Habari zaidi tusomeni hapa chini
Saturday, 02 April 2011 09:27
Fidelis Butahe
CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimeuponda muswada wa marejesho ya Katiba ya Tanzania wa mwaka 2011 kwa kuwa unampa mamlaka makubwa Rais, yakiwamo mamlaka ya kuunda Tume ya Kutunga Katiba. Pia chama hicho kimesema muswada huo ambao utajadiliwa Bungeni Juni mwaka huu, hauna lolote kwa kuwa umenakiliwa ‘neno kwa neno' kutoka Sheria ya Kenya ya Marejeo ya Katiba namba 9 ya mwaka 2008.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alisema maudhui ya muswada huo yanaonyesha wazi serikali imekamia kuunda Tume ya kutunga katiba ambayo itateuliwa na Rais. "Pendekezo hilo linamaanisha kuwa Rais ndiye mdau katika mchakato wa kutunga katiba mpya, vifungu vya 5,6(1) na (2) katika muswada huu, vinampa mamlaka makubwa Rais.
"Viko vifungu vingi vinavyompa mamlaka rais ni kifungu cha 8(1), 13(2), 13(4), 14(2), 16(2), 16(3), 21(1), 21(3), 23(3), 23(4) na 25(2)," ,"alisema Mbatia. Mbatia alisema kazi ya kutungwa kwa katiba lazima liwashirikishe Watanzania kwa kuwa katiba ni kauli ya umma kuhusu utawala wa nchi na jinsi wanavyotaka kuishi.
"Rais ni mtumishi namba moja wa taifa lake, hana nafasi au mamlaka ya kulitungia taifa lake katiba,"alisema Mbatia. Alisema rais anapaswa kuviachia vyombo huru vya umma ili vianze mchakato wa kutunga katiba mpya.
"Kwa kuwa hatuko katika nafasi sifuri, yaani bila taifa wala dola, ni vyema kiutaratibu kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya ibara ya 98 ili iruhusu bunge kutunga sheria ya baraza la kutunga katiba na sheria ya kura za maoni,"alisema Mbatia.
Alisema hatua ya pili ni kupelekwa bungeni muswada wa sheria ya baraza la kutunga katiba na sheria ya kura za maoni na kusisitiza kuwa mambo hayo mawili yanaweza kufanywa wakati mmoja katika kikao kijacho cha bunge. Baraza la kutunga Katiba
Mbatia alifafanua itungwe sheria ya baraza la kutunga katiba na wabunge wa bunge la Jamhuri wawe wajumbe wa baraza hilo huku likiwa na wajumbe wengine.
"Wajumbe wengine wawe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano na la Serikali ya Zanzibar, mwakilishi wa chama cha wafanyakazi kilichosajiliwa, mwakilishi wa asasi ya kitaifa ya kijamii, makamu wakuu wa vyuo vikuu, wawakilishi wa vyama vya siasa.
"Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, majaji wa mahakama za rufani, marais wastaafu, mawaziri wakuu, wawakilishi wa madhehebu ya dini, watu 10 mashuhuri watakaopendekezwa na bunge pamoja na wakuu wa vituo vya sheria," alisema. Alisema baraza hilo linapaswa kuwa na mamlaka ya kuteua Tume ya Kutunga Katiba.
Serikali imenakili sheria ya Kenya
Mbatia alisema muswada wa marejeo ya katiba wa mwaka 2011 umenakiliwa kutoka sheria ya Kenya ya Marejeo ya Katiba namba 9 ya mwaka 2008 na kufafanua kuwa sheria hiyo iliridhiwa na Rais wa Kenya, Desemba 11, 2008 na kuanza kutumika, Desemba 22, 2008.
"Kuiga au kunakili moja wa moja sheria ya nchi nyingine si jambo la ajabu, lakini lazima ujihadhari na mambo ambayo hayaihusu nchi yako na hasa hatari ya kuiga sheria isiyoandamana na mila, desturi, siasa, utamaduni na mahitaji ya wakati huo," alisema Mbatia.
Alisema kama mazingira ya Kenya yalihitaji marejeo ya Katiba, mazingira ya Tanzania hayahitaji suluhisho kama hilo bali yanahitaji katiba mpya na kuhoji kwamba iweje muswada huo unakiliwe neno kwa neno wakati Tanzania kuna wataalamu wengi wa masuala ya katiba na sheria.
"Kenya ni nchi yenye muundo rahisi kikatiba ‘simple state', wakati Tanzania ni nchi yenye muundo mgumu ‘complex state' , Tanzania ni Jamhuri ya Muungano, Kenya wao ni Jamhuri tu, sasa wapi na wapi," alisema Mbatia.
Naye Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa chama hicho, Dk Sengondo Mvungi alifafanua kwamba hawana lengo la kufungua kesi mahakamani kupinga muswada huo bali watawatumia wabunge wa chama hicho kuomba mabadiliko ya muswada huo bungeni.
"Inawezekana kabisa wataalamu wa Rais wakawa wamempotosha kuhusu hili la muswada, Rais hasipelekwe kabisa katika hili, maana hapa kwetu Zanzibar tayari nchi, Tanganyika je, ni mkoa au, wananchi wanatakiwa kulitambua hili," alihoji Mvungi.
Mwananchi newspape