SoC01 Shairi: Kushajihisha watu kuinua uchumi wa nchi yetu ili tuzidi kuendelea na kushika nafasi za juu kiuchumi

SoC01 Shairi: Kushajihisha watu kuinua uchumi wa nchi yetu ili tuzidi kuendelea na kushika nafasi za juu kiuchumi

Stories of Change - 2021 Competition

AbduAbdulla09

New Member
Joined
Sep 6, 2021
Posts
4
Reaction score
9
SHAIRI KUHUSU UCHUMI WETU

1.La mgambo limelia, leo nataka wambia
Mjini nimeingia, nataka wasimulia
Kampeni kuwatia, ya kiuchumi sikia
Rabi nijaalie njia, wapate kunisikia

2.Tumeipiga hatua, sasa uchumi wa kati
Kila hatua ni dua, na tueke mikakati
Hatua kuzichukua, tena zilo madhubuti
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

3.Mikakati mingi mno, kwetu tulijiekea
Sasa twakula vinono, vibaya twaviachia
Mabaya yao maneno, sisi tumepuuzia
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

4.Yalipozuka maradhi, katika hii dunia
Nchi zikaeka wazi, vikwazo kujiekea
Ila wetu kiongozi, ndipo alipopania
Mjaalie malazi, huko alikoendea (AAMIN)

5.Hakuvieka vikwazo, watu ndani kufungia
Aliondosha mzozo, na woga kuuondoa
Uchumi wetu kwa mzo, juu tuka uinua
Uchumi ni mkombozi, hapa kwetu Tanzani

6.Shime wananchi shime, uchumi na usishuke
Tuupandishe kiume, juu juu na ubake
Mashambani tukalime, viwanda tujumuike
Uchumi ni mkombozi, hapa kwetu Tanzani

7.Tanzania ya viwanda, kwetu inawezekana
Sasa tuvae magwanda, tujenge na karakana
Iwe sadiki ukipenda, kwa marefu na mapana
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

8.Tuache ya kizamani, ya sasa tuendeleze
Ili tupate amani, uchumi tusi ubeze
Yapaswa tuwe makini, acha rege tujikaze
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

9.Ulimwengu umekua, kazi umerahisisha
Ujuzi tunachukua, uchumi kuuboresha
Bilaya kwenda nunua, ndio twajimilikisha
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

10.Sayansi na teknoloji, ndio mhimili wetu
Tuna vumbua vipaji, katika uchumi wetu
Katika hi letu jiji, Tanzania nchi yetu
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini


11.Hatutumii majembe, katika yetu maheka
Matrekta ya kazimbe, yaendelea kubweka
Yafanya kazi kwa mbinde, ardhie kuchimbika
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

12.Kilimo kumwagilia, katika mashamba yetu
Na mabwawa kujengea, kuhifadhi maji yetu
Hiyo ni teknolojia, kuilisha miti yetu
Uchumi ni mkombozi, wa hapakwetu nchini

13.Mabibi na bwana shamba, kazi nzuri wafanya
Huwa waenda sambamba, si hasi bali ni chanya
Hawajawahi kuyumba, uchumi juu huufanya
Uchumi ni ukombozi, hapa kwetu Tanzani

14.Matunda yajaa tele, bara pia visiwani
Hata ukenda kibele, utajaza pakachani
Kuna kule mtambile, matunda kama majani
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

15.Twamshukuru Raisi, huyu wetu mteule
Mola ampe wepesi, apitie mule mule
Aizidishe na kasi, nchi yetu yende mbele
Nchi yetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

16.Kazi kubwa anafanya, ku-unyanyua uchumi
Matokeo yalo chanya, ni ukweli si uvumi
Bila hata kudanganywa, twaona ma tiviini
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

17.Miundo mbinu imara, bado anaendeleza
Usafiri barabara, kwa sasa vina pendeza
Uchumi mekua bora, mawasiliano kwanza
Uchumi ni mkombozi, hapa kwetu Tanzani

18.Kajenga uhusiano, na chi zetu jirani
Anajitahidi mno, kutengeneza chanali
Ondosha mfarakano, uchumi wetu ujali
Uchumi ni mkombozi, hapa kwetu Tanzani

19.Hukaa na kufikiri, kwa maslahi ya nchi
Kila siku kusafiri, sio kujikalia chi
Lakini yote ni kheri, kwa wake wanawanchi
Uchumi mkombozi, wa hapa kwetu nchini

20.Wakulima wa mahindi, wapanie kweli kweli
Wameibuka washindi, raisi kawa fadhili
Wazalishe kwa kipindi, uchumi kuubadili
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

21.Uchumi tunaposema, neno hili kila mara
Maana yake huduma, ziletazo itijara
Katika nchi nzima, toka pwani hadi bara
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

22.Viwanda na ukulima, na tatu ni biashara
Haya mambo ni daima, ni cha uchumi kinara
Kinara cha kuusema, uchumi wetu imara
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

23.Viwanda vinavyofuma, zetu nguo za kung’ara
Au vya kuchinja nyama, au vito vya sonara
Au vya kuchimba chuma, na viundavyo sigara
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

24.Biashara ninasema, tena ni kwa nyingi sera
Uchumi humu ni kama, tuuzapo matambara
Vyombo chai na mtama, hata picha za kamera
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

25.Na kilimo ndio mama, mwongozo wa msafara
Msafara wa kuchuma, huyu kashika bakora
Dunia na kila umma, kilimo chashikakura
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

26.Wananchi ni lazima, tukitaka tuwe bora
Ni lazima tuwe bora, tukitaka kusimama
Wa visiwa na mlima, kwa kazi si kuzurura
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

27.Waume na kina mama, walo oa na kapera
Kila aliye mzima, tuwe kwenye mduara
Si mduara wa ngoma, wenye kuleta hasara
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

28.Mduara wa heshima, uchumi kuupa dira
Ardhini kuinama, alfajiri majira
Watu wasirudi nyuma, mpaka saa ashara
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

29.Tutaacha kulalama, tukifanya biashara
Biashara ni lazima, bila kufanya papara
Na tuiweke hazina, uvuvi tuupe dhara
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

30.Biashara zilo njema, sio kwenye barabara
Kuweka nyama kuchoma, au kuuza mapera
Uchumi hatutafuma, kwa biashara uchwara
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

31.Biashara huko Bama, tupeleke nyingi sana
Na viwanda view wima, vizalishe kwa mapana
Na kilimo hima hima, tupanie kila dhama
Uchumi ni mkombozi, hapa kwetu Tanzani

32.Kila mtu na atende, tuiendeleze nchi
Twendeni kwenye mabonde, tukakate parachichi
Miwa korosho tupande, minazi njugu kabichi
Uchumi ni mkombozi, hapa kwetu Tanzani

33.Kama hatutakazana, weupe hawatuachi
Watazidi kutubana, mithili kinu na mchi
Ngao kubwa kuungana, tuijenge yetu nchi
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

34.Vijana msizubae, kukaa katika kochi
Kumngoja alimae, aliyeko Makunduchi
Na wewe wende nyumae, ukale ucheze nachi
Uchumi ni mkombozi, Hapa kwetu Tanzani

35.Huduma tuhudumishe, na uzembe tuuache
Kila mtu aoneshe, kundini asijiache
Nchi yetu ing’arishe, majani rangi kibichi
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

36.Tujikomeshe kuomba, misaada toka nchi
Feza zetu wanasomba, twabaki twakaa uchi
Tuzilime nyingi pamba, furushi tujaze pochi
Hapa kwetu Tanzani, uchumi ni mkombozi

37.Jumla tushikamane, nakwambia sikufichi
Ni lazima tuungane, kama meno pachipachi
Na tulime na vingine, ndizi na maparachichi
Uchumi ni mkombozi, wa hapa kwetu nchini

38.Mwisho ninaa malizia, la mgambo kulitua
Nchi yangu kuiombea, dua ilo maridhia
Mikono kuinyanyua, amina kuitikia
Rabi takabali dua, kwako tunaelekea

39.Kwa dua nabembeleza, Mola mazuri tutende
Tuishi kwa kupendeza, kwa mwenendo na tuendee
Udumu kutuongoza, minong’ono tuishinde
Tuwe ni nchi ya kwanza, kwa uchumi na tushinde
 
Upvote 2
Back
Top Bottom