Shairi: Binti kurudi shule

Shairi: Binti kurudi shule

ramadhani kimweri

Senior Member
Joined
Apr 22, 2016
Posts
181
Reaction score
179
Binti kurudi shule

Bado nalitafakari, hatima ya jambo hili
Nawaza na kufikiri, matamko mbalimbali
Jambo hili ni hatari, siasa tuweke mbali
Binti kujifungua, arudi shuleni tena.

Mimi linanitatiza, acheni niseme wazi
Sisemi ninakataza, nasema kama mzazi
Ninani atamtunza, na kumpa matumizi
Na sabuni za kufua, chakula chake na mwana.

Mama akienda shule, mtoto abaki ndani
Baba yupo jela kule, ni miaka thelethini
Yapo mahitaji tele, atayatimiza nani
Hivi kulea mwajua, au mwaleta utani.

Jambo hili siafiki, ukweli ninausema
Weka mbali unafiki, hebu fikirini vyema
Twampa mtoto dhiki, kukosa nyonyo la mama
Kichanga kikiugua, mamaye yupo shuleni

Binti akishazaa, huyo sio binti tena
Watoto watasambaa, na kujaa kila kona
Huku wakilia njaa, maa enda shule tena
Mlango mlofungua, faida yake ni duni.

Na kusoma ni lazima, haki yake mwanadamu.
Na ujinga ni kilema, dawa yake ni elimu
Akijifungua mama, akiwa hajahitimu
Atasoma kuchagua, sio kurudi shuleni..


Ibn kimweri
Ramadhani Juma Kimweri
0746328046.

Mashairi mengine soma Shairi: Hakuna siri tena
 
Back
Top Bottom