Emc2
JF-Expert Member
- Sep 26, 2011
- 16,808
- 16,887
Ukubwa huwa ni dawa, ni msemo wa wahenga
Sasa namtuma njiwa, Awe kwenu ni mkunga
Leo ninatoa dawa, Ili muache kuringa
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Hii ngoma ya kukesha, Asubuhi unatamba
Jirani unachekesha, Hujui haijabamba?
Wewe acha kujichosha, Subiri kuanza dimba
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Kila kitu umetoa, Wewe ni mdogo sana
Data unaongezea, Watu wako kuwachuna
Jirani utapotea, Sasa ni mapema sana
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Akiba wewe hauna, Dogo unakopa sana
Nguo nzuri wazishona, Nyumbani mlo hakuna
Kila siku mwagombana, Udugu kwenu hakuna
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Wenzako wajiandaa, mwenzangu umeshachoka
Macho sasa wakodoa, Umeanza kuropoka
Kila kitu wandandia, Kitu huna wakitaka
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Zigo hilo la kichina, Nani utambebesha?
Limeshaanza kuchina, Kipya sisi tunashusha
Wenzako wameshaona, Zigo wamekubebesha
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Tulikuwa tumelala, twasubiri huo muda
Sisi huku tunakula, watu wetu kuwalinda
Ni shida kwenu chakula, Kila mtu amekonda
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Jirani tumeamka, Unapiga makelele
Wewe sasa umechoka, cha kwetu hicho kilele
Hakuna cha kufichika, udugu wetu ni mbele
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Unajivunia nini, hebu sasa nieleze
Unakaa mabatini!, wataka nikupongeze?
Maisha ni ya zizini!, samadi kwako zeze
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Pesa za kwenye kitabu, na nyingi kujitungia
Kipi kinachokusibu, dunia imegundua
Huyajui mahesabu, takwimu kujitugia
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Kalamu chini naweka, Ujumbe umeupata
Watu wakubwa twacheka, vile unapwatapwata
Njiwa sasa amefika, salamu umeipata
Kweli ngoma ya watoto, Siku zote haikeshi
Shairi limetungwa na Bw. Annael