Shairi:Nimerudi tena Linah

JOTO LA MOTO

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2018
Posts
758
Reaction score
555


MTUNZI:MSANII JOTO LA MOTO.

Linah tena nimerudi,ule ujumbe nakazia,
Vipi nimebisha hodi, bado waninyamazia,
Kumbuka niliahidi, sitolishusha pazia,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia

Ngoja nijitambulishe,kidogo unifahamu,
Walau nikujulishe, vile niko hendisamu,
Sio mtu wa kasheshe,kutwa ninatabasamu,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.

Linah kimya umekaa,sauti sijasikia,
Macho pima nimekaa,nakungoja malikia,
Mbona unakuwa kaa,ni nini wanitakia,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia

Linah ninakuja Dar, unipe dawa nipone,
Nipo ninajiandaa,naja huko nikuone,
Usidhani ni hadaa,sitanii hata tone,
Linah nakukumbushia,ujumbe nilokutumia

Si utani wa Masudi, kipanya nakichukia,
Usifanye makusudi, majanga wanitakia,
Ndio maana nimerudi, ongea nitasikia,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.

Kuitwa ndege mnana, wamekupatia dia,
Leo ndio nakuchana, sautiyo bomba dia,
iwe usiku mchana, nacheza kwa kurudia,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia

Moyo umenipa ufa, hutaki kuja kuziba,
Ni nani huyo mshefa, nafasi ananiziba,
Basi hata nikikufa, usije kwenye msiba,
Linah nakukumbushia,ujumbe nilokutumia.

Ukizidi nichunia,jiandae kwa lolote,
Jinsi nimekupania, nitakusaka kokote,
Jukwaa nitavamia, nikubusu kotekote,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.

Basi sema nisikie,maoni yako nipate,
Imani inibakie,nitakuja nikupate,
Usiache nichukie,mwenzio nije nidate,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.

Lina punguza mapozi, ujumbe nasisitiza,
Hebu kuwa siriazi,roho nisije poteza,
Sitaki pata uchizi,acha shere kunicheza,
Linah nakukumbushia,ujumbe nilokutumia.

Mimi hapa natulia, nadhani umenisoma,
Najizuia kulia,ujumbe ninavyotuma,
Narudi kuugulia,mpaka jibu ukituma,
Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…