Mkuchika ajitosa siasa za Mbeya
na Christopher Nyenyembe, Mbeya
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kapteni mstaafu George Mkuchika, amejitosa katika siasa za Mbeya.
Habari zilizopatikana jijini hapa zinaeleza kuwa, katika ziara yake hivi karibuni mkoani humu, Mkuchika alifikia hatua ya kuwakemea baadhi ya viongozi katika vikao vya ndani.
Imeelezwa kuwa, katika vikao hivyo, Mkuchika, ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, alisema chama hicho kimechoshwa na misuguano ya kisiasa inayoendelea mkoani hapa.
Aliwataka viongozi wa chama hicho ngazi za wilaya na mkoa kuacha ugeugeu na kutumia majukwaa na mgawanyiko wa makundi kumgombanisha Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya.
Habari za ndani ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka kwenye vikao kadhaa vilivyofanyika mkoani hapa wakati wa ziara ya Mkuchika, zinaeleza kuwa Mkuchika alitumia fursa hiyo kuonya na kukemea makundi yanayowachafua viongozi wa chama hicho, kwa kuwa viongozi hao ni safi na hawana ugomvi wowote.
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu na kile cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa, zinaeleza kuwa Mkuchika alionya dhidi ya tabia zilizofanywa na watendaji wa chama hicho, hasa makatibu ngazi za wilaya na mkoa, ambao walitumia nafasi zao kumpiga vita Profesa Mwandosya.
Habari ambazo zimekuwa zikishika kasi na kushabikiwa na baadhi ya viongozi wa CCM mkoani humu, zinadai kuwa kuna msuguano kati ya Rais Kikwete na Waziri Mwandosya.
Inadaiwa kuwa msuguano huo ndio unamfanya Rais Kikwete asite kuutembelea Mkoa wa Mbeya, na kukwama kwa baadhi ya miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe.
Mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, aliyeomba jina lake lisitajwe kwa sababu zilizo wazi, alisema kuwa, naibu katibu mkuu huyo hakutaka kuficha kitu na kuwapasha ukweli viongozi waliojiingiza kwenye makundi na kuharibu sifa nzuri ya chama hicho mkoani humu.
Migongano hii yote na makundi mliyoyaunda ya kuchafuana, kumchafua rais na Profesa Mwandosya ndio iliyovipa umaarufu vyombo vya habari mkoani Mbeya ambavyo vimekuwa vikiandika migogoro ambayo nyie wenyewe ndio mliokuwa mkiianzisha. Sasa nataka yaacheni yote yaliyopita, kijengeni chama na wapeni ushirikiano wanachama wenzenu walioshinda, chanzo hicho kilimnukuu Waziri Mkuchika.
Mkuchika alisema kuwa, anazo taarifa kuwa makundi hayo yalishughulika sana kuhakikisha kuwa Profesa Mwandosya hashindi ujumbe wa NEC taifa kwa kumfanya aonekane ana ugomvi na Rais Kikwete.
Katika mazingira hayo, inadaiwa kuwa, Mkuchika aliweka bayana uhusiano mzuri uliopo kati ya Profesa Mwandosya na Rais Kikwete, na kwamba wanachama wa chama hicho wanaotumia fursa zao kuwachafua na kuwagonganisha, wajue wazi wanafanya hivyo kwa viongozi wa chama na serikali ambao ni marafiki na hawana ugomvi wowote.
Alinukuliwa akisema: Rais Jakaya Kikwete hana ugomvi wowote na Profesa Mark Mwandosya, na kuonyesha kuwa hawana ugomvi huo, ameweza kumteua mara mbili mfululizo kuingia kwenye Baraza la Mawaziri na kwamba ni marafiki wakubwa ndani ya CCM. Aliongeza kuwa iwapo kungekuwa na uhasama wowote, isingekuwa rahisi kwa waziri huyo kuteuliwa mara mbili mfululizo kuwa waziri.
Mkuchika alimwelezea Profesa Mwandosya kuwa ni mwanachama muhimu na mashuhuri anayetegemewa ndani ya CCM na serikali, na ndiyo maana anaheshimika.
Katika kuhakikisha kuwa uongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa unaacha migongano, mjumbe mwingine alisema kuwa kazi kubwa sasa ipo mikononi mwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Nawab Mullar, ambaye kwa kushindwa kusimamia katiba na kanuni, amekuwa akiitisha vikao vyenye nia ya kuwadhalilisha viongozi wengine, wakiwemo wabunge, kinyume cha utaratibu wa vikao vya chama.
Aidha, Mkuchika alipinga tuhuma kuwa Rais Kikwete hatembelei Mbeya kutokana na kutoelewana na Profesa Mwandosya na kuwahakikishia wajumbe kuwa, ziara za kiongozi huyo wa juu wa serikali zitafanyika mkoani humu kutokana na ratiba aliyopangiwa, na kwamba hawezi kuwaogopa wananchi wake waliompa dhamana ya kuiongoza nchi.