Si ufisadi, ni urais 2015 (2) na Absalom Kibanda

Si ufisadi, ni urais 2015 (2) na Absalom Kibanda

Kipokola

Senior Member
Joined
Apr 16, 2013
Posts
175
Reaction score
93
Jumatano, Mei 22, 2013 09:53

Na Absalom Kibanda

MWAKA 2009, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Absalom Kibanda, aliandika makala katika safu yake ya Tuendeko iliyokuwa ikiutizama mwenendo wa kisiasa nchini na harakati za wanasiasa wenye majina makubwa hususan walio ndani ya chama za kujipanga kushika hatamu za dola baada Rais Jakaya Kikwete kung'atuka.

Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hizo aliyoiandika Jumatano ya Aprili 15, 2009, ambayo hadi sasa, ujumbe uliokuwa ndani yake unaendelea kuakisi hali ya kisiasa ya taifa letu na wanasiasa wetu. Kwa sababu ya umuhimu wake, tunazichapisha tena ili kuwakumbusha watanzania tulikotoka, tulipo sasa na huko tuendako.

HII ni wiki ya pili nikiwa katika mada hii inayohusu tafsiri yangu binafsi na kimsingi mtazamo wangu kuhusu mwenendo wa masuala ya siasa katika nchi hii.

Nilianza kuandika mada hii wiki iliyopita, nikieleza japo kwa muhtasari - mambo hasa yaliyokuwa yameanza kujitokeza nyuma ya pazia la vita dhidi ya ufisadi iliyoanza miaka miwili au mitatu iliyopita.

Vita hiyo ina lengo jema la kukabiliana na vitendo vinavyojumuisha ukiukwaji wa maadili ya kimadaraka ndani ya serikali, kupitia katika mtandao mahususi ndani ya chama tawala.

Makala yangu ya wiki iliyopita iliibua maswali, kebehi, furaha, hasira na changamoto kutoka kwa watu wa karibu na wa kutoka miongoni mwa watu na wadadisi wanaowakilisha makundi mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mgawanyiko huo wa kimtazamo ulikuwa mkali zaidi miongoni mwa makada wa makundi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na namna ilivyowagusa kwa namna ya kuwaumiza, kuwaridhisha, kuwaogopesha na wakati mwingine kutishia mustakabali wa kimakundi ndani ya chama hicho tawala.

Pamoja na kupokea changamoto zenye miguso inayotofautiana na kukinzana, bado ni ukweli kwamba mambo yote haya yalinitia hamasa zaidi kuendelea kuwaandikia Watanzania wenzangu wanaofuatilia mwenendo wa mambo haya, kupata fursa ya kuzifungua bongo zao na kupima kwa makini zaidi kitu hasa kilichokuwa kikiendelea katika nchi yetu hii.

Mmoja wa watu wa mwanzo kuwasiliana nami na kuijadili makala yangu alikuwa mwanahabari mwenzangu na rafiki yangu wa siku nyingi. Hivi sasa maandishi yake na kazi za kihabari anazozifanya zimemfanya ajipambanue kimatendo kuwa mwanaharakati mkubwa wa vita dhidi ya ufisadi.

Mwahabari huyo ambaye msimamo wake dhidi ya ufisadi si wa kutiliwa shaka hata kidogo, alinieleza bayana jinsi anavyosumbuliwa na hoja zangu zilizokuwa zikionyesha dhahiri kutofurahishwa na uamuzi wangu wa kuukosoa waziwazi msimamo wa baadhi ya wanasiasa wa ndani ya CCM - ambao katika siku za hivi karibuni wamejipambanua kuwa watu walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi.

Kwa maneno yake mwenyewe, pamoja na kukubaliana na msingi wa hoja yangu, mwanahabari mwenzangu huyo aliniasa kuachana na hoja hiyo, kwani ingeweza kudumaza na kufisha vita takatifu ya ufisadi ambayo kila mwananchi mzalendo alipaswa kuiunga mkono.

Katika maelezo yake, mwahabari huyo alikiri kukubaliana na ukweli kwamba msimamo wa kikundi kidogo cha wabunge wa CCM ‘waliojitoa mhanga' kuupiga ufisadi, ulichagizwa kwanza na matakwa yao ya kimakundi ndani ya chama hicho tawala na malengo yao ya kisiasa ya siku zijazo na si uchungu walio nao kwa nchi yao.

Mwanahabari huyo alikwenda mbele zaidi na kuwaita wanasiasa hao wanaharakati wa vita ya ufisadi kuwa ni mamluki au askari wa kukodiwa katika vita takatifu. Malengo ya msingi ya mamluki hayafanani kwa namna yoyote ile na wanaharakati halisi na wa kweli wa vita ya ufisadi. Na hao si wengine bali ni wanasiasa wachache wa vyama vya upinzani na wanahabari wenye mawazo huru na ya kizalendo.

Mtu mwingine aliyewasiliana nami na kujadili hoja hiyo aliniomba sana nifanye kila ninaloweza kuwalinda baadhi ya wanasiasa wa kundi hilo, akisema - japo walikuwa wakifanya hivyo kwa sababu tu ya kujitafutia umaarufu wao binafsi - bado kwa kufanya kwao hivyo angalau walisababisha baadhi ya mambo kubadilika na tatizo la ufisadi kuanza kupungua serikalini.

Lakini msomaji wa tatu wa ile makala yangu alitofautiana na hao wawili na hata mimi binafsi. Alikwenda mbele zaidi na kuuponda mtazamo wangu akisema - tena kwa kujiamini - kwamba makala yangu ilikuwa ikijaribu kuwatetea mafisadi waliolitafuna taifa hili kwa miaka mingi.

Binafsi baada ya kukaa chini na kutafakari changamoto hizo tatu na nyingine nyingi nilizotumiwa kwa njia moja au nyingine, nilijikuta nikilazimika kuzikataa na kuendelea na uamuzi wangu wa kuwaeleza Watanzania kile kilichokuwa kikitokea katika taifa hili hivi sasa.

Wiki iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa kuyataja baadhi ya majina ya watu yaliyoanza kutajwatajwa na kuhusishwa ama na urais kwa kupitia CCM au nje ya chama hicho tawala kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 au 2015.

Awali, kabla sijafikia hatua hiyo nilieleza mapema kwamba kwa hali ilipofikia sasa, kwa kiwango kikubwa (si kiwango chote), kulikuwa na nafasi ndogo kwa mtu mwingine kutoka ndani ya CCM kupata fursa ya kumng'oa Kikwete katika urais wake mwaka ujao.

Ukweli kuhusu hali hiyo ya sasa ndiyo ambayo kwa hakika iliwafanya wazee kadhaa wa CCM kwa mafungu na kwa wakati tofauti wajikute wakianza kujitokeza sasa na kujifanya wakianza kumuunga mkono Kikwete, hata kufikia hatua ya kusema eti alikuwa amefanikiwa kusimamia ipasavyo Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Ni jambo la wazi kwamba baadhi ya wazee hao au wote walifikia hatua ya kusema hivyo si kwa sababu walikuwa wakiridhishwa na namna Kikwete alivyokuwa akiiingoza serikali, la hasha, bali kutokana na matakwa ya sasa ya kimazingira na mustakabali mwema wa chama chao katika siku za usoni.

Watu wanaojua vyema siasa za kimakundi ndani ya CCM ni mashahidi wazuri kwamba, baadhi ya wazee hao ambao leo hii wamekuwa wakijidai kumuunga mkono Kikwete ndiyo hao hao, katika vikao visivyo rasmi vya majumbani mwao na katika vijiwe vyao, wamekuwa mstari wa mbele kueleza kukerwa kwao na namna serikali na hususan rais mwenyewe anavyoiendesha nchi.

Lakini kikubwa zaidi kinachoweza kuzusha maswali mengi, ni kitendo cha wazee hawa hawa ambao leo wanajifanya wakiwa mstari wa mbele kumtetea Kikwete, hata kumpa sifa za kuwa jemedari wa vita dhidi ya ufisadi kuwa na rekodi ya kufanya kila linalowezekana kwa maneno na vitendo vya kumtenganisha kabisa kiongozi huyo na kundi la makomredi zake ambao kwa namna moja au nyingine ndiyo waliokuwa nyuma ya ajenda ya sera, mwelekeo na hata uandishi wa ilani ya uchaguzi iliyomwingiza madarakani zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Huu ni unafiki wa hatari wa siasa za ndani ya CCM.

Kwa hakika kikundi hiki cha wanasiasa wanaojifanya kuwa wanaharakati wa vita ya ufisadi, ndiyo ambao baadhi yao miaka miwili tu iliyopita walikuwa wameshaanza kuhaha wakipita mitaani na kuwahamasisha wapinzani wajipange sawasawa kwa ajili ya kuwasaidia kumng'oa Kikwete wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010.

Aina hii ya wana-CCM ndiyo ambao katika mazingira ya kushangaza wakati huo walikuwa wakihimiza umoja, mshikamano, ushirikiano na ikibidi muungano wa vyama vya upinzani na baadhi yao wakafikia hatua ya kujaribu kujenga mazingira ya kuviunganisha vyama vya CUF na CHADEMA, eti ili viweze kusimamisha mgombea mmoja bora wa urais mwaka 2010.

Kama hiyo haitoshi, wanasiasa hawa wa CCM na wafadhili wao kadhaa wafanyabiashara, wakiwamo watu wazito kabisa walifikia hatua kuviunga mkono vyama vya upinzani katika harakati za kusaka ubunge wakati wa chaguzi ndogo, Kiteto, Tarime na baadaye Mbeya Vijijini.

Baadhi ya wanasiasa hao wa CCM wakiwamo wabunge, wajumbe wa Halmashauri Kuu na si ajabu Kamati Kuu (CC), walifikia hatua ya kushiriki katika mikakati ya ushindi ya vyama vya upinzani na wengine wakachangia hata fedha, kwa kiwango cha kuonyesha namna walivyokuwa na uzalendo kwa taifa lao. Kwa hakika hawa ni matapeli wa kisiasa.

Watu tunaowajua vyema wanasiasa hawa, tunaweza kusema pasipo shaka kwamba, wengi miongoni mwa wanasiasa hawa ambao leo wanajibandika ubia na Kikwete nyuma ya pazia la ufisadi, ndiyo ambao muda si mrefu uliopita walikuwa wakijaribu kujenga ushawishi ambao ungewawezesha wanasiasa wenzao wa ndani ya CCM wa aina ya Profesa Mark Mwandosya kuchukua fomu za kukabiliana na Kikwete mwakani na si kusubiri hadi mwaka 2015.

Kwa maneno yao wenyewe wanasiasa hawa, waliopokuwa wakiulizwa ni kwa nini basi walikuwa wamefikia hatua hiyo ya kumuona rais wao wa CCM kuwa ni wa kutawala katika kipindi kimoja, majibu waliyokuwa wakiyatoa yalikuwa rahisi kabisa; ameshindwa kazi.

Baada ya ajenda zao hizo kuanza kuonekana si chochote si lolote ndani ya chama chao na kisha kuonekana zikisaidia kuvijenga vyama vya upinzani ambavyo vilishaanza kupanda majukwaani na kufichua uoza wa kutisha ndani ya CCM na miongoni mwa viongozi wa serikali, vinyonga hawa wa kisiasa kwa ustadi mkubwa wakaamua kujitafutia uhalali mpya ndani ya chama chao.

Wakati wakianza kujitafutia uhalali wa kisiasa, kiuchumi na kimadaraka ndani ya chama chao, wakabaini kwamba juhudi zao hizo zilikuwa haziwezi kamwe kufanikiwa wakati wanasiasa wa aina ya Edward Lowassa, Rostam Aziz, Yussuf Makamba na Nazir Karamagi wakiwa bado na nafasi kubwa kimamlaka ndani ya chama hicho.

Zilipoibuka hoja za Buzwagi, Richmond na EPA ndani na nje ya Bunge na kugeuka kuwa ajenda dhidi ya CCM, zikiratibiwa na vyombo vya habari na wanasiasa wa kambi ya upinzani, kundi hilo la mamluki wa kisiasa wa ndani ya CCM, mara moja wakauona mwanya wa wazi wa kuanza kutimizwa kwa malengo yao ya kisiasa.

Huku wakijua kile wanachokitaka, wakapata uhalali wa kuwashughulikia ipasavyo wabaya wao wote wa kisiasa, lengo lao la awali likiwa ni kumfikia hata Rais Kikwete mwenyewe kabla ya mipango yao hiyo kuvurugwa kiufundi na mtandao wa kiusalama unaomzingira rais.

Walipobaini kwamba wamekwama kumfikia rais, haraka haraka wakatafuta kufanya naye ubia wa kimkakati, hatua ambayo kwa bahati njema, katika hatua za mwanzo, Kikwete mwenye akaonyesha dhahiri kuungana na kundi hilo.

Hatua hii ya Kikwete kuungana na kundi hili lililianza kujijenga ndani ya Bunge na nje na miongoni mwa makada viongozi na wafanyabiashara wa chama hicho tawala, ikalipa mwanya kundi hilo kuanza kujipanga upya kwa ajili ya ajenda mpya ya kisiasa ya siku zijazo.

Katika hali ya ustadi mkubwa, wanasiasa wawili wa kundi la mtandao - Samuel Sitta na Bernard Membe - wakaamua kujitanabaisha na kundi hili, wakijipenyeza na kuwaacha wabia wao wa miaka mingi - Lowassa, Rostam, Karamagi, Msabaha na wenzao wengine wengi wakishangaa.

Wakati kila mmoja miongoni mwao akitafuta kujiweka mahali salama kisiasa, Membe, mwanaharakati na mwanamtandao anayezijua mbinu za kiusalama kujiimarisha akaamua kutumia turufu yake binafsi na akajipambanua kuwa mwanasiasa anayeweza kuwa tegemeo na tumaini jipya na safi la kumrithi Kikwete, baada ya kuwaengua kina Lowassa.

PIA, SOMA:

- Absalom Kibanda (Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri) avamiwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa

 
Duniani hakuna siri

Only time will tell

Sent from my Nokia X2-01 using Jamiiforums
 
Back
Top Bottom