Shairi: Poleni Watanzania

Bin Eifan

New Member
Joined
Sep 22, 2018
Posts
3
Reaction score
5
Shairi langu natunga, kuwapa pole raia,
Na nyinyi tunajiunga, sote huku tunalia,
Kukumbwa na hili janga, pole kwa zao familia,
Poleni wa Tanzania, ajali haina kinga.

Ajali haina kinga, poleni wa Tanzania,
Wamejitoa mhanga, masikini abiria,
Haraka bila kuchunga, Kivuko kukivamia,
Poleni wa Tanzania, ajali haina kinga.

Raisi hivi majuzi, Mwanza alihutubia,
Alionya viongozi, makosa kutorudia,
Kawakanya wakaguzi, wasidharau sheria,
Poleni wa Tanzania, ajali haina kinga.

Utafanywa uchunguzi, tujuwe mwenye hatia,
Imekua ni zoezi, kuwapandisha mamia,
Kuhimili hakiwezi, chombo kikadidimia,
Poleni wa Tanzania, ajali haina kinga.

Lazima wawe wakali, wahusika baharia,
Roho za watu ni mali, si mchezo angalia,
Ipo mbio serikali, mazuri kuwafanyia,
Poleni wa Tanzania, ajali haina kinga.

Tunamuomba Mkwasi, peponi kuwajalia,
Awaepushe mikosi, mabaya kuyazuia,
Hapa shairi ni basi, ninaifunga pazia,
Poleni wa Tanzania, ajali haina kinga.

Abdallah Bin Eifan,
(Kinyamkera)
Jeddah, Saudi Arabia.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…