Utangulizi
Kujiua au kujaribu kujiua ni kitendo cha mtu kusababisha au kujaribu kusababisha kifo chake mwenyewe kwa makusudi kwa njia mbalimbali. Mara nyingi chanzo huwa ni matatizo ya kihisia, kisaikolojia, maradhi ya akili, changamoto za maisha na matatizo mengine makubwa yanayoweza kuathiri afya ya akili ya mtu.
Kujiua ni suala zito sana linalohitaji uelewa mpana na msaada wa kitaalamu ili kuzuia matukio kama hayo na kusaidia watu wanaopitia hisia za kutaka kujiua kuondokana na hisia hizo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2023, inakadiriwa zaidi ya watu 700,000 hujiua kila mwaka duniani kote, hii ni sawa na kupoteza mtu kila baada ya sekunde 40, ilhali pia idadi ya wanaojaribu kujiua na kuokolewa ikikadiriwa kuwa juu. Tanzania pia hali si shwari.
Hili ni janga kubwa la dunia nzima, linalonasibishwa na matatizo ya afya ya akili ukiwemo msongo mkali wa mawazo, kutokana na mfumo wa maisha ulivyo kwa sasa. Wanaume wakiwa wanaongoza kwa kujiua.
Sheria
Nchi mbalimbali duniani kote zimebadili na zinaendelea kuifanyia mabadiliko sheria dhidi ya tendo la kujaribu kujiua; kwa kuacha kulichukulia kama kosa la jinai. Na badala yake, tendo hili linachukuliwa kama yowe la mtu kuhitaji msaada wa kisaikolojia haraka sana, na matibabu mengine muhimu katika mazingira yanayofaa.

Kijani: Kujiua/kujaribu kujiua si kosa kisheria, kumsaidia mtu kujiua ni kosa kisheria.
Bluu Bahari: Kujiua/kujaribu kujiua na kumsaidia mtu kujiua si kosa kisheria.
Chanzo: Wikipedia
Nchini Tanzania, kwa mujibu wa Kifungu cha 217, cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kujaribu kujiua ni kosa la jinai. Jinai ni tendo lolote lililokatazwa kisheria, mtu anayelitenda anakuwa ameikosea Jamhuri. Mtuhumiwa wa kujaribu kujiua hukamatwa kama watuhumiwa wengine na huwekwa kituo cha polisi kabla ya kufikishwa mahakamani. Endapo mtuhumiwa atakuwa na hali mbaya kiafya, mfano kuwa na majeraha, hufikishwa hospitali akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Adhabu ya kosa la kujaribu kujiua inaweza kuwa kifungo cha jela kisichozidi miaka mitano kama inavyoelezwa katika Kifungu cha 35 kinachofafanua adhabu ya jumla kwa makosa ambayo hayajapewa adhabu ya moja kwa moja. Ingawa pia, kifungu cha 13 kinatoa kinga na msamaha kwa watu wanaofanya makosa wakiwa katika hali ya ugonjwa unaoathiri akili zao.
Kwanini kuna ufa katika sheria hii?
Mazingira yetu halisi ya ukamataji watuhumiwa tunayafahamu. Vituo vingi vya polisi nchini havina mazingira rafiki kwa mtu mwenye msongo mkali wa mawazo. Elimu na uelewa wa watu wengi kwenye jamii yetu, ikiwemo kada ya polisi, juu ya matatizo ya afya ya akili, bado ni mdogo. Hivyo, sheria hii inakinzana na namna bora ya kumsaidia mtu mwenye hisia za kutaka kujiua.
Kumkamata mtuhumiwa, kumsweka kwanza rumande, kusubiri kumfikisha mahakamani, kumsubirisha zaidi siku ya kwenda kufanyiwa uchunguzi wa akili ilhali anaenda mahakamani na kurudi katika mazingira yanayomwongezea msongo (rumande), si sahihi kwa afya yake ya akili.
Hakuna sababu ya kumpitisha mtuhumiwa katika hekaheka nyingi kabla ya kumpatia huduma anayostahili kama binadamu aliyepitia hali ngumu kisaikolojia hadi kujaribu kusitisha uhai wake. Zaidi, akiwa hana makosa mengine ya jinai yanayomlazimu kuwa chini ya ulinzi.
Sheria inapotoa msamaha kwa kuzingatia hali ya ugonjwa unaoathiri akili ya mtuhumiwa, inamaanisha wapo watu wanaohukumiwa kwenda jela kwa sababu imethibitika kuwa wamefanya kosa hilo wakiwa na afya njema ya akili. Jambo hili linawezekana vipi? Ni nani mwenye afya njema ya akili atajaribu kujitoa uhai kwa kukusudia ikiwa hana tatizo lolote na hakimbii jinai yoyote?
Wanasaikolojia wabobevu wanakiri sababu kubwa mojawapo inayopelekea watu wengi kujaribu kujiua ni kuyumba kwa afya ya akili. Ikiwa mtu huyu ataachiwa huru baada ya kuthibitika kuwa na tatizo la kisaikolojia/akili, sheria hii inakuwa imemtesa bila hatia.
Sheria hii ilitungwa na kufanyiwa marejeo miaka mingi iliyopita, ambapo afya ya akili ilikuwa haijaeleweka sawasawa. Na inaendelea kutumika nyakati ambazo maisha na mambo mengi yamebadilika na kuanza kueleweka vyema. Marekebisho yanahitajika ili kuendana na uhalisia wa maisha na changamoto za sasa. Tunapopambana kuelimisha kuhusu afya ya akili, unyanyapaaji na mengine yanayohusu maradhi ya akili, huku tukiendelea kushikilia sheria inayokwenda kinyume na kile tunachoelimisha. Tunaichanganya jamii.
Mabadiliko gani yazingatiwe?
- Sheria hii ibadilike, iwazingatie watuhumiwa wanaotaka kujiua kama njia ya kukwepa kuwajibika kwa kosa lingine la jinai walilofanya; na yeyote anayesaidia kufanikisha mtu kujiua ilhali anajua mhusika amevurugwa kiakili.
- Tanzania inahitaji Toll-free numbers (Namba za msaada wa haraka) maalumu zinazojitegemea kabisa kwa ajili ya wanaokabiliwa na hisia za kutaka kujiua. Namba hizo ziwe wazi mitandaoni, zinazopatikana kirahisi, na zenye wataalamu. Sheria iwabane watakaotumia namba hizo kufanya mzaha. Mf: kuzifungia namba korofi.
- Tanzania inahitaji vituo vingi vya umma vya ushauri nasaha vinavyosaidia changamoto za afya ya akili. Inahitajika kampeni kubwa ya kubadili mitazamo ya watu kuwa vituo vya ushauri nasaha vipo kwa ajili ya wapima UKIMWI. Vituo hivi vijengewe uwezo wa kumsaidia mtu mwenye changamoto ya afya ya akili.
- Mabadiliko ya sheria yatafungua uelewa zaidi juu ya masuala ya kujiua ambayo kwa sasa watu wengi bado wako gizani. Wengi wana hofu na aibu ya kutafuta msaada, wanaogopa kuzungumzia majaribio waliyowahi kufanya kwa sababu tendo hili ni jinai. Ni nani atataka kukiri kuwa amewahi kutamani kufanya kosa la jinai? Ni nani atapiga simu kujishtaki anajisikia kufanya kosa la jinai?
- Marekebisho ya sheria hii yatafungua milango mingi ya majadiliano ya wazi yanayoweza kusaidia sana kupunguza kasi ya watu kujiua hususani vijana chini ya miaka 18, ambao hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya wao kujiua.
- Sheria hii imlinde mhusika na kuzuia udhalilishaji wa aina yoyote. Jamii itatambua mipaka yake kwenye vitu vinavyogusa maumivu ya kihisia ambavyo wakati mwingine hutokana na maradhi/changamoto na si maamuzi binafsi ya mtu.
Maendeleo ya taifa yanategemea zaidi uimara wa wananchi. Uimara wa mwili unategemea uimara wa afya ya akili. Tuko katika zama ambazo mfumo wa maisha una mambo mengi yanayovuruga utulivu wa akili na kusababisha msongo mkali na maradhi mengine ya akili.
Sheria iwepo kusaidia na si kuwaweka wananchi katika hali ya kuzidi kuchanganyikiwa na kujificha. Ni wakati sasa, ianze mikakati ya kuijenga Tanzania yenye uelewa mpana kuhusu masuala ya kujiua. Miaka mitano ijayo Tanzania iwe imetimiza lengo namba tatu la maendeleo endelevu (SDGs) 2030 - Kuhakikisha Afya Njema na Ustawi wa Watu wa Rika Zote .
Mungu ibariki Tanzania.

Upvote
4