Siasa inaua elimu yetu!

Siasa inaua elimu yetu!

tpaul

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2008
Posts
24,225
Reaction score
22,632
SIASA NA ELIMU
Serikali yetu kwa muda mrefu imeiingiza Elimu katika siasa tasa ya Tanzania na kuuwa viwango tangu mwaka 1967. Na kuna lengo zima kwa Serikali kuisiasisha mno Elimu. Lengo lao ni kupunguza idadi ya wasomi ili waweze kuwakandamiza zaidi na kujihalailishia utawala. Na hoja yangu hii inaungwa mkono na tafiti lukuki hapa nchini hivi sasa na tangu zamani.

Mfano mzuri angalieni kisa kilichopelekea Serikali kutuwekea Sera ya lugha mbili ya Elimu hapa nchini yaani ‘Bilingual language policy’. Sera hii ni zaidi ya sera za kikoloni zilizotumika kuikandamiza nchi yoyote duniani na haijatumiwa na hata mkolini mmoja duniani katika koloni lake. Tunaitumia sisi Tanzania leo.

Kwa kurahisisha maneno, hii ni sera inayolenga kuwa Kiswahili kitumike kufundishia Shuleni, kuanzia shule za msingi na Kiingereza kitumike shuleni Sekondari. Huu kama si ujuha ni kitu gani. Ikiwa mwanafunzi amesoma na kukulia katika kiswahili tangu mdogo hadi anafika miaka 15 ndio anaanzishwa kusomeshwa kwa kizungu alichokuwa hajakilalia wala kukiamkia, miujiza hii ya lugha itaotka wapi?

Jambo lolote laanza na msingi, na ikiwa kiingereza hakikuanzwa mapema tena kwa misingi madhubuti mwanafunzi atatarajiwa wapi kukijua akifika Sekondari baada ya miaka nane ya Kiswahili? Isitoshe kwa mujibu wa tafiti, Kiingereza hakina walimu kwani hao walimu wenyewe wa Kiingereza akija mkaguzi wa Kizungu au wakimuona mzungu njiani huingia mitini wasijekuulizwa ‘Good Morning’.
Hebu leo nambieni waumini wa vitendawili; ‘Wafu kwa wafu wakokotana?’ – Jahazi na Tanga. Lakini hali hii haiji kwa mwalimu asiejuwa kitu akamfundisha mwanafunzi ajue kitu. Na hivi ndivyo Serikali ilivyotujenga. Walimu wengi wanaosomesha wametokana na mfumo huu wa elimu ya kuhifadhi midesa, kwa vile kizungu hakimo, na wakipewa ualimu huwa kama makasuku, tu maana hawakusoma wala kuelimika. Katika hali kama hii tutegemee nini?

Tatizo hasa ni Serikali, tatizo ni sera ya lugha. Nakumbuka mwaka 1978 Waziri wa Elimu bara Thabitha Siwale walijadili sana juu ya hoja hii. Ikaundwa Tume ya Jackson Makweta mwaka 1983, na ikapeleka ripoti kwa Mwalimu Nyerere kwamba Kiswahili kitumike moja kwa moja shuleni kwani Kiingereza hakisikiki shuleni. Nyerere alikataa. Miaka ya 1990 hali hii ikasemwa, hakuna mwanasiasa aliyejali. Kwanini? Wanachokifanya wanakijua vizuri. Ni kutunyima Elimu ili watunyonye na kututawala.
Mbali ya suala la Sera ya lugha, Serikali imeondosha vipaumbele vya kuisimamia na kuihudumia Elimu. Matokeo yake Elimu imefanywa kuwa Biashara badala ya haki ya lazima ya kila mwananchi. Shule za Serikali zinanuka uvundo, hazina lolote lilioko. Nani anajali, wenye nchi watoto wao husoma ng’ambo, watajuaje shida zetu hapa?

Baraza la mitihani limefanywa Biashara. Na bila haya wala aibu, wanawafelisha vijana kwa kuwapangia alama maalum wanazoamini watashajiika kununuwa tena mitihani kwa wingi ili wapate fedha zile zile za mnyonge anaekubali kukosa nguo ya kuvaa na kula vizuri kumlipia mtoto wake akasome tena. Tena bila kujua kuwa mtoto huyo atasoma lakini sio kwa kunufaika yeye bali kuwanufaisha maafisa wa baraza la mitihani wanaukanyaga mgongo mnyonge huyo kama daraja la kupitia kuelekea katika utajiri wao na familia zao.

Tunapofika hatua kama hii, tufike tukubali kuwa Serikali haina nia nzuri na wananchi wake. Na matokeo haya mabaya hakuna anaestahiki kubeba lawama asilimia mia moja na khamisni kama sio Serikali. Na bahati mbaya Serikali hata haina habari juu ya maumivu tuliyonayo dhidi ya janga hili la taifa lililotupata mwaka huu.

Tena mimi nashangaa sana Rais Kikwete ni mtu hodari sana wa kuhani, kwenda mazikoni, na kujulia wagonjwa, kwa hili tunamshukuru sana, lakini cha ajabu haoni haja kutangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka huu kuwa janga la taifa au angalau kuuita msiba wa kitaifa na kuyafuta matokeo haya kabisa. Kwa vile haoni haja wala haoni kuwa huu ni msiba na janga la taifa, tutaachaje kuamini kuwa Serikali imeyapanga haya tunayoyaona?
Natoa hoja
 
Back
Top Bottom