WASOMI na wanasiasa nchini wamesema kitendo cha kurejeshwa bungeni kwa sheria ya gharama za uchaguzi kwa lengo la kujadiliwa upya ni ishara kwamba serikali haipo makini na inafanya kazi kwa kukurupuka.
Kurejeshwa bungeni kwa sheria hiyo iliyopitishwa na bunge mwezi Februari na kutiwa saini kwa mbwembwe Machi 17 mwaka huu na rais Jakaya Kikwete , kunafuatia hoja ya mbunge wa Karatu Dk Willbrod Slaa kuwasilisha mapendekezo katika Kamati ya Bunge ya Uongozi iliyokutana juzi jijini Dar es Salaam.
Juzi Spika wa Bunge Samuel Sitta aliliambia gazeti hili kwamba sheria hiyo itarejeshwa bungeni kujadiliwa upya baada ya kugundua kasoro nyingi.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, Profesa Abdallah Safari, Dk Sengondo Mvungi na Profesa Mwesiga Baregu walisema kuwa pamoja na mapungufu yaliyolalamikiwa na Dk Slaa, sheria hiyo haina jipya na imejaa mapungufu.
Profesa Safari alifananisha sheria hiyo kuwa ni sawa na kumweka farasi nyuma ya mkokoteni ili ausukume badala ya kumweka mbele ili auvute.
Alisema mbali na mapungufu yaliobainishwa na Dk Slaa pia sheria hiyo imejaa utata na kwamba ipo kwa ajili ya kukadamiza wapinzani.
"Hatua ya Bunge kuridhia kurejeshwa kwa sheria hiyo kujadiliwa upya Bungeni ni ishara ya serikali kutokuwa makini na kukurupuka katika utendaji wake ambao mara nyingi inazingatia kuwaridhisha watu fulani.
"Hii sheria itaendelea kukosolewa tu kwa kuwa haikidhi vigezo vya sheria za kimataifa kama vile tamko la dunia kuhusu haki za binadamu na sheria ya kimataifa kuhusu haki za kisiasa na kiraia," alisema Profesa Safari
Profesa Safari alifafanua kwamba athari za sheria hiyo ya gharama za uchaguzi zinaweza kuonekana zaidi katika sheria nyingine za uchaguzi ikiwemo Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Uchaguzi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliongeza kwamba athari hiyo pia zinaonekana kupitia ripoti mbili maarufu za tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1992 na ile ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998.
Alisema Sheria ya Gharama za Uchaguzi yenye vifungu 32 ambayo ni fupi ikilinganishwa na sheria nyingine nchini ina mapungufu katika vifungu kadhaa ambavyo alivikosoa.
Alivitaja vifungu vyenye mapungufu kuwa ni kifungu cha 8 (1) na (2), kifungu cha 9 (1),(2),(3), kifungu cha 11(4), 12, 13 na kifungu cha 15 (1)na (2).
"Moja ya madhumuni ya sheria hii ni kuweka utaratibu utakaowesha serikali kuchangia gharama za kampeni na uchaguzi kwa vyama vya siasa, kifungu cha 32 kimefanya nyingeza kidogo tu katika kifungu cha 13 (2) cha sheria ya vyama vya siasa.
Hivyo hakuna utaratibu mpya wa serikali kuchangia gharama za uchaguzi zaidi ya ule ulioainishwa na vifungu vya 13 (1), 16 na 17 ya sheria ya vyama vya siasa," alifafanua Safari.
Naye Dk Sengondo Mvungi alisema matatizo hayo yanatokana na kutofuatwa kwa katiba ya nchi.
âUtawala bora wa sheria hatufuati kabisa, hatumo katika nchi zinazofuata utawala bora, tumeingia kwenye mtaro moja kwa moja,âalisema Dk Mvungi na kuongeza:
"Katiba inaeleza juu ya kutunga sheria, lakini sasa inashangaza sana kuwepo na makosa kwenye kitu muhimu kama sheria ya uchaguzi."
Alifafanua kuwa makosa yaliyojitokeza yalitakiwa yafanyiwe kazi nje ya bunge na kurekebishwa kama marejeo ya sheria hiyo.
Kwa upande wake Profesa Mwesiga Baregu alisema rais Jakaya Kikwete alisaini Sheria ya Udhibiti Matumizi ya Fedha katika Uchaguzi kwa mbwembwe akilenga kuwaonyesha nchi wahisani kuwa anaongoza kwa kupambana na rushwa nchini.
Alisema pia rais alisaini sheria hiyo ili kuwaonyesha wananchi kuwa ametimiza ahadi aliyoahidi mwaka 2005 alipoingia madarakani.
"Hii ni dalili ya kukosa umakini kwa serikali na Bunge, kwa sheria iliyopitishwa na Bunge na kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania ikasainiwa kwa mbwembwe katika viwanja vya Ikulu, kuhudhuriwa na mabalozi kurudishwa tena bungeni ikiwa haijaanza hata kutumika!
"Rais Kikwete alitaka kujionyesha kwa mabalozi kuwa ni makini katika kupamba na rushwa na kuwaambia wananchi kuwa anachoahidi anatekeleza," alisema Profesa Baregu.
Profesa Baregu alieleza kuwa kurudishwa bungeni kwa sheria hiyo ni funzo kwa serikali na Bunge na kwamba iache kufanya mambo yenye maslahi kwa taifa kwa pupa na bila umakini.
âHii ni aibu sana, kama ingekuwa nchi nyingine iliyoendelea, vyama vya upinzani vingeshinikiza rais ajiuzulu. Lakini kwa sababu hapa kwetu ndiyo chama hiki kimoja tuu kikubwa hali inakuwa tofauti,â alisema Profesa Baregu.
Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Hamad Rashid alisema kuwa mjadala huo unarudi bungeni kwa kuwa Dk Slaa hakuridhika na majibu ya mwanasheria mkuu wa serikali.
âDk Slaa aliniambia hiyo ni moja ya mambo ambayo atataka ufafanuzi wa kina, sitaki nimsemee sana lakini ni hoja ya msingi,â alisema Rashid.
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa sheria hiyo pamoja na kuamuliwa kurudishwa bungeni, ni vigumu kutekelezeka kwa kuwa ina makosa mengi na imetungwa kwa maslahi ya watu binafsi.
Alisema kuwa wataalamu wamefanya kazi sio kwa utaalamu wao bali kwa kutumwa na kufuata maagizo ya wenye maslahi yao.
âTulisema wataalamu waachiwe wafanye kazi yao, lakini muda walioutumia wa miezi miwili haukutosha na ndiyo maana haina kichwa wala miguu na imetungwa kwa nia mbaya, vile vile uongo umeshakuwa ni uhai wa taifa hilo,âalisema Mbatia.
Alisema sasa inatakiwa serikali irudi kwenye katiba kwa kuwa makosa haya ni madogo tu sheria nyingi zina makosa, na zinahitaji marekebisho makubwa.
âKutungwa kwa hii sheria hakuna nia ya kupambana na fedha chafu bali ni maslahi ya watu wachache,âalisema.
Naye Ismail Jusa wa Chama Cha Wananchi (CUF), ambaye hivi karibuni baada ya muafaka wa Chama Cha Mapinduzi CCM na CUF Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa mbunge wa kuteuliwa, alisema kitendo cha sheria hiyo kusainiwa ikiwa na mapungufu hayo na sasa kurudishwa tena bungeni inaonyesha jinsi serikali isivyokuwa makini juu ya masuala muhimu yenye maslahi na taifa.
âSerikali ingekuwa makini yote haya yasingetokea, pesa za walipa kodi zinateketea bure, siku moja kwa bunge kukaa ni gharama kubwa sana, hii inaoyesha kuwa CCM imeshindwa kuongoza nchini,â alisema Jusa.
Juzi Dk Slaa aliliambia gazeti hili kuwa amewasilisha mapendekezo hayo kutokana na kile anachoamini kuwa Rais Kikwete amedanganywa na kusaini sheria hiyo kimakosa.
Alisema aliamua kuliwasilisha suala hilo kwanza kwenye kamati ya uongozi ya Bunge ili kama angepuuzwa, alifikishe suala hilo bungeni mwenyewe kwa namna anayoona inafaa.
"Mapambano ndio yameanza; mimi ni mjumbe wa kamati ya uongozi ya Bunge na leo (jana) tulikuwa na kikao, nimehoji suala hilo kabla sijalifikisha bungeni kwa namna ambayo nitaona inafaa," alisema Dk Slaa.
"Bado nasisitiza kuwa Mwanasheria Mkuu amedanganya kwa kusema vifungu hivyo viko sahihi kwa kuwa Ofisi ya (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera na Uratibu wa Bunge-),Phillip Marmo ndio iliyovifanyia marekebisho. Ofisi ya Marmo haina mamlaka ya kubadili vifungu vya sheria iliyopitishwa na Bunge.
http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=19165