SEHEMU YA 08.
Asubuhi na mapema Masalu akaamka na kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuijaribu simu ya Aisha kama kawaida yake. Alitaka kujua kama alikuwa akipatikana ama la. Alimpigia na kumpigia lakini msichana huyo hakuwa akipatikana.
Kichwa chake kikauma, moyo wake ukamuuma mno, hakuamini kama kweli angemkosa msichana huyo mara baada ya kumzingua mara mbili. Alijijua hakuwa na kosa lolote lile, ni kweli alimzingua lakini alifanya hivyo si kwa kukusudia, bali kulikuwa na jambo fulani ndilo lililomfanya kuwa hivyo.
Sasa mawazo yakaongezeka, alichokifanya ni kuondoka nyumbani kwake na kuanza kuelekea Mburahati. Alikumbuka kwamba siku iliyopita alikwenda huko, cha ajabu kabisa, eti hakupakumbuka mahali alipokuwa akiishi Aisha na wakati alikwenda naye na ndani akaingia.
Alichukua bodaboda ambayo ilimpeleka mpaka huko. Alipofika, akateremka na kuanza kuelekea kwenye njia ileile aliyopita siku ile. Kwa siku hiyo aliikumbuka vilivyo kwa kuwa ilikuwa ni asubuhi, akawaza inawezekana jana hakupakumbuka kwa kuwa ilikuwa ni usiku.
Alitembea, alikata vichochoro na hatimaye kukutana na nyumba hiyo. Uso wake ukajawa na tabasamu pana, akakenua na kuanza kuufuata mlango kwa lengo la kugonga hodi. Alipoufikia, akaanza kugonga.
Sauti ya msichana ikasikika kutoka ndani. Aliifahamu sauti hiyo, ilikuwa ni ya Aisha, akajawa na tabasamu pana kwamba sasa ulifika muda wa kuzungumza na msichana huyo na kumuomba msamaha kwa yote yaliyokuwa yametokea.
Mara akatokea na macho yake kutua kwa Aisha! Ni kweli alikuwa yeye! Alipendeza, japokuwa ilikuwa ni asubuhi lakini uzuri wake haukujificha hata kidogo, tabasamu lake likamfanya kuvutia mno.
“Karibu sana!” alimkaribisha msichana huyo.
Masalu akaingia ndani. Alimwangalia Aisha, aliendelea kumpenda, tena siku hiyo alimpenda zaidi na zaidi, wakaelekea sebuleni na kukaa kwenye kochi. Aisha akatoka hapo na kwenda kumchukua soseji kwenye friji ambazo alikuwa ameziandaa kwa lengo la kunywa nazo chai, akampa Masalu. Akaanza kuzila.
Aisha hakuongea kitu chochote kile, alikaa kwenye kochi na kuanza kumwangalia Masalu aliyekuwa bize akila. Kwa kumwangalia tu aligundua mwanaume huyo alikuwa na furaha tele kumkuta mahali hapo, alikuwa na kesi naye na ilikuwa ni lazima azungumze naye.
“Naomba unisamehe mama!” alisema Masalu kwa adabu zote.
“Unajua kosa lako nini?”
“Ndiyo! Kosa langu ni kukuzingua kwa mara mbili ila naomba nikwambie jambo moja,” alisema Masalu.
“Jambo gani?”
“Sikukusudia kukukosea!”
“Hilo wala sio kosa hata kidogo! Dharura hutokea,” alisema Aisha huku akiwa pale kwenye kochi na miguu yake ikiwa kwa juu.
“Najua!”
“Kwa hiyo kosa lako umelijua ama hujalijua?”
“Nilijua ni hilo, kama si hilo, hebu niambie unalotaka kuniambia!” alisema Masalu.
“Kosa lako ni kuokotaokota hovyo wanawake na wakati una mke,” alisema msichana huyo huku akimwangalia Masalu aliyekuwa bize akila soseji.
Masalu akashtuka kidogo kusikia hivyo, ni kitu ambacho hakutegemea kukisikia kutoka kwa mtu kama Aisha, mtu ambaye aliwasiliana naye sana mpaka wakakubaliana kuonana loji na kufanya mapenzi, sasa alikuwa akizungumza maneno gani?
“Ni kwa sababu ninakupenda!” alisema Masalu.
“Kampende mkeo! Si kule kanisani ulisema utampenda maisha yako yote, imekuwaje tena baba?” aliuliza Aisha huku akitoka kicheko cha chini.
“Hebu tuachane na masuala ya mke wangu kwanza!” alisema Masalu, alionekana kummaindi kidogo.
“Sawa. Nakuja!” alisema msichana huyo na kuondoka kuelekea chumbani.
*
Watu walisimama pembeni ya makaburi wakimwangalia mwanaume mmoja aliyekaa kwenye kaburi moja na kula majani. Hawakujua mwanaume huyo alikuwa nani na alikuwa akifanya nini mahali hapo. Kila mmoja alikuwa akisema lake, kuna wengine walisema alikuwa kichaa lakini wengine wakasema alikuwa na akili timamu.
Sasa wakaanza kubishana. Kwa jinsi mwanaume huyo alivyovaa, ilikuwa ni vigumu kukubaliana kwamba alikuwa kichaa, alipendeza, alionekana kuwa mwanaume nadhifu sana, sasa swali likawa moja tu, kwa nini alikuwa akila majani?
Huyo hakuwa mwanaume wa kwanza kuwa kwenye kaburi hilo, kulikuwa na watu wengi, hasa wanaume waliokuwa wakifika mahali hapo na kukaa juu ya kaburi hilo. Kuna wengine walikuwa wakifika na kula mchanga, wengine udongo, huyo wa siku hiyo alifika hapo na kuanza kula majani.
Watu walikusanyika, walikuwa ni zaidi ya ishirini, kila mmoja alikuwa akimwangalia, wale waliokuwa wakiendelea na mambo yao, sasa wakaacha na kusimama wima na macho yao yakiwa kule makaburini. Huyo mwanaume aliwashangaza.
“Huyu kama mwanaume wa tano hivi kuja hapa makaburini na kukaa pale,” alisema kijana mmoja, alikuwa fundi viatu aliyekuwa na kibanda chake pembeni ya makaburi.
“Acha utani!”
“Kweli tena! Kuna mmoja alikuja wiki iliyopita, alikaa palepale kwenye lile kaburi na kuanza kula mchanga. Aisee nilimshangaa sana. Sasa leo amekuja mwingine,” alijibu fundi huyo.
“Kwa hiyo huyu si wa kwanza?”
“Ndiyo! Halafu jamaa alikuja juzi hapahapa, akaenda kukaa kwenye lilelile kaburi!”
“Ama la ndugu yake?”
“Hamna! Lile kaburi la demu fulani hivi anaitwa Aisha! Alikuwa anaishi mtaa wa nyuma hapo!”
“Sasa kwa nini watu wanakwenda kwenye kaburi lile?”
“Hata najua basi kaka!”
Mwanaume huyo alishangaza mno, watu waliokuwa na simu zao, wakazitoa na kuanza kumpiga picha, kwao ilionekana kama kituko fulani hivi, mtu kwenda makaburini na kuanza kula majani, hakika iliwashangaza.
Baada ya watu kujaa na kufikia hamsini, hatimaye mwanaume mmoja akajitolea na kwenda kumshtua mwanaume huyo, alihitaji kwanza kujua kama alikuwa kichaa ama la! Akaanza kupiga kelele huku akimsogelea, baada ya kumfikia, akamshika begani.
Mwanaume huyo alikuwa Masalu.
Masalu akashtuka baada ya kuguswa begani. Alimwangalia mwanaume aliyemgusa, alimshangaa, hakumfahamu na hakujua alikuwa akifanya nini mahali hapo.
Aliangalia vizuri alipokuwa.
Tobaaaa!
Hakukuwa ndani ya nyumba ya akina Aisha, alikuwa juu ya kaburi moja akiwa amekaa, alishangaa mno, hakujua alifikaje mahali hapo. Ilikuwaje mpaka kuwa makaburini?
Akasimama na kuanza kuangalia huku na kule. Kulikuwa na idadi kubwa ya watu, wote hao walikuwa wakimshangaa, alishangawa kwa kuwa alikaa makaburini, mkononi mwake alikuwa na majani.
Hapo ndipo alipogundua hakuwa akila soseji bali majani. Akayatupa chini.
“Bro! Imekuwaje tena?” aliuliza mwanaume huyo.
Masalu hakujibu lolote lile, bado alipigwa na bumbuwazi kwa kile kilichtokea, alishangaa, alijiuliza ni kwa namna gani alifika hapo makaburini, hakuwa na jibu lolote lile.
“Imekuwaje umekaa makaburini na kula majani?” aliuliza jamaa huyo.
“Nimefikaje makaburini?”
“Tukuulize wewe!”
“Hapana! Nilikuwa kwa akina Aisha!”
“Aisha ndiye nani?”
“Aisha.....” alisema Masalu, aliyageuza macho yake na kuangalia kaburi lile, liliandikwa Aisha Majidi, yaani huyo Aisha alizikwa hapo.
Akashtuka mno! Hakuamini alichokuwa akikiona mbele yake, ni kama alikuwa amechanganyikiwa na jamaa huyo akagundua, kwanza akamtoa humo makaburini na kumpeleka pembeni, alijua alichanganyikiwa.
Wanaume wengine watatu wakamsogelea na kumjulia hali. Hawakumjua lakini kwa maelezo ya fundi viatu alisema hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwake kumuona jamaa huyo, walitaka kujua kilichokuwa kimetokea.
Kwa kuwa hakujua lolote lile, akawa hana jinsi, ikabidi aanze kuelezea kuhusu huyo Aisha, jinsi alivyokutana naye, walivyojenga urafiki na mpaka kuanza kwenda nyumbani hapo, kumbe alipelekwa kaburini.
“Aisee! Pole sana!”
Huku akiwa haelewi kilichokuwa kikiendelea, mwanamke mmoja akatokea hapo na kuuliza kilichotokea, akaambiwa, alichokisema ni kwamba mama Aisha alitakiwa kuonana na mwanaume huyo aliyekwenda hapo makaburini, angeongea naye na kumpa dawa ambayo ingemfanya kutokusumbuliwa tena na marehemu Aisha.
Kila mtu ambaye alikwenda hapo makaburini, ilikuwa ni lazima kupelekwa nyumbani kwa mwanamke huyo na kupewa dawa. Aisha alifariki zamani sana, tangu mwaka 1999 na walichokuwa wakikutana nacho watu hao hakuwa Aisha bali jini.
Kwa nini alikuwa hivyo?
Kwa nini hakuwaua?
Siri zote alikuwanazo mwanamke huyo. Hivyo Masalu akachukuliwa na kupelekwa nyumbani kwa akina Aisha huku akiwa bado hajakaa sawa kichwani mwake. Alikuwa na mawenge fulani hivi.
Je, nini kitaendelea?