Shairi: Sirudii matapishi

Shairi: Sirudii matapishi

ramadhani kimweri

Senior Member
Joined
Apr 22, 2016
Posts
181
Reaction score
179
Siwezi kula makombo, ijapo niyakunona
Umesha jipaka shombo, siwezi kuramba tena
Yaliopita kitambo, yaliniumiza sana
Kurudi kwako siwezi, kurudi kudanganyana..

Kula nilichotapika, kwangu hilo ni haramu
Napaswa kukiepuka, hatakama ni kitamu
Yakwako nimetosheka, hayanipi hata hamu
Penzi lako la kishenzi, penzi la kudanganyana..

Bora niishi mpweke, sirudishi penzi lako
Lanifanya niteseke, siwezi kurudi kwako
Kheri nife wanizike, kuwa na wewe ni mwiko
Nataka sana mapenzi, lakini kwako hapana..

Donda ulonitonesha, nadhani halitopona
Ulonitenda yatosha, wala hamu sina tena
Yakwetu yameshakwisha, yaleo sio ya jana
Kuwa na wewe siwezi, yatosha niloyaona..

Sasa hivi sikupendi, nilikupenda zamani
Nakutoa kwenye kundi, la watu wenye thamani
Nawaza kile kipindi, kwangu ulikosa nini
Ukanitoa machozi, nikawa sina maana..

Kwaheri tena kwaheri, mie ninaenda zangu
Na kurejea sikiri, hiyo si tabia yangu
Kwako sirudi fedhuli, natunza heshima yangu
Kurudi kwako siwezi, kurudi kudanganyana..

[emoji2398]Ibn kimweri.
Ramadhanikimweri07@gmail.com

Mashairi mengine soma Shairi: Hakuna siri tena
 
Back
Top Bottom