Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda alaani Waajiriwa wa TAMISEMI kutofuata Utaratibu na Matakwa ya Sheria za Uchaguzi Mkuu 2020.
Mgombea urais huyo kupitia chama cha ADA TADEA na Mwenyekiti wa Chama hicho, amelaani vyama vya Upinzani kuwekewa Mapingamizi yasiyoeleweka na kudai hatua hiyo ni kudidimiza Demokrasia nchini kwa uroho wa madaraka.
Shibuda amesema kinachoendelea nchini ni udhalilishaji kwa Rais aliyesema Uchaguzi huu wa 2020 utakuwa huru na haki na kuongeza kuwa kinachoendelea ni Demokrasia bandia na Dunia nzima inaona.
Shibuda ametolea mfano kuwa Wagombea wake wamesingiziwa kuwekea pingamizi wagombea wa Vyama Vingine na barua za kughushi zikaandikwa wakati chama chake hakijaweka pingamizi kwa Mgombea yeyote wa Urais, Ubunge wala Udiwani.
Amesema kitendo hicho cha kusingizia ni Uhuni kwani hakuna chama kafara kwa chama kingine.
Shibuda amemtaka Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kuangalia viapo vya Watendaji wanaosimamia Uchaguzi kwani Wasimamizi wa Uchaguzi ni Waajiriwa na Watumishi wa TAMISEMI ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais.
Amemtaka Balozi Kijazi awakutanishe TAMISEMI na Tume ya Uchaguzi waangalie jinsi ya kuwachukulia hatua watu wote wanaoharibu Uchaguzi huu na kushauri waangalie viapo vya Maadili kwa hawa watendaji wa TAMISEMI wasiofuata kanuni zinasemaje.
Shibuda ameongeza kuwa kwa sasa John Magufuli ni Mgombea Urais, hawezi zungumza lolote juu ya hili linaloendelea bali katibu Mkuu Kiongozi.
Amesema imefika wakati wa kuangalia kama waajiriwa wa TAMISEMI wanakidhi matakwa na Sheria za Tume ya Uchaguzi Tanzania.
Shibuda ametoa rai kuwa ni muda muafaka kwa Baraza la Vyama vya Siasa kukutana na kutoa Maoni mapema kuhusiana na Uchaguzi huu ili uwe Huru na wa Haki ili kutunza amani iliyopo.