Siku moja na Prof. Taji Ahmed Muhidin rafiki mkubwa wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Siku moja na Prof. Taji Ahmed Muhidin rafiki mkubwa wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
SIKU MOJA NA PROF. TAJI AHMED MUHIDIN RAFIKI MKUBWA WA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE

Hakuna mwanafunzi wa marehemu Prof. Haroub Othman ambae hakupata kupewa rejea za Prof. Ahmed Muhidin kusoma katika kozi ya Development Studies ambayo ilikuwa ‘’compulsory,’’ lazima uisome na baadhi ya ‘’topic,’’ akisomesha yeye mwenyewe.

Nyakati hizo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kilikuwa chuo cha kuwapika vijana watakaokuja kuendeleza Tanzania na kuijenga kuwa nchi ya kijamaa kamili.

Wanafunzi wakisomeshwa vitabu vilivyoandikwa na waandishi wa fikra kali za mrengo wa kushoto za maendeleo ya watu.

Wanafunzi wakimsoma Ernest Mandel, Walter Rodney, Andre Gundre Frank kwa kuwataja wachache hawa ndiyo wale wakijulikana kama wasomi wa ‘’Ki-Marxists.’’

Nakumbuka siku moja niko London na Ahmed Rajab akanipeleka mahali akaniambia, ‘’Unaona hapo? Mwalimu wako Prof. Haroub Othman alipokuja London kwa mara ya kwanza nilimleta hapa kumuonyesha mahali ambapo Karl Max alikuwa akikaa nyakati za mchana na kuandika fikra zake.’’

Sikumbuki hata siku moja kumsikia Prof. Ali Mazrui akitajwa kwa kheri pale chuoni kwani yeye alikuwa katumbukizwa kwenye kundi la ‘’bourgeois scholars,’’ hafai kusomwa kwani ni ‘’adui’’ anaeshirikiana na wanyonyaji.

Lakini hawa wote wawili Prof. Muhidin na Ali Mazrui ni kutoka Mombasa na watu waliocheza na kukua pamoja katika mitaa ya Mombasa ya 1940s.

Si wengi wenye kujua urafiki wa Prof. Muhidin na Mwalimu Nyerere na kwa kiwango gani cha mapenzi Nyerere alimpenda Prof. Muhidin na kuwa karibu na yeye hadi alipofariki.

Hii na pia achilia mbali ukitoa duru la wasomi wa mrengo wa kushoto wa Tanzania lakini ni Watanzania wangapi wamepata kumsikia au kumjua Prof. Ahmed Muhidin.

Wengi wetu pia laiti kama si kusoma chuo cha Ki-Marxist, Prof. Muhidin tungemsikia kwa mbali tu.

Yeye mwenyewe Prof. Muhidin anawajua Watanzania wengi katika duru la siasa za kijamaa na usomi na wasomi wake.

Laiti kama nisingepata bahati ya kukutananae uso kwa uso nami kama wengi ningebaki gizani sina moja nilijualo na kwa hakika ningekuwa nimepunjika na kupitwa na mengi sana.

Nilikuwa kwenye gari ya rafiki yangu, Prof. Mohamed Khalil Timami tunaingia katika moja ya majengo yaliyopo katika viwanja vya Fort Jesus, Mombasa kuhudhuria kongamano, ‘’Swahili Literary Festival.’’

Sahib yangu mwingine Abdulaziz alikuwa kabla kesha nifahamisha kuwa Prof. Muhidin atakuwapo kwenye kongamano na atazungumza.

Nilimfahamisha kuwa namfahamu Prof. Muhidin kwani nimemsoma sana wakati nikiwa mwanafunzi na isitoshe ni ‘’ndugu wa ndugu,’’ wa mmoja wa jamaa zangu Tanzania.

Huyu ‘’ndugu wa ndugu,’’ Juma Mwapachu, mmoja wa wasomi na waandishi mahiri na ni yeye siku moja nilipomtaja Prof. Muhidin mbele yake akaniambia ni ndugu wa mkewe.

Basi tulipomkaribia Prof. Muhidin mwenyeji wangu alishusha kioo cha gari kumwamkia.

Mimi sikumpa hata nafasi ya kunitambulisha baada ya kumtokea salamu nikamwambia, ‘’Prof. Muhidin mimi ni mwanafunzi wako nimekusoma sana wakati nasomeshwa na Prof. Haroub Othman Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kwani alisema ikiwa tunataka kupasi kozi yake basi tukusome.’’

Kusikia jina la Prof. Haroub Othman, Prof. Muhidin alinyanyua mikono na kumtakia maghufira.’’

Prof. Muhidin jina langu kalisikia na kisa chake ni kuwa nimeandika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika inayomuhusu rafiki yake Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa siku tatu mfululizo nashukuru nilipata nafasi ya kumsikiliza Prof. Muhidin wenyewe watu wa Mombasa wamezoea kumwita kwa jina moja tu la ‘’Taji.’’

Hili ndilo lilikuwa jina lake toka udogoni.

Kila nilipopata fursa nilimfuata pale ukumbini nizungumzenae na nilifurahi sana pale wenyeji wangu waliponiambia kuwa baada ya mkutano nisifanye haraka ya kuondoka nibakie nyuma siku mbili tatu wanipeleke kwake Kikambala kiasi cha kama kilomita 50 kutoka Mombasa mjini.

‘’Sheikh Mohamed kuifaidi maktaba ya Taji unahitaji siku nzima kuanzia asubuhi hadi jioni na hutoimaliza ana vitu vingi sana, ’’ Prof. Mohamed Khalil Timamy alinifahamisha.

Tumemkuta Prof. Muhidin na katupokea kwa bashasha kubwa kavaa T- Shirt ya McDonald’s lakini katikati ya ile ‘’M’’ kuna picha ya V.I Lenin.

Nyumba ya Prof. Muhudin ya gorofa tatu iko ufukweni kabisa ukiwa ndani ya nyumba hiyo kwenye ukumbi wowote Bahari ya Hindi unaiona na mchanga wake mweupe.

Jirani yake pembeni kabisa alikuwa amepakana na Muyua Waiyaki aliyepatakuwa Waziri wa Nchi za Nje wa Kenya, ambae Prof. Muhidin amemsifia kwa uzalendo, ukweli wake na uungwana aliokuwanao kwa kila mtu.

Ofisi ya Profesa na maktaba yake imeenea nyumba nzima vitabu vipo kila mahali na kila unapopita na kutupa jicho vimejaa vitabu.

Vitabu ukutani, vitabu kwenye mashubaka, vitabu sakafuni kiasi ikanikumbusha shairi la ‘’Ancient Mariner,’’ nililosoma miaka mingi iliyopita kuna ubeti unasema, ‘’Water, water everywhere, nor any drop to drink...’’

Mimi nikiwa nimesimama nimezungukwa na msitu wa vitabu nikabadili nikasema,’’books, books everywhere nor empty space to see...’’

Hivi niandikavyo najishauri nianze na lipi?

Nianze na maktaba ya vitabu, muziki wa jazz au maktaba ya picha?

Nimeelewa na kuelemewa hata bado Prof. hajanionyesha kitu.

Jicho linaanguka kwenye kitabu cha Mahatma Ghandhi, Nehru, Nelson Mandela, Lord Frederick Lugard, James Baldwin, Basil Davidson, jicho halina subira linataka lione kila kitu tena kwa mara moja.

Jicho langu limerukia kwenye jazz – Abdullah Ibrahim, Hugh Masekela, John Coltrane, Wes Mntgomery, Jimmy Smith kwa kuwataja wachache.

Kabla hajawa Muislam huyu Abdullah Ibrahim kutoka Afrika ya Kusini akijulikana kama Dollar Brand.

Mwenyeji wangu alinipeleka msikiti mmoja New York, Manhattan akaniambia huu msikiti miaka ya nyuma wanamuziki Waislam ndiyo ulikuwa msikiti wao na Abdullah Ibrahim alikuwa kila akija New York kutoka Johannesburg alikuwa akiswali pale.

Jicho limerudi kwenye DVD za historia ya Kenya – Kungu Karumba, Bildad Kubai, Paul Ngei, Jomo Kenyatta hawa walikuwa katika kundi lililokuja kujulikana kama, ‘’The Kapenguria Six,’’ wapigania uhuru sita wazalendo waliohusishwa na Mau Mau.

Prof. Muhidin akataka aniweke kitako kidogo baada ya kuona nimepita kwingi na camera yangu haipigi picha tena nimebakia nimeduwaa kwani kwa hakika kama nilivyoelezwa kuwa siwezi kuimalizza maktaba ya Prof. Muhidin.

Nnilikuwa mfano wa nahodha aliyepwelewa mchangani na anaiona bahari lakini hajui vipi chombo chake atakifikisha kwenye maji.

Prof. Muhudin akanieleza uhusiano wake na Mwalimu Nyerere toka miaka ya 1960 wakati wa Azimio la Arusha na siasa ya ujamaa na akanifahamisha pia kuhusu Common Man’s Charter ya Milton Obote wa Uganda na mchango wake yeye mwenyewe Profesa kama mjamaa.

Profesa akasema, ‘’Mwalimu amenilea mimi.’’

Profesa akanionyesha picha nyingi alizopiga na Mwalimu, ‘’Mwalimu alipokuwa anastaafu alinialika na tukaonana nyumbani kwake Msasani.’’

Alinitolea picha kakaa na Mwalimu na picha wakienda nje ya nyumba wameongozana kupiga hiyo picha na picha nyingine ikiwaonyesha wanarejea ndani baada ya kutoka nje kupigwa picha.

Profesa kanionyesha cassette za hotuba za Mwalimu Nyerere kuanzia mwaka wa 1954 na akaniambia kuwa nikizisikiliza hotuba zake za mwanzo nitakisikia Kiswahili cha Nyerere akizungumza kama mtu aliyetoka bara hasa.

Profesa akanionyesha sehemu anakohifadhi hii mikanda ya hotuba za Mwalimu Nyerere.

Mikanda hii imehifadhiwa kwa unadhifu ndani ya friji kwa kuweka ubaridi maalum ili zisiharibike.

Kama ilivyokuwa haiwezekani kuimaliza maktaba ya Prof. Muhidin halikadhalika si rahisi kummaliza yeye pia.

Wakati tunashuka ngazi kuondoka kama mtu aliyekumbuka jambo akanipitisha kwenye mlango unaotokea sehemu ya wazi na kuna meza kubwa hii ni sehemu ya kupumzika kwani ukiwa hapo unaiona anga na bahari.

‘’Hii meza alikaa Juma Mwapachu aliponitembelea wakati alivyokuwa Katibu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki."

Juma Mwapachu ndiye ndugu wa ndugu niliyemtaja mwanzoni.

Tunaagana na Prof. Muhidin tumesimama nje ya nyumba yake mimi na Prof. Mohamed Khalil na kiza kimeshaingia.

Profesa akanivuta pembeni akanionyesha kontena tukaliendea na akafungua mlango wake.

Kontena zima kuanzia chini hadi juu limejaa vitabu na akaniambia kuwa humo kuna ‘’paper,’’ nyingi.

Tukaagana na Prof. Khalil alipokuwa anataka kuondoa gari nilimweleza kiasi gani safari hii kwa Profesa ilivyoniathiri kisha nikamuomba afungue dirisha nipate kumuaga tena Prof. Muhidin na kumshukuru kwa hisani aliyonifanyia na kuniruhusu niandike kitu kuhusu yeye na nitumie picha zake.

“Prof. uniwie radhi ikiwa nitakuwa ninakuambia neno ambalo kwangu alistahiki kukuambia wewe. Prof. sithubutu mimi kukuambia kuwa wewe hujui thamani ya hazina hii uliyokuwanayo na umenionyesha hii leo. Unazo kumbukumbu adimu sana na najua kuwa unajua thamani yake huhitaji kuelezwa na mimi thamani ya vitu ulivyokuwanavyo. Profesa nakusihi uandike kumbukumbu zako ikiwa hujaandika.’’

Prof. aliniangalia usoni huku anatabasamu, ‘’Mimi sitaandika kumbukumbu zangu kwani napenda mimi niwaandike wengine si kujiandika mimi.’’

Majibu haya nimeyazoea.

Tuliagana kwa mara nyingine na mimi na Prof. Khalil tukaondoka Kikambala kiza kimeshaingia huku tukisindikizwa na sauti ya mbwa wakali wa Prof. Ahmed Muhidin wanaolinda nyumba yake.
 

Attachments

  • PROF. MUHIDIN NA LENIN.jpg
    PROF. MUHIDIN NA LENIN.jpg
    71.4 KB · Views: 7
  • PROF. MUHIDIN MAKTABA.jpg
    PROF. MUHIDIN MAKTABA.jpg
    82.8 KB · Views: 6
  • PROF. MUHIDIN NA MWALIMU.jpg
    PROF. MUHIDIN NA MWALIMU.jpg
    22.3 KB · Views: 7
Mzee wangu Mohamed Said
Naomba uniambie picha hii ilipigwa wapi na mwaka gani na lilikuwa tukio gani.

Samahani kwa kuwa nje ya mada

View attachment 1386342View attachment 1386342
Dos...
Hao ni Sheikh Sayyid Omari Abdallah maarufu kwa jina la Mwinyibaraka na Mwalimu Julius Nyerere.

Sina zaidi ya haya.

Leo anafanyiwa kisomo Zanzibar soma ujumbe:

*TAARIFA YA HAUL*
Mnaarifiwa Haul ya Syd. Omar Abdalla (Mwinyi Baraka) siku ya *Ijumaamosi* 14/3/2020, mara tu baada ya Swala ya *Magharibi* Msikiti wa *Sharifu Aboudu.* Mnaombwa kuswalia Magharibi msikitini hapo.
Wabi Llah Taufiq.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Shukran sana Alhabib Mohamed Said

Dos...
Hao ni Sheikh Sayyid Omari Abdallah maarufu kwa jina la Mwinyibaraka na Mwalimu Julius Nyerere.

Sina zaidi ya haya.

Leo anafanyiwa kisomo Zanzibar soma ujumbe:

*TAARIFA YA HAUL*
Mnaarifiwa Haul ya Syd. Omar Abdalla (Mwinyi Baraka) siku ya *Ijumaamosi* 14/3/2020, mara tu baada ya Swala ya *Magharibi* Msikiti wa *Sharifu Aboudu.* Mnaombwa kuswalia Magharibi msikitini hapo.
Wabi Llah Taufiq.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Shukran sana Alhabib Mohamed Said

Dos...
Hao ni Sheikh Sayyid Omari Abdallah maarufu kwa jina la Mwinyibaraka na Mwalimu Julius Nyerere.

Sina zaidi ya haya.

Leo anafanyiwa kisomo Zanzibar soma ujumbe:

*TAARIFA YA HAUL*
Mnaarifiwa Haul ya Syd. Omar Abdalla (Mwinyi Baraka) siku ya *Ijumaamosi* 14/3/2020, mara tu baada ya Swala ya *Magharibi* Msikiti wa *Sharifu Aboudu.* Mnaombwa kuswalia Magharibi msikitini hapo.
Wabi Llah Taufiq.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Nyerere aliwapenda sana waislamu, alikuwa karibu na Rashid Kawawa kupita viongozi wengine wote, Nyerere alitaifisha shule za miission, ili watanzania wote bila kujali dini zao wasome.
 
Back
Top Bottom