Mkapa uzalendo umemshinda
Ashangaa kwa nini wapemba hawarudi kwao
Wananchi wasema CCM haiuheshimu tena Muungano
Na Mwandishi Wetu
KAULI ya Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Benjamin Mkapa kuwashangaa Wapemba ni kwa nini hawawekezi kwao Kisiwani Pemba, imeshutumiwa vikali na wananchi kwa madai kuwa Bw. Mkapa, kama Mtanzania mwenzao amekosa uzalendo.
Bw. Mkapa anadaiwa kutoa kauli hiyo katika mkutano wake wa kampeni alioufanya Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba, Oktoba 19, mwaka huu.
Wananchi waliozungumza na gazeti hili katika nyakati tofauti kufuatia kauli hiyo ya mgombea urais wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake wamesema ni jambo la kusikitisha kuona Rais mwenyewe ameshindwa kufanya uchambuzi wa kina kuweza kujua tatizo halisi la kisiwa cha Pemba kuwa nyuma kimaendeleo.
Wamesema wapemba ni sehemu ya raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo wana haki kamili ya kuishi sehemu yoyote ile ya Jamhuri.
"Watanzania sote ni kitu kimoja ndio sababu Wahaya na Wamachinga wanafanya biashara zao hapa Dar es Salaam lakini hakuna anayewagusa; kadhalika, Wachaga wanaendesha biashara zao Mwanza, Tabora na kwingineko lakini hakuna anayestaajabia jambo hilo", alieleza mwananchi mmoja mkazi wa Sinza Madukani jijini ambaye hakutaka atajwe gazetini.
Akichambua sababu za kitaalamu zenye kumfanya mtu yeyote atake kuwekeza sehemu fulani , Mwalimu mmoja katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), pia cha jijini, amesema ni kuwepo kwa huduma za kiuchumi ambazo ni pamoja na njia bora za uchukuzi, mawasiliano, huduma za kibenki, maji na umeme.
"Lakini huduma hizi za kiuchumi katika nchi zetu hizi ni jukumu la serikali... barabara zote hizi hapa Dar es Salaam au Arusha au Moshi au mkoa mwingine wowote ule zimejengwa na serikali, vivyo hivyo vituo vya kuzalisha umeme na network zake (mitandao yake) ni kazi ya serikali", alisema mwalimu huyo na kuongeza kuwa mambo hayo ndiyo yenye kupelekea mji kukua na watu kukimbilia kuanzisha biashara mbalimbali.
Wananchi hao wamesema alichotakiwa kusema Bw. Mkapa ni kwa nini serikali ya CCM kwa miaka yote hii tangu muungano mwaka 1964 haikukiendeleza kisiwa hicho cha Pemba kiasi cha kuwavutia watnzania wakimbie kuwekeza kisiwani humo.
"Kama yeye Rais (Mkapa) aliona chama chake hakina sababu ya msingi za kushindwa kuanzisha huduma za kukuza uchumi huko kwa wapemba, angekiri tu kwamba walizembea na akaahidi kuwa jambo hilo litarekebishwa", alisema Bw. Valentine Muro wa Mwenge Dar es Salaam na kuongeza: "...lakini tabu ya rais wetu anataka kuhalalisha hata lisilo halali".
Aidha, wananchi hao wamesema hakuna mfanyabishara anayeweza kufungua biashara mahali ambapo wakazi hawana uwezo wa kununua bidhaa anazoiuza.
"...unapotaka kuanzisha biashara ni lazima ugalie purchasing power (uwezo wa watu kumudu kununua bidhaa), bila hivyo bidhaa zitadorora dukani ... matokeo yake ni mabaya na kama ulikopa mtaji ujue ndio umekwisha kwa sababu benki watakufilisi kwa kushindwa kulipa hela yao."
Kadhalika, wananchi hao waliuozungumza na gazeti hili pia wamehoji ni kwa nini serikali haijafanya juhudi za makusudi za kuinua kipato cha wakazi wa Pemba.
"Kwa kawaida serikali huwa inaiinua miji fulani ili kuwaletea hali bora wakazi wake; kwa mfano serikali iliamua kujenga kiwanda cha nguo cha Mutex katika mji wa Musoma ingawa kiuchumi kiwanda hicho hakikufaa kuwekwa huko kwa vile tayari kulikuwa na kiwanda kingine cha nguo cha Mwatex pale Mwanza... lakini ile ilikuwa ni njia ya kuwapiga jeki wakazi wa Musoma", alidai mwalimu huyo wa CBE.
Mwishoni mwa wiki vyombo vya habari viliripoti habari kuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Bw. Mkapa amesema hali ya umasikini iliyopo kisiwani Pemba haikutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na akaongeza kuwa wapemba walioko nje ya kisiwa hicho warudi kuja kuwekeza.
Likiripoti habari hizo gazeti moja la kila siku toleo la Oktoba 21, mwaka huu lilimnukuu mkapa akisema: "wafanyabiashara wapemba wamejaa toka Kinondoni hadi Kahama Shinyanga, wapinzani wangewashauri hao wote warudi kuweka vitega uchumi hap kisiwani".