Short Story: Simba wa Mizimu

Short Story: Simba wa Mizimu

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
9,189
Reaction score
16,128
SIMBA WA MIZIMU

Siku moja nilikwenda katika kijiji kimoja kilichokuwa kikishambuliwa na ndovu mara kwa mara. Nilipokuwa nikipitia njiani, nilimwona mtu mmoja juu ya dungu lake akiezeka paa la dungu kwa makuti ya mkoche. Nilipopita pale chini la dungu, yule mtu akanitazama kisha akacheka. Nikamwuliza, "Unacheka nini?" "Ah," akanijibu, "nimefurahi tu, bwana." Baada ya kuzungumza naye kwa muda mchache, akanihadithia kuwa akishajenga dungu lake, anataka kulima shamba la mtama mahali pale. Mkewe na wanawe watakuja kukaa mle dunguni kwa kumsaidia katika kazi zao za makulima. Nikapatazama mahali pale nikapaona ni pazuri sana kwa yote aliyokusudia. Kwa mbele kidogo kulikuwa na mkuyu mkubwa uliotandaza matawi yake na kutoa kivuli cha haja. Uwanja mzuri wa majaní mabichi ulitambaa pote na kupapa mahali pale sura nzuri. Palionyesha kuwa swala na wanyama wengine wengine wanaweza kupatikana kwa urahisi sana mahali pale.

Dungu lile lilijengwa na mtu niliyekwisha mtaja, lilinipendeza mno hata nikamwomba yule bwana anipe nafasi nikae mle dunguni mpaka kumaliza kazi yangu na kuhama mahali pale kama ilivyo kawaida yangu. Hata hao ndovu niliowaendea katika kijiji hicho bila shaka ni rahisi kuwapata kwake kama ukikaa katika kibanda au dungu la huyo bwana ninayemhadithi. Tukapatana aniuzie. Akaniuzia kwa shilingi kumi. Nikanunua, yeye akatafuta mahali pengine karibu na pale akajenga dungu lingine.

Tulipokwisha tua mizigo yetu pale chini ya dungu, tukaenda kuwinda nyama karibu karibu kwa chakula chetu cha jioni. Njiani, watu niliofuatana nao wakaanza kunitisha.

Wakasema, "Pale uliponunua dungu, ni mahali pabaya sana. Yuko simba mtu anayependa sana kupitapita. Simba huyo, hapo kale alikuwa mke wa sultani aliyeuawa na Majerumani. Aliuawa katika vita ya maji maji. Hakuna hata mtu mmoja aliyepata kujenga mahali pale isipokuwa yule mpungufu akili aliyekuuzia dungu. Labda naye ni mchawi wa kutosha hata akathubutu kujenga mahali pale. Kwanza Korogeo si mwenyeji wa nchi hii wala si Muislamu."

Nikaisikiliza hadithi yao ya kuogofya kwa utulivu. Ingawa hadithi yao ilikuwa ni ya mambo ya ushirikina mtupu, nilingiwa na woga kidogo. Yeyote aliye mgeni katika nchi fulani au mahali fulani mara nyingi huogopa jambo lolote la hatari atakaloambiwa. Wakazidi kuniambia kuwa simba huyo huja masika hata masika tu. Hukaa chini ya mkuyu ulio karibu na dungu na kuvizia chochote kitakachopita chini ya mkuyu. Hapakuwa na mti wa kupanda kama mtu akikutana na simba huyo, isipokuwa mkuyu huo huo anaokaa simba chini yake akivizia kinachopita. "Shida sana kuponyoka ukikutana naye," wakaendelea. "Kama tulivyokwisha sema, kuwa si simba wa kawaida bali ni simba wa mizimu. Yanini kusema mengi; masika sasa ni karibu sana; na kila masika simba hufika kutoka mizimuni; basi kama bado upo, ataona mwenyewe na kuhakikisha badala ya kuhadithiwa."

Mwezi ukapita pale dunguni bila ya kuona lolote. Masika ya kawaida. Mtama wa Korogeo ukakua na kuonyesha dalili ya mavuno mazuri sana. Korogeo alifurahi sana kwa kuuona mtama wake unaahidi mavuno mazuri. Ulifunga shamba zima hata ukaonekana kama msitu kamili. Uwanda ule wa majani mazuri ukageuka mbuga ya nyasi hata mtu akipita pale chini ya mkuyu ni vigumu kumwona kwa urahisi. Ndovu wakaja kwa wingi katika mashamba ya watu na kuharibu mimea. Niliwaua na kuwafukuza wengi. Korogeo na shemeji yake wakajenga madungu yao hatua mia kulia ya dungu langu.

Usiku mmoja nilisikia kama kishindo cha mnyama fulani anapita nje ya dungu langu. Nikaamka, nikatoka nje na kujibanza. Ulimwengu mzima ulikuwa umelala. Nikamulika kurunzi yangu huko na huko lakini sikuona kitu. Nikarudi dunguni nikalala. Punde si punde nikasikia sauti ya Korogea ikiita kwa hofu. "Bwana! Bwana ! Bwana! Kuna dudu huku!" Bila ya kukawia nikafika dunguni kwa Korogeo na taa na bunduki. Korogeo akashuka akihema na kusema, "Lilikuwa dudu hapa, sasa hivi." Tukatafutatafuta lakini hatukuona kitu. Nilipomulika taa chini karibu na lile dungu nikaona alama ya unyayo wa simba mkubwa sana. Ni ajabu kabisa lakini unyayo ule ulionekana mmoja tu. Tena, ulijulisha dhahiri kama simba huyo ndiyo kwanza amekanyanga mahali pale. Kwa kuwa ardhi ilikuwa nyevu, ule unyayo ukaanza kujaa maji. He! kumbe upande mmoja wa nyumba ya Korogeo ulikwisha bomolewa. Bila ya shaka simba yule alikuwa amejificha katika majani marefu karibu sana na dungu lake. Nuru ya taa haikuweza kumwonyesha. Kama tulivyokwisha ambiwa na wenyeji, simba wa mizimu alikuwa amekwisha tuingilia.

Upepo wa mvua ukaanza kupepea na mawingu yakafunga na kutia kiza kikuu ajabu. Mara mvua kubwa ikaanza kuanguka. Umeme ukamulika nchi nzima kwa ghafla na kutoa ngurumo kama mzinga wa motoni.

Majani, nyasi na mtama vyote vya ulimwengu ule vikapeperushwa. Radi ikaunguruma mara ya pili. Umeme na ngurumo, na umeme na ngurumo. Korogeo na mimi tukasimama pale pale mbele ya dungu na taa yetu ikazidi kufifia. Umeme ulipomulika mara ya mwisho, kwa mbele tukaliona simba kubwa limesimama. Tukaingia katika chumba cha chini cha dungu na kujificha.

Kila mtu akakaa karibu na mwenzie tukimfikiria simba wa mizimu yule. Hakuna aliyejua nani atakayechukuliwa kwanza kama simba akiingia mle dunguni. Saa nzima ikapita bila ya hatari yoyote. Mvua ikanyamaza na nchi ikwa shwari tena. Kiza kikapungua kidogo. Korogeo na mimi tukaondoka pamoja mpaka dunguni kwangu. Korogeo akakaa karibu nami mahali nilipolala katika kiti cha kulala. Bunduki yangu mapajani na Korogeo mkuki wake mkononi. Hakuna hata mtu aliyeweza kuupata usingizi kwa hofu. Hatukuwa na la kuzungumza wala kufanya. Tukabaki tukitazamana na kucheka kama wapumbavu. Mara nikamwona Korogeo anatazama chini huku macho ameyatoa.

Nikamwuliza, "Nini Korogeo?"

"Tazama!" akanionyesha chini karibu na taa. Lo! nilipotupa macho, nikauona unyayo wa simba pale chini ndani ya dungu langu. Unyayo wenyewe ulifanana sana na ule tuliouona karibu na dungu la Korogeo. Nilipozidi kutazama nikaziona kwa wingi mle ndani ya kibanda changu. Kumbe yule simba alikwenda mle dunguni mwangu nilipokuwa ndani ya dungu la Korogeo. Hatukuweza kujua simba alipokuwa wakati ule. Kila mtu akajitayarisha na kuyakaza macho yake mlangoni; kwani ndiko tulikodhani atatokea kama atakuja. Tukakaa vivi hivi lakini hakutokea.

Bila ya kupenda nikapitiwa na usingizi mdogo. Sikujijua kama nilipitiwa na usingizi mpaka nilipoamshwa na sauti ya kitu kizito kilichonirukia kifuani, Korogeo akaita kwa woga tena; "Bwana !" Aliyenirukia kifuani, alikuwa Korogeo. Nimemwona akichungulia! Sasa hivi tena! Si simba bwana! Nasadiki kama ni simba mtu! Nikatega bunduki yangu na kuilekeza mlangoni, Dungu zima likajaa harufu ya mnyama wa porini hasa ya simba. Nikauona umauti umekaribia saa ile ile. Mara pale mlangoni nikaona kama kitu kinasogeasogea. Kwa woga niliokuwa nao, sikungoja nikione vizuri; nikaelekeza bunduki pale pale na kupiga. Mshindo wa bunduki ukavuma mpaka mbali karibu na alfajiri ile. Mara mkoromo wa maumivu ukasikilikana nje ya dungu. Hakuna aliyethubutu kutoka na kwenda kutazama. Mara kulipoanza kupambazuka tu, tukatoka na kwenda kutazama. Kwa furaha yetu simba lile lilikuwa kaputi hatua ishirini tu toka dunguni kwangu. Watu walipopata habari, walifurahi sana. Wengi wakasema kuwa Mzungu hadhuriki na mashetani ndiyo maana akaweza kumwua simba yule. Wengine wakasema kuwa simba yule hakufa asilani. Yote yale yalikuwa ni mazingaombwe tu. Kwa vyovyote hivyo, kama alikuwa simba wa mizimu au simba wa kawaida, simba yule aliyeitisha nchi kila masika alikuwa amekufa siku ile. Haikosi Korogeo bado anaukumbuka usiku ule kama niukumbukavyo mimi.

Mwisho​
 
Back
Top Bottom