Simba sasa yaituhumu uchawi yanga
Na Erasto Stanslaus
UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa, mchawi namba moja wa kuihujumu timu yao ni mchezaji mmoja wa Yanga ambaye anatumika kuwashawishi wachezaji wao kutokana na ukaribu wake na wachezaji wa klabu hiyo.
Simba imekuwa na matokeo mabaya katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na matokeo hayo yanahusishwa na hujuma kupitia kwa baadhi ya wachezaji.
Kutokana na hali hiyo, inadaiwa timu hiyo imewafukuza wachezaji wake wawili, Emmanuel Gabriel na Ramadhani Wasso huku ikiwaweka katika wakati mgumu wengine watatu Henry Joseph, Mussa Hasan 'Mogosi' na Amani Simba wakisubiri kujadili adhabu ya kupewa.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo, mchezaji huyo amekuwa akitumiwa na watani wao wa jadi kuwashawishi wachezaji hao kwa lengo la kuihujumu timu yao.
Chanzo hicho kilisema kwamba, tatizo hilo wameligundua na kuchukua hatua ikiwa pamoja na kuwafukuza wachezaji wawili na wengine wakiendelea kuchunguzwa kabla ya kutolewa adhabu.
Chanzo hicho kiliendelea kupasha kuwa, lengo kubwa la watani wao wa jadi ni kutaka kuivuruga timu yao ambayo imeonekana kuwa na uwezo mkubwa kulinganisha na wao ili kutoweza kuchukua ubingwa katika msimu huu.
"Ujanja wao tumeugundua na hawatafanikiwa kwani tayari tumeng'oa mizizi yao kwa kuwaadabisha wachezaji hao na malengo yao hayatatimia," kilisema chanzo hicho.
Baada ya kumaliza matatizo hayo, kikosi chao kinatarajiwa kuwa katika hali nzuri ya ushindani kama walivyokuwa katika michezo ya mwanzo
Simba waligundua hujuma hizo kabla ya mchezo dhidi ya Polisi Dodoma ambapo wachezaji walioihujumu timu hiyo walikuwa wamepangwa katika kikosi cha kwanza siku hiyo walivuliwa jezi muda mfupi kabla ya mchezo kuanza.
Majira 24 sept 08