Date::11/19/2009Kikwete:Tusipobadilika tutakuwa watazamaji milele.
Rais Jakaya Kikwete, akiwa na kombe la dunia katika uwanja wa Taifa, baada ya kulipokea kombe hilo mjini Dar es salaam Alhamisi.Na Dorice Maliyaga
RAIS Jakaya Kikwete jana alilipokea Kombe la Dunia la fifa na Coca-Cola kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku kuwalaumu wadau wa soka kwa kukwamisha maendeleo ya mchezo hapa nchi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kupokea kombe hili Rais Kikwete alisema kuwasili kwa taji hilo ni jambo la kihistoria, imeleta changamoto kubwa kwenye maendeleo ya michezo hapa nchini.
"Kutwaa Kombe la Dunia ni ndoto ya kila mchezaji na kufika kwa taji hili Tanzania ni bahati ya pekee kwa kutimiza malengo yetu ya soka," alisema.
“Itatuchukua miaka elfu moja kabla yaTanzania kufuzu kwa kombe la Dunia kama tusipobadilika kwenye mfumo wetu wa soka,†alisisitiza rais.
Rais alishutumu shirikisho la soka la Tanzania 'TFF' kwa kushindwa kubaini vigezo vinavyosababisha kuzototesha mchezo huo hapa nchini.
"TFF iachane na tabia ya kutilia mkazo suala la mapato na ushabiki kwenye kupanga ratiba zake kama kweli wanataka kuendeleza soka."
Alisema; ''Kama TFF itaachana na mambo hayo na kutilia suala la ukuzaji wa soka ya vijana kwa kuhakikisha klabu zote zinakuwa na timu za vijana.''
Rais alilipigia vita suala la adhabu zinazotolewa na kamati zake TFF kwani kwa kiasi kubwa zinachangia kuua vipaji vya wachezaji.
"Ni jambo la kushangaza kuona TFF inawafungia wachezaji miezi sita au mitatu si sawa kawaida mchezaji angetakiwa kufungiwa michezo mitatu kama anafanya kosa kubwa."
Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa ziara ya kombe hilo kwenye uwanja wa Taifa jijini jana, Kikwete alisema kamwe Tanzania haitoweza kusonga mbele kisoka kama viongozi na wadau wote wa soka wasipokubali kubadilika.
Alisema ni lazima kufanywe jitahada za makusudi ya kujenga shule za soka kwa vijana na kuachana na tabia ya kusajili wachezaji hao wazee ambao watacheza kwa msimu amoja na mwingine huachwa kutokana na umri wake.
''Watafutwe walimu wengi wa michezo kwenye mashule, vijijini mitaani na sehemu zote ili kuwapa nafasi na kuutambulisha mchezo huo kwa wingi.''
Alisema ujio wa kombe hilo ni deni kwa Taifa kuhakikisha wanaongeza bidii na kuacha kuwa watazamaji kila siku.
Hata hivyo Kikwete alizitaka klabu kuachana na tabia ya kuwa na malumbano ya kila kukicha kwani ni moja ya sababu ya kudidimiza soka kwa kuwa zenyewe ndiyo mizizi ya fitina.
Alisema ili kuuendeleza mchezo huo lazima kupata walimu wenye uzoefu na hodari wa mpira na kuwaepuka wachambuzi wa soka uchwala ambao wao kazi yao kila siku kusubili makosa ilikukosoa.
"Tuwasikia wakisema kocha hafai kwanini asingemtumia mchezaji furani wakati hawana wanalojua."
Rais alisifu uteuzi wa vijana kwenye timu taifa ya Tanzania kwani unasaidia kuibua vipaji vipya ambao wataweza kusaidia nchi siku za usoni.
Kombe hilo liliwasili nchini majira ya saa 10:30 jioni na kupokelewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendela kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwl Nyerere kabla ya kuelekea Uwanja wa Taifa.
Kombe hilo lilopo kwenye safari ya kuelekea Afrika Kusini ilikuwa hapa nchini kwa siku mbili, leo walitakuwa visiwani Zanzibar na kesho Jumamosi ilitakuwa uwanja wa Taifa na kushudia na mashabiki mbalimbali wa mchezo wa soka hapa nchini. Watu waliojitokeza kwenye uwanja wa ndege walibaki wakiduwa wasijue nini kinaendelea baada ya ndege kuwasili, na kushitukia tayari limeshangia kwenye magari maalumu yalioandaliwa na msafara kuanza ukiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na Helkopta.
Source:Mwananchi