JOTO LA MOTO
JF-Expert Member
- Apr 11, 2018
- 758
- 555
TANGULIA AGINESI
KUTOKA KWA:MSANII JOTO LA MOTO.
Mshumaa umezima,mapema kutarajia.
Sasa huwezi kuhema,umeifuata njia.
Hatunayo ya kusema,msiba umetujia.
Tangulia Aginesi,nasi tu njiani twaja.
Ni tarehe ishirini, majira ya alasiri.
haki hatukuamini,kusikiliza habari.
Kuwa eti masikini,Agy kaenda tayari.
Tangulia Aginesi, nasi tu njiani twaja.
Sanaa uliifanya, maisha kujipatia.
Wapo wale walisonya,na maneno kutupia.
Iwe hasi iwe chanya, Mola ndiye mlipia.
Tangulia Aginesi, nasi tu njiani twaja.
Tangulia Masogange, na sisi tupo njiani.
Tuache Mola apange, hatujui siku gani.
Tusichonge kama kenge,kujidai watu gani.
Tangulia Aginesi, nasi tu njiani twaja.
Sote tutafika huko,siku itapowadia.
Wazazi na ndugu zako, wakukosa wao dia.
Kimwili sasa hauko,hakuna wa kufidia.
Tangulia Aginesi, nasi tu njiani twaja.
Waliondoka mitume, kwani sisi nani haswa.
Ipo siku tusiheme, roho zetu zitachotwa.
Hata yote tuyaseme,hakuna atayeachwa.
Tangulia Aginesi, nasi tu njiani twaja.
Kuna wale watasema, yao wanayofikiri.
Utadhani wao wema,kumbe ni watu kafiri.
Vile bado wana hema,siku yao wasubiri.
Tangulia Aginesi, nasi tu njiani twaja.
Ingawa unatuliza,tuna imani ulipo.
Twakubali kupoteza,kama vumbi na upepo.
Uachayo tutatunza,mpaka tukija ulipo.
Tangulia Aginesi, nasi tu njiani twaja.