KWELI Simba kutoka hifadhi ya Taifa ya Ruaha wamevamia Makazi ya Watu Mkoani Iringa

KWELI Simba kutoka hifadhi ya Taifa ya Ruaha wamevamia Makazi ya Watu Mkoani Iringa

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Mkoa wa Iringa umekumbwa na sintofahamu kubwa baada ya kuenea kwa taarifa zinazodai kuwa baadhi ya Vijiji vya kwenye Mkoa huo vimevamiwa na Simba wanaokula mifugo na kushambulia watu.

Lion_(Panthera_leo)_(30941994012).jpg


Baadhi ya watu wameanza kuogopa kutembelea mkoa huo na wengine wakitaka kujua ukweli zaidi juu ya suala hili.

Tusaidieni kuthibitisha taarifa hizi.
 
Tunachokijua
Habari za kuonekana kwa simba kwenye Mitaa ya Mkoa wa Iringa zilianza kusambaa Juni 13, 2023 baada ya Wanakijiji wa Kata ya Maboga kulalamikia uwepo wa Wanyama hao wanaotajwa kutoroka kutoka kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Madai haya yalivuma zaidi Juni 19, 2023 baada ya kuripotiwa kuwa Vijiji 3 vya Magunga, Kiponzero na Makongati vilivamiwa, ambapo Simba hao walikula Ng’ombe 13, Nguruwe 1 na kuku 1.

Mkuu wa Mkoa athibitisha uwepo wa Simba kwenye Makazi ya Watu
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama Mkoa akiambatana na wajumbe wa kamati hiyo, Juni 21, 2023 alithibitisha uvamizi wa Simba hao. Alisema;

“Kuanzia tarehe 13 mwezi huu wa 6 ambao Wanyama hao waliingia katika Kijiji cha Magunga na wakaleta athari katika mifugo yetu ambayo wananchi hao wanafuga.

Na kuanzia tarehe hiyo na kuendelea, hawa Wanyama wamekuwa wanatembea, wanazunguka, kwa sababu wakiingia kwenye zizi wakileta uharibufu, wakiua Wanyama, wananchi wanaingiwa na taharuki wanapiga kelele kwa hiyo Wanyama wanaondoka”


Mkuu huyo wa Mkoa alielezea pia sababu ya simba kuzunguka ni kutafuta chakula, na walikuja kwenye mazingira yasiyo rafiki sana.

Hadi kufikia Juni 21, 2023, Simba hao walikuwa wamefika eneo la Tanangozi.

Aidha, mnamo Juni 27, 2023, Mtumiaji mmoja wa Mtandao wa twitter aliweka chapisho lake linalothibitisha pia iwepo wa Simba hao linalosema “Iringa tunaishi na Simba kama ndugu”. Chapisho hilo linaonesha kupokelewa kwa hisia tofauti na wachangiaji ambapo mmoja wao alisema “Kaja kutoa gwala”

Siku hiyo hiyo, mtumiaji mwingine wa Mtandao wa Twitter aliweka chapisho lingine linalodokeza uwepo wa simba hao. Linasema;

“Wiki 2 sasa, wakazi wa Iringa tunaishi kwa taharuki kufuatia uwepo wa kundi la Simba lililotoroka hifadhini na kuingia kweye makazi ya watu. Wameshadhuru wanyama wengi ikiwemo ng'ombe 33! Mungu saidia hakuna madhara kwa binadamu yaliyoripotiwa mpaka sasa”

Watu hawa wote walitumia video moja kuonesha tukio husika. JamiiForums imebaini kuwa video hiyo haihusiani na tukio la Simba wanaoonekana kwenye vijiji vya Iringa, lakini ujumbe wao ulikuwa sahihi kwa mantiki ya uwepo wa Simba hao. Hii inaweza kuthibitishwa kwa kurejea kauli ya Mkuu wa Mkoa.

Jitihada za kukabiliana na tatizo hili
Jumatatu ya Juni 26, 2023, Gazeti la Mwananchi liliripoti kuwa Serikali ya Kijiji cha Lupembe Lwa Senga, Kata ya Lyamgungwe, wilayani Iringa ilikuwa imetoa rai kwa wananchi kurudi majumbani kwao ifikapo saa 11 jioni wakati jitihada za kumtafuta mnyama huyo zikiendelea.

Kwenye mahojiano hayo, Mwananchi mmoja anayefahamika kwa jina la Ezekiel Mhhehe alinukuliwa akisema;

“Kijijini kwetu wamekula ng’ombe wawili, tunaomba jitihada ziongezeke kwa kweli tunaogopa sana, tunachofanya nikuwasisitiza wananchi watulie majumbani hasa kuanzia saa 11 jioni. Na kweli ikifika muda huo humkuti mtu mtaani”

Hata hivyo, siku moja kabla ya ripoti hii, Juni 25, 2023, Hifadhi ya Taifa Ruaha tayari ilikuwa imeanza kutumia helikopta kuwasaka wanyama hao.

Mkakati wa Serikali kupambana na Wanyama wakali na Waharibifu
Mjadala huu ulipata pia nafasi ya kujadiliwa Bungeni Jumatatu, Juni 26, 2023.

Akijibu Swali la Mbunge wa Viti Maalum Grace Tendegu aliyehoji hatua za serikali katika kudhibiti uvamizi wa simba katika baadhi ya maeneo mkoani Iringa, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja alisema Serikali tayari ilikuwa imepeleka helkopta ya kuwasaka Simba hao kwa lengo la kuwachukua na kuwarudisha katika maeneo yao husika huku akiwaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kutotembea usiku sambamba na kwa wafugaji kuwasha moto kuzunguka maeneo ya mifugo wao.

Waziri Masanja alisema pia miongoni mwa mipango ya Serikali katika kupambana na wanyama wakali ni kujenga fensi na kujenga vituo vitakavyosaidia kupambana na wanyama hao.

Afisa hifadhi azungumza
Akizungumza na Mwananchi Digital, Afisa Uhifadhi daraja la pili Said Stuard alisema miongoni mwa mbinu zingine zinazotumika kuwasaka Simba hao ni kutumia Mbwa aliyepewa mafunzo maalumu anayeitwa Mayele. Alisema;

"Uwezo wa mbwa Mayele umetusaidia kuona njia aliyopita Simba na watoto wake, na tumefanikiwa kuwaona,”

“Alikuwa na watoto wadogo katika msitu, njia inayoelekea kijiji cha Makongati japokuwa tumeshindwa kumdhibiti kutokana na mazingira, maana kuliwa na wananchi; hivyo kwa kuhofia usalama wao tukashindwa.”


Hivyo, JamiiForums inakubaliana na madai yanayosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii yanayoeleza kuwa baadhi ya maeneno ya Mkoa wa Iringa yamevamiwa na Simba.
Back
Top Bottom