Muhoro kwamba baadhi ya wafanyibiashara na wanasiasa wa Pwani wanafadhili kundi hilo.
Akizungumza mjini Voi alipofungua afisi ya chama chake cha Republican Congress Party (RCP), Bw Balala, aliitaka Serikali ifanye uchunguzi kwa makini kabla ya kufanya uamuzi ambao unaweza kuwahujumu baadhi ya washukiwa haki zao.
Serikali inafaa kufanya uchunguzi wa kutosha kabla ya kuwatia nguvuni washukiwa kwa madai ya uongo na uvumi, alisema.
Vilevile, aliitaka Serikali wakati inapowatia mbaroni wanachama wa kundi hilo, kufanya hivyo kwa njia ambayo haitazua hofu na taharuki miongoni mwa wenyeji wa Pwani.
Tunataka eneo hili liwe na amani ili tuweze kuimarisha maendeleo, akasisitiza.
Hata hivyo, aliwaonya wafuasi wa MRC dhidi ya kuvuruga mitihani ya kitaifa pamoja na upigaji kura.
Alisema kwa kuwa hakuna nchi inayoitwa Pwani, wakazi wa mkoa huo bado wanategemea matokeo bora kwenye mitihani pamoja na kuchagua viongozi wazuri ili kuboresha maisha yao.
Aliwaonya wakazi wa eneo hilo dhidi ya kushiriki katika ghasia ambazo zinanuia kutatiza mitihani ya kitaifa itakayoanza wiki hii.
Bw Balala alisema kuwa kiwango cha masomo mkoani Pwani kimeenda chini mno na ikiwa kundi hilo litasababisha vurugu, basi kutashuhudiwa matokeo mabaya zaidi.
Si vyema kuvuruga masomo ya watoto wetu wakati ambapo wanafanya mitihani yao ya kitaifa. Wamekuwa wakijitayarisha kwa muda mrefu na wana haki ya kufanya mitihani hiyo, alisema.
Kuhusu upigaji kura, aliwataja wanaopinga shughuli hiyo muhimu kama maadui wa Wapwani.
Kwa miaka 50 tumekuwa tukilia kama Wapwani kuwa tunanyanyaswa. Inafaa sasa tuchague viongozi ambao wataweza kututatulia masaibu yanayotukumba, akasema.
Mbunge asema kufadhili MRC si hatia - HABARI ZA MIKOANI - swahilihub.com