SoC01 Simulizi: Kipofu aliyeiona 5x5 ageuka kuwa engineer

SoC01 Simulizi: Kipofu aliyeiona 5x5 ageuka kuwa engineer

Stories of Change - 2021 Competition

Eng Inc

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2017
Posts
631
Reaction score
944
Ni takribani miaka ishirini (20) sasa imepita tangu kutokea kwa tukio adhimu kabisa ambalo kwa kiasi kikubwa nadiriki kusema liliweza kubadili historia ya maisha yangu. Sakata zima linaanzia nikiwa shule ya msingi Chamwino iliyopo katika Manispaa ya Dodoma au Dodoma Mjini enzi hizo (kwa sasa ni Jiji).

Muda ni mwalimu mzuri sana na pia tunapokua kwenye nafasi fulani ya kusaidia watu busara ituongoze zaidi kuliko matumizi ya nguvu. Kupitia kisa hiki au historia hii fupi utaweza kujifunza jinsi watu wanavyoweza kukudharau leo na endapo ukiweza kukataa dharau hizo ni suala la muda kibao kugeuka na hatimae itabaki tu historia.

Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha wasomaji wote wa stori hii kuhusiana na nguvu za asili (law of attraction) ambazo kila mmoja wetu kwa namna yake ameumbwa nazo na wengi wetu mara nyingi hatujui kama tunazo na zinafanyaje kazi katika maisha yetu, nguvu za asili ni somo pana sana ambapo kwa leo nilifupishe kwa kutambua uwezo wa hizo nguvu kufanya kazi endapo mtu utajiamini na kukisimamia kile unachokitaka bila kuyumbishwa. Pia nikiri wazi kupitia uzoefu nilioupata katika kipindi cha miaka hii kadhaa naona kabisa law of attraction jinsi ilivyofanya kazi pasipo mimi kujua maana kuna kitabu kinaitwa ASK AND IT IS GIVEN by Abraham Hicks kuna maneno aliyaandika akisema nanukuu "NOTHING CAN OCCUR IN YOUR LIFE EXPERIENCE WITHOUT YOUR INVITATION OF IT THROUGH YOUR THOUGHT", akimaanisha hakuna kinachoweza kukutokea katika maisha yako kama hujakiita kupitia mawazo yako, mwisho wa kunukuu. Naomba tujumuike pamoja hadi mwisho wa mada.

Mwaka 2001 nikiwa nipo darasa la tatu (3) katika shule tajwa hapo juu yamkini naweza kuwa ni kijana mdogo tu kwa sasa ila itoshe tu kusema nikiwa kijana mdogo zaidi hasa kiumbo na kimo tena nikiri kwa kusema nikiwa mjinga kabisa.

Mwalimu wetu mmoja aliyekuwa akitufundisha somo la hisabati (hesabu) ambaye kwa sasa ni marehemu (Mungu ampumzishe kwa amani), nakiri na nadiriki kusema kwa kupitia mwalimu huyu jina lake nalihifadhi aliweza kuwa chachu ya leo hii mimi kuwepo hapa nilipo na siwezi kumsahau hadi siku naondoka katika ulimwengu huu. Mwaka huo wa 2001 unaweza pia ukawa ni miongoni mwa miaka ambayo ilikuwa ni migumu katika safari yangu ya kuitafuta elimu lakini hatimae leo hadi napata muda wa kuandika nakala hii fupi kumbe ulikuwa ni mwaka wa kubadili na kuitengeneza historia ya maisha yangu. Nichukue fursa hii kumshukuru sana mwalimu yule na namuombea kwa Mungu ampumzishe anapostahili maana huenda kwa kupitia yeye aliweza kunifungulia njia na kufanya safari yangu ya elimu isije kuwa ngumu tena.

Siku moja wakati tupo darasani majira ya mchana, kama ilivyo kawaida kwa shule zetu za msingi hasa za serikali kuna somo linaitwa “Kuzidisha” maarufu kwa jina la “TABLE”, tulisimamishwa darasa nzima na atakayejibu ndo ataruhusiwa kukaa ambapo mwalimu akiuliza swali unanyoosha kidole akikuchagua kama ukitoa jibu sahihi ndipo utaruhusiwa kukaa au vinginevyo ukishindwa kujibu kuna fimbo zako kadhaa zinakusubiri na kama mnavyojua tena jinsi walimu wa miaka ile walivyokuwa wanajua kucharaza. Mwalimu akauliza 5x5 ni ngapi? Wanafunzi kadhaa tukanyoosha vidole na ndipo aliponichagua mimi ili nijibu swali hilo, baada ya kujibu swali hilo tena kwa ufasaha kabisa gafla nafsi yangu iliingia kwenye huzuni na sononeko kuu maana wenzangu wote ambao walitangulia kujibu pindi tu wanapojibu maswali walikua wanakaa chini lakini katika hali nisiyo itarajia na ya kushangaza mwalimu yule alinikejeli kwa maneno haya: “Leo Kipofu Kaona Mwezi”, licha ya mwalimu yule kuwa ni mkali na hanaga masihara lakini mara tu baada ya yale maneno yake darasa zima liliangua kicheko kwa kunicheka kiasi kwamba nilijuta ni kwanini hata nilijibu lile swali, kwakweli nilijisikia vibaya sana siku hiyo kiasi kwamba hadi leo tukio lile nashindwa kulisahau maana nilihisi kama nimetukanwa, moyoni nikasema "mimi sio kipofu” na sitaki kuchekwa tena, huu ujasiri sijui hata ulitokea wapi.

Nakumbuka vizuri baada ya tukio lile kupita niliishi maisha ya unyonge sana na kujiona sina uwezo wowote katika masomo ukichanganya ukali wa yule mwalimu sikuweza tena kujibu swali lolote lile darasani nikihofikia kuchekwa. Kisa hiki nimekuja kukiona kikitaka kidogo kufanana na historia ya Ben Carson katika kitabu chake cha Think Big ambacho kwa bahati nzuri nilikuja kukisoma pindi hayo yote yakiwa tayari nimeyapitia pia katika safari yangu ya elimu. Siku hazikuwa nyingi baada ya lile tukio kutokea tulifunga shule kwa ajili ya kumaliza muhula wa kwanza.

Katika msimu wa baridi wa mwaka 2001 yani kati ya mwezi wa sita (6) hadi wa nane (8) nilifanikiwa kwenda jando (wanaume wanaelewa) na kwa bahati nzuri hii ilikuja kuwa ni moja ya nguzo kubwa ya mimi kubadilika na kuanza kuishi kwa kujielewa na hata uwezo wa kujiamini ulikuja kuongezeka zaidi sikukujua ni kwanini hasa ilikuwa hivyo. Shule ilipofunguliwa kwa ajili ya muhula wa pili sikuweza kuudhuria maana nilikuwa bado sijapona vizuri na ilipelekea kushindwa kuhudhuria masomo kwa takribani mwezi mzima, katika hili naweza pia kuishauri jamii kutahiri watoto kabla ya kuanza masomo isije kuleta usumbufu kwa mtoto na kupelekea kukosa baadhi ya mambo na masomo au pia kutoa taarifa mapema katika maeneo au taasisi husika ambayo inamuhudumia mtoto.

Siku ya kwanza tu nafika shule na kuingia darasani baada ya mimi kutoka jando nilikiona cha mtema kuni, mwalimu yule wa hesabu alitoa zoezi ambapo nakumbuka moja kati ya maswali ambayo yalikuwepo kwenye zoezi lile yalikuwa ni maswali ya kugawanya na kwa bahati mbaya wakati anafundisha sikuwepo darasani na sikuwa na mtu wakunielekeza jambo lolote kuhusu shule kipindi nipo jando. Wakati nimelala chini naugulia maumivu mwalimu yule akiendelea kunicharaza, gafla nilihamaki kuona kuna mwanafunzi mwenzangu ambaye sikuwezaga kumtambua hadi leo huenda ni kutokana na maumivu niliyokuwa nayaugulia muda huo alipata wapi ujasiri wa kunitetea mbele ya yule mwalimu (R.I.P) na akaweza kumueleza kwamba “Mwalimu, huyo ametoka jando wakati unafundisha hili somo hakuwepo”, hiyo ikawa ponea yangu. Kusema ukweli mwalimu yule alijisikia vibaya ikapelekea hadi kuniomba msamaha jambo ambalo kwangu mimi niliona kama ni muujiza kuombwa msamaha na mwalimu yule. Mara tu baada ya tukio lile kutokea siku ile, ukiachilia mbali ujinga na utoto niliokuwa nao kabla, mwalimu yule hadi namaliza ule mwaka hakuwahi kunichapa tena na binafsi niliweza kubadilika na kuwa na bidii ambapo hadi namaliza elimu ya juu sikuwahi kufeli hata darasa moja au kupata changamoto yoyote ya kiufundi.

Katika kufupisha urefu na mlolongo mzima wa safari na mazingira ya elimu niliopitia nifupishe kwa kusema kwamba, mfumo wetu wa elimu una mapungufu mengi sana hasa
kwa uzoefu wangu wa baadhi ya shule za serikali nilipopata nafasi ya kupita huko ambapo watoto na makundi mengi ya vijana yanapotea na ni watoto wachache sana wanaweza kuhimili changamoto lukuki zilizopo.

Nilifanikiwa kufaulu katika ngazi zote za kielimu yani msingi, sekondari (O level and A level) na chuo kikuu, pia kwa sasa naendelea na masomo yangu ya shahada ya pili (masters in structural engineering) katika moja ya vyuo vikuu hapa nchini.

Sipendi sana kuongelea mafanikio yangu ya kielimu na kimaisha kwa ujumla ila nikidokeza kwa ufupi tu kutokana na stori yangu hii fupi, mara tu baada ya kuhitimu shahada yangu ya kwanza niliweza kupata nafasi ya kuajiriwa serikalini katika moja ya wizara zinazojihusisha na masuala ya ujenzi ambapo kipofu mimi nilifanya kazi kwa miaka mitatu kabla ya kuacha kazi serikalini na kufungua kampuni yangu mwenyewe inayotoa ushauri kuhusu masuala ya ujenzi (consulting firm), niliweza kusajiliwa kama moja kati ya wahandisi wabobezi katika fani ya ujenzi kama inavyojionyesha katika picha hapa chini na pia kwa sababu za kimaadili na kiusalama sitoweza kuweka baadhi ya nyaraka sambamba na kuonyesha umiliki.

Kwa hapa nilipofika nimejifunza kusamehe, kushukuru na kutokuwasema watu vibaya hasa unapokuwa kwenye nafasi ya kuwasaidia watu na jamii kwa ujumla. Wito wangu ni kwa sisi vijana kuacha kujisikia unyonge hasa kwa wale watu waliotuzidi vitu fulani kwenye maisha, maneno yao makali yawe ni chachu katika kusimamia kile tunachokiamini na tukipiganie kweli kweli pasipo kutegemea msaada kutoka upande wowote.

Sikukubali hali ya kuwa kipofu, maneno huumba, uchungu na maumivu ambayo mtu anaweza kuyapata na kuyapitia yana mchango mkubwa sana katika safari ya mafaniko. Maneno ya mtu kamwe yasikurudishe nyuma inatakiwa usimame daima katika kile unachokiamini na pia kila wakati utambue Mungu ni mwema na yupo kwa ajili yetu sote.

Engieer Kipofu.PNG
 
Upvote 2
Back
Top Bottom