TAMKO LA VYAMA VYA SIASA; CHADEMA, CUF, NCCR MAGEUZI NA TLP KUHUSIANA NA HATIMA YA WANAFUNZI WA KITANZANIA WANAOSOMA UKRAINE. 27/5/2007
Ndungu Wananchi,
Ndugu Wanahabari,
Mabibi na Mabwana,
Tumewaita hapa kuwazungumzia hoja nzito kuhusu wanafunzi wa kitanzania wanaosoma nchini Ukraine. Wanafunzi hawa wapatao 29 waliondoka nchini kuanza masomo nchini Ukraine katika mwaka wa masomo 2006/2007. Wanafunzi hawa walidahiliwa katika vyuo vya Ukraine katika mwaka wa masomo 2005/2006 lakini kutokana na kuchelewa kupatiwa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa vyuo Vikuu, waliahirisha kuanza masomo ili waanze mwaka 2006/2007 kwa maelewano na vyuo vilivyowadahili na serikali ya Tanzania.
Walipoondoka nchini mwaka 2006 kuanza masomo yao nchini Ukraine, wanafunzi hao walipata baraka zote za serikali kwa ahadi kwamba watatumiwa fedha zao za mikopo wakishaanza masomo nchini Ukraine. Taarifa tulizopewa na wazazi wa wanafunzi hao, serikali haikutimiza ahadi yake ya kuwapelekea mikopo yao na haitaki kueleza kwa nini haijafanya hivyo.
HALI HALISI YA WANAFUNZI UKRAINE
a. Wanaishi katika mazingira magumu ambayo yanatishia siyo tu usalama wao bali pia afya zao. Tayari wameshaitiwa vyombo vya usalama vya serikali ya Ukraine kuwachunguza.
b. Vyuo vyao vikuu viliwapa hadi tarehe 20 ya mwezi huu wa tano kama tarehe ya kufutwa chuoni. Hatua ya kufutiwa udahili wao itamaanisha kuwa wanafunzi hao hawana uhalali tena wa kuishi nchini Ukraine na hivyo watahesabiwa kuwa ni wahalifu ambao wanaweza kukamatwa na kufungwa kama watakuwa hawajalipia ada pamoja na madeni ya gharama za kujikimu walizokuwa wametumia kwa muda wote wakiwa wapo chini Ukraine.
c. Jitihada za wanafunzi hawa kuwasiliana na viongozi wa wizara zimekwama. Kila mara wanaishia kuzungushwa zungushwa na viongozi wa wizara hiyo akiwemo Waziri wa Wizara hiyo Prof. Msolla ambaye amefikia kukata simu kila wanafunzi hao wanapompigia simu. Mwenyekiti wa Chama cha TLP Mhe Augustino Mrema alimuandikia Raisi Jakaya Kikwete kuhusu tatizo la wanafunzi hawa tangu tarehe 23/1/2007. Hii inamanisha kuwa Wizara hiyo hiyo imeshindwa kushughulikia matatizo ya wanafunzi hao. Habari tulizozipata zinaonesha kuwa wanafunzi wengine walioko nje ya nchi wanaokabiliwa na matatizo yanayolingana au kukaribiana na yale ya Ukraine ni wale wanaosoma nchini Cuba, na Urusi. Inamithilika sasa kuwa Wizara na Bodi ya Mikopo wanayo sera za kibaguzi dhidi ya nchi zilizokuwa zikifuata siasa za kijamaa. Hatujapata habari kama wanafunzi wanaosoma katika nchi za kibepari na hata wanaosoma nchi jirani kama vile Uganda na Kenya wanafanyiwa kama wanafunzi walio nchini Ukraine.
d. Jitihada za wazazi wa vijana hao kuwasiliana na viongozi wa Bodi ya Mikopo na wizara hazijazaa matunda kwa kuwa maofisa waliowahudumia hawakutoa ushirikiano wa kutosha. Jambo ambalo limejionesha wazi ni kuwa hakuna ofisa aliye tayari kusema wazi msimamo wa serikali na hivyo wazazi wamekuwa wakipigwa kama mpira kutoka ofisi moja hadi nyingine bila mafanikio yoyote.
e. Aidha tumepata pia habari kwamba Ubalozi wa Uingereza nchini Ukraine uliipa serikali ya Tanzania ufadhili wa kuwasaidia na kuwalipia vijana hao na kuwapa misaada mingine ya kibinadamu endapo tu serikali ya Tanzania itaandika barua ya kurudisha fedha hizo kwa serikali ya Uingereza. Serikali ya Tanzania haikuwapa jibu hadi leo hii.
f. Habari tulizonazo zinasema pia kwamba ahadi ya serikali ya kutuma ujumbe kwenda nchi hizo kuangalia matatizo hayo mwanzoni mwa mwezi huu imefutwa na hakuna ahadi nyingine au mpango unaoeleweka wa kufanya ziara hizo.
g. Matokeo ya haya ni kuwa wanafunzi hao 29 wamesimamishwa masomo, hawana chakula wala fedha za kulipia pango katika nyakati hizi za majira ya baridi. Imewalazimu wanafunzi hao kujisalimisha ubalozi wa Uingereza kule mjini Kiev, kwa vile Tanzania haina Ubalozi nchini Ukraine kwa takribani zaidi ya siku kumi na nne sasa wakiomba yala saidia maskini ili wasaidiwe.
h. Habari tulizonazo sasa ni kuwa wanafunzi hao wamepewa hadi Jumanne tarehe 29 mwezi huu kulipa fedha wanazodaiwa vyuoni au watanyanganywa hati zao za kusafiria na kasha kufukuzwa kwenye mabweni wanamoishi. Wanafunzi hawa hawaruhusiwi kurejea Tanzania kwa vile wanadaiwa na vyuo vyao. Hali ni mbaya mno kwa wanafunzi hawa kiasi kwamba ipo haja ya kufikiriia hatua za dharura za kuokoa maisha ya raia wetu.
SERIKALI ITENDE UUNGWANA
Sisi tuko hapa kwa wadhifa wetu kama vyama vya siasa na pia kama wazazi. Tunaona wazi kuwa Dhamana ya Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na tekinolojia imekabidhiwa pasipo. Mheshimiwa Profesa Msolla hafai kushikilia wadhifa wake wa uwaziri, hamsaidii Rais Jakaya Kikwete ila anambomoa. Ni hatari kuwa na waziri wa elimu ambaye kazi yake ni kugombana na wanafunzi badala ya kwaongoza. Sisi tumeona nyaraka zinazoonesha kuwa Wizara ilitoa baraka zake kwa wanafunzi hawa kuondoka nchini kwa ahadi kuwa itawakopesha fedha za kugfharamia masomo yao huko waendako.
Pia tunatambua kuwa serikali ilitoa hahadi kuwa inazo fedha za kutosha kutoa mikopo kwa kila mwanafyunzi aliyedahiliwa. Hatuoni kwa nini serikali inakwepa wajibu wake wa kutenda uungwana kwa kutekeleza ahadi zake. Ikiwa serikali imeshindwa kuongoza, basi ni vyema ama ijiuzulu yote au ikiwa ni tatizo la Profesa Msolla pekee, basi mheshimiwa huyu aombwe kupisha nafasi hiyo ipewe anayeimudu. Tunatamka wazi kuwa Profesa Msolla ajiuzulu haraka kwani hajaiangamiza serikali nzima ya Rais Jakaya Kikwete.
Wazazi na wanafunzi husika wametuhakikishia kuwa wamejaribu kuwasiliana na ngazi zote za serikali na hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa. Wanafunzi wamediriki kuwasiliana na Rais Jakaya Kikwete ambaye amewarejesha kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Elimu na Bodi ya Mikopo. Waziri Mkuu amepatikana kwenye mtandao wa simu lakini hakuwa na nafasi ya kuzungumza na wanafunzi hao kwa kuwa alikuwa mezani anakula. Waziri wa Elimu ya juu Profesa Msolla hapatikani na hukata simu ili asigasiwe. Kweli matatizo kama haya yanaudhi, lakini haya ni matokeo ya utekelezaji mbaya wa sheria na sera za nchi kuhusu mikopo ya wanafunzi. Tunawashauri waheshimiwa wahudika wasihamaki na kukata simu bali wakubali kuwa huo ndio wajibu wanaotakiwa kuutimiza katika nyadhifa walizozipokea kutoka kwa wananchi.
Hivyo basi tunaitaka serikali ifanye mambo yafuatayo.
1. Ilileleze taifa kama inawatambua wanafunzi 29 walioko nchini Ukraine ama laa.
2.Ilieleze taifa kwa nini wanafunzi wale wametelekezwa ama ni sababu zipi zimepelekea hadi vijana wale kuachwa kwenye hali mbaya kiasi hicho hadi kulifanya taifa lidhalilike.
3.Tunamtaka waziri wa elimu ya juu Prof,Msolla ajiuzulu mara moja kwa uzembe wa kutolishughulikia jambo hili kama inavyopasa.
4. Serikali iwakopeshe fedha wanafunzi hao na zipelekwe haraka iwezekanavyo ili waweze kuendelea na masomo yao.
5. maofisa wa serikali wizarani na kwenye bodi ya mikopo ya wanafunzi waliozembea wajibu wao wawajibishwe.
KWA WANANCHI WOTE KWA UJUMLA
Kwa kuwa hali ya wanafunzi kule Ukraine ni mbaya, tunaliona jambo hili kuwa ni janga linalohitaji misaada ya kibinadamu. Wakati jambo hili linatafutiwa ufumbuzi lazima tuchukue hatua za kuokoa maisha ya watanzania wenzetu. Tunayaomba mashirika yanayohusika na haki za binadamu waliangalie swala hili kwani vijana wale wanaishi kwenye mazingira magumu sana na hili linahatarisha hata mustakabali wa maisha yao kwani huenda wengine wakapatwa na matatizo ya kiakili na kuamua kufanya jambo lolote ambalo nlitayahatarisha maisha yao.
Hivyo basi sisi binfsi kama wazazi: Mhe Ibrahim Haruna Lipumba , Mhe Augustino Mrema , Mhe James Mbatia, Freeman Mbowe tunaanzisha mchango wa dharura kuokoa maisha ya wenzetu nchini Ukraine kwa kutoa shilingi millioni moja kwa ajili hiyo. Tunaomba wenye nia njema na wanaoguswa na mahangaiko ya wenzetu nchini Ukraine wachangie pamoja nasi.Tumeliomba Shirika la Elimu ya Sheria Tanzania ( TANLET) wafungue akaunti benki kwa ajili hiyo ya kuweka michango hii na tutawatangazia namba ya akaunti hiyo mara itakapofunguliwa.
Mungu ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Aksanteni kwa kutusikiliza..