Shirika la Posta ni taasisi inayojipeleka kaburini

Shirika la Posta ni taasisi inayojipeleka kaburini

Guus

JF-Expert Member
Joined
Jul 16, 2013
Posts
1,139
Reaction score
842
Historia ya Shirika la Posta Tanzania
Huduma za Posta kama taasisi zilianzishwa nchini na Serikali ya kikoloni ya Ujerumani. Huduma ya kwanza ya barua iliyobandikwa stempu ilianzishwa hapa nchini mwaka 1893.

Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba 1961, huduma za Posta ziliendelea kusimamiwa chini ya Sheria iliyoanzisha Taasisi ya Posta na Simu ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, kutokana na kusambaratika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Tanzania iliteua kamati ya kuandaa sheria ya kuunda Shirika la Posta na Simu Tanzania ili kuchukua nafasi ya Shirika la Posta na Simu la Afrika ya Mashariki.

Shirika jipya liliundwa kwa Sheria ya Bunge Nambari 15 ya mwaka 1977 iliyoanza kutumika rasmi tarehe 3 Februari mwaka 1978.

Pamoja na mengine, jukumu la Shirika hili la Posta ni kutoa huduma za Posta ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Changamoto Zinazoikumba Shirika la Posta
Ukiondoa matatizo ya kiuendeshaji na kuchukulia mambo kikawaida kwa wafanyakazi wengi wa umma, Shirika la Posta lipo kwenye wakati mgumu kutokana na mabadiliko ya dunia.

Kuna changamoto nyingi zinazolikumba Shirika la Posta kutokana na maendeleo ya sayansi, teknolojia, na upanuzi wa TEHAMA. Mfano:

  1. Watu wengi sasa wanatumia barua pepe, ujumbe mfupi wa simu, na majukwaa ya mitandao ya kijamii badala ya barua za kawaida.
  2. Kupungua kwa mapato kunakotokana na kupungua kwa utumaji wa nyaraka za kiofisi na binafsi kupitia njia za Posta.
  3. Kupanuka kwa huduma za kidijitali za kutuma na kupokea nyaraka kama PDF na e-signatures ambazo zimepunguza hitaji la nyaraka ngumu.

Kujielekeza “Kibra”
Pamoja na changamoto hizi za kiteknolojia, bado zile huduma ambazo walitakiwa kuziboresha wamekuwa wakiziharibu.

Mfano, mimi nipo Dodoma na nimekuwa na sanduku binafsi la kupokea barua kwa takribani miaka 12. Mara kwa mara nikienda kulifungua, nakutana na barua au nyaraka ambazo:

  • Anuani iliyoandikwa ni tofauti kabisa na sanduku langu.
  • Anuani ya sanduku langu ipo sahihi, lakini mkoa ni tofauti. Mfano, sanduku langu ni 2021 Dodoma, lakini napata nyaraka zilizoelekezwa 2021 Dar es Salaam.
Mbaya zaidi, hata ukizirudisha kwenye sanduku la kurejesha barua zilizokosewa, bado unaweza kuzikuta tena siku nyingine kwenye sanduku lako.

Hali kama hii inaleta changamoto kubwa. Mfano, kuna watu wanaoomba kazi au tender, lakini nyaraka zao hazifiki zinakotakiwa. Matokeo yake wanapoteza nafasi si kwa sababu walichujwa, bali nyaraka hazijawahi kufika kabisa.


Dunia Inavyokwenda
Dunia inabadilika, na wawekezaji wanazidi kuongezeka huku sekta binafsi ikiingilia huduma za Kiposta kwa kasi.

Makampuni mengi ya usafiri sasa yanaingia kwenye huduma za Kiposta. Hii inatakiwa kuwa “wake-up call” kwa Shirika la Posta kwamba wanakutana na ushindani mpya.

Ikiwa sasa wanaona usambaaji wao kama nafasi ya kushikilia soko, wanapaswa kufahamu mambo yanabadilika kwa kasi.

Rai
Shirika la Posta, Tanzania boresheni na ongezeni kasi ya utoaji wa huduma kabla ya kulizika kabisa.
 
Back
Top Bottom