Sheria kandamizi zaumiza wanahabari Tanzania

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
KWA UFUPI
Ripoti ya CPJ inasema kutokana na mashambulizi dhidi ya wanahabari baadhi yao wameamua kufyata mkia.



Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania mara nyingi huwa inapongezwa na kumwagiwa sifa kem kem na wafadhili kwa kile ambacho wanakifikiria ni ufanisi wake katika kuendesha utawala kwa misingi ya uwazi na demokrasia.

Wafanyapo hivyo huwa wanaweka kando makosa au malalamiko yanayotokana na wananchi. Pia huwa hawazingatii hali halisi katika jamii

Almradi tu wakopeshaji, wawekezaji na wafadhili huwa wanapenda sana kutoa sifa kwa watawala wetu. Ni mara chache sana huwakosoa. Wanakosoa pale tu mitaji yao au maslahi yao inapoathirika. Waandamanaji wanapopigwa marungu au hata wanapofyetuliwa risasi ni nadra kusikia mabalozi, wawekezaji au wafadhili wa kigeni wakilaani.

Na ndivyo ilivyofanyika Julai mwaka huu, wakati tulipotembelewa na Rais Barack Obama aliyekuwapo hapa nchi kwa muda wa siku moja, si mbili kama waandishi wengine walivyokuwa wakirudia kusema

Ziara hiyo ilijaa propaganda na mbwembwe. Haya nimekwisha kuelezea kwa kifupi katika safu hii. Ila ninachotaka kusema mara hii ni kuwa Rais Obama alimmwagia sifa Rais Jakaya Kikwete na kusema “Tanzania imejizatiti katika masuala ya uwazi, ukweli na uendelezaji wa demokrasia.”

Alipoonana na waandishi ilidhihirika kuwa wanahabari wetu hawakuwa na hamu sana ya kuuliza maswali ya kumtahayarisha au ya kumdadisi. Labda ni kwa ajili ya kulinda maslahi yao. Labda na Rais Obama aligundua hilo na ndiyo maana akawasifu pia na waaandishi wa Tanzania ambao alisema; “wanatekeleza wajibu wao katika kusukuma mbele utawala bora na uwazi ambao ni msingi wa maendeleo katika jamii.”

Wakati Obama anamwaga sifa hizo kwa watawala na waandishi wetu, kuna ripoti iliyotoka huko New York, Marekani, iliyotayarishwa na asasi ya kuwatetea waandishi (CPJ). Ripoti hiyo ya mwaka 2012 inazungumzia mambo tofauti kabisa na yale yaliyosemwa na Rais Obama.

Inazungumza kuhusu ukandamizaji wa habari na wanahabari hapa Tanzania. Inazungumzia sheria kandamizi, mashambulizi dhidi ya wanahabari na ufungiaji wa gazeti la MwanaHalisi, ambalo lilikuwa likiwaumbua watawala kwa kufichua na kuibua mambo wanayoyafanya kinyume cha maadili na utawala bora

Ripoti hiyo inasema kumekuwapo na mashambulizi kama 10 dhidi ya wanahabari tangu Septemba mwaka jana, kitu ambacho kimewafanya baadhi ya wanahabari kupatwa na hofu. Matokeo yake huwa wanaamua kutowaandika vibaya watawala, hata kuficha baadhi ya habari.

Wengine wanaamua kuwa waandishi wapiga vigelegele na washangiliaji ili kujipendekeza kwa watawala, mradi tu mdomo ufike kinywani, kama wasemavyo. Nasikia baada ya kuondoka kwa Rais Obama baadhi yao walituzwa kwa kazi “nzuri” walizofanya. Nilielezwa kuwa karamu za kukata na shoka zilifanyika katika vyumba vya habari ili kupongezana. Najiuliza, alilipa nani gharama?

Almuradi ripoti ya CPJ inasema kutokana na mashambulizi dhidi ya wanahabari baadhi yao wameamua kufyata mkia. Mashambulizi haya ni pamoja na mauaji ya Daudi Mwangosi alipokuwa akipiga picha katika mkutano wa chama cha upinzani. Polisi mmoja amefunguliwa mashtaka lakini waliotoa amri ya kumfyatulia bomu la machozi wamepandishwa cheo.

CPJ pia inazungumzia kuhusu mashambulizi ya Absalom Kibanda, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, aliyepigwa vibaya, akaachwa akiwa amepoteza jicho mpaka ikabidi apelekwe nje akatibiwe.Ukiacha mashambulizi haya, pia kuna sheria takriban 17 ambazo zinakandamiza uhuru wa habari. CPJ inasema ingawa kumekuweko na mazungumzo ya muda mrefu pamoja na ahadi za kuzirekebisha au kuzifuta sheria hizo, hata hivyo bado hakuna hatua zilizochukuliwa.
Ahadi zilizotolewa wakati wa kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano na uwazi (Open Government Partnership Initiative), yenye lengo la kuendeleza sera ya uwazi. Hata hivyo hakuna hatua iliyochukuliwa kuunda au kurekebisha sheria ili kutekeleza makubaliano hayo kwa vitendo.

CPJ imeitaka serikali ya Tanzania kufanya uchugunzi huru na wa kina kuhusu mashambulizi ya Kibanda, pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa tukio hili. Serikali pia inashauriwa kufuta sheria ya magazeti inayoipa serikali mamlaka ya kupiga marufuku chombo chochote cha habari.

CPJ pia imeitaka Serikali kufanya uchunguzi kuhusu mauaji ya Daud Mwangosi kwa madhumuni ya kuwawajibisha maofisa wote wa polisi waliohusika katika kifo chake.

Sote tunakumbuka jinsi Serikali ilivyofanya uchunguzi usioridhisha. Ndiyo maana uchunguzi mwengine ukafanywa na baraza la habari (MCT) na kutoa ripoti yenye habari za kina zilizoambatana na vielelezo kama video zilizoonyesha jinsi Mwangosi alivyouawa. Zinaonyesha jinsi maofisa angalao sita walihusika katika kifo cha Mwangosi. Ripoti hii huru inapaswa izingatiwe ili mashtaka mapya yafunguliwe

Kuhusu mashambulizi dhidi ya Absalom Kibanda, polisi ilisema kuwa ingali inafanya uchunguzi. Lakini uchunguzi ulioongozwa na Deodatus Balile kwa niaba ya asasi za waandishi umeonyesha kuwa polisi haijafikiria kumkamata mtuhumiwa yeyote mpaka sasa

Ripoti ya CPJ inapendekeza kuwa serikali ifanye uchunguzi kamili na ulio wazi kuhusu mashambulizi dhidi ya Kibanda, ili wale waliohusika na unyama huo wachukuliwe hatua za kisheria.

Ripoti hii ya CPJ inasemekana iliwasilishwa katika ofisi ya Rais Kikwete lakini hakuna majibu yoyote kutoka huko. Hata hivyo Rais Kikwete aliwahi kumtembelea Kibanda alipolazwa hospitali, na hata akalaani kitendo hicho. Kwa upande wa pili Rais hajasikika akiwalaani polisi waliohusika kumuua Mwangosi

Halafu ukiangalia usimamishaji wa gazeti la MwanaHalisi mnamo Julai 2010, utaona kuwa hatua hiyo ya kiserikali ilichukuliwa baada ya jarida hilo kuandika habari za uchunguzi kuhusu Dk Ulimboka na mgomo wa madaktari. Gazeti hilo liliwalaumu maofisa wa usalama wa taifa katika kumtesa na kumjeruhi daktari huyo ambaye aliongoza mgomo.

Serikali iliitisha mkutano wa waandishi na kutangaza kufungiwa kwa MwanaHalisi bila ya kumtaarifu mhariri wa jarida hilo. Halafu hakuna sababu maalumu iliyotolewa ila tu kusema kuwa matoleo yake matatu yalikuwa na maandishi yenye chochezo

Ukweli ni kuwa hata katika sheria ya magazeti serikali inatakiwa iwape watuhumiwa fursa ya kukana tuhuma. Gazeti hili halikupewa nafasi hiyo. CPJ iliomba maelezo kutoka Mkurugenzi wa Habari na jibu lake lilikuwa: “Itabidi kwanza waombe msamaha kabla ya kufikiria kuliruhusu gazeti hilo”. Haeleweki iwapo kuomba radhi ni matakwa ya sheria, au iwapo mshtakiwa kabla ya kusikilizwa anatakiwa aombe msamaha kwanza

Ndipo mhariri alipowasilisha ombi lake kwa Rais lakini hakujibiwa. Baadhi ya asasi na mabalozi waliomba pia gazeti hilo liruhusiwe lakini hawakujibiwa Baada ya yote haya kuna hisia kuwa baadhi ya waandishi wameamua kutojiingiza katika “majanga” haya. Hivyo wameamua kutoandika habari za kuwakasirisha watawala. Mfano mmoja ni matukio ya huko Mtwara ambako inasemekana wananchi walioandamana walishambuliwa na wanajeshi wenye silaha.
Ni wachache wameandika kwa kina matukio hayo. Hii imesababisha baadhi ya wananchi wa Mtwara kuwalaumu waandishi, kuwashutumu na hata kuwashambulia kwa sababu ni “vibaraka” wa watawala

Wakati ripoti ya CPJ ilipotangazwa, waandishi walijaribu kupata maoni ya wakuu wa serikali. Simu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ilikuwa imefungwa. Naibu wake alikataa kusema lolote kwa sababu alikuwa likizoni. Akaongeza kuwa hata hivyo hakutaka kusema lolote kwa njia ya simu. Naye Waziri wa Habari alikuwa ameifunga simu yake, na makamu wake hakupokea simu iliyokuwa ikiita

Hivi ndivyo asasi za kimataifa zinavyoiangalia sekta ya habari nchini mwetu. Lakini ni muhimu pia kuona jinsi Watanzania wenywe wana maoni gani. Kwani mara nyingi kuna tabia ya sera zetu na ajenda zetu kutawaliwa na asasi, wafadhili na mabalozi wa kigeni

Haya tutayaangalia baadaye katika safu hii 0713-562181.

Chanzo.
Sheria kandamizi zaumiza wanahabari Tanzania - Habari - mwananchi.co.tz



 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…