SHAIRI: Thamani ya mtumishi hung'ara akishalala

SHAIRI: Thamani ya mtumishi hung'ara akishalala

mgt software

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
13,778
Reaction score
7,145
THAMANI YA MTU MWEMA, HUNG’ARA AKISHALALA!

Tenda wema nenda zako, msemo tangia enzi,
Timiza wajibu wako, kwa watu na kwa Mwenyezi,
Iache alama yako, kwa kizazi na vizazi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Wema msalaba wako, ubebe bila simanzi,
Wema ni hazina yako, isiyoibwa na wezi,
Wema ni kisima chako, cha Baraka za Mwenyezi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Katika Maisha yako, utakutana vihunzi,
Kisa ni kwa mema yako, utendayo kwa uwazi,
Bila kaza moyo wako, utajitia kitanzi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Heshimu dhamira yako, kwa kufanya maamuzi,
Dhihirisha utu wako, kafanye yenye kuenzi,
Mwisho wa Maisha yako, uwake kama kurunzi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Mpende Jirani yako, ni amri ya Mwenyezi,
Upendo salama yako, na msingi wa mapenzi,
Kuna siku jina lako, litakuwa kumbukizi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Uweke msingi wako, na kuikita mizizi,
Tumikia watu wako, kwa gharama na machozi,
Wataona pengo lako, ukishapoteza pumzi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Kati yao ndugu zako, wapo waso na ujuzi,
Waletao hoja kwako, uwe kwao ni mwamuzi,
Tumia talanta yako, waunganishe kwa uzi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Itoe sadaka yako, kwa ajili ya Mwenyezi,
Mungu Alo ndani mwako, hakika Atakujazi,
Jitoe kwa moyo wako, kwa jamii na kizazi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Muamini Mungu Wako, Aliyekujaza pumzi,
Bwana Ndiye Chanzo Chako, pia Ndiye Mwenye Enzi,
Yale yote mema yako, Ataonesha vizazi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Palipo malalamiko, wewe fanya uchunguzi,
Ujue nini kuliko, na peleka ufumbuzi,
Katende yenye mashiko, ukumbukwe na wakazi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Usione kama mwiko, kuombwa kuwa mwamuzi,
Simamia Maandiko, Akutakavyo Mwenyezi,
Hata wawe ndugu zako, haki tenda kwa uwazi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Yajapo matetemeko, ya kuharibu makazi,
Huja na mifadhahiko, kwa watoto na wazazi,
Tumia uwezo wako, wakatulie wakazi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Kautenge muda wako, ukimuomba Mwenyezi,
Mungu Akupe Upako, ukawajue wakwazi,
Fadhili wabaya wako, wakapigwe bumbuwazi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!

Mimi ni mjumbe kwako, kupitia beti hizi,
Nawasilisha Andiko, lisome na limaizi,
Tenda wema nenda zako, utalipwa na Mwenyezi,
Thamani ya mtu mwema, hung’ara akishalala!
 
Back
Top Bottom