Simulizi: For You

Pole sana Mkuu Elton Tonny, we are glad that you are back. Tushushie vitu. Najenga picha ya Kendrick Jabari namfananisha na Ben Carson haiba yake. [emoji2][emoji2][emoji2][emoji2]
 
Dah Elton Tonny kutokea tarehe 24 mpaka tarehe mbili hola[emoji849][emoji849][emoji849] Mbn mwanzo ulianza fresh Mkuu ila sa hiv imekuwa kipengeleee[emoji2955][emoji2955][emoji2955][emoji2955][emoji2955] Anyway akitumaa mnishtue wacha nikazunguke kwenye majukwaa mengine ya JF
 
FOR YOU

Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

SEHEMU YA AROBAINI NA SABA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…


Baada ya Nora kuwa ameambiwa kila kitu na kundi la Mess Makers na kujiweka upande wao, Torres alimwonyesha ushahidi ule ili kuthibitisha zaidi mambo aliyosema. Alimwonyesha video kadhaa, rekodi za sauti, na makablasha mbalimbali yalioonyesha ukweli wa mambo aliyosema. Nora sasa aliweza kuona ni jinsi gani Raisi Paul Mdeme na wenzake walivyokuwa wanyonyaji, walaghai, wakatili, na wauaji wakubwa. Alichukizwa sana kujua kwamba baba yake alikuwa mwovu kupita jinsi alivyomchukulia, na hii ikaongezea nguvu nia yake ya kutaka kukomesha maovu hayo kwa kuisaidia timu hii ya Kendrick Jabari.

Torres ndiye aliyekuwa akimwelekeza Nora mambo mengi kuhusu yale waliyofanya na yale watakayofanya. Alimfundisha vizuri njia yao ya kufanya mambo, na uzuri wa Nora ni kwamba alishika vitu upesi sana, hivyo Torres hakuhitaji kuelezea mambo mengi kupita kiasi. Jambo muhimu zaidi baada ya kumwonyesha Nora njia zao lilikuwa ni kumjulisha kuhusu mpango wao ambao ungefuata, yaani, kuzisambaza pesa zote kwa wale walionyonywa na utawala wa Mdeme.

Nora alipata kujua sasa kwamba pesa zile zilizoibiwa na kundi hili zilikuwa zikipelekwa kidogo kidogo kwenye zile kampuni za kibinafsi za Kendrick, kule Geita na Dar es Salaam. Kumbe wakati huu wote waliokuwa wanautumia kufanya mambo mengine na visa mbalimbali kutokea, Kendrick alikuwa akizipitisha pesa zile kwenye mifumo yake halali ya kampuni zake, na hasa kwa sababu ziliunganishwa moja kwa moja na makampuni ya nchi za nje, hakusumbuliwa na serikali hii hata kidogo.

Siku ile Kendrick alipokuwa amekwenda Dar kwenye kampuni yake na kukutanishwa na Azra kwa mara ya kwanza, utakumbuka Torres alikuwa akifanya taratibu fulani huko, na hizo zilikuwa ni kuziweka pesa zote walizokuwa wameshaziweka kwenye mifumo yao tayari ili kuanza kuwasambazia watu walioibiwa. Kwa kipindi kirefu, tayari Torres alikuwa ameshatafuta taarifa zote za watu walioibiwa na kuishi maisha ya hali ya chini kwa sababu ya kunyonywa na serikali ya Mdeme, naye akawa ameziunganisha akaunti zao zote kwenye mifumo yake, akapiga hesabu ya kiasi ambacho KILA MMOJA wao alistahili kurudishiwa, na kuiweka mitambo tayari ili akituma tu, wote wanapata.

Sehemu hiyo ya mpango huu ilikuwa imeshakamilika lakini baada ya hitilafu zilizojitokeza kwa kusababishwa na Kevin, wakawa wametulia kwanza mpaka wakati ambao wangeona ni mzuri wa kupiga hatua hiyo. Nora kuwa pamoja nao sasa ndiyo uliokuwa wakati mwafaka. Kwa kuwa alijua vitu vingi pia, alimsaidia Torres kuuboresha zaidi mfumo huo, huku akiwa amevutiwa sana na ustadi wa hali ya juu wa mwanaume huyo.

Kwa sababu sasa hivi walikuwa wamejulikana hadharani, Kendrick alikuwa amebuni njia mpya ya kuweza kufanikisha mipango yao hiyo. Alijua kampuni zake zingekuwa zikichunguzwa baada ya yeye kutambulika, lakini hiyo haikumaanisha kwamba vyombo vya usalama vingeweza kuzifungia akaunti zao kutokana na yeye binafsi kuwa mmiliki. Kwa hilo ingehitajika labda akamatwe kwanza, lakini kwa kuwa hakuna mtu aliyejua alikokuwa, mpango huu mpya ungepiga tiki tu.

Nora alionyesha kuafikiana na mpango huu mpya, akisema kwamba yeye pia angejitoa vilivyo ili kuhakikisha wanafanikiwa; na hata kama wasingefanikiwa, basi haingekuwa kazi bure kwa kuwa angeridhika tu kujua amepigania upande ulio sahihi kwa njia kubwa.

β˜…β˜…

Basi, baada ya muda fulani, Nora akawa akimsaidia LaKeisha kutengeneza vyakula kwa ajili ya jioni. Kula jioni ilimaanisha kabla ya giza kuingia, kwenye mida ya saa 12, na ilikuwa kawaida ya Mess Makers kula kwa pamoja asubuhi, mchana, na hiyo jioni, ingawa mtu mmoja mmoja angeweza kujipatia chakula muda wowote aliotaka, hivyo kuwa huru kuchukua ambacho kilikuwa kimeshatengenezwa na kula kibinafsi.

Ingawa wanawake hawa wawili hawakusemeshana sana, LaKeisha kwa kiasi fulani alipendezwa na roho ya ujitoaji ya Nora, hivyo walifanya kazi kwa ushirikiano mzuri. Nora alianza kuuona utu mzuri wa LaKeisha alipotambua kwamba angalau sasa mwanamke huyo alikuwa anamtendea kwa njia yenye staha, ingawa hakujiachia sana kwake. Kwa hiyo akawa anajitahidi kumsemesha jambo moja na lingine ili kujenga hali nzuri zaidi baina yao.

Walipomaliza kutengeneza vyakula, LaKeisha akamwacha Nora sehemu ya jikoni akiwa anapangilia mambo vizuri. Akiwa anaangalia-angalia mboga walizopika, Nora alianza tena kutafakari mambo yote yaliyotokea na ambayo yangetokea muda si mrefu. Alimuwaza pia mdogo wake, Asteria, ambaye bila shaka kufikia wakati huu angekuwa amemtafuta sana, lakini kwa usalama wake, Nora alijua hangetakiwa kujaribu kumtafuta.

Akiwa amesimama karibu na sehemu ya kuwekea vyombo wakati huu, akahisi kiuno chake kikishikwa na mikono kutokea nyuma yake, na hii ikamshtua kiasi. Lakini hakugeuka nyuma kabisa kwa sababu alijua ni Lexi baada ya kuivuta harufu yake nzuri, naye akatabasamu kwa hisia huku akiangalia upande wa bega lake baada ya mshtuko huo kugeuka kuwa msisimko mzuri. Lexi alikuwa ameubana mwili wake nyuma ya mwili wa Nora, akiweka uso wake karibu na sehemu ya nyuma ya shingo ya mwanamke huyu, naye Nora akaishika mikono ya Lexi iliyokuwa kiunoni kwake.

Lexi akaibusu shingo laini ya Nora, naye Nora akafumba macho taratibu.

"Chakula kinanukia vizuri sana," Lexi akasema kwa kunong'oneza.

"Siyo kama wewe," Nora akaongea kwa sauti ya chini.

Lexi akatabasamu na kumbusu tena shingoni.

Nora akageuka taratibu na kuipitisha mikono yake kiunoni kwa Lexi kumkumbatia, akilaza uso wake kifuani kwake kama mtoto anapomkumbatia mzazi anapohisi kuogopa. Lexi akawa anasugua-sugua mgongo wa Nora taratibu, akihisi pia kwamba Nora alikuwa akificha hisia fulani hivi. Akakishika kichwa chake na kukitoa kifuani kwake taratibu na kumwangalia usoni, nao wakawa wanatazamana kwa ukaribu. Lexi alimzidi Nora urefu kwa kama inchi mbili za macho, hivyo Nora akiwa ameilegeza shingo yake kwa nyuma Lexi akawa akimtazama kama anamwangalia kutokea juu huku bado amekishika kichwa chake.

"Vipi?" Lexi akauliza.

Nora akatikisa kichwa kuonyesha hakuna kitu.

"Tell me. Unawaza nini?" Lexi akauliza.

Nora akashusha pumzi na kusema, "Asteria."

"Ndiyo nani?" Lexi akauliza.

"Mdogo wangu," Nora akajibu.

"Mpenda bata?"

"Ahah... yeah..."

"Natumaini itafika siku nikutane naye... tufahamiane," Lexi akasema.

"Anakujua," Nora akamwambia.

"Ananijua? Unamaanishia kwa sababu sasa hivi nimetambulika publicly?"

"Hapana. Alishawahi kukuona kitambo... wewe na Oscar..."

Lexi akakaza macho yake kimaswali.

"Walikuwa wanatoka pamoja. Lakini Asteria hakujua kuhusu Oscar... na inaonekana Oscar hakujua kuhusu yeye kuwa mdogo wangu. Au, inawezekana alijua? Ilikuwa ni sehemu ya mipango ye..."

"No, hapana. Sikujua kuhusu hilo. Oscar alikuwa na mizunguko mingi sana, huenda walikutana tu kawaida," Lexi akasema.

"Alikuwa anampenda sana. Kifo chake kilimtikisa mno Aste. Nilipokuja kujua hilo, nilihisi ni kama mimi ndiyo nilisababisha," Nora akasema.

"Hey... usiwaze hivyo. Look... tuna muda mchache sana hapa kabla ya kuianzisha mipango yetu. Naomba tutumie muda huo... ku-enjoy pamoja badala ya kustress sana, okay?" Lexi akasema.

Nora akabaki kumtazama tu machoni.

"Unaonaje mheshimiwa?" Lexi akauliza.

Nora akatabasamu, kisha akamkumbatia tena mpenzi wake. Akiwa amemkumbatia bado, Nora aliweza kumwona Isiminzile sehemu ya mlango wa kuingilia ndani hapo, akiwa amesimama kwa njia ya kujibanza kama mtu aliyekuwa anasikiliza maongezi yao, na baada ya Isiminzile kutambua kuwa Nora alimwona, akaamua kujitoa hapo na kuingia. Nora akalivunja kumbatio lake na Lexi taratibu na kumwonyesha kwa ishara ya macho kuwa kuna mtu anakuja nyuma yake, naye Lexi akageuka na kumwona Isiminzile pia.

"Samahani jamani kwa... kuwasumbua," Isiminzile akasema.

"Haina shida bro. Vipi?" Lexi akamsemesha.

"Nilikuwa naomba unisaidie hapa. Hiki kifaa sijui jinsi ya kukitumia, nilifikiri ni kama Bluetooth lakini kila nikiunganisha na subwoofer ndogo haki...." Isiminzile akawa anaongea huku anampatia Lexi kifaa fulani kidogo.

"Ohohoo... no, no, siyo kama Bluetooth. Una-slide tu hii sehemu halafu unakipachika nyuma ya sikio. Kina-sense tu wakati utakapounganisha flash na subwoofer kwo'...."

Lexi akiwa anamwelezea Isiminzile, Nora akawa anamtazama sana mwanaume huyo, naye Isiminzile akawa anamwangalia kwa macho ya kuibia-ibia.

"Aaa... asante sana. Ingawa nafahamu vitu fulani vya teknolojia lakini bado kuna mambo mengi sijaona," Isiminzile akamwambia Lexi baada ya kuelezewa.

"Sema tu ni ushamba dogo," Lexi akatania.

Isiminzile akacheka kidogo, kisha akamshukuru na kuanza kuondoka.

Lexi akamgeukia Nora na kukuta anamwangalia Isiminzile kwa umakini sana, naye akajiuliza ni kwa sababu gani.

"Hey... don't look at his ass (usiangalie kalio lake)," Lexi akasema kiutani.

Nora akatabasamu na kumwangalia usoni.

"Vipi?" Lexi akauliza.

"Huyo kaka... sijui tu ni kwa nini lakini ananipa chill za kushoto sana," Nora akasema.

"Unamaanisha nini?"

"Alivyo tu. Anafanya ionekane kama ni mtu mpole na mstaarabu ila kila nikimwangalia inakuwa ni kama anaficha jambo fulani..."

"Ahahah... hiyo ni Nora sense inafanya tingling yake au siyo?"

Lexi akatania namna hiyo, lakini Nora akabaki kumwangalia tu kwa umakini.

"Okay. Isiminzile ni rafiki tokea zamani. Yuko namna hiyo tokea nilipomjua na angalau naweza kusema sasa hivi amekua. Kipindi hicho alikuwa mwoga sana, alikuwa hajichanganyi na watu kabisa. Ni sehemu tu ya utu wake, lakini ni mtu mzuri," Lexi akasema.

"Ana familia yake?"

"Aliniambia yuko mwenyewe kabisa sasa hivi..."

"Haikushangazi sana kwamba out of nowhere amekuja tu na kukupa aid wakati huu mgumu?"

"Unataka kusema kwamba anaweza kunisaliti?"

"Inaweza ikawa siyo hivyo, kwa kuwa naelewa hilo juu yangu ni kubwa kuliko hata yeye..." Nora akatania.

Lexi akacheka kidogo.

"Nachomaanisha tu ni kwamba... yeye kujitoa na kuwa hapa, akijua kabisa aina ya hatari inayowazunguka... yaani... naona kama ni zaidi ya kuwa rafiki tu ndiyo kitu kinachofanya ajitoe namna hiyo. Yuko aware kwamba atapoteza vitu vingi sana lakini bado kachagua kuwa nawe na kuyaacha maisha yake ya kawaida... nahisi kuna kitu kingine kinamsukuma, na ni kama hakwambii," akasema Nora.

Lexi akabaki kutabasamu.

"Nini?" Nora akauliza.

"Nothing. Ni kwamba tu kila kitu ulichosema kinaendana na mtu fulani hivi nayemjua," Lexi akasema.

Nora akatabasamu na kutikisa kichwa taratibu huku akiangalia pembeni.

"Ahahah... usijali. Nitatafuta njia kuhakikisha namlinda Isiminzile, lakini nakuhakikishia yeye siyo mtu wa kuleta shida kwetu," Lexi akasema.

"Sawa," Nora akakubali.

Lexi akaanza kuyachezea mashavu ya Nora taratibu, naye Nora akajisogeza karibu yake zaidi ili ambusu.

"Hey lovebirds," LaKeisha akaingia na kuwakatisha.

"Ah... muda mwafaka," Lexi akamwambia.

"Save it for later. Ni vizuri umejileta, tusaidie kuandaa vyakula," LaKeisha akasema huku akifata vyombo.

Nora na Lexi wakaanza kusaidiana naye kuandaa vyombo na kuviwekea vyakula kwa ajili ya mlo huo wa
jioni, na baada ya hapo wakaziandaa meza za vyakula na kuwaita "wanafamilia" wengine ili wapate chakula kwa pamoja.


β˜…β˜…β˜…β˜…


Msako maalumu wa kuwatafuta Mess Makers usiokuwa na matokeo mazuri bado uliendelea. Ndani ya wiki yote ya kwanza iliyoisha tokea Lexi alipowatoroka wanajeshi mpaka kufikia wakati ambao Nora alifanikiwa kumpata Lexi na kujiunga naye, timu za kijeshi na maaskari hazikuwa zimebaini wapi watu hawa walipokuwa.

Raisi Paul Mdeme, angalau kwa wakati huu alikuwa amefanikiwa kujiingiza kwenye mifumo ya utajiri na mali za Salim Khan kwa ulaghai wake, hivyo kwa kiasi fulani aliweza kuongeza nguvu yake iliyokuwa imepotea. Alitumia mbinu mbalimbali kujaribu kuonyesha kwamba bado alikuwa na uwezo wa kuuinua uchumi wa nchi ingawa walikuwa wamepata hasara kubwa kutokana na wizi wa Trillioni 20. Benki zingine kubwa kubwa za kibinafsi zilimpatia mchango wa kuyatimiza masilahi yake, na bado aliendelea kusisitiza kwamba Mess Makers wangekamatwa tu.

Jenerali Jacob pia, alikuwa amesambaza watu wake maalumu nchini kufatilia mambo kwa umakini sana ili kuwafikia maadui wake wale. Alikuwa akifanya hayo sambamba na Luteni Jenerali Weisiko, na moja kati ya makundi yake hayo ndiyo lile lililoifikia nyumba ya maficho ya Mess Makers usiku uliotangulia. Watu wake walikuwa hatari na wenye kasi sana, ingawa kwa Mess Makers tayari walikuwa wamefeli. Kwa hiyo dhumuni lao likawa pale pale, kuwakamata haraka isivyo kawaida, hasa kwa kuwa wawili hawa walitaka sana kuwamaliza maadui zao na kuwarudisha mabinti zao; Nora, na "Mary," yaani Azra.

Timu iliyokuwa chini ya mwongozo wa Kanali Oswald na Luteni Michael iliendelea na tafiti zake pia, lakini wakati huu nusu ya timu hii walikuwa Geita, na wengine upande mwingine wa jiji la Dar es Salaam, isipokuwa Luteni Michael na Bobby pekee. Manengo, Alex, Mario, na Rachel ndiyo waliokwenda Geita, huku Tariq, Zachary, Hussein, na Aliyah wakiwa upande huo wa Dar. Walikuwa wamejigawa namna hii tokea siku kadhaa nyuma, na wote walikuwa sehemu zile zilizokuwa na kampuni za kibinafsi za Kendrick Jabari zilizohusiana na madini.

Walikuwa sehemu hizo wakifanya uchunguzi mwingi, pamoja na maaskari na wapelelezi wengine kutokea vitengo maalumu. Habari zozote ambazo zingekuwa na faida kwao kuwasaidia kupiga hatua fulani katika msako huu zilikusanywa na kuchunguzwa, kisha wangemtumia Bobby, ambaye alikuwa kule Dar kwenye nyumba yao ya utafiti. Angezipitia pia na kuwaambia ikiwa zingesaidia au la, na kama wangepata za muhimu basi angewapanga kuhusiana na nini walitakiwa kufanya.

Lakini siku hii, Luteni Michael hakuwa katika mjumuiko na wenzake wa kikazi. Alikuwa amekwenda Tanga, kwenye sherehe ya harusi ya mdogo wake pekee wa kike. Ndiyo, alikuwa na dada. Mwanamke mdogo tu aliyekuwa amemaliza chuo kikuu na kuanza kazi kwenye kitengo fulani cha juu cha kampuni/shirika la TLS. Aliolewa na mwanaume mtu mzima aliyekuwa mtu wa Mwanza, hivyo kwenye "sendoff," Luteni Michael alitakiwa kuwepo hasa kwa sababu hawakuwa na ndugu wengine zaidi yao tu, na kwa mambo mengi mdogo wake alishirikiana na marafiki zake na wazazi na ndugu za mume. Ilikuwa ni sherehe kubwa iliyotumia gharama nyingi sana.

Akiwa huko, Luteni Michael alijitahidi kuonyesha furaha kwa ajili ya mdogo wake, ingawa bado akili yake ilifikiria mambo mengi kuhusiana na kazi, hasa Nora. Alikutana na watu wengi na kuongea na baadhi yao, na ndipo akakutana na mtu mwingine ambaye alikuwa na jambo lililofanana na lake, yaani kazi. Alikuwa ni kaka ya bwana harusi, naye pia alikuwa ni mwanajeshi. Huyu hakuwa mwingine ila Khalid Juma, yule yule ambaye alimfanyia kazi nyingi haramu Luteni Jenerali Weisiko, kama kumbeba Azra kwa helicopter usiku ule ambao Salim Khan aliuliwa naye.

Kwa kuwa wawili hawa walikuwa na fani moja, maongezi yao yalikuwa rahisi zaidi kwa sababu walizungumzia vitu ambavyo wote wameshawahi kupitia katika utumishi wa kijeshi, hivyo kwa muda mrefu kwenye sherehe hii wangekaa pamoja hasa kutokana na jinsi Khalid Juma alivyomwonyesha Luteni Michael urafiki wa hali ya juu, hiyo ilifanya ionekane ni kama wanajuana kwa kipindi kirefu. Haikumchukua Luteni Michael muda mrefu sana kutambua kwamba mwanaume huyo alipenda sana starehe, kwa sababu aliongelea zaidi pesa na wanawake, na ili tu kumfanya ajiachie zaidi, Luteni Michael akawa anasindikiza maongezi kwa kuongelea wanawake na pesa pia.

β˜…

Baada ya harakati za sherehe zenye kuburudisha kwa usiku huo kuisha, Khalid Juma alikuwa amelewa kwa kadiri kubwa, hivyo Luteni Michael akajitolea kumsaidia kurudi alikokuwa amechukua chumba kwa siku hiyo mkoani hapo. Alimpeleka mpaka huko kama mdogo anavyomsaidia kaka yake, na baada ya kumfikisha kwenye chumba chake, Khalid Juma akaketi tu na kuendelea kuongea mambo mengi kilevi, akionekana kufurahia sana pombe iliyokuwa kichwani.

Luteni Michael akawa anamtazama tu kwa umakini alipoendelea kutoa malalamiko yake kuhusiana na mambo mengi yaliyomkera.

"...yaani anatumia dakika mbili... nzima kwenye wimbo ku..ongea vitu visivyoeleweka... eti mara gaddem olalala... yeeh baaba... hivi kweli hapo kuna mziki' tena..." akasema Khalid.

"Kweli, hamna muziki kabisa hapo," Luteni Michael akamuunga mkono.

"Ni disgusting! Huyo Kininini huyo... she should be ashamed of themselves... anatengeneza pesa kwa kutulisha utumbo kwenye nyimbo zake tu...."

"Okay, Khalid, pumzika sasa. Mimi ninakuacha..."

"Aa-aaaa unaenda wapi? Bado hatujamaliza hapa. Sikia, sikia, sikia..."

"Sawa nasikia..."

"Ukiwa na mpenzi... bila pesa... wewe ni mpenzi mtazamaji wandugu. Hawa watu hawa... wanachuma pesa kwa... jasho la watu wengine lakini bado hata kulinywa hawataki. She makes enough money, kaka... but wants more...."

"Nani tena huyo?"

"Wote hao! Kuanzia huyo... yule, wote. Mimi nakwambia... nimemfanyia kazi kama kichaa, zinazo..stahili milioni 20 na zaidi...."

"Mm-hmm..."

"...lakini sipati vya kutosha siku hizi... sherehe zinakuja kama hivi... sipewi nachostahili, na sasa mademu wakija... unategemea itakuwaje?"

Luteni Michael akatabasamu na kusema, "Okay, bwana Khalid, nakuomba upumzike."

Akaanza kumsaidia kuulaza mwili wake kitandani.

"Ah... it is impossible... watu tunamenyekaaa... mtu mpaka natekwaaa... nanyanyaswaaa... lakini sipati faida ya kazi yangu eti kisa... ahh..."

Luteni Michael alikuwa ameanza kugeuka ili aondoke pale Khalid aliposema maneno hayo, na umakini wake ukavutwa. Akamsogelea tena, huku Khalid akiendelea kubwabwaja tu.

"Subiri, subiri, Khalid... nani alikuteka?" Luteni Michael akamuuliza.

"Eeh... kumbe hujaondoka... kumbe... unasema?"

"Umesema kuna mtu alikuteka... lini ilikuwa?" Luteni Michael akauliza.

"Aagh... si hapo juzi... nimetoka na bonge la toto... ndiyo wale nyau wakanivamia... ningewaua wote wana bahati nilik...."

"Wakina nani walikuteka?"

"Si wale mafala wanaowasumbua vichwa nyie..."

"Mess Makers?"

"Eeeeh... hao hao... mafala sana hao..."

"Eeh ndiyo, ndiyo mafala sana. Kwa nini walikuteka?" Luteni Michael akauliza kiudadisi zaidi.

"Aagh... hayo masuala kusema si... sitakiwi... tuyaache tu..."

"Hapana, niambie. Kwa nini wale wajinga waje kukuteka wewe... hawajui wewe ni nani, au? Uliwaonyesha wewe ni nani, au siyo?" Luteni Michael akamtega.

Khalid akajinyanyua na kusema, "Hawakuwa wanajua mimi ni nani! Tena wangenikuta sijalewa... (akatulia kidogo)... ningewaua wote..."

"Dah! Wakakusababishia hadi usipewe unachostahili kabisa, eti?"

"We acha tu! Pale hata ningekufa. Nimefanya... mambo mengi sana kwa ajili... ya mkubwa, lakini zamu hii shukrani niliyoonyeshwa... aaaaa... utaelewa kwa nini sasa hivi kwangu ni mwendo wa kubenjuka tu... kubanju... kubenjukw... kubanjaku tu... yaani..."

"Kwani mkubwa hakukulipa?" Luteni Michael akamuuliza, kama vile anamjua huyo mkubwa.

"Sikiliza nikwambie. Alik..alikuwa ameshanipa mwanzo, kazi ikamilike, angemalizia, kama kawaidaa. Lakini kama ningemwambia... waliniteka halafu wakamfata na huyo ninja wake, basi ndugu yangu ungesaidia kubeba jeneza langu..."

"Kwa nini?"

"Kwani we haumjui Weisiko? Waliniteka... wakaniambia tu... nilikuwa... wangenikata masikio na... labda hata viungo vyangu, wakaniacha msituni... kwa hiyo nikawaambia pa kumpata. Sijui kama walimtoaje ila...iiila... kama mkubwa angejua nime-snitch... ai ai... usimwambie yeyote kaka..."

"No, no, siwezi kumwambia yeyote, namwelewa mkubwa," Luteni Michael akasema.

"Unajua nini kingine?"

"Nambie..."

"Wale hawakuwa watu wa Salim. Waliniambia ni watu wa Salim lakini mimi nilijua tu ni hao... hao Makasimeska... walikuwa wanamtaka huyo mtu aliyemuua Salim maana..."

"Subiri... subiri kwanza. Unasema kwamba... aliyetoa order ya kumuua Salim, ni Weisiko?"

"Karibu kwenye treni ya abiria dogo. Unafikiri ni hao wahuni ndiyo waliomuua... aaaaa... no, no, no, no..."

Luteni Michael akawa amechanganywa sana na jambo hilo.

"Watu wengine... hawana hata maji safi, magonjwa ndiyo usiseme... halafu yeye eti kwa sababu huyo punda wake wamemkamata ndiyo akaona asimalizie deni langu... upuuzi mtupu mkubwa amenifanyia... nimepoteza upendo kwake kabisaaa..."

"Mess Makers walikuwa wanataka nini na huyo mtu aliyemuua Salim?" Luteni Michael akamuuliza.

"Sijui. Kesho tuwafate tuwaulize au unaonaje?"

"Kwa nini sasa wakuteke wewe?"

"Aagh... hivi hujaelewa? Mimi nilimbeba huyo naniu... akaenda kumuua Salim. Sijui hata walipataje hata walijuaje ni mimi lakini wakaniacha tu msituni. Wakanitisha weee... hawana lolote zito wale..."

"Kwa hiyo ukaamua ku-shh... mkubwa asijue..."

"Angeniua kama angejua. Roho inauma... inaniuma sana kwamba hajanimalizia hela yangu, tena hadi niliilipua helicopter kumfichia trace kabisa... ila... lakini sasa hivi nikimwambia kuhusu hilo atageuka... yule hapana. Kaa mbali. Tena... naona bora tu nisimsemeshe, nasikia aliwaua walinzi wote wa yule ninja wake maana hawakumlinda vizuri. Unafikiri na mimi ningekuwa wapi? Aah... bora kupiga pombe na miziki ya utumbo kwenye bakuli... maisha yaende... na bila kusahau dem mama gangs... unalikumbuka lile lililokuwa limevaa zambarau kwenye sherehe saa zile na makope ya...."

Khalid Juma akaendelea kuongea kilevi tu na kuchanganya mambo mengi kwa wakati mmoja, lakini Luteni Michael akawa ametazama pembeni akitafakari mambo ya siri aliyokuwa ametoka kujua. Hapa katikati kulikuwa na mambo mengi yenye utata sana yaliyofichika.

Akatoka ndani ya chumba hicho akiwa bado anajiuliza vitu vingi. Ikiwa ni Weisiko ndiye aliyeamuru kifo cha Salim Khan, kwa nini isemwe kwamba ni Mess Makers? Sababu yake ya kumuua Salim ingekuwa ni nini? Na kwa nini Mess Makers walimfata muuaji wa Salim Khan kutoka kwenye himaya ya Weisiko? Kitu cha kwanza alichohitaji kufanya baada ya kurejea Dar es Salaam ingekuwa ni kuzungumza na Kanali Oswald kuhusiana na jambo hili, ili aweze kupata mwanga wa mambo mengi ambayo alihisi huenda Kanali wake alijua pia.

Akaondoka upesi kwenda kupumzika pia, ili asubuhi na mapema aianze safari.


β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

ITAENDELEA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

WHATSAPP +255 787 604 893
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…