Siku moja Asubuhi moja Hamisi Hababi na Mimi nyumbani kwa Kanali Ayubu Simba

Siku moja Asubuhi moja Hamisi Hababi na Mimi nyumbani kwa Kanali Ayubu Simba

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
SIKU MOJA ASUBUHI MOJA HAMISI HABABI NA MIMI NYUMBANI KWA NA KANALI AYUBU SIMBA

Hamisi Hababi kama walivyo Wamanyema ni watu wa ari sana.

Hamisi anakwepa sana kuitwa msomi au kumwita mwanahistoria mzigo huu huu yeye siku zote ananisukumia mimi anitwike kichwani niubebe peke yangu.

Hamisi ana maktaba kubwa na yeye mwenyewe ni kamusi yenye miguu, inatembea.

Majuzi hapa nimeandika historia ya vijana wa TANU Abdallah Said Kassongo na Rashid Ramadhani Nyembo.

Kumaliza kuisoma tu kanipigia simu kwanza kaniambia ataniletea picha ya ujana ya Mzee Nyembo.

Hakuishia hapo.

Akasahihisha jina la mfanyabishara mmoja aliyetoa msaada kwa vijana hawa wa TANU walipopita Nzega kwenda Mwanza kwa Paul Bomani kwenda kuwachukua viongozi wa PAFMECA pamoja na Mwalimu Nyerere kuwaletea Tabora wenyewe wanasema waje kuwasalimu wananchi.

Hababi akanipa jina la yule mfanyabishara- Yahya Ahmed Al Kindy.

Haukupita muda Hamisi Hababi siku ya pili ya tatu kaniletea picha ya Rashid Ramadhani Nyembo.

Makala imekamilika wasomaji sasa wanamuona marehemu Mzee Nyembo ndani ya koti na tai alipokuwa kijana mwana TANU Youth League.

Hamisi Hababi yeye ndiyo kaniletea kitabu cha maisha ya Kanali Ayubu Simba na kunambia tuweke miadi tukamwamkie.

Nyumba ya Kanali kuanzia lango kuu kila kitu kimekaa mahali pake kwa unadhifu mtindo wa majeshi hadi unaingia ndani.

Gumzo lilikuwa tamu.
Kanali ana mengi kichwani kuliko aliyotuwekea katika mswada/kitabu.

Katueleza hicho tulichonacho ni mswada/kitabu hajakikamilisha amechapa mswada kama kitabu kutusikiliza wasomaji tunasemaje.
Sikivunjika moyo.

Nikamwambia Kanali kuwa hayo niliyosoma katika mswada yamenitia shule kusoma mengi niliyokuwa siyajui.

Mimi sikumbuki kusoma kitabu ambacho mpigania uhuru kaandika hali ilikuwaje ndani ya TANU wakati wa mapambano ya uhuru kati ya mwaka 1954 - 1961.

Pengine hata kusema kule "kuandika" si sawa kwani kimeandikwa nini kuhusu TANU hadi leo?

Saadan Abdul Kandoro kaandika, "Mwito wa Uhuru," (1961) lakini yeye kapita njia tofauti aliyochukua Kanali Ayubu Simba.

Kanali anatuhadithia kibri cha Ivor Bayldon yeye anamwita "Kaburu," kwa ule unyanyasaji wake wa Waafrika.

Kanali anazungumza kwa utaratibu sana.
Sauti yake haipandi hata anapokueleza jambo la kuchukiza.

"Bayldon anawafukuza Waafrika katika ardhi ya nchi yao Tanganyika anadai ati wanachafua maji yake kwa hiyo wahame wampishe yeye."

Utafurahi ukimsikia Kanali apoeleza vipi walivyomzunguka Mwingereza kwanza wakampiga tepe TANU ikamweka kati hana pa kutokea pale ilipokuja Kamati ya Udhamini ya UNO kupokea maoni ya wananchi mwaka wa 1957.

TANU ilimchagua Ayubu Simba kutoa maoni ya vijana.

Kanali akawa anatuhadithia mikakati na mbinu za TANU akiieleza Tanganyika kwa mfano wa nchi iliyovamiwa na adui kutoka nje.

Mkalimani wake mbele ya kamati ile alikuwa Dr. Michael Lugazia na alipokuwa anatafsiri alikuwa anapoza lugha ya Ayubu Simba na mara kadhaa akimkatisha akimwambia atumie neno stahiki asibadili amweleze Mwenyekiti wa Kamati ya Udhamini ya UNO kuwa Waingereza ni "Oppressors," 'Wakandamizaji."

Alimtaka Dr. Lugazia ayaseme maneno hayo kama ilivyokusudiwa na kuandikwa.

Kijana Ayubu Simba alikuwa na uelwea wa kutosha wa Kiingereza kuweza kuelewa mahali neno linapogeuzwa.

Nikawa najiambia mwenyewe kumbe hii damu ya vita ya Kanali kupambana kwa mikakati na mbinu za ushindi wa vita alikuwanayo toka enzi za TANU Youth League.

Inaelekea Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wa TANU waliliona hili kwa kijana wao na ndiyo wakamfungulia milango ya kuongoza mapambano.

Mbinu za mapambano kama hizi ndizo zilizomtia adabu Bayldon pale alipomuona kijana Ayubu Simba yuko bega kwa bega na Mzungu Lady Chesham kuingia LEGCO kwa tiketi ya TANU mwaka wa 1958 wakati wa Uchaguzi wa Kura Tatu.

Nasi hatukuacha mkochoza Mzee Simba kwa kumtania kumwambia, "Mbona mwanzo wa kitabu Kanali unatisha watu kwa kusema wewe kachero wa serikali?"

Mara mbili kiasi mara tatu katika mazungumzo tukimrushia haya madongo.

Hapo Kanali akawa anaangua vicheko tu na sisi sote tunacheka.

Gumzo lilikuwa tamu sana.

Anasema aliingizwa Ofisi No. 1 baada ya kutoka masomoni Czechoslovakia.
Hapa pana mengi.

Kachero Mwanajeshi.
Nikamtajia ''Comandate'' Ali Mahfudh.

''Ukisikia ''Comandante'' hiyo ni Cuba,'' Kanali Ayubu Simba alipokea.

''Tulifanyakazi pamoja kwa karibu sana alisaidia sana Kusini."

Tofauti na mara nyingi tunavyowadhania watu hawa katika tasnia ya ukachero Kanali tabasamu likiwa usoni pake alituambia kuwa wengi ni watu waungwana wenye tabia za kupendeza.

Nikamtaja Hassan Upeka.

TANU walimchukua mara tu alipomaliza masomo Tabora School mwaka wa 1956 na wakamtia TANU Intelligence.

Kanali ananisikiliza anatabasamu.

Nikamwambia ndiye aliyenifungulia milango ya Maktaba ya CCM Dodoma kufanya utafiti wakati naandika kitabu cha Abdul Sykes.

Nikamtaja Charles Mzena nikamwambia nimesoma na wanae.

Kanali akasema, "Mtu muungwana sana aliyejua kujishusha.

Kasomeshwa na Waingereza."
Nikamtaja Amri Kweyamba.

Special Branch.
Kanali akacheka.

Nilijua kwa nini alicheka.

Akatuambia, ''Amri Kweyamba alikuwa kijana wa Kihaya kasomeshwa na Waingereza.''

Kweyamba aliwanyoosha vizuri wapigania uhuru wa TANU hasa Ally Sykes.

Huwezi kuchoka kumsikiliza Kanali Ayubu Simba.


1676491355049.png

1676491415664.png
 
Back
Top Bottom