FOR YOU
Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA HAMSINI
★★★★★★★★★★★★★★
Alfajiri na mapema ya siku iliyofuata ikafika. Hii ikiwa ni alfajiri ya siku ya Jumatatu, siku ambayo kwa ukawaida huonwa kama ya kwanza ingawa ni Jumapili ndiyo siku ya kwanza kwenye juma.
Mess Makers tayari walikuwa wamemaliza kujipanga vizuri sana na kuanzisha hatua ya kwanza ya mpango wao, na hiyo hatua ilikuwa ni kusambaza video fulani kwenye kila aina ya mtandao kuzunguka nchi nzima, na bila shaka hata mataifa jirani yangeanza kuzipata. Hatua ya pili ilikuwa ni kuondoka kwa Kendrick na vijana wake kutoka huko kwenye nyumba yao, wakijigawa, na wakiwa na lengo la kwenda Dar es Salaam ili kufanya mambo mawili muhimu; kumkamata Jenerali Jacob, pamoja na Luteni Jenerali Weisiko. Ilikuwa ni muhimu zaidi kuwashika hao wawili kwa kuwa walikuwa nguvu ya kundi la Raisi Paul Mdeme, na ili hatimaye haki ambayo Kendrick na Lexi waliihitaji kwa kipindi kirefu itimie.
Lexi, Nora, Azra, Mensah na Victor wangeondoka kwenye gari moja, huku Kendrick, Torres, LaKeisha na Kevin wangetakiwa kuondoka kwa gari lingine. Ni Isiminzile tu ndiye aliyetakiwa kubaki, kwa sababu bado kundi hili lilikuwa limehakikisha kwamba sehemu hiyo ya maficho haijajulikana, na hivyo wakawa wamempatia kijana huyo maelekezo muhimu ya jinsi ya kukaa hapo na kumhudumia Zelda akiwa ndani ya nyumba yake ndogo. Walijua kutokana na video walizokuwa wameachia, macho yote ya serikali nzima yangekuwa yamezikazia uangalifu kwa siku hii, hivyo safari yao isingekuwa na vikwazo njiani kutoka kwa watu wa usalama.
Lexi na wenzake wanne ndiyo walioanza kuondoka sehemu hiyo, lakini wakati Kendrick alipotaka kuondoka na vijana wake waliobaki, Torres akabadili mpango. Alimtaka LaKeisha abaki kwenye nyumba hiyo, akimwambia ilikuwa ni muhimu sana kwa sababu alihisi kuna jambo fulani lingetokea kinyume na matarajio yao. LaKeisha alimuuliza ni kwa nini alifikiria hivyo, lakini Torres hakumweka wazi kwamba alihisi Kevin ndiye aliyetaka kuwavurugia mambo, bali tu akamwambia LaKeisha amwamini na atii hilo. Kubaki kwake kwenye nyumba hiyo bila Lexi kujua ingekuwa msaada endapo kama hali isiyotazamiwa ingetokea ili Torres amjulishe LaKeisha, na yeye LaKeisha aweze kumwonya Lexi haraka. LaKeisha akambusu Torres kwa upendo baada ya kukubali kubaki hapo, nao wakaagana.
Torres alipojiunga na Kendrick pamoja na Kevin, ambao tayari walikuwa kwenye gari wakisubiri, walishangaa na kuuliza kwa nini LaKeisha hakutoka ndani. Torres akamwambia Kendrick kwamba amempa LaKeisha maelekezo mengine, lakini angewafuata tu muda si mrefu, hivyo wao watangulie tu naye angekuja baadae kufikia sehemu waliyodhamiria kwenda. Alimwangalia Kevin kiufupi na kuona jinsi alivyoonyesha hila fulani isiyo ya moja kwa moja usoni kwake, na baada ya Kendrick kuridhia akawaondoa hapo pia upesi.
Safari ya kutoka Arusha kuelekea Dar es Salaam ikaendelea kwa watu wa kundi hili, wakiwa wamebeba vifaa vingi kwa ajili ya mambo ambayo wangefanyia kazi siku hii, na wakiwa na lengo la kumaliza mambo yote yaliyotokea kwa muda mrefu mpaka kufikia sasa.
★★★★
Luteni Michael tayari alikuwa kwenye jengo lile la utafiti ambalo kwa muda mrefu alitumia pamoja na timu yake. Tokea siku ya jana aliposikia jinsi Kanali Oswald alivyoongea kwa hofu kuhusiana na mambo ambayo Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko walikuwa wamefanya, alikuwa amezama kwenye utafiti wa mambo mengi yaliyotokea kipindi kile cha "enzi za Demba Group."
Ilikuwa wazi kwake sasa kwamba matukio ya hivi karibuni yalihusiana moja kwa moja na kisa hicho, hasa kutokana na Kendrick na Lexi kuhusiana nacho moja kwa moja. Alianza kutambua kwamba wawili hao, pamoja na kundi lao zima, walikuwa wakilipiza kisasi kuwaelekea Jenerali Jacob na Weisiko, na huenda kulikuwa na sababu iliyofanya waibe zile pesa, mzigo wa dhahabu za Mdeme, na hata kulazimika kumteka Khalid Juma ili tu wampate mtu aliyemuua Salim Khan. Na akafikiri huenda hiyo ndiyo iliyokuwa sababu iliyofanya hata Nora, mwanamke mnyoofu aliyependa haki, ajiunge na kundi hilo.
Asubuhi hii, akiwa peke yake ndani ya jengo hilo, akapigiwa simu na Rachel, na baada ya kupokea, mwanamke huyo akamwambia kwamba kuna video fulani zilikuwa zimeanza kusambazwa kila kona, na ziliwahusu Mess Makers. Alimwambia zilipangana kwa mfuatano maalumu kabisa, na zilikuwa zimeanza kuzua gumzo na balaa zito. Luteni Michael akakata simu upesi, naye akaziwasha kompyuta za hapo ili azitafute video hizo na kuziangalia kwa umakini.
Ikawa ni wakati huo huo ndipo Bobby akawa amefika, tena akiingia jengoni humo kwa kasi huku akimwambia Luteni Michael kwamba kimenuka. Akafika na kuketi kwenye kiti chake na kuanza kubofya keyboard upesi, huku Luteni Michael akisimama karibu yake na kusubiri video hizo zifunguliwe. Bobby akazipata, naye akazicheza. Luteni Michael alikuwa amekunjia mikono yake kifuani, lakini baada ya video ya kwanza kufunguka tu, akaishusha na kubaki anaitazama kwa umakini sana.
Video hiyo iliwaonyesha Mess Makers wakiwa wamekaa ndani ya chumba fulani cheupe, huku aliye mbele zaidi akiwa ni Kendrick Jabari. Wengine hapo walikuwa ni Lexi, Torres, Victor, LaKeisha, Mensah, Kevin, pamoja na Nora. Mtoto wa Jenerali Jacob Rweyemamu akajionyesha waziwazi kwamba naye sasa alikuwa upande wa watu hao, na wote walikuwa wamevalia T-shirt nyeusi zenye picha ya Oscar kifuani.
Kendrick alianza kuongea, na alisema mambo mengi ambayo yalishangaza wengi. Alieleza kwamba kisa chote cha Demba Group miaka nane iliyopita hakikuwa ugaidi wa watu au waasi tu wa kawaida, bali kilitengenezwa na Raisi Paul Mdeme, akishirikiana na Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko, pamoja na watu kama Makamu wa Raisi wa sasa, Waziri Mkuu, Gavana wa Benki Kuu, pamoja na marehemu Salim Khan. Akaeleza jinsi walivyowatumia vijana wa jeshi kuua watu wengi kwa masilahi yao ya kibinafsi, na jinsi yeye pekee na mtoto wa Meja Casmir walivyokiponyoka kifo kutoka kwa watu hao wabaya baada ya wao kuziangamiza familia zao. Akasema wakati ambapo video hii ingemalizika, ushahidi wote wa mambo maovu ya kundi la Mdeme wangeuonyesha kupitia video, sauti za kurekodi, na mafaili mbalimbali ambayo wangeyaachia waziwazi kotekote ili watu wauone ukweli hatimaye.
Torres akaongea pia, akielezea kuhusu ni nini kilichofanya mpaka kundi lao likawaibia Trilioni 20 watu wa serikali. Alieleza njia waliyotumia, na kusema kwamba lengo lao lilikuwa kuwarudishia wanyonge wote pesa zao zilizonyonywa na utawala mbovu wa Mdeme kwa ajili ya starehe zake na mafisadi wengi kama yeye, na akaweka wazi kwamba jambo hilo ndiyo lililofanya wakae kimya kwanza kwa muda wote huo, ili kufanikisha mpango huo, kisha ndiyo wangewajulisha watu wote siri hizi kama walivyokuwa wanafanya sasa. Akawaeleza watu jinsi ambavyo kundi la Mdeme lilipata pigo kubwa sana baada ya wao kuwaibia pesa hizo, kitu kilichofanya wavurugane na Salim Khan mpaka kufikia hatua ya kumuua mwanaume huyo. Akasema kwa uhakika kwamba pesa hizo zote zingeanza kusambazwa kwenye akaunti za watu walioibiwa, tena siku hii hii, na hata kama kuna mnyonge aliyeibiwa ambaye alikuwa amekufa ndani ya kipindi hicho, pesa hizo zingekwenda kwa watu wa familia waliobaki bila upendeleo.
Nora pia akaongea. Alijitambulisha waziwazi kwa wote ambao hawakumfahamu yeye kuwa binti ya Jenerali Jacob, na kusema kwamba kwa kipindi fulani alipambana dhidi ya kundi hili la Mess Makers akiamini wao ndiyo walikuwa wabaya. Lakini sasa alikuwa ameingia upande wao baada ya kuthibitisha kwamba upande wa serikali ndiyo uliofanya maovu mengi, na alikuwa anawasaidia ili kutimiza makusudi yao ya kuwatendea kwa haki wanyonge wote.
Baada ya hapo, Kendrick akaomba radhi kwa wale ambao waliumizwa na matendo yao katika hilo sakata lote. Akasema nia yao tokea mwanzo haikuwa kumuumiza yeyote, lakini msaada ambao wangewapatia wote kwa wakati huu ungewapa nguvu mpya ya kupigania haki, kwa sababu walikuwa wakitawaliwa kimabavu lakini kwa njia isiyoonekana wazi sana. Akamalizia maneno yake kwa kusema kwamba hawakufanya haya ili kutafuta umati wa watu wa kuwaunga mkono, bali kutoka mioyoni mwao walitamani kuwasaidia wengi. Kile ambacho watu wangeamua kufanya kuelekea haki walizostahili wangepaswa kuchagua wenyewe, kwa sababu lengo la Mess Makers lilikuwa limetimia. Akasema wale wote waliofanya maovu hayo mengi wangelipwa tu, na mwanzo ulikuwa ni siku ya leo. Kisha video ikakata.
Luteni Michael akatazamana na Bobby kiufupi, wakiwa kama wamepigwa na butwaa kwa kile walichotoka kusikia, naye Bobby akaanza kuzicheza zile video zingine zilizofuata. Zilionyesha baadhi ya mambo mabaya kama mauaji, uonevu, na unyanyasaji kutoka kwa Jenerali Jacob na Weisiko, na tena walionekana kufurahia sana. Kulikuwa na zingine zilizoonyesha wenzao wakiongelea kuhusu njia za kuendelea kuwanyonya watu mali zao, kuuza madawa ya kulevya, na hata jinsi ya kuwalaghai walemavu kwa kujifanya wanawasaidia. Ilihuzunisha sana. Kulikuwa pia na rekodi za sauti ya Torres pamoja na Mdeme kutokea siku ya kwanza alipoanza kumtisha atoe pesa mpaka walipowachengua wanajeshi wake na kufanikiwa kutoroka nazo. Na pia kukawa na mafaili yenye taarifa hususa za upunjaji mwingi kutoka serikalini, zilizothibitisha hata zaidi kwamba watu wengi walikuwa wakinyonywa isivyo haki kwa kipindi cha utawala wa Mdeme.
Bobby akabaki kutikisa kichwa kwa kusikitishwa na mambo yote hayo. Luteni Michael alikuwa pembeni yake akitafakari vitu vingi sana. Kama ni majibu ya maswali yaliyokuwa akilini mwake sasa aliyapata, lakini kwa njia ambayo hakuwa ametarajia kabisa. Bobby akamwambia yaani kuanzia hapo miswada na vurugu ambayo ingeanzishwa ndani ya nchi hii ingekuwa kubwa sana, na hakujua ikiwa bado wangetakiwa kuwatetea viongozi hao kwa kufata walichosema au kuunga mkono upande wa wanyonge.
"Tutafanya nini kuhusu hii kitu Luteni?"
Bobby akamuuliza hivyo, lakini Luteni Michael hakutoa jibu, bali akaanza tu kuondoka akiwa amekunja ngumi. Bobby hakujua ni nini kiongozi wake huyo alikuwa anataka kufanya, naye akaanza kuwatafuta wenzake kutoka kwenye kampuni za Kendrick na kuwaambia warejee huku aliko ili wajadili kwa kina kuhusiana na utata huu uliokuwa umezuka.
★★★★
Mambo hayo yote yalikuwa yameshawafikia watu wote wa Mdeme, na sasa ikawa wazi kwamba hakukuwa na siri yoyote iliyobaki tena. Kila kitu kilikuwa wazi. Raisi Paul Mdeme alichanganyikiwa sana. Yaani alikuwa kwenye simu tu muda wote akijaribu kuzungumza na watu ili kuhakikisha kwamba wengi bado wanakuwa upande wake, lakini alielewa kwamba hatari isingeacha kumwandama sasa baada ya watu kujua ukweli kuhusu matendo yake, na hasa wale waliokuwa upande wa Salim Khan baada ya ukweli wa kwamba alimuua kuwa umejulikana. Alikuwa Ikulu tu na familia yake ambayo nayo ilipata kujua ukweli, naye akawa anawasihi wasiamini mambo hayo kwa kusema hayakuwa kweli.
Jenerali Jacob alikuwa kwenye nyumba yake ile kubwa, akiwa amekaa kwa kutulia tu baada ya kuona mambo hayo yote. Kuna vitu vilikuwa vikipita kwenye akili yake, naye alikuwa ameshafikiria achukue hatua gani ili kujitoa katika sheshe hiyo mbaya sana kwake. Luteni Jenerali Weisiko akamtafuta na kumwambia kwamba hawangepaswa kuogopa lolote kutoka kwa wananchi, lakini alielewa kwamba watu wa Salim Khan wasingeacha kuwaandama, hasa wale Mafia wake kutoka nje ya nchi. Kwa hiyo akauliza sasa wangetakiwa kuchukua hatua gani upesi, naye Jenerali Jacob akamwambia anafanya mpango ili waweze kuondoka haraka sana kutoka kwenye hii nchi.
Weisiko alishangaa kiasi, hasa ukitegemea alijua wazi ingekuwa ngumu kufanikisha hilo kwa kuwa sasa wangesakamwa sana kila kona, lakini Jenerali Jacob akamwambia ajiandae tu ili mida fulani wakutane na waondoke upesi. Weisiko alipouliza kuhusu hawa wenzao kama Mdeme, Yustus, Gimbi, na Eliya, Jenerali Jacob akamwambia hawakuwa na wajibu wowote kuwaelekea kuanzia sasa, kwa kuwa wangefanya mambo kwa njia waliyotaka na siyo kubeba mizigo ya wengine tena. Akamwambia ilikuwa ni muhimu wafanye hivi haijalishi wangeacha nini nyuma, kwa kuwa hali hii ilikuwa nzito kuliko walivyofikiri.
Basi, baada ya kumaliza kuongea na Weisiko, Jenerali Jacob akawaita wanaume wake maalumu kwa ajili ya kufanya jambo fulani muhimu sana. Alitaka kuhakikisha jambo hili linakamilika kabla ya yeye kuondoka, kwa sababu kuna ishu nyingine ilikuwa imezuka iliyoingiliana kwa undani na mambo haya yaliyokuwa yanaendelea sasa. Wakawa wamefika kwake hapo upesi, wakiwa wamejiandaa vizuri sana kimapambano, naye akawapa maelekezo ya kazi aliyotaka waifanye. Walipomwelewa, akawapa sanduku kubwa lenye pesa nyingi sana, nao wakaondoka hapo kwenda kuimaliza hiyo kazi upesi.
Jenerali Jacob alitafutwa sana na watu wengi aliofanya nao mambo haramu, kutia ndani hadi wenzake wa kundi la Mdeme, lakini hakumjibu hata mmoja wao. Aliyekuwa anamwamini hapa ni Weisiko pekee. Akawa akiangalia runinga na kuona jinsi watu wengi walivyokuwa wameanzisha maandamano kuipinga serikali, na jinsi ambavyo viongozi wa vyama pinzani na utawala walimkashifu Raisi Mdeme na kuchochea watu wasiogope kujitoa ili kuuangusha utawala wake.
Raisi Paul Mdeme alimtafuta sana Jenerali Jacob mpaka akachoka. Watu walikuwa wameanzisha maandamano na vurugu zilikuwa nyingi sana. Wengi walidai viongozi hao walipwe kwa matendo yao maovu, hasa ukitegemea wengi walikuwa wamepoteza wapendwa wao wengi kipindi kile Mdeme na kundi lake walipofanya mauaji kwa jina la Demba Group. Ndipo mkuu wa majeshi maalumu ya vijana, kutia ndani JKT, Meja Jenerali Sebastian Tambwe akajitokeza (Major General), akiwa sambamba na Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, mwanamama Emiliana Ngoyi, nao wakasema wangehakikisha haki inatendeka, na wale wote waliokuwa wametambulika kwa maovu yao wangekamatwa bila kujali vyeo walivyokuwa navyo kwa kuwa haki ilitakiwa itekelezwe. Meja Jenerali Sebastian akasema tayari walikuwa wameshaanza kufanya mchakato wa kuwafuata watu hao wote wa kundi la Mdeme, na baada ya kuhakikisha wanawakamata, sheria ingefuata mkondo wake.
Ingawa hivyo, wengi kutoka vitengo mbalimbali vya usalama walionekana kusua katika kuunga mkono jambo hilo kwa sababu walielewa ni jinsi gani watu kama Jenerali Jacob na Weisiko walivyokuwa na uvutano mkubwa sana kwa wanajeshi na maaskari wengi. Ijapokuwa haingekuwa rahisi, bado Meja Jenerali Sebastian alionyesha msimamo imara kwa kukusanya wanajeshi ambao walikuwa tayari kufanya yote ili kutekeleza haki, na mchakato wa kuwakusanya watu hao wabaya ukaanza haraka. Ni Waziri Mkuu Yustus Kagame, Gavana Laurent Gimbi, na Makamu wa Raisi Eliya Kajuna ndiyo waliokamatwa kwanza na kutiwa pingu, na sasa waliokuwa wamebaki ikawa ni Weisiko, Jacob, na Mdeme.
Hili lilikuwa ni jambo lililompa ahueni Kanali Oswald Deule, kwa sababu alielewa kama Jenerali Jacob na Weisiko wangetiwa mikononi mwa sheria, hangepaswa tena kuwaza kuhusu wao kumfanyia ubaya, ingawa bado aliona kwamba angetakiwa kuwa makini sana na nyendo zake ili kujilinda kwa sababu hangeweza kuwa na uhakika juu ya usalama wake kwa asilimia zote. Kwa hiyo na yeye akaunga mkono upande uliokuwa dhidi ya majenerali wale, ili kuonyesha yuko upande sahihi lakini kwa unafiki.
★★
Mpaka inatimia mida ya saa 10 jioni siku hii, bado nchi ilikuwa kwenye tafrani kubwa kutokana na hasira za wananchi, lakini wengi walifurahi sana baada ya kupokea pesa nyingi kwenye akaunti zao binafsi, kama tu jinsi ambavyo Mess Makers walikuwa wameahidi. Hii iliwatia moyo sana na kuwaongezea nguvu ya kupigania haki zao, kwa hiyo kuendelea kuandamana ili kuiangusha serikali ya mtawala wao mbaya bado likawa jambo kuu. Raisi Paul Mdeme aliendelea kukaa tu Ikulu mpaka kundi la wanajeshi lilipofika hapo na kupazunguka, wakiwa wamewazidi nguvu ya wingi wale wote waliokuwa hapo kumlinda Raisi, na hapo Mdeme akatambua kwamba habari yake ilikuwa imekwisha.
Jenerali Jacob, akiwa bado kwenye nyumba yake, alipata kuona kwamba wanajeshi waliotumwa na Meja Jenerali Sebastian ili kwenda kumkamata walikuwa wamefika maeneo hayo, naye kwa kujiamini akatoka kabisa nje na kusimama, kama anawasubiria kuwakaribisha vile. Yalikuwa yamefika magari saba ya kijeshi yaliyobeba wanaume 37 wa kijeshi, nayo yakasimama hapo, na wanajeshi hao wakashuka na kumzunguka Jenerali Jacob, aliyekuwa amesimama tu bila kuonyesha jitihada yoyote ya kukwepa kilichokuwa kimemfata. Walikuwa wamemnyooshea bunduki, na aliyekuwa amekiongoza kikosi hicho akasogea karibu yake na kumwambia walikuwa wamekuja kumchukua kwa sababu alionwa kuwa mhalifu sasa, naye Jenerali Jacob akamwambia wamchukue tu.
Kiongozi wa kikosi hicho alitulia kidogo, kwa sababu alihisi kuna jambo halikuwa sawa. Yaani hata yeye alimfahamu vizuri sana Jenerali Jacob, na kuona kwamba hata eneo hilo halikuwa na watu waliomlinda kulimfanya ahisi ni kama kuna mtego. Lakini Jenerali Jacob akamwambia asiogope, naye akanyoosha mikono mbele ili mwanaume huyo amfunge kwa pingu. Jenerali Jacob alionyesha utulivu wa hali ya juu sana, na mwanaume huyo akaanza kuifunga mikono yake huku anamtazama machoni.
Papo hapo kichwa cha mwanaume huyo kikapasuka mbele ya Jenerali Jacob, na kusababisha damu zirukie usoni mwake! Hii ilishtua sana wengine, lakini hawakuwa hata na muda wa kukisia ni nini kilikuwa kimetokea, na mmoja baada mwingine, wakaanza kupasuka vichwa vyao pia! Wachache waliokuwa wamejitahidi kuinama ili kujilinda lakini hawakufanikiwa kufanya hivyo kwa muda mrefu, kwa sababu nao walikufa kwa njia hiyo hiyo ya kupasuliwa vichwa upesi sana bila kuelewa ni nini kilikuwa kinaendelea. Wanaume wote 37 wakabaki kulala chini, wakiwa mbali na maisha.
Jenerali Jacob, akiwa ndiye pekee amebaki kusimama, akatoa kitambaa mfukoni mwa suruali yake na kujifuta damu zilizomrukia usoni, naye akatabasamu kidogo na kugeuka nyuma. Kutokea juu kabisa ya nyumba yake, kulikuwa na mtu, mtu maalumu mwenye mafunzo ya kupiga risasi kwa shabaha za mbali (sniper), naye ndiye aliyefanya wanajeshi wale wote waliofika hapo walale chini kwa kutobolewa bongo zao. Akashuka kutoka huko juu mpaka alipokuwa amesimama Jenerali Jacob, naye akazikata pingu zile zilizokuwa mikononi mwa Jenerali, kisha akamwashia sigara nene na kumpa ili aanze kuvuta.
"Sebastian ana bahati sana kwamba nahitaji kuondoka, la sivyo ningemwonyesha nini maana ya kucheza na mimi," Jenerali Jacob akasema.
"Tokea zamani amekuwa anakuonea wivu..." Sniper wa Jenerali akaongea.
"Mhm... aombe nisirudi kwenye hii nchi, maana nitaikata puru yake na kumpa aitafune," Jenerali Jacob akasema.
Sniper wake akacheka.
Kutokea upande mwingine wa eneo hilo, magari sita meusi yakaonekana yakija kuwaelekea, na baada ya kufika usawa wao yakasimama, kisha wakashuka wanaume waliomfanyia kazi Jenerali Jacob, wakiwa wamevalia nguo nyeusi mwilini, kofia ngumu kichwani, na mabuti miguuni, huku wakishikilia bunduki mikononi. Mmoja wao akasogea mpaka usawa wa Jenerali Jacob na kumsalimu.
"Mmemleta?" Jenerali Jacob akauliza.
"Ndiyo General... yupo kwenye gari..."
"Na ule mzigo?" Jenerali Jacob akauliza.
Mwanaume huyo akatazama upande wa gari moja, na wanaume wanne wakaonekana wakitoa sanduku fulani kubwa na kumwonyeshea. Jenerali Jacob akatabasamu na kutikisa kichwa kwa kuridhika, kisha wakalirudisha.
"Tunahitaji kuondoka, ndege itakuwa tayari kwenye saa 2," mwanaume huyo akamwambia.
"Usijali. Kuna kamchezo nataka tukacheze kwanza," Jenerali Jacob akasema.
Kisha akaelekea kwenye gari mojawapo na kufunguliwa mlango wa nyuma, naye akaingia na kukaa. Magari hayo yakaanza kuondoka haraka sana baada ya wote kuingia ili hatimaye mwanaume huyu aweze kutoroka nchi hii. Lakini, kama alivyosema, alitaka wacheze mchezo fulani kwanza, kisha kutoroka ndiyo kungefuata. Wakiwa mwendoni bado, akampigia simu Weisiko na kumwambia atoke huko aliko haraka sana na kwenda mpaka kule atakapomwambia ili wakutane, naye Weisiko akakubali na kusema angeharakisha.
★★★★
Luteni Jenerali Weisiko alikuwa ameanza kuondoka kule alikokuwa ili kwenda kukutana na Jenerali Jacob kama alivyomwahidi. Yeye alikuwa akizunguka peke yake tokea mkasa huu wa siri zao kuvuja hadharani ulipoanza, kwa sababu hakuwaamini watu wengine, na ili kuhakikisha anakuwa salama. Aliyekuwa anamtegemea zaidi sasa ilikuwa ni Jenerali Jacob pekee, hivyo hicho ndiyo kilichokuwa kimebaki kwa sasa kabla ya mambo mengine kufuata endapo wangefanikiwa kuondoka nchini humo haraka, yaani kuendelea kuwa salama.
Wakati huu alikuwa ndani ya gari lake, akiendesha kwa umakini kupitia barabara zisizo rasmi, pale simu yake ilipoanza kuita. Namba ilikuwa ngeni kabisa, na kuna hisia fulani aliyoipata kwamba huenda haikuwa ikileta jambo zuri, hasa kutoka kwa mpigaji mwenyewe, ingawa hakujua ni nani. Hakupokea mpaka ilipoita kwa mara ya 7 mfululizo, naye akaamua kupokea na kusikiliza nani angeongea.
"Hello..."
Sauti hiyo aliyoisikia ikamfanya afunge breki za gari lake ghafla sana, naye akaweka umakini zaidi kwa sababu aliitambua vizuri.
"Hello... dad?" mpigaji akasema.
"Mary?" Weisiko akauliza.
Ilikuwa ni Azra, na kwa Weisiko ilikuwa ni Mary.
"Dad... please help me... I really need... I nee... help me please.... (Baba... tafadhali nisaidie.. ninahitaji sana... nina... naomba unisaidie tafadhali..." Azra akasikika akisema hivyo kwa presha.
"Mary... what's going on, where are you? (Mary.. nini kinaendelea, uko wapi?)" Weisiko akauliza.
"I'm here... Dar... I escaped... (niko huku Dar... nimetoroka...)" Azra akasema.
"Escaped... where? (umetoroka.. wapi?)"
"They kidnapped me... they, they... please dad help me... they are looking for me... they'll kill me... dad please... (waliniteka.. tafadhali nisaidie baba.. wananitafuta.. wataniua.. baba tafadhali..)" Azra akawa anazungumza kwa sauti iliyoonyesha taabu kali.
"Okay, okay, Mary, niambie... nielekeze... tell me where you are. Can you describe the place you are in? (..niambie uko wapi. Unaweza kuielezea sehemu uliyopo?)" Weisiko akamuuliza.
"Yes... there's this place near an old orphanage, I'm hiding under the little bridge here... (ndiyo.. kuna hii sehemu karibu na nyumba ya watoto yatima, nimejificha chini ya daraja dogo hapa..)" Azra akasema.
"How did you get there? (umefikaje hapo?)" Weisiko akauliza.
"Please help me dad... I'll explain everything... I'm really tired... (naomba unisaidie baba.. nitakueleza kila kitu.. nimechoka sana..)" Azra akaongea.
Weisiko akabaki kimya kiufupi. Kufikiria kuhusu kwenda kumsaidia binti huyu aliyemwona kama mtoto wake ilikuwa ni kitu cha kwanza kwenye akili yake, lakini tena akawa anajiuliza ikiwa angetakiwa kumwambia Jenerali Jacob au la.
"Dad...?" Azra akaita.
"Naam... yes... I'm coming. Nakuja my dear... wait for me..." Weisiko akamwambia.
Kisha akakata simu na kuanzisha mwendo tena, wakati huu akibadili njia ili aelekee huko alipokuwepo "Mary." Aliona kwamba angeweza kwenda kumfata upesi na kumchukua ili aelekee kwa Jenerali Jacob pamoja naye, kwa kuwa bado aliamini kwamba kumbukumbu za nyuma za binti huyo hazikuwa zimerudi, na ndiyo sababu bado aliamini kwamba yeye ni baba yake. Akaendesha gari kwa dakika zaidi ya 20 na kufika maeneo hayo aliyoelekezwa. Alikuwa ametumia kifaa cha GPS cha gari lake kufatilia simu ya "Mary" kumwonyesha alikokuwa kabisa, kwa sababu hangeweza kujua kirahisi nyumba hiyo ya mayatima ilikokuwa, na baada ya kufika kweli aliona daraja dogo upande mwingine karibu na nyumba hiyo, hivyo akaelekea usawa huo na kuegesha gari lake.
Weisiko akashuka na kuyaangalia maeneo hayo kwa umakini. Hakukuwa na watu kabisa kwenye eneo hilo, na sehemu zake zilizungukwa na miti mingi na vichaka, na hata kwa kuiangalia tu nyumba ile kwa ajili ya mayatima alitambua kuwa ilikuwa imeacha kutumiwa. Akaitoa bastola yake kiunoni na kuanza kuelekea kule chini ya daraja lile fupi, na baada ya kuiangalia sehemu hiyo, akamwona "Mary" akiwa ameketi chini ya nguzo iliyolishikilia daraja. Wakati huu hakukuwa na maji kwenye sehemu hiyo ambayo ingekuwa ni mto kwenye misimu ya mvua, hivyo upesi Weisiko akaanza kumfata huku akimwita.
Azra akageuka na kusimama taratibu, akiwa anamwangalia Weisiko alivyokuja kwa njia iliyoonyesha kwamba aliwaza sana kuhusu usalama wake.
"Mary... Mary... are you okay?"
Weisiko akasema maneno hayo na kumfikia karibu zaidi, kisha akamkumbatia.
Azra alikuwa ametulia tu, na hata hakurudisha kumbatio lake.
Weisiko akamwachia na kumshika usoni. "We have to go. You'll explain everything on the way, okay? Come on," akasema maneno hayo kwa kuharakisha.
Lakini kutokea nyuma yake, Weisiko aliweza kuhisi kama kuna hatua zikija, naye kwa haraka akageuka akiwa ameiinua bastola yake ili ampige kwa risasi aliyekuwa anawafata, lakini ghafla akashtukia mikono yake inaishiwa tu nguvu na kuidondosha bastola yake, na kabla hata ya kuelewa kilichotokea, akapigwa sehemu ya shingo kwa nyuma iliyomfanya apoteze fahamu zake na kudondoka chini. Ilikuwa ni Azra ndiye aliyempiga namna hiyo baada ya Weisiko kumpa mgongo, akiwa ametumia mtindo wake wa Marmakkala wa kumaliza nguvu mwilini.
Azra akabaki kumwangalia tu huku akipumua kwa hisia kali, naye akanyanyua uso kuwaangalia wale waliokuwa wanakuja. Ilikuwa ni Lexi, Nora, Mensah, na Victor. Wakamfikia karibu zaidi, na Mensah akasaidiana na Victor kuanza kumnyanyua Weisiko.
"That was easy (hiyo ilikuwa rahisi)," Mensah akasema.
"Yeah, he didn't suspect a thing (ndiyo, hakushuku jambo lolote)," akasema Victor.
"Azra... you okay?" Lexi akamuuliza kwa kujali.
"Yeah, let's just get this over with (ndiyo, tumalize tu haya yote haraka)," Azra akasema na kusogea pembeni.
"Okay, Victor, Mensah, mpelekeni huyu kule, sisi tunaelekea upande wa uncle Kendrick," Lexi akasema.
"Tukishampeleka, Mensah atawafata pia," Victor akasema.
"Si mnatakiwa kumlinda pamoja huyu?" Nora akauliza.
"Usijali, Victor atamwangalia vizuri. Harakisheni, watahitaji msaada wenu huko... nami pia nitawahi," Mensah akasema.
Wawili hao wakaanza kuondoka wakiwa wamembeba Weisiko, nao walimpeleka mpaka kwenye gari lake Weisiko na kulitumia hilo hilo kumtoa maeneo hayo. Lexi na Nora na Azra wakaanza kuondoka pia, wakiwa na dhumuni la kuelekea kule ambako Kendrick, Torres, na Kevin wangekuwepo. Lexi alikuwa na kifaa kile muhimu cha mawasiliano kati yake na Torres, naye akamwambia walikuwa njiani baada ya kukamilisha mpango wao wa kumkamata Weisiko.
★★★★
Upande wa Kendrick Jabari. Mwanaume huyu, akiwa pamoja na Torres na Kevin, walikuwa wamefika sehemu ambayo walijua wazi kwamba Jenerali Jacob angepita katika mchakato wake wa kutaka kutoroka. Torres kama kawaida yake alikuwa ameshapigia mahesabu sehemu hiyo mapema, na sasa wakiwa wameshafika hapo, wakaweka mitego barabarani, kisha wakasogea sehemu za pembeni na kujificha, wakisubiri mzee wa kazi apite. Jua lilikuwa limeshaanza kutua na giza kuingia kwa mbali, na sasa ulikuwa umepita muda mrefu bila matarajio yao kufanikika.
Torres akawa anamwangalia sana Kevin, jinsi jamaa alivyokuwa anaangalia saa yake ya mkononi mara kwa mara.
"Vipi, kuna sehemu unataka kuwahi?" Torres akamuuliza.
Kevin akamtazama tu, lakini hakutoa jibu na kuangalia pembeni.
"Something's wrong... (kuna kitu hakiko sawa)" Kendrick akasema.
"Yeah, no kidding," akajibu Torres.
"LaKeisha atakuwa wapi? Kwa nini amechelewa?" Kendrick akamuuliza Torres.
"Nilimwambia abaki," Torres akasema.
Kendrick na Kevin wakamwangalia kimaswali.
"Ume... kwa nini? Na kwa nini unaniambia hilo sasa hivi tu?" Kendrick akauliza.
"Nilihisi kuna kitu hakitakwenda sawa, na kama niko sahihi, LaKeisha atakuwa msaada kwetu. Atamwonya Lexi ikiwa sisi tutashindwa," Torres akasema.
"Ahah... hivi kweli Torres una akili? Kwani Lexi haji hapa pia? Boss, huyu anazingua sana. Umemwacha LaKeisha nyuma bila kumwambia boss kwa sababu tu unajifanya uko makini zaidi eti kuliko sisi wote," Kevin akaongea.
"No, ni kwa sababu yako," Torres akasema.
"Nini?" Kendrick akauliza.
"Boss, Kevin amekuwa akifanya mambo fulani kisiri bila nyote kujua. Nimemwangalia tu kumfanya adhani sioni, lakini ninajua anataka kutuharibia mambo," Torres akasema.
Kevin akaingiwa na wasiwasi. "Are you crazy? Boss, anaongea nini huyu? Ningekuwa hapa pamoja nanyi kama ningekuwa nataka kuwaharibia mambo?" akauliza kiukali.
"Nimekuacha uje na sisi ili mimi mwenyewe nithibitishe kama niko sahihi au la, lakini hilo halimaanishi nisingefikiria njia mbadala ya kuyashughulikia mashaka yangu," Torres akasema.
"Hivi, boss kweli... yaani..." Kevin akawa anababaika.
"Niliona ametafuta info personal za General Jacob. Tena kwa kutumia lugha ngumu ya kompyuta zangu," Torres akamwambia Kendrick.
Kendrick akamtazama Kevin.
"Nini? Una kichaa Torres? Aisee... kama ni mambo haya ya kuzinguana kise(...) mimi siwezi tena. Fanyeni mipango yenu bila mimi. Nimemaliza," Kevin akaongea kwa hasira.
Akanyanyuka na kuanza kuondoka, lakini Kendrick na Torres wakamfata na kumzuia. Kevin akawa anawaangalia kwa mashaka, kwa sababu walikuwa wamemkingia asipite popote.
"Ulitaka info za Jacob za nini?" Kendrick akamuuliza.
"Sijatafuta mimi info za yeyote!" Kevin akafoka.
Kendrick akamwasha kofi zito usoni! "Usinisemeshe hivyo," akamwambia.
"Boss, mimi sijafanya hivyo!" Kevin akasema.
"Kinachokufanya utake kukimbia ni nini?" Kendrick akauliza.
Kevin akatulia tu huku akipumua kwa hasira.
"Ulikuwa unataka kumwambia Jacob kuhusu sisi, siyo?" Kendrick akauliza.
Kevin akaangalia saa yake kiufupi, kisha akamwangalia Kendrick na kusema, "No. Siyo nilikuwa. Nimeshamwambia!"
Torres akakaza macho kwa kushangaa, na papo hapo yeye na Kendrick wakatoa sauti za maumivu baada ya kupigwa kwa risasi sehemu za chini za miguu yao! Wakadondoka chini bila kuelewa kilichotokea, kwa sababu hakukuwa hata na sauti ya nguvu ya mlio wa risasi, na haikueleweka zilitokea wapi. Lakini sauti za mingurumo ya gari zilisika kutokea ule upande mwingine, na ikawa wazi kwamba kuna mtu au watu fulani walikuwa wamefika hapo. Kwa kugundua hii ilikuwa ni njama ya Kevin, Torres akajikaza na kujitahidi kukitoa kifaa chake cha mawasiliano ili amtumie LaKeisha tahadhari, lakini Kevin akamwahi na kumkanyaga mikononi vibaya sana. Akamtolea na silaha yake upesi na kuirusha pembeni, kisha akamsogelea na Kendrick na kufanya hivyo hivyo pia.
"Kevin hhssss... unafanya nini?"
Kendrick akauliza swali hilo, akiwa anahisi maumivu makali miguuni, lakini Kevin hakumjibu, bali akabaki tu kumtazama kwa chuki kubwa. Kisha macho yake yakaanza kulekea upande wa nyuma yake Kendrick, na tayari Kendrick alikuwa ameanza kusikia hatua za mtu zikija kutokea nyuma yake. Torres akajigeuza na kumwona aliyekuwa akija sehemu hiyo, mwanaume mrefu aliyekuwa na mwonekano kama mwarabu, huku mkononi akiwa amening'iniza bunduki ndefu ya shabaha ya mbali, naye akaelewa kwamba bila shaka huyo ndiye aliyewapiga kwa risasi kutokea mbali.
Mwanaume huyo, akiwa ndiyo yule yule Sniper wa Jenerali Jacob, akasimama umbali mfupi kutokea alipokuwa Kendrick, huku akimtazama Kevin kwa umakini. Kutokea kushoto kwake, wakaanza kuja wanaume wale wengine wa Jenerali Jacob, wakiwa wameelekeza bunduki zao kwa watatu hao. Kevin akanyanyua tu mikono yake juu kama tahadhari, na kutokea nyuma zaidi akapata kumwona sasa Jenerali Jacob akiwa anakuja taratibu na sigara yake mdomoni. Wanaume hao wa Jenerali wakawazunguka hatimaye, huku baadhi wakiwafata Kendrick na Torres na kuwanyanyua kwa nguvu ili wapate kumwona Jenerali vizuri zaidi.
Kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi kirefu sana, Kendrick akawa amekutana uso kwa uso na adui yake mkuu, lakini hivi siyo alivyotarajia mambo yangekuwa kabisa. Akawa anamwangalia mwanaume huyo kwa hasira sana, huku bado akihisi maumivu miguuni mwake. Jenerali Jacob akafika usawa wa Kevin na kusimama, naye akaitoa sigara yake nene mdomoni na kumshusha, kisha kumpandisha tena kwa macho yenye dharau.
"Shusha mikono dogo," Jenerali Jacob akasema.
Kevin akaishusha mikono yake.
"Mbona wako wawili tu?" Jenerali Jacob akamuuliza.
"Wengine wanakuja. Walikuwa na mpango wa kumkamata Weisiko kwanza, halafu ndiyo waje na huku kukushika wewe," Kevin akasema.
"Kwa hiyo inamaanisha wameshamkamata Weisiko?"
"Ndiyo. Lexi na wengine wanakuja huku, lakini pia... kuna mmoja amebaki kule nilikokuelekeza... kule tulipokuwa... nadhani..."
"Usiwaze kuhusu hilo. Lishashughulikiwa," Jenerali Jacob akamkatisha.
"Unamaanisha nini?" Torres akauliza.
"Ooh... kale kanyumba kenu mnakojifichia hahah... yeeah, nimetuma watu huko wakalipue kote," akasema Jenerali Jacob.
"Hhh... kweli Kevin... sss... aaghh... nini kimekufanya uamue kutusaliti?"
Torres akauliza hivyo akihisi maumivu, na akiwa anahofia usalama wa LaKeisha kwa kuwa ndiye aliyekuwa huko kwenye nyumba yao ya maficho. Lakini Kevin hakumpa jibu, bali akaendelea tu kumtazama Jenerali.
"Chukua simu, or whatever mnachotumia, wapigie... now," Jenerali Jacob akamwambia Kevin.
Alikuwa anamaanisha awapigie wakina Lexi. Kevin akachukua kifaa kile na kuanza kuwatafuta. Alikuwa akifanya hayo yote huku akihisi hofu kiasi kumwelekea mwanaume huyu.
"Waambie mmeshanikamata, na mko njiani kwenda huko walikomweka Weisiko, kwa hiyo warudi huko haraka maana ndiyo mtakapokutana. Harakisha," Jenerali Jacob akamwambia.
Kevin akasogea pembeni ili kwenda kufanya kama alivyoambiwa.
Jenerali Jacob akasogea karibu na aliposhikiliwa Kendrick, naye akatabasamu na kusema, "At last."
"Jacob... huu siyo mwisho..." Kendrick akasema.
"Ahahahah... uko sahihi, na hauko sahihi. Huu utakuwa mwisho kwako, siyo kwangu," Jenerali Jacob akasema.
"Boss... sss... am sorry... kama ningewaonya mapema...." Torres akasema kwa huzuni na maumivu.
"Majuto hayatasaidia chochote sasa hivi mdogo wangu. See Kendrick... bado huelewi. Yaani you haven't grabbed the grasp of the f(......) situation you put yourself in, even the least of it. Hakukuwa na haja ya kujizungusha huku kote. Shida ilikuwa ni mimi, si ndiyo? Ungefanya tu mpango, ukatafuta hitman wa bei chee tu ili animalize. Lakini ukaona u-enjoy muda wako wote kufanya hivi vi-plot vya kijinga kijinga... vimekufikisha wapi?" Jenerali Jacob akamwambia.
"Hhh... utaanguka tu Jacob. Hata kama haitakuwa mimi ninayekuangusha... lakini najua utaanguka tu," Kendrick akasema.
"Ahahahah... nani? Nani atakayeniangusha mimi, mtoto wake Casmir? Umemwingiza mtoto mdogo, wa wazazi marehemu, yatima, kwenye huu upuuzi wako. Hakutakuwa na chochote kwake kinachobaki zaidi ya kifo tu. Uzuri wangu mimi huwa sipendi kujizungusha, kwa hiyo kwa hilo sitachelewesha," Jenerali Jacob akasema.
Kevin akawa amerudi usawa wa Jenerali Jacob na kumwambia kwamba tayari alikuwa ameshamwambia Lexi kwamba wako njiani kwenda kule walikomweka Weisiko, naye Lexi akawa amekubali kurudi huko.
"Kifo utakachokufa Kevin, kitakuwa kibaya kuliko unavyofiki...."
Jenerali Jacob akawa ametoa ishara kwa wanaume wake, na kabla Torres hajamaliza kuongea maneno hayo, wanaume hao wakaanza kuwapiga sana yeye na Kendrick. Waliwapiga mno bila kuacha, na wakati huo Jenerali Jacob akawa amesogea pembeni na Kevin.
"Huyo mtoto wa Casmir... yuko pamoja na Nora, si ndiyo?" Jenerali Jacob akauliza.
"Ndiyo, wako pamoja," Kevin akajibu.
"Okay. Ni vizuri umetambua unapopaswa kuwa kijana. Uko kama Weisiko, na huwa nina tendency ya kuwa-favor sana wale wanaonionyesha uaminifu. Lakini ukithubutu kuni...."
"No, hapana. Siwezi kukugeuka," Kevin akamkatisha.
"Oh, siwezi kuwa na uhakika kwa sababu... umemgeuka Kendrick," Jenerali Jacob akasema.
"Ndiyo, na nimefanya hivyo nikijua kabisa kwamba kwako itakuwa tofauti. Nilipokutafuta na kukwambia kila kitu, nilijua upande wako ndiyo wenye nguvu zaidi, kwa sababu hawa wasingeweza kukushinda wewe hata kidogo na tumipango twao twa chooni..." Kevin akasema.
Jenerali Jacob akatabasamu.
"Nitakuwa mwaminifu kwako. Nitapigania upande wako. Sikuzote za maisha yangu zilizobaki nitakuwa upande wako tu," Kevin akasema.
"Okay. Inatosha," Jenerali Jacob akawaambia wanaume wake.
Wakaacha kuwapiga Kendrick na Torres. Kufikia sasa walikuwa hoi, wakivuja damu nyingi sana usoni, na wakihisi kama miili yao imekufa ganzi kabisa kwa kupigwa vibaya sana.
"Sijali sababu zako. Lakini nataka unithibitishie zaidi kwamba kweli utakuwa upande wangu," Jenerali Jacob akamwambia Kevin.
Kevin akabaki kumtazama kwa umakini, na mwanaume huyo akamweleza kile alichotaka afanye wakishatoka hapo...."
★★★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★★★
WHATSAPP +255 787 604 893