Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi : ELIZABETH NEVILLE
Mwandishi : HALFANY SUDY
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
Ni asubuhi na mapema ndani ya mji wa Mafinga uliopo mkoani Iringa, Tanzania. Baridi likiwa kali sana. Watu walikuwa wanatembea mitaani huku wakiwa wamevaa makoti makubwa kupambana na baridi hiyo.
Katika hoteli moja iliyopo katika mtaa wa Pipeline ndani ya mji huo kulikuwa na kikao cha siri cha watu wawili. Saa tatu sasa walikuwa wanapanga mikakati yao.
"Sasa Martin fanya juu chini umpate Elizabeth Neville, ni yeye pekee ndio anajua kila kitu kuhusu mimi, na nina hakika endapo atathubutu tu kusema basi nimeangamia na ndoto yangu ya kuja kuwa rais wa Tanzania itakuwa imefikia kikomo." Lucas alisema kwa sauti ya upole na kusisitiza.
"Usiwe na hofu yoyote Mheshimiwa Lucas. Mimi ndiye Martin, sijawahi kushindwa kazi yoyote ile.
Ukiwa na tatizo lolote lile jua lifikapo kwa Martin limekwisha. Nipe siku tatu tu nitakuletea Elizabeth Neville mikononi mwako na utaamua mwenyewe nini cha kumfanya. Nakuhakikishia siri yako haitotoka katika mdomo wa Elizabeth Neville kwenda katika sikio lolote lile lingine hapa duniani." Martin alisema kwa kujiamini.
"Nakuamini Martin Hisia. Sasa nakupa hizi milioni kumi za awali, na nitakupa milioni kumi na tano baada ya kukamilisha kazi hii. So milioni ishirini na tano ulizozihitaji zitakuwa zimekamilika" Lucas alisema huku akimkabidhi Martin bahasha yenye milioni kumi. Martin alizipokea, wakaagana
"Huyo Elizabeth Neville atakuwa anaijua siri gani ya waziri?. Maana kumpeleka kwake hiko kiumbe dhaifu tu katoa milioni ishirini na tano. Nitaifanya kazi hii siku mbili tu ili animalizie milioni zangu kumi na tano nilale mbele." Martin aliwaza akiwa ndani ya gari yake.
"Namwamini sana Martin atakamilisha hili kwa ufanisi mkubwa. Jamaa anaonesha yupo makini sana kazini. Huu ndio utakuwa mwisho wa Elizabeth Neville na marecord yake, na safari ya kuelekea ikulu itakuwa nyeupee" Lucas alikuwa anawaza.
Martin alirejea katika nyumba yake iliyokuwa katika mtaa wa Pareto. Alipiga honi na mlinzi wake alifungua geti. Baada ya kushuka garini alimsalimia mlinzi wake na moja kwa moja aliingia ndani. Alienda katika chumba chake anachotunza zana zake za kazi, akachukua bastola yake pekee na kuiweka kiunoni vizuri akiifunikia na shati.
"Sihitaji kubeba zana nyingi, hii ni kazi ndogo ingawa malipo yake ni makubwa sana" Martin aliwaza.
Alitoka nje na kuondoka na gari yake ndogo aina ya Toyota vitz. Naenda kumchukua Elizabeth Neville, akijifanya mjuaji naitoa roho yake mara moja. "
Dakika ishirini baadae ilimkuta Martin mbele ya nyumba akiyoishi Elizabeth Neville. Nyumba kubwa na nzuri iliyokuwa katika mtaa wa Kinyanambo.
"Bila shaka hii ndio nyumba ya Elizabeth Neville" Martin alisema wakati akishuka garini.