Simulizi: Msegemnege

Tupio la XXXI – Milioni sita


Ilipoishia…


“Sasa hapa kuna cha kujadili?! Wewe orodhesha mahitaji yako ya safari kisha mtumie tuone sinema hii itaishia wapi!” Baba Omari alisema.

Hivyo ikanibidi niandike mahitaji yangu:-

  • 250,000 Passport na maandalizi yake
  • 2,500,000 Nauli na mahitaji yake
  • 200,000 manunuzi ya nguo
Hivyo nikamuambia nahitaji dola 1,200 ili kukamilisha safari.

Alichonijibu Nasreen ndio sikutarajia..

“1,2000 USD?, okay Omari, I will see what I can do” Nasreen alijibu meseji.

Nikawa na wasiwasi, sijui ataniona nina tamaa nimeandika hela nyingi! Kwa kweli sikuwa na furaha kama ya mwanzo baada ya jibu lile.


Sasa endelea…

Siku iliyofuata saa mbili na nusu usiku…

Whatsapp chat


Nasreen: “Assalaam alaikum Omari”

Omari: “Wa alaikum salaam Nasreen, how are you today?”

Nasreen: “I’m okay. I discussed with my family about your issue and we concluded that I will send you three thousand dollars for your preparation…”

Nasreen: “We found that you are so honest and not greedy as far as our conversation sisnce we came to know each other is concern…”

Nasreen: “My family is now eager from seeing you”

Omari: “Thanks Nasreen”

Nasreen: “Do all what is needed and when it comes to air ticket we will sort it out…”

Nasreen: “You will let me know every step in getting your travel documents”

Omari: “Thank you very much Nasreen, I am so gratefull”

Nassreen: “We also found the easiest way to send you money…”

Omari: “How?”

Nasreen: “As we saw, we bet that you don’t have a bank account, so we thought of using Western union money transfer but my brother tipped us the best ways…”

Omari: “Enhe!” (Omari alijisahau tena akaandika Kiswahili)

Nasreen: “ My elder brother suggested that we better use Somali wire channels but my other brother suggested to use Pemba channels whereby the transfer fee is very cheap and its safe as Somali channels and good enough Pemba channel agents in Dar es Salaam are so many…”

Nasreen: “You will go to Sikukuu/Tandamti streets, call this number tomorrow (aliiandika), they will give you equivalent to three thousand united states dollars. Your name and this secret code (aliiandika) will be your passport to get your money…”

Omari: “Thanks you Nasreen, I can’t thank you enough”

Nasreen: “You are welcome Omari”

Nasreen: “Ok Omari, got to go, we will chat tomorrow”

Omari: “Ok, tomorrow then”

Ni kwamba Omari alipewa namna ya kuweza kupokea zile hela kwa ajili ya maandalizi ya safari. Familia ya Nasreen ilifurahia uaminifu wa Omari katika mazungumzo yake na Nasreen. Sijui walitumia kipimo gani lakini walimuona hivyo. Badala ya dola elfu moja mia mbili wakaamua kumtumia dola elfu tatu ambapo ni hela ndefu sana kibongo bongo na kwa hali ya Omari ilivyokuwa.

Omari anasimulia…

Asubuhi mapema mapema nikajiandaa kutoka nyumbani. Mazungumzo yangu na Nasreen ya jana sikuwashirikisha wazazi wangu. Nilitaka nione matokeo kwanza kisha ndipo niwashirikishe.

Saa moja na nusu tayari nilikuwa Kariakoo na begi langu dogo la mgongoni ambayo niliweka magazeti yaliyopitwa na wakati, nikatafuta ule mtaa nilioelekezwa hadi nikafika. Nikapiga simu ikapokelewa, nikajieleza nikaeleweka na nikaambiwa nisubiri maana bado hawajafungua duka.

Kariakoo ilikuwa imeshachangamka lakini vurugu za wamachinga bado zilikuwa hazijakolea. Ilipofika saa mbili kamili nikaona duka lililokuwa jirani na kona ya makutano ya barabara tajwa likifunguliwa. Alikuwa anafungua jamaa mmoja mwarabu hivi alikuwa amevalia kanzu na amefuga ndevu nyingi.

Moja kwa moja nikahisi lile ndio duka husika, basi kwa kuwa ndio walikuwa wanafungua duka wala sikufanya haraka kwenda pale, nikaenda pembezoni mwa soko la kariakoo ili kutafuta kifungua kinywa.

Nikapata maharage niliyochanganya na maandazi mawili niliyo yakatakata pamoja na chapati moja, ilikuwa ni kifungua kinywa maarufu sana na kitamu kweli kweli. Wakati nikiwa hapo nakunywa chai nilishuhudia matukio mawili ya wizi, moja lilikuwa la jamaa sijui ni kutoka nchi gani maana hata lugha yake ilikuwa haieleweki vizuri ingawaje alikuwa mbantu, alikuwa anakimbia huku akipaza sauti kwa kikwao, dakika chache zilizopita alipita msukuma mkomkoteni ile midogo ya matairi ya baiskeli, alikuwa anakimbia na mkomkoteni hatari akiwa amepakia mizigo kadhaa ya maboksi…

“Jamaa wameshamliza…” Yule jamaa muuza chai alisikika akisema

Nami akili yangu ikafunguka; ni kwamba hawa wageni wanaonunua bidhaa Kitumbini au Kariakoo, wasipokuwa makini huwa wanaibiwa sana na vijana wasio waaminifu wasukuma mikokoteni. Yani akinunua anapakia kwenye mkokoteni na kuelekezwa sehemu ya kupeleka huku wakiongozana, lakini mara nyingi wasukuma mikokoteni wao huwa fasta zaidi na mwenye mali akizubaa anaweza kupotezwa asijue mzigo wake umeelekea wapi.

Tukio la pili nililoshuhudia pale asubuhi ile lilikuwa la jamaa kupewa ‘kanyaboya’. Inaoneka huko nyuma walishindwana bei, na mteja akawa anaondoka, sasa yule muuzaji alikuwa anamfuata na kumuambia ongeza kidogo, ongeza kidogo, ongeza kidogo, mwisho ndio akasema, leta hiyo hela. Sasa kitendo cha yule mteja kuingiza mkono mfukoni na kutoa hela na yule muuzaji mwizi alibadilishana mfuko na jamaa mwingine aliyekuwa akifuatana naye lakini wakijifanya wala hawapo pamoja.

Muuzaji alipopokea hela tu, akapotea kwenye uchochoro, yule waliyebadilishana mfuko yeye aliendelea na safari kama hawajuani. Munuzi sijui machale gani yalimcheza, si akafungua ule mfuko na kukuta viatu chakavu na wala siyo vile alivyooneshwa mwanzo, ule mfuko ukaanguka chini naye akashika kichwa na ukulele ukasikika…

“Mamaaaa nimeibiwa!”
---


Nilivyomaliza kunywa chai na kupumzika kidogo na kusikiliza maelezo ya yule aliyeibiwa pamoja na watu wengine tuliomzunguka kusikia kilichojiri nilielekea kule dukani ambapo sasa lilikuwa watu wengi wakinunua mahitaji yao mbalimbali. Lilikuwa ni duka la nafaka na viungo. Niliposogea zaidi ndio nikajuwa kuwa kumbe wale si waarabu bali ni wapemba.

“Assalaam alaikum” Nilisalimia

“Wa alaikum salaam, karibu…” nilijibiwa na muuzaji aliye upande wangu maana pale kuna wauzaji wawili waliosimama, wa tatu amekaa nyuma akifanya mahesabu lakini pia niligundua kuwa kuna wenzao wengine wamesimama kwa nje wakiangalia nyendo za wateja. Walikuwa wamejipanga vizuri, nadhani kwa sababu ya historia ya maeneo hayo yalivyo na duka lao muda wote kuana wateja wanao nunua kwa jumla na kwa rejareja.

“Eee mimi naitwa Omari Juma, nimetumiwa pesa sasa nimeelekezwa nije hapa…” Nilisema

“Anhaa, wewe ndio ulipiga simu asubuhi ee?!” Aliniuliza

“Ndiyo” Nilijibu.

“Okay, karibu, pesa umetumiwa kutoka wapi!” sasa ikawa ni maswali na majibu, lakini jinsi anavyouliza ni ‘very politely & friendly’ huku kama hayuko makini hivi akiendelea na shughuli nyingine…”

“Imetoka Bahrain” Nilijibu.

“Jina la aliyekutumia?”

Nikataja

“Passcode uliyopewa” Aliuliza hili kisha akawa anapitia simu janja yake

Nikataja.

“Kiasi ulichotumiwa?”

Nikataja, kisha akaniambia…

“Okay, subiri dakika moja”

Akawa anaandika kitu kwenye smartphone yake. Mimi nikarudi nyuma kidogo ili kuwapisha wateja wengine waendelee kuhudumiwa ndipo nikaona kuwa kwa nje napo wapo ‘walinzi fiche’ ambapo walikuwa wamesimama kila mmoja kwenye nafasi yake kuangalia wateja na eneo la duka kwa ujumla.

“Sheikh Omari!” mara nikasikia naitwa kwa kupewa cheo cha ushehe…

Ni kawaida sana watu kuitana hivyo hususan kwa jamii ya kipemba.

Yule muuzaji akaniambia…

“Leo chenji haiko vizuri, utapokea saba kasoro kadhaa” (akataja kiasi pale) Ni kwamba siku hiyo dola ilipanda hivyo hela tarajiwa ilipungua kiasi kidogo sivyo kama ilivyotarajiwa kwa chenji ya jana yake.

Milioni sita “cash”, mabunda 6 ya elfu kumi kumi niliyaweka kwenye ile begi katikati ya magazeti kisha nikaliivaa kwa mbele kifuani. Zile zingine nikaziweka kwenye mifuko ya suruali ya jeans niliyovaa na zingine kiasi nikaweka kwenye wallet.

Nikasogea pembeni kidogo wala sikufanya haraka kuondoka. Siku hiyo nilivalia tshirt iliyopauka kiasi pamoja na jeans hizi za viraka viraka vya urembo na chini nilikuwa nimevaa yeboyebo za mtumba. Yebo yebo za mtumba zipo ‘very confortable’, ukianza kuzifaa huwezi kuacha kuwa nazo katika stock yako ya viatu vya wazi, lakin ipia ilikuwa ni mbinu ya kuonekana wa kawaida ili usifuatiliwe na vibaka.

Kutokana na matukio yale mawili niliyoyaona wakati nakunywa chai nikawa makini zaidi. Nikawashukuru na kuwaawaaga kisha nikashika barabara ya Sikukuu kuelekea makutano ya barabara ya mkunguni na livingnstone.

Lakini wazo likanijia fasta nilipoona gari inapiga honi mgongoni ikitaka njia ya kupita. Barabara hiyo siku hiyo na siku zote huwa bize sana kwa watu na magari. Nilipogeuka ndio nikaona ni taxi iliyo sajiliwa na kupigwa mstari maalum wa kuitambulisha…

Pale makutano ya mtaa wa mkunguni na livingstone kuna kijiwe cha taxi, bila shaka na huyu alikuwa anaelekea pale, basi nikamsimamisha kwa kuashiria kuwa nahitaji huduma, akasimama nami nikafungua mlango baada ya kuhamia upande wa kushoto wa barabara. Nikaingia kwenye siti ya nyuma kisha nikalock mlango upande wangu na dereva aliona kile kitendo na yeye akabofya kitufye cha kufunga milango yote, akawasha AC kisha akafunga vioo maana vile vya mbele vilikuwa wazi.

“Tunaelekea wapi ?” aliuliza yule dereva mtu mzima hivi.

“Twende Posta” Nilijibu bila wasiwasi

Gari ikakunja kufuata barabara ya mkunguni tukavuka barabara ya Lumumba hadi tukaingia barabara ya bibi titi, tukaelekea upande wa kushoto, tulivyovuka taa za makutano ya barabara ya Morogoro na bibi titi tukakaa kulia kabisa ili kuingia barabara ya Zanaki…

“Unashukia sehemu gani?” Aliuliza yule dereva

“Twende hadi jengo la Mkapa…” Nilijibu baada ya kupata wazo la kufungua akaunti benki pia kupoteza kufuatiliwa kama kuna mtu alikuwa ananifuatilia.

Dereva akakunja kushoto barabara ya Jamhuri na akasimama eneo la Benjemin Mkapa Pension Tower.

“Bei gani?” Niliuliza kabla sijashuka.

“Elfu kumi tu boss” Alijibu kwa kunipa bei kubwa

“Du! Kumi utaniua, fanya saba basi, au kwa kuwa sijakuuliza kabla?” Niliomba kupunguziwa kiasi.

“We mwenyewe si umeona foleni ilivyo na bei ya mafuta si unajuwa imepanda, haya leta nane basi” Alipunguza.

Nikatoa noti moja ya elfu kumi kwenye wallet kisha nikampatia. Hapo moyoni japokuwa alikuwa amenipiga bei lakini niliona afadhali kwakuwa niliondokana na hatari yoyote ambayo ingeweza kutokea. Nikawa nafungua mlango natoka…

“Chenji yako hii…” yule dereva alinipatia elfu mbili wakati tayari nimeshashuka nipo nje ya gari.

Nikapokea na kuvuka barabara kwa uangalifu na kujongea eneo la benki.

Wakati wa harakati za kutaka kujiunga na Jeshi nilikuwa nimeweka sawa nyaraka nyaraka zangu zote muhimu hadi kadi ya kitambulisho cha Taifa nilikuwa nayo. Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam tulibahatika kupata vitambulisho vya Taifa mapema mara tu baada ya watumishi wa Serikali kupatiwa ingawaje ilichukuwa mwaka mmoja kusubiri.

Pale benki kwa nje nilikuwa wahudumu wawili na meza yao na makaratasi kadhaa, niliwaambia hitaji langu kisha wakaniambia hata wao wanaweza kunifungulia akaunti kwa haraka. Wakaniomba NIN (namba ya utambulisho wa Taifa) nikawapatia, pia wakaniomba kadi yenyewe kama ninayo, nikawapatia na hatua za ufunguaji akaunti zikaendelea…

“Utanataka kuanza kuweka kiasi gani?” Yule dada aliniuliza hela ya kuanza nayo kwenye akaunti huku tayari akiwa amejaza sehemu kadhaa za ili karatasi ya kuingizia fedha…

“Elfu hamsini” Nilimjibu kisha naye akajaza na wakati huo huo nilikuwa nampatia noti tano za elfu kumi kumi kutoka kwenye wallet.

Akazikusanya zile pesa na ile karatasi aliyokuwa anaandika kisha akanipatia zote na kunielekeza niende kwa mhudumu anayepokea pesa mle ndani.

Baada ya lile zoezi kuisha pale benki nikaelekea maeneo jirani na CRDB bank Azikiwe na kudandia Coaster iliyokuwa inaelekea Mwenge.

Mpang o wangu ulikuwa zile hela niziweke benki na kubakisha kiasi kama cha milioni tatu cash ili ndio niende nazo nyumbani. Mwenge pake nikaenda kwa wakala wa huduma za kifedha na kudeposit milioni mbili kwa wakala wa kwanza na milioni mbili zingine kwa wakala mwingine kisha nikaelekea kupanda daladala za kwenda Kawe.

Nilikuwa mwenye furaha sana na mawazo sasa yakawa kwenye utaratibu wa kupata hati ya kusafiria.



Itaendelea kesho in shaa Allah
 
Tupio la XXXII – Kaniki, Shuka jeupe, Jogoo mwekundu na Sembe


Ilipoishia…


Polisi kitengo cha saiba kikaingia kazini, kweli wakakuta huo mtadao wa kusaidia kupatikana kwa wafanyakazi wa ndani www.housemaidaidchap.co.tz na kweli wakakuta kuna mtiririko huo uliomhusu mtoto Gift.

Katika fomu yake ilionekana imejazwa kuwa mtoto Zawadi ana miaka 17, kabila Mhehe, lakini hana baba wala mama bali alikutwa mtaani akiwa katika mazingira magumu.

Aliyemuokota na kujaza zile nafasi alikuwa anaitwa Nghenakwe Nghaminyigwe, hapakuwa na picha yake wala namba za simu.

Polisi walipofuatilia majina yale ilibidi wafunge jalada la upelelezi huo na kuacha kama ilivyo. Ni kwamba waliaza kupata mauzauza na walipotaka kujua asili ya majina ‘Nghenakwe Nghaminyigwe’ waliambiwa kuwa ni asiyejulikana na mwenye kuona mambo yake yeye mwenyewe na asili yake ni Ukaguruni.


Sasa endelea

Kihonda Morogoro


Mama Junior na mama Rose walipatwa na ukiwa baada ya kumsindikiza mtoto Zawadi Msavu, walirudi nyumbani wakiwa wanyonge…

“Sasa itakuwaje kuhusu huduma…” Aliuliza mama Junior

“Mmh, mwenzangu, hata sijui, itabidi tufanye tu hivyo hivyo tuangalie upepo utaendaje” alijibu mama Rose kwa kujipa moja kiasi.

Junior wakati huo alikuwa darasa la saba, tayari alishasoma darasa la tano na la sita kwa mwaka mmoja. Alikuwa kijana sasa anayechipukia ingawaje umri na umbile bado alionekana mdogo sana.

Nyumbani kwao huduma ikaanza kudorora, waumini walianza kupungua, hasa wale waliokuwa wanatoka mbali. Kadri siku zilivyozidi kwenda waumini walizidi kupungua hadi wakabaki wale wana maombi wa Roman waliokuwa wakija siku za Jumamosi kufanya ‘jumuiya’ kabla ya ujio wa Zawadi na wale wa Jumapili wa kanisa la kilokole.

Flash forward

Nyumbani kwa mama Onesmo, mwezi Disemba siku moja kabla ya majibu ya darasa la saba kutoka, usiku wa Ijumaa wakiwa katika maandalizi ya masomo ya kesho kwenye Jumuiya, ghafla umeme ukakatika…

“Hebu ngoja niangalie kwa majirani kama unawaka” Alisikika mama Rose akisema

“Kwa majirani unawaka!” alisema tena mama Rose alipochungulia nje kwa jirani.

“Au umeme umeisha?” Alisema mama Onesmo. (Wanatumia LUKU)

“Hapana, mbona juzi tu nilinunua wa elfu thelathini, haujaisha, labda kuna tataizo…” alijibu mama Rose.

Muda huo ilikuwa ni usiku kama was aa tano hivi , umeme ukawaka tena na kuzimika, na sfari hii kulikuwa kama kuna shoti hivi kwenye chumba alichokuwa analala mama yake Vai, bibi yake Junior.

Wote wakaingia kile chumba, ambacho kilikuwa hakina samani ndani zaidi ya zulia la kawaida, walikifanya kama ni chumba cha kuchezea watoto.

Walifika pale na kukuta bulb inatoa moshi…

“Mmh, hii bulb imeungua…” Alisema Mama Junior

“Ngoja niitoe ili kesho tuibadilishe, huenda hii ndiyo inaleta shoti…”

Mama Rose akaenda kuchukuwa stuli ili apande aitoe ile bulb, wakati huo nyumba yote ni giza, simu za mkononi ndizo zilitumika kutoa mwanga kupitia tochi ndogo.

Wakati mama Rose anahangaika kuitoa ile bulb iliyoungua ghafla stuli ikayumba na kumfanya aanguke hadi chini na kupoteza fahamu…

Mama Onesmo alichanganyikiwa asijuwe la kufanya, huku akitumia simu yake kumulika alimuona mama Rose amelala pale bila kujitingisha…

“Mungu wangu, sijui nini hiki, Mama Rose, Mama Rose! Unanisikia, mama Rose amka jamani, mama Rose!...” Vai alihangaika kumtingisha mwenzake ili aamke bila mafanikio…

Mara akapata wazo la kupiga simu kwa jirani ili pate msaada…

Wakati akitafuta namba ya kupiga ukatokea mwanga mkali mbele yake katika chumba kile, mwanga ambao ulimfanya asiweze kuona mbele kitu kingine zaidi ya ule mwanga naye Vai akawa anajikinga macho kwa mkono wake mmoja na ule mkono ulioshika simu uliachilia simu na kuanguka chini na kusambaratika kama ilivyosambaratika simu ya mama Rose.

Sauti kutoka katika ule mwaka mkali ikasikika…

“Vailet Mwanangu, usihuzunike kwa mtoto Zawadi kuondoka, mimi ni mama yako, nilifariki kwa ajali ya kutengenezwa lakini muda wangu kwa kufa kabisa bado…”

“Nilikulea kwa tabu sana baada ya kutelekezwa na baba yako…”

“Nilikuacha ukiwa mkiwa lakini nilipopata uhuru tu huku nilipo niliamua kukulinda kwa kila namna niwezayo…”

“Ninamlinda mjukuu wangu kwa kila namna, na sasa amefaulu vizuri mtihani wake wa darasa la saba…”

“Atachaguliwa shule ya Serikali, lakini hakikisha unampeleka shule ya seminari ili akamilishe malengo ya kuja kumtumikia Mungu…”


Kisha ule mwanga ghalfla ukatoweka na taa za nyumba zikawaka zote zilizokuwa wazi kasoro chumba hicho walipokuwa mama Rose na mama Junior.

Baada ya kufikicha macho, mama Junior akawa sasa anaona vizuri japo mle chumbani kulikuwa na kiza hafifu sasa, akakumbuka kuwa chini hapo kuna mama Rose alianguka, akainama tena na kumtingisha na kuita…

“Mama Rose, we mama Rose!”

Mama Rose safari hii akaitikia japo kwa sauti ya chini, kisha ainuka na kukaa…

“Nini kimetokea?” Aliuliza mama Rose

“Ulianguka ulipokuwa unajaribu kubadilisha bulb…” Mama Junior alijibu

“Aaaah, Kiuno changu jamani!” Mama Rose alilalamika kwa maumivu ya kiuno.

Ni kwa bahati nzuri tu hakupigiza kichwa vinginevyo ingekuwa ni hadithi nyingine. Mama Junior akamsaidia kuinuka kisha wakashauriana wamtafute fundi aje kubadilisha ile bulb pamoja na kuangalia sehemu iliyokuwa ina shoti.

Mama Junior wala hakumshirikisha mwenzake kuhusu ile hali ya mwanga mkali na sauti iliyomtokea. Baada ya kuwa sawa waliamua kwenda kupumzika vyumbani mwao maana muda ulikuwa umeshaenda sana.

Asubuhi kama kawaida mapema walikuja majirani na baadhi ya wanamaombi kwenye jumuiya ya kila Jumamosi. Ratiba yao ilikuwa baada ya jumuiya za kawaida kwisha sehemu zao ndipo wengine huja kwenye hii jumuiya nyumbani kwa mama Junior kutafakari maneno ya Mungu pamoja ya mambo yao binafsi.

Baada ya ibada hiyo kwisha, mama Junior alisimama na kusema…

“Tumsifu Yesu Kristo!”

Waumini wakaitikia “Milele, amina”

“Bwana Yesu asifiwe” akajibiwa “Amen.”

Mama Junior: “Jamani, nawashukuruni kwa ibada ya leo, Mungu atawalipa mara dufu, lakini mwenzenu bado kuta vitu vinanitokea, nomba ushauri wenu…”

Akaelezea jinsi ilivyokuwa jana pale umeme ulipokatika na ile sauti iliyomsemesha na mwanga mkali.

“Itakuwa mapepo hayo!” Mmoja wa waumini alisema

“Ha! Mama Junior, mbona hukuniambia kama ulitokewa na jambo” Alilalamika mama Rose

“Niliona na umechoka na maumivu, nilitaka upumzike ile leo niliseme hapa nipate ushauri”

“Labda mzimu wa mama yako huo” alisikika mwingine akisema.

“Jumamosi ijayo tutafanya maombi maalum kwa ajili ya jambo hili…” Mama mmoja mtu mzima alisikika akishauri.

Katika wale waumini kuna mmoja alibaki wakati wengine wameondoka, kisha akamshawishi waende kwa mganga wa kienyeji wenye kujuwa mizimu ili akapate ufafanuzi kule.

“Mwenzangu, Mungu yupo lakini pia mizimu ipo na kuna watu wanafahamu hiyo mizimu, inabidi nawe ujisaidie ili ujue kulikoni…” Hayo yalikuwa maneno ya ushawishi ya muumini yule aliye baki.

Basi baada ya chai, wakawaacha watoto wao nyumbani baada ya kuwaandalia chakula cha mchana kabisa kisha wao wakaelekea maeneo ya Kilakala wakapita mbele zaidi hadi karibu na mlima wakafika kwenye nyumba moja hivi ndogo. Nyumba ilikuwa imeezekwa kwa nyasi na banda lingine ndio lilikuwa limeezekwa kwa bati, kulikuwa na uwanja baina ya nyumba hizo mbili ambao ulikuwa umefagiliwa vizuri, pembeni kidogo ya huo uwanja kulikuwa na chungu kikubwa kinachemka.

Baada ya kujieleza kwa mganga waliambiwa wakalete kuku jogoo mwekundu, kaniki, shuka jeupe, na unga kilo moja, vifaa vingine wangepata kwa mganga kwa ajili ya tambiko la awali kubisha hodi mzimuni.

Jioni walirudi nyumbani tayari wakiwa wameshapitia sokoni na madukani kuchukuwa vifaa kwa ajili ya kwenda navyo kesho kwa mganga.

Wakati wa chakula cha jioni kwenye taarifa ya habari kwenye runinga walisikia kutangazwa kwa matokeo ya wanafunzi wa darasa la saba na ufaulu ukiwa umeshuka kwa asilimia chache kulinganisha na matokeo ya mwaka uliopita. Wote mle ndani wakawa na hamu ya kutaka kujuwa Onesmo amefaulu kwa kiwango gani maana hapakuwa na msamiati wa kufeli kwa Onesmo.

Ghafla…

“Mama, kesho msiende kwa mganga!” Junior alibadilisha hali ya hewa wakati wakiendelea kula …

“We Junior, kwa kuwa umeona kuku ndio unadhani tunampeleka kwa mganga?” Alidakia mama Rose

“Hapana mamkuu, ninajuwa mmetoka kwa mganga na mmeambiwa mpeleke vifaa kadhaa akiwemo huyo kuku…” Onesmo alikuwa anamwita mama Rose mamkuu. Alijibu kwa kujiamini kwa kile alichosema.

“Mmh, we mtoto wewe! Nani kakuambia kuwa sisi tulienda kwa mganga?!” Mama yake sasa aliuliza kwa kushangaa.

“Hakuna aliyeniambia, lakini najuwa mmenunua shuka jeusi na jeupe, unga wa sembe na huyo kuku ili mpeleke huko kwa mganga kwa ajili ya matambiko…” Onesmo alifunguka na akaendelea…

“Jambo mnalolitafutamajibu yake mtayapata hapa hapa, majibu utapata kwa yule aliyekuambia kuwa usinipeleke shule ya Serikali…”

Wote pale wakashangaa na kuanza kusikiliza kwa shauku.

“Ndiyo mama, uliambiwa unipeleke Seminari ingawaje nitachaguliwa kwenda kusoma kwenye shule ya Serikali kwa kuwa nimefaulu daraja ‘A’ ingawaje sinto kuwemo kwenye kumi bora kitaifa, lakini pale St. Anne nimekuwa wa kwanza kishule…”

Wote wakashusha pumzi na kupigwa na butwaa huku wakiangaliana…

“Huyo kuku kesho tumchinje tule wenyewe, nina hamu sana ya nyama ya kuku…” Onesmo alisema.

Mama Rose na mama Junior wakawa wanaangaliana kisha wakamfukuza Onesmo aende chumbani kwanza, tayari alikuwa ameshaacha kula, bila shaka alikuwa ameshiba. Onesmo akanawa kisha akaelekea chumbani hapo mezani akawaacha mama zake pamoja na Rose.

“Shoga, sasa tufanyeje, kesho tuende kwa mganga au?” Mama Junior alimuuliza mama Rose

“Wee Rose, chukuwa chakula chako kamalizie kule chumbani mnapochezaga” Mama Rose naye alimuamuru mwanawe atoke pale mezani. Rose alitii na kuondoka eneo lile pamoja na sahani yake ya chakula.

“Mwenzangu, haya maajabu, lakini twendu tu kesho tukishatoka Kanisani tumsubiri mama wawili aje twende naye kama jana ili tuone tutaambiwa nini…” Mama Rose alitoa Rai.

Pamoja na kuwa Junior alikua ni mtoto wa Vai, lakini kwa pale nyumbani hakuonesha kipaji chochote cha ziada zaidi ya akili ya uelewa wa masomo. Na ilikuwa kawaida ya Junior kusema jambo pindi anapoulizwa tu, lakini siku hiyo aliamua kuwaambia wazazi wake mambo ambayo hawajawahi kuyasikia kutoka kinywa chake. Waliokuwa wanajua hali ya utabiri wa Onesmo ni watoto wa shule hususani wa darasa lake nao walikuwa wakiuliza maswala ya kitoto tu kutokana na umri wao labda na Onesmo hakuwa na hiyana, alikuwa anawajibu na maisha yalikuwa yanaendelea.
---


Kesho, Jumapili baada ya kutoka Kanisani, (mama Junior alienda KKKT na Mama Rose alienda Roman…) walienda kule kwa mganga.

Baada ya ‘vimbwanga’ vya awali vya mganga walielekea usawa wa mlimani ambako kulikuwa na mti mkubwa hapo na vichaka kisha mganga akawa anasema maneno ya kubisha hodi kwa kilugha…

“Hodi wakubwa, hodi wenye mji, hodi Kingalu chifu wa wakubwa wa hapa, hodi wote….” Mganga aliendelea kusema maneno mengi yasiyoeleweka kikawaida lakini mradi ulikuwa ni kubisha hodi na kutambulisha wageni waliofika pale ili wasikilizwe shida yao…

Baada ya kitambo kadhaa cha muda kupita, yule mganga aliwaambia kuwa wamekaribishwa, hivyo wavue vilemba vyao, wavue na viatu kisha wajongee jirani na mti…

Mganga akiwa anaendelea ‘kubonga’ kiganga alimuashiria msaidizi wake ambaye walikuja naye amchinje yule jogoo mwekundu, yeye Mganga akachukuwa sehemu ya ule unga na kuanza kuumwaga kwa mapozi, yani anamwaga kiasi kisha anasema maneno, anamwaga kaisi kingine na kusema tena hadi mara ya tatu alipomaliza akamkamwambia mama Junior naye achukuwe ‘gao’ la ile sembe na kumwaga kiasi huku akiwa anasema niya yake kwa sauti kama alivyokuwa anasema yule mganga…

Sehemu za ile kaniki na ile shuka nazo zilikatwa kisha kufungwa kwenye mti lakini sehemu kubwa ya nguo zile zilikunjwa na kuwekwa kwenye mkoba wa mganga.

Damu ya yule kuku iliachwa imwagike pale chini ya mti jirani kabisa na ile sembe ilipomwagwa. Moto ulikokwa na jungu la maji likachemshwa kwa ajili ya kumnyonyoa yule kuku.

Baada ya saa chache ugali ulipikwa, ulitumika ule unga uliobaki na yule kuku akawa tayari amechemshwa, wakapakuwa na kabla ya kuanza kula, sehemu za kuku yule, paja na mgongo yule mganga akaviweka pale kwenye ule unga uliomwagwa pomoja na tonge la ugali kisha sehemu zilizobaki zikaliwa na wote waliokuwepo pale pamoja ya mganga mwenyewe.

Haukuwa ugali wa kushibisha watu watano waliokuwepo, ni kama walionja tu. Baada ya kula yule mganga akafanya vimbwanga vyake tena na kubonga kwa lugha ya kiganga, haukufahamika mara moja kama ni kiluguru ama lugha gani lakini hatimaye akawageukia wageni wate na kuwaambia kuwa asubuhi na pamepa waje nyumbani kwa mganga ile waje hapo mzimuni kusikiliza majibu ya maombi yao.

Walitoka eneo la mzimuni kinyumenyume na kuondoka kurudi nyumbani kwa mganga…

Mama Rose: “Mganga, hujatuambia itatugharimu shilingi ngapi kwa kazi yako…”

Mganga: “ Eeee mizimu itasema, mimi sipangi bei, ni wao wanapanga, watatuambia watakavyokuwa wanatupa majibu…”

Haooo, mama Rose, mama wawili na mama Junior wakaondoka kurudi Kihonda ambapo muda huo tayari alasiri ilikuwa imeshaingia mamana kulisikika kengele ya saa kumi kanisa la Kigurunyembe.

Mama Rose na Vai walipofika nyumbani waliwakuta watoto wao wakiwa mezani wanakula wali na maharage waliyopikiwa kabla wazazi wao hawajaondoka lakini pia walikuta wakila nyama ya kuku iliyochemshwa ambapo kulikuwa na paja na sehemu ya mgongo…




Itaendelea Jumamosi usiku panapo majaaliwa
 
unaupiga mwingi mzee jasusi
 
Unyama mwingi sana [emoji41][emoji41][emoji41]
 
Tupio la XXXIII – Kulipa Kisasi bila kutarajia


Ilipoishia…


“Boss, leo haupo kawaida, unawaza nini!?” Yule mhudumu alirudia swali lake…

“Umemuona yule pale…” nilimuonesha yule mhudumu alipo Emmy kisha nikaendelea..

“Yule ni Ex wangu, actually ni dear ex maana bado nampenda! Lakini pale namuona ana jmaa mwingine, mara ya mwisho hatukuagana vizuri na hatujawasiliana tangu siku ile, leo nimemfuma hapa na jamaa mwingine, lakini ngoja, nitamkomesha, hanijui vizuri, anadhani mimi ni Alex yule wa zamani…



Sasa endelea…


Fast forward…


Nilimpuuza Emmy na kuendelea kuangalia mpira huku mara kwa mara yule mhudumu kiongozi akinitembelea pale maana nilimpa ofay a kinywaji chake hivyo alikuwa akifanya kazi yake na akipata nafasi kidogo anakuja kupiga funda zake na kunipigisha stori kidogo kisha anaenda kuhudumia tena.

Saa nne na nusu nilitoka pale baada ya matangazo ya mpira kwisha, nikaelekea nyumbani kupumzika. Nyumbani sasa ‘tafuta usingizi tafuta nawewe!’ hadi usiku mwingi ndio nikapata kupitiwa na usingizi. Kila nikijaribu kulala nakumbuka sebene la Mourine, mara nakumbuka ishu za Emmy, mara ujenzi mara safari ya dada Kenya, mara mambo ya chuo yani kichwa kilikuwa kinavurugwa na mawazo mchanganyiko.
---


Sauti ya mtoa adhana ya asubuhi ndiyo iliyoniamsha, ninapoishi ni jirani tu na msiki, mwendo wa kutembea dakika mbili tatu hivi. Niliamka na kwenda kujisaidia kisha kurudi ndani na kuanza kupitia masomo kulingana na ratiba ya leo chuoni.

Tukiwa chuoni wakati wa break, minong’ono ikaanza kwamba Emmy sasa anatoka na msanii wa kizazi kipya, amembwaga Alex, amamuacha John n ahata mahudhurio yake kwenye ‘lekcha’ yamepungua. Marafiki zake walikuwa pia hawafurahii tabia za Emmy, basi kutokana na picha niliyoiona jana kule Rombo green view hotel na minong’ono ya hapo chuoni niliamua kumuacha moja kwa moja Emmy, lakini bado nilikuwa natamani nilipe kisasi.

“Sijui nimpelekee moto kisha ndio nimuache, sijui nimuonyeshe kuwa mimi nina hela zaidi ya hao watu wake na sivyo kama anavyo nidhania yani nilikuwa nataka naye apate uchungu fulani hivi…” niliwaza

Kwa upande mwingine pia nikawa namkumbuka Mourine na michezo yake. Nikimkumbuka Emmy napatwa na hasira lakini nikimfikiria Mourine najikuta natabasamu.

“Hivi huyu Mourine ana nia gani nami, si kwa kujilengesha kule, au tuseme ndio upwiru!?” niliwaza.

Siku iliisha, wiki zikapita.

Siku moja wakti nipo chuoni, alinifuata Zaituni, (yule rafiki yake na Emmy) kwenye gari, ilikuwa siku ya Ijumaa baada ya muda wa masomo.

“Hi Alex!” alinisalimia.

“Helo Zai, mambo?” nilimjibu.

“Ndio unatakata kurudi home muda huu? Zai aliniuliza.

“Ndiyo, kwani vipi?” nilijibu na kuuliza niliuliza…

“Nilikuwa nataka unisindikize sehemu…” Zai alisema.

“Ingia basi kwenye gari mbona unazungumzia nje…” Nilimshauri ili nisikilize vizuri ombi lake.

“Gari lako safi! Na linanukia vizuri?” Zai alianza kusifia

“Kawaida tu Zai, enhe, niambie unatakaje?” Niliuliza

“Nilikuwa naomba unisindikize Kigamboni, nataka niende kwa Aunt yangu kisha unirudishe, anakaa mbali nikienda kwa daladala nitachelewa kurudi na usafiri wa kurudi hadi Kimara utakuwa tabu…”

Zai alieleza shida yake nikamwelewa, kwa kuwa nilikuwa na ratiba moja tu siku hiyo ya kupitia site pale ili nikabidhiwe nyumba, nilifanya mawasiliano kumtaka radhi fundi mkuu ili badala yake tukutane Jumamosi baada ya kuwasiliana asubuhi hiyo ya kesho.

Zai kwa wiki kadhaa sasa amekuwa si mwenye furaha kama aliyokuwa nayo mwaka jana. Kigamboni alikuwa anataka kwenda kwa Shangazi yake. Nilimpeleka hadi Kibaoni Mjimwema Kigamboni ambapo aliniomba nisimame nimsubirie hapo jirani na Nolasco pup, yeye akateremka na kutembea kwa miguu kuingia vichochoroni akapotelea huko.

“Kuna jambo nataka niongee na Aunt, situmii muda mrefu nisubiri please!” Zai aliongea wakati akitaka kurudishia (kufunga mlango wa gari)

Njiani wakati tunakuja nilimuuliza kuhusu yeye kutokuwa na furaha siku hizi ndipo alinifungukia…

“Sina mawasiliano na Hemedi tangia aondoke nchini kwenda South…” Hemedi alikuwa ndiye bwana wake Zai, actually walikuwa wachumba maana walisha tambulishana kwenye familia zao.

“Namuona tu kwenye status za whatsapp lakini hajibu meseji zangu nikimuandikia…”

“Alisema anaenda kufanya kazi aliyounganishiwa na ndugu yake kiukoo ambayo anaishi huko Durban. Sasa tangia alivyoondoka December 27 mwaka jana hadi leo hatujawasiliana…”

“Text msg namtumia, voice not namtumia lakini yeye ndio hajibu ingawaje kwenye status naona tu anavyo jirusha na marafiki zake wa huko…”

“Hali hii inaninyima raha ndio maana siko sawa hata ‘UE’ iliyopita sikufanya vizuri kwa sababu yake, sijui hatma ya uhusiano wetu upoje…”

Zai alijieleza vya kutosha kuhusu masahibu yanayomkuta na huko kwa Shangazi yake alikuwa anaenda kushtakia na kupata ushauri maana ni rafiki yake sana na yeye Shangazi ndiye aliyekuwa wa kwanza kutambulishwa.

Zaituni alikuwa ni binti mzuri mwenye kuvaa nguo za kujisitiri maungo, muda wote ushungi na yeye, yeye na ushungi, hakuwa na mambo mengi na kwa miaka miwili alikuwa na uhusiano na Hemedi ambaye alimtangulia mwaka mmoja wa wanafunzi wote wa mwaka wetu tulijuwa kuwa wataoana kwa jinsi uhusiano wao ulivyokuwa imara.

Nilimsubiri Zai nikiwa kwenye gari nikifanya mambo mengine madogo madogo kwenye simu ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii. Baada ya dakika kama sabini hivi Zaituni alirudi akiwa amesindikizwa na Aunt yake. Nikashuka kwenye gari tukasalimiana, Zai akanitambulisha kisha tukasalimiana tena kwa kupeana mikono.

“Aunt, huyu ni rafiki yangu, anaitwa Alex, ndiye aliyenipa simu hii…” Zai alisema kisha akanigeukia na kusema…

“Alex, huyu ndiye Shangazi niliyekuambia…”

Zai alikuwa amefanana sana na Shangazi yake, yani ‘kopirait’, ila yeye alikuwa amevaa sketi na blauz, ambazo zilimchora vema maumbile yake hususani afrika bambataa.

“Sasa mbona mgeni umemuacha huku mbali, si angekuja na gari hadi nyumbani jamani…” Aunt alihoji …

“Yeye alisema ana kazi kidogo anafanya kwenye gari maana hata kuja huku nilimkatisha safari zake…” Zai alijitetea na kudangaya kidogo.

Zai na shangazi yake hawakupisha sana umri na ndio maana marafiki sana, unaweza kudhani ni mtu na dada yake.

Basi tukaagana na shangazi kisha sisi tukaanza kurudi.

“Alex, nichangie shilingi ngapi mafuta?” Zai alivunja ukimya wakati gari ilikuwa imeshashika kasi kurudi…

“Acha masihara Zai, kwani umesikia hii ni teksi bubu?” Nilimjibu

“Najuwa kuwa siyo teksi bubu, lakini kuna mambo mawili, nimekuharibia ratiba zako na mafuta pia, basi angalau nichangie mafuta…” Alisema Zai.

“Hatukukubaliana unilipe, wewe ulikuja kuniomba nikulete huku nami nikakubali, au nilikuambia kuwa utachangia mafuta?” Nilimkazia

“Hapana, hukuniambia, lakini ki binadamu tu naomba nikupatie elfu arobaini uweke mafuta kisha unipeleke hadi Kimara…” Alisema huku akiweka elfu arobaini jirani na ‘gear lever’ sehemu ya kuweka vitu vidogo vidogo

“Hiyo hela sintoichukuwa, sikiliza Zai, kwanza haikuwa makubaliano unilipe, pili gari hii ni hybrid, hivyo haitumii mafuta mengi, hivyo baki na hiyo hela utakusaidia kwa mambo mengine…” nilizidi kumkazia

Kukawa na ukimya kwa muda kidogo kila mmoja akiwaza yake na tayari tulikuwa kwenye foleni ya kusubiri kuingia getini pale feri ng’ambo ya huku kigamboni.

Dakika chache baadaye tulivuja sheria kwa wote kubaki ndani ya gari tukiwa ndani ya pantoni tukivuka, utaratibu unataka abiria wote kwenye gari washuke abakie dereva tu, lakini sisi kwa mazoeza ya kibongo bongo tuliendelea kuwemo ndani ya gari tukipiga stori huku pantoni ikijongea upande wa magogoni.

Dakika arobaini na tano hivi baadaye tukawa tumevuka daraja la Manzese na uelekeo ukiwa ni Ubungo, Jua lilishazama kitambo, isingekuwa taa za barabarani basi nje kungekuwa giza sana maana tarehe zilikuwa za mwezi kuchelewa kuchomoza…

“Zai, saa tatu na nusu hii, naomba tupitie hapo Rombo tupate chakula cha jioni kwakuwa muda huu siwezi kwenda kupika…” Nilipendekeza pendekezo ambalo halikuwa na kipingamizi.

Tukiwa ndani ya bar ya Rombo view green hotel, mimi niliagiza mchemsho wa samaki na Zai yeye aliagiza mchemsho wa kuku wa kienyeji.

“Huyo kuku siyo wa kienyeji wala nini, ni broiler, mwambie akubadilishie akupatie samaki…” Nilimwambia Zai wakati alipofunuliwa poti lake la mchemsho wa kuku…

“Hapana, nitakula hivyo hivyo, nimemiss kuku, hii oda yote nitailipia mimi…” Alisema Zai huku akianza kumshikashika kuku baada ya kunawa mikono.

“Nimwagilizie maji nami nianze kula maana nina njaa sana…” Nilimuambia mhudumu ambaye alianza kumnawisha Zai

Mara akaja mhudumu wa vinywaji, na kwa bahati alikuwa yule yule mhudumu kiongozi…

“Mmesikilizwa vinywaji boss?” Mhudumu Aliza

“Bado, afadhali umekuja, niletee kama kawaida, na huyo msikilize….” Nilijibu.

“Niletee fanta peshen…” Zai alisema.

Alipoondoka, nikamwambia Zai, “Ofa yako ya msosi ziwezi kuikataa, ila nami nitakupa ofa nyingine maalum”

“Ofa gani hiyo…” Zai akawa anacheka huku akitafuna taratibu kuku wake.

“Nitakupa ofa ya kupajuwa nyumbani kwangu kabla sijakupeleka kwako….” Nilijibu na kukawa na ukimya fulani hivi.

“Kwani Alex unakaa Kimara?” Zai aliuliza baada ya kimya kupita

“Hapana, sikai Kimara, nakaa jirani tu na hapa ila tumepapita, ni kule kwa mfuga mbwa Manzese…”

Zai: “Duu, basi leo nitachelewa sana kufika nyumbani…”

Mimi: “Kwakuwa usafiri wa uhakika upo hakuna shida, hata kama itakuwa saa tano usiku nitakupeleka tu.

Niliangalia saa na kuona inakaribia kabisa kuwa saa nne za usiku.

“Mbona hujanitambulisha shemeji?” Yule mhudumu kiongozi alikuja mezani kwetu na kuchombeza maana siku chache zilizopita alijuwa historia fupi ya uhusiano wangu.

“Aaaa, nilisahau, huyu ni shemeji yetu sote, ni mchumba wa rafiki yangu…” Nilimjibu huku nikimuangalia Zai usoni..

Zai baada ya kusikia majibu yale niliona amebinua mdomo ile kama vile hakufurahia nilivyojibu.

“Karibu shemeji, Alex ni mteja wetu mzuri kwa wiki hakosi angalau mara tatu hapa…” Alisema yule mhudumu kiongozi.

Leo huyu mhudumu kiongozi hakuchukuwa kiti kujumuika nasi kama ilivyo kawaida yake lakini mara kwa mara alikuwa anakuja mezani kwetu kuangalia kama tunahitaji chochote.

Niliwaita watu wa jikoni na Zai alifanya malipo ambayo yalimgharimu zaidi ya elfu ishirini na tano. Tuliendelea kula na kunywa hadi tulivyomaliza, kisha nikamuonesha Zai uelekeo wa maliwato ilipo ili ‘akarekebishe ushungi’ wake vizuri, alivyorudi nami nikaelekea kumaliza haja zangu huko msalani kisha nikamuashiria tuondoke.

Wakati tumesimama tunaondoka pale nilimpatia yule mhudumu kiongozi noti ya elfu kumi na kumwambia kuwa anywe ‘soda’, pamoja na malipo ya vinywaji. Mita chache kabla ya kutoka pale baa nilisikia sauti ninayo ifahamu ikiita …

“We Zai!” ile kugeuza shingo ndio nikakutana uso kwa uso na Emilia, Emmy huyu huyu akiwa na jamaa yake yule wa siku ile tulipokutana hapo hapo.

“Emmy!, mambo? Sijakuona class tangia juzi…” Zai alijibu baada ya kugeuka, akamsogelea…

“Msalimie shemeji yako…” Emmy alimuambia Zai

Mimi nilikuwa jirani tu lakini sikupiga hatua kuwasogelea na wala sikuwasalimia.

“Za jioni shemeji, mmependeza!” Zai alijibu na kuwasifia kinafiki.

Ukweli ni kwamba walikuwa hata hawaendeani maana Emmy alikuwa mrembo na yule jamaa yake ambaye ni msanii wa kizazi kipya alibebwa na jina kubwa tu la kazi yake.

Msanii: “Nanyi mmependeza sana na mpenzi wako!”

Emmy: “Wala siyo mpenzi wake na sijui walikuja kufanya nini hapa usiku huu…”

Emmy alimkatisha jamaa yake na kuonesha kujuwa zaidi uhusiano wetu kinyume na jamaa yake alivyodhani.

Zai: “Emmy, tambua kuwa sasa Alex ndio mpenzi wangu mpya!” Zai alisema kisha akageuka na kunifuata ili tuendelee na safari…

“Wee Zai, unasema nini!” Emmy alihamaki baada ya kusika vile kisha akasema kwa sauti…

“Vina muda basi!?”

Zai alivyosikia vile akanishika begani kwa mkono mmoja na tukawa tunaelekea usawa wa gari ambapo safari hii nililipaki jirani na maduka yaliyopo hapo Rombo. naye akasema kwa sauti... "Kweli bhana, kwani vina muda basi!!?"

Huko nyuma hatukujuwa kilichoendelea sisi hao tukaelekea nyumbani, niliingilia sehemu iitwayo ‘engo’ (angle) hadi Malembe ambapo nilipaki gari kisha tukawa tunaenda kwa miguu kuelekea nyumbani.

“Nitarudi baadaye kidogo kulichukuwa gari lakini nafasi yangu msipaki gari nyingine, nitarudi kulala…” Nilimwambia mlinzi wa zamu aliyekuja kuandikisha.

“Zai, kwangu siyo mbali kutoka hapa, nimeona ni vyema nikabe nafasi mapema maana siku kama leo magari hujaa sana hapa kiasi cha kufanya mtu uweze kukosa nafasi nzuri ya kuegesha gari…”

Tukawa sasa tunaelekea usawa wa nyumbani kwangu uswahilini.



Itaendelea Jumanne au Jumatano panapo uhai na afya.
 
Sawa Mwamba JB
 
Bado mwandishi anasema ni hadithi ya kusadikika, hii ni hadithi ya kweli kabisa.... Anyway Kibaoni kwa Kigamboni zipo mbili mjimwema jirani na ungindoni na Mwongozo....
Hadithi njoo utamu kolea...
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…