Shule iliyoshika mkia kidato cha pili 2012 hii hapa

Shule iliyoshika mkia kidato cha pili 2012 hii hapa

kasyabone tall

JF-Expert Member
Joined
Sep 13, 2009
Posts
254
Reaction score
63
atika mtihani wa kidato cha pili uliofanyika mwaka jana na matokeo yake kutangazwa Januari mwaka huu, mikoa ya Lindi na Mtwara ilitoa shule 10 za mwisho. Kwa Mtwara, pamoja na maelezo mengine, vurugu za wananchi na kuwapiga walimu zinaelezwa kuwa sababu ya baadhi ya shule mkoani humo kufanya vibaya.

Moja ya shule ambazo kufanya kwake vibaya kunahusishwa na vurugu hizo ni Mihambwe iliyokuwa ya mwisho kitaifa. Shule hii ipo katika Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara.

Shule hii ilifungwa Aprili mwaka jana kutokana na vurugu za wananchi waliokuwa wakishinikiza kulipwa malipo ya awamu ya pili ya korosho.

Kutokana na vurugu hizo, wananchi wanadaiwa kuwapiga walimu pamoja na watumishi wengine wa Serikali waliokuwa wanafanya kazi katika kata hiyo iliyopo umbali wa takribani kilomita 10 kutoka Tandahimba mjini.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, wanasema baada ya walimu hao kupigwa, wengi walihamishiwa katika shule za maeneo mengine, jambo lililowafanya kukaa bila walimu kuanzia kipindi hicho mpaka mwisho mwa mwaka jana walipotakiwa kufanya mitihani ya taifa.

Kutokana na suala hilo, wanafunzi wa kidato cha pili na wale wa kidato cha nne, waliripoti shuleni hapo Januari mwaka huu tangu ilipofungwa Aprili mwaka jana.

Walimu wapigwa
Kwa mujibu wa wanafunzi, sababu kubwa iliyofanya wanakijiji kuwapiga walimu wao ni kitendo chao cha kudai michango mbalimbali ikiwamo karo za shule na mtihani.

“Wazazi walikuwa wanaona sisi tunarudishwa nyumbani kwa sababu ya ada wakati wao hawajalipwa malipo yao ya pili ya korosho,” anasema Makake Habasi.

“Waliona bora wawapige watumishi wote wa Serikali kwa sababu wao wanalipwa mishahara wakati wananchi hawalipwi fedha zao za korosho,” anaongeza.

Hali hiyo ilisababisha shule ifungwe, mpaka wanafunzi walivyotakiwa kufika shuleni Novemba mwaka jana kwa ajili ya kufanya mtihani wa kidato cha nne na pili.

Ni kwa sababu hiyo, wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kidato cha pili mwaka jana, bado wanajihesabu kuwa kidato hicho hicho, kwani hawajapata matokeo yao kutokana na wengi wao kutolipa ada ya mtihani huo na pia hawatarajii kufaulu.

Wanafunzi hao wanasema kuwa, hata ikitokea baadhi yao wakafaulu, wataomba kurudia darasa kwa kuwa masomo mengi ya kidato cha pili hawakuyasoma.

Hali kama hiyo ipo kwa wanafunzi wanaotakiwa kuingia kidato cha nne mwaka huu ambao pia wanasema kuwa, kwa kuwa karibu mada zote za kidato cha tatu hawajazisoma, wanataka kurudia darasa.

Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo,Hassan Abdallah, anasema vurugu hizo zilipotokea, shule hiyo ilikuwa na walimu sita.

Anaeleza kuwa, wananchi walipofanya vurugu kushinikiza Serikali iwalipe malipo yao ya pili ya korosho, baadhi ya walimu wa shule mbalimbali zilizopo kwenye kata hiyo walipigwa na kukimbilia mjini.

Baada ya takribani miezi 10 tangu kutokea kwa vurugu hizo, sasa shule hiyo ina walimu wawili ambao hata hivyo mahudhurio yao siyo mazuri.

Hali hiyo inathibitishwa na baadhi ya wanafunzi wanaoleza kuwa, siyo jambo la ajabu wao kufika shuleni na kukaa mpaka mchana bila kuwapo kwa mwalimu hata mmoja.

“Mkuu wa shule anakaa Tandahimba mjini, mwingine yupo hapa kijijini, siku kama ya leo hakuna hata mmoja aliyefika.

Huyu wa hapa kijijini tumeambiwa amesafiri na mkuu wa shule ndiye huyo hajafika,” anasema mwanafunzi mmoja.

Kwa pamoja wanafunzi hao wanasema , wakati mwingine walimu hufika saa nne asubuhi, na kama wasipofika ikifika saa tano wanafunzi huamua kurudi nyumbani.

Mwandishi wa makala haya alifika shuleni hapo Januari 28. Aliwasili hapo saa moja asubuhi lakini mpaka alipoamua kuondoka ilipotimu saa nne, hakuna mwalimu aliyekuwa amehudhuria kazini.

Kwa muda wote aliokaa hapo aliwashuhudia wanafunzi wakirandaranda, huku wengine wakipiga soga katika vikundi.
Aidha, baadhi ya wazazi waliofika kuandikisha watoto wao, nao waliamua kurudi walipotoka baada ya kuwasaubiri walimu bila ya mafanikio.

Wazazi wazungumza
Baadhi ya wazazi waliozungumza na Mwananchi wanasema kuwa hawakuwapiga walimu wa shule ya sekondari bali waliopigwa ni wale wa shule za msingi.

Kutokana na hali hiyo, wanaeleza kuwa Serikali iliamua kuhamisha walimu kwa makusudi ili kuwakomoa.

Dida Said mkazi wa eneo hilo, anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakiambiwa walimu watapelekwa jambo ambalo halitelezwi.

“Tatizo hapa tukifanya kitu chochote tunaonekana hatujasoma, hakuna mwalimu wa sekondari aliyepigwa.

Waliamua tu kuwahamisha kwa sasa hivi ni mwalimu mmoja tu huwa namuona hapa na leo nashangaa hayupo,” anasema.

Anasema shule za msingi zilizoathiriwa na fujo hizo ni pamoja na Mihambwe ambayo kwa sasa ina mwalimu mmoja, Ruvuma walimu watatu, Mkaha mwalimu mmoja na Mitumbatu mwalimu mmoja.

Kabla ya fujo hizo, baadhi ya shule hizo zilikuwa na zaidi ya walimu 10, baada ya kupigwa na wanakijiji, walimu walihamishiwa shule nyingine.

Uongozi wa elimu
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mtwara, Hipson Kipenya, anasema shule hiyo ilifungwa kutokana na wananchi kufanya fujo na kuwapiga walimu.

Anasema kuwa, kutokana na usalama wao, waliamua kuwahamisha walimu kwenda kwenye maeneo yaliyokuwa na uhitaji kwani walimu wenyewe walikuwa hawataki kuendelea kukaa katika kata hiyo.

“Malipo ya korosho na shule wapi na wapi, hawa walitaka kumpiga mpaka ofisa elimu wetu, watu kama hawa utasawaidiaje?” anahoji na kuongeza:

“ walimu wamepigwa mpaka wakaenda kulala kwenye ofisi za halmashauri bado unataka tuwaache, wengi walikataa kurudi kwenye shule zao na sisi tukaona bora tuwapeleke kwenye maeneo yenye uhitaji ambayo na wazazi wapo tayari kushirikiana nao,” anasema

Kuhusu mtihani wa kidato cha pili, Kipenya anasema pamoja na kutambua kuwa wanafunzi hao hawakuwa wamesoma kwa kipindi kirefu, waliwapelekea mitihani kwa sababu walikwishasajiliwa kufanya mtihani huo shuleni hapo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mihambwe Chimeta Abdallah, anasema mbali na suala la walimu kukimbia kutokana na fujo hizo, sababu ya shule ya Mihambwe kufanya vibaya ni kutokana na baadhi ya walimu wanaopangiwa hapo kutokuwa na taaluma ya kutosha.

Anasema kuwa, walimu wengi wa shule hiyo elimu yao ni ndogo na haitoshi kuwafanya wanafunzi waelewe vyema masomo yao.

“Walimu wanaoletwa hawana sifa, wanachaguliwa ilimradi tu waje kujaza shule, hawawezi kabisa kuwasaidia watoto wetu,” anasema diwani huyo.
 
Hii ndo TANZANIA ndugu na haya yote hayawezi kutokea mahali popote duniani.Isipokuwa TANZANIA TU.eti walimu wawili.
 
Hii ndo TANZANIA ndugu na haya yote hayawezi kutokea mahali popote duniani.Isipokuwa TANZANIA TU.eti walimu wawili.KHAAA
 
kesho nao watakuwa ktk mkumbo wa kumuondoa ndalichako ktk baraza ili wapite bila kupachua ntiani,
 
Back
Top Bottom