Sehemu ya XII – Barua kutoka Manama.
Ilipoishia
Omari akafanya hima kumaliza kazi ya kuwaadaa samaki wake kisha akarudi hadi kwao uswahilini Ukwamani na kumkabidhi mama yake samaki wale, kisha akasafisha kapu lake kama kawaida na akaingia chumbani kwake na kuifungua ile chupa…
Sasa endelea…
Akiwa amekaa kwenye stuli, akaifungua mfuniko wa chupa huku uso akiwa ameuweka mbali, kama vile kuchukuwa tahadhali ya hewa ya sumu au chochote kitokacho mle kwenye chupa, lakini kwa bahati nzuri hakukuwa na la ajabu lolote zaidi ya harufu nzuri ya manukato ya kawaida. Aliendelea kwa kuitoa ile karatasi nyeupe ambayo sasa ilionekana imehifadhi kitu kingine ndani. Akaivuta kwa nguvu hadi ikatoka, chupa akaiweka pembeni sakafuni, na akaanza kufungua ile karatasi ambayo nayo ilionekana ikiwa imeandikwa kwa wino wa bluu, lakini pia alikuta kiasi cha noti za kigeni, mpya kabisa.
Alipoangalia vizuri aliona zote zimeandikwa 20 kisha maneno ya kiarabu, na upande wa pili zilikuwa zote zimeandikwa Central Bank of Bahrain, Twenty Dinar ingawaje alisoma kwa kuchapia matamshi. Akafurahi sana akazihesabu akaona zipo jumla ya noti kumi na moja, lakini hakuweza kujuwa mara moja ni kiasi gani.
Akili ikamjia na akachukuwa ile karatasi ili ajaribu kuisoma aone imeandikwa nini. Lo! Karatasi ilikuwa imeandikwa kwa lugha ya Kiingereza na mwandiko wa wino wa bluu. Akaamua kutoka kimya kimya baada ya kuihifadhi ile chupa chini ya uvungu wa kitanda chake, akiwa ameichukuwa ile karatasi na noti moja. Moja kwa moja akaenda ‘Stationery’ iliyopo Ukwamani zinapogeuzia daladala.
“Dada za jioni?” alimsalimia mhudumu..
“Shwari tu Ommy, karibu…” alijibiwa kwa kuchangamkiwa.
Omari anafahamika sana maeneo ya hapo Ukwamani kwakuwa alikuwa konda wa daladala pia alipiga debe kiasi hapo.
“Naomba nitolee kopi karatasi hii..” alisema Omari
“Nakala ngapi Ommy…” Yule dada alipokea na kuiweka kwenye mashine ya kutolea nakala bila kuisoma…
“Toa mbili tu” alijibu Omari na yule dada akabofya mashine ya kutoa nakala (photocopier) na zikatoka nakala mbili safi.
Baada ya kukabidhiwa zile nakala mbili na ‘orijino’, Omari alitenga nakala moja na orijino pamoja na nakala moja akazikunja kwa pamoja na kuziweka mfukoni.
“Samahani sista, naomba nitafsirie hii karatasi…” Omari aliomba msaada baada ya kulipa shilingi mia kama gharama ya kutolea ‘fotokopi’.
“Mmh, mwenzangu, kwenye kutafsiri hapo sasa!, nisije nikakuongopea bure!, ngoja nikuelekeze sehemu…” alijitetea yule binti hata bila kutaka kuisoma karatasi yenyewe.
“Nenda pale ‘opposite’ na oilcom kwa Frank, pale anapofundishia tuition atakusaidia…” alisema yule Dada.
Baada ya dakika chache, Omari alifika kwa Frank kwenye tuition centre yake maarufu wakati huo hapo Kawe na kukuta darasa likiendelea…
Baada ya kukaribishwa na kueleza shida yake, Frank alimuambia…
“Nitakuchaji ‘buku’ mbili kwa kukutafsiria, na buku kuyaandika…”
Omari wala hakuwa na pingamizi, akatoa noti ya elfu tano na kumpatia Frank…
“Nije baada ya dakika ngapi kuifuata?” aliuliza Omari wakati akipokea chenji yake…
“Aah, hii fasta tu, subiri hapo kwenye kiti” alijibu Frank huku akiipitia ile karatasi.
Karatasi yenyewe ilisomeka hivi…
Date xx-xx-xxxx
Assalaam alaykum.
My name is Nasreen, I am from Manama Barhain.
Whoever will bring this original writtings to me inperson will be my friend. Use dinar bill attached as transport fee, add yours if fare is not enough and I will refund you. Do NOT forget to bring also one note bill attached.
Eager from seeing you, my ideal lucky friend.
May God Almighty bless you.
Nasreen. (+973xxxxxxxxx)
Frank wala haikumchukua muda kuitafsiri na kuichapa upya ile karatasi kisha aka-print na kumkabidhi Omari. Frank alikuwa ‘bize’ na wanafunzi wake hivyo aliendelea kuwafundisha na Omari akaondoka bila hata ya kuisoma ile tafsiri.
Jua lilikuwa limeanza kuzama, alipofika nyumbani chumbani kwake ndipo akanza kuisoma. Awali alivyotoka nyumbani pia alitaka ajue ile noti moja ina thamani kiasi gani lakini kulingana na mazingira ya siku hiyo hakuweza kupata ufumbuzi.
Alifurahi sana baada ya kuelewa yale maandishi na sasa akawa na shauku ya kutaka kujuwa thamani ya noti moja iliyoandikwa ‘20’.
Kesho yake mapema sana alipanda daladala hadi Shoppers Plaza ambako kuna sehemu ya kubadilishia fedha za kigeni…
“Naomba nibadilishie hii nipate Shilingi…” alisema Omari baada ya kusalimiana na mtoa huduma wa ‘bureau de change’ ile…
“Oh, hapana, hii sisi hatubadilishi hapa, sisi tunabadili dola, paundi, rand …” akataja pale orodha ya fedha wanazobadili na kumrudishia noti yake…
“Kwani kama mngekuwa mnabadili ningepata kiasi gani…?” alimpachika swali ambalo ni muhimu sana kwake Omari.
“Kwa hii unaweza kupata laki moja hadi laki na kumi hivi…eee nenda kule mtaa wa Lumumba kuna Hoteli (akaitaja) pale utabadilishiwa kirahisi tena kwa reti nzuri…” alijibu yule mhudumu kisha akaendelea na mambo yake kama vile hataki maswali mengine…
“Mida ya kazi hii, lakini ‘potelea pote’ ngoja niende huko Kariakoo.” Omari alijisemea.
---
Alifuata maelekezo vizuri kisha akafika pale hotelini na kueleza shida yake mapokezi.
“Subiri kidogo nikuitie mhusika…” Yule dada wa mapokezi alimjibu Omari kisha akaanza kuita kwa kupaza sauti…
“Mediiiii, Mediiii, njoo kuna mteja huku…” aliongea kwa sauti ya juu.
Kumbe Omari alipoingia mle hotelini, alimuacha nje huyo anayeitwa Medi. Medi ni kijana halfcast wa kiarabu na mwafrika, ndiye alikuwa akisimamia kitengo cha kubadilisha fedha kwenye hoteli hiyo. Hapakuwa rasmi sana lakini maeneo hayo watu wengi wanapajuwa kwa shughuli hiyo na kwa rate ‘nzuri’.
“Eee unataka chenji ya dola ngapi…” Aliuliza Medi huku akiingia kwenye kijiofisi chake kilicho nyuma ya ngazi hapo hotelini.
“Siyo dola, ni hii hapa…” Omari akatoa ile noti akamkabidhi Medi kupitia kidirisha kidogo ambacho kilikuwa kina kimewekwa ‘tint’. (kioo cha giza maarufu kama tinted).
“Aaa kumbe ni Dinari ya Bahrain, eee kwa hii bosi nitakupa laki na ishirini, si unajua tena hizi haziji mara kwa mara…” alisema Medi.
Omari hakuamini masikio yake alipotajiwa hela ile. Kisha akasema…
“Poa tu, nipatie…”
Medi akamuhesabia noti 12 za elfu kumi kumi, kisha akasema hesabu bosi…
“Wakati anahesabu, Omari akasema, nitakuletea nyingine baadaye kama hizi 9”
“Poa, usiponikuta, namba hiyo hapo kwenye kioo utanicheki…”
Omari wala hakuwa na simu ya mkononi, ‘kitochi chake’ kilishasambaratika kitambo wakati akifanya kazi kwenye daladala.
“Sawa, nitakucheki hiyo baadaye…” alijibu kisha akaelekea Kariakoo kununua simu kwa hela aliyopata.
---
Saa kumi kasoro hivi jioni, Omari alikuwa tena pale hotelini Lumumba, na kwa bahati nzuri alimkuta Medi, wakafanya biashara.
Omari Juma siku hiyo alikuwa na zaidi ya shilingi milioni moja na ushee. Akarudi nyumbani na kumkuta mama yake akiwa nje kwenye kigenge chake.
“Mama, nina habari njema mbili, ukishafunga genge lako nitakuambia…” Yalikuwa maneno ya Omari akimtamkia mama yake kwa furaha.
“Sawa Omari, na leo nitafunga mapema naona biashara tangia jana wala haichangamki…” alijibu mama Omari.
Baba yake Omari naye muda si mrefu alifika akitoka matembezini maana siku hiyo alikuwa ‘ofu’ , akiwa amelewa akaanza kumwambia mke wake…
“Nipatie elfu ishirini hapo…” ilikuwa ni sauti ya kilevi…
“Sina mume wangu, tangia jana biashara wala si nzuri, hapa nina elfu nne tu zingine nimefanyia matumizi ya nyumbani…”
“Lete hizo hizo zingine nitajua huko mbele kwa mbele…” alisema afande yule
Mama Omari akafunua gunia kwenye meza ya genge lake kisha akatoa noti moja ya elfu mbili, moja ya elfu moja na chenji chenji zilizofanya jumla kuwa elfu nne. Akampatia mumewe na muda ule ule mumewe akaondoka kupitia uchochoro uliokuwepo jirani kuelekea bar iliyo jirani.
Ilikuwa ni kawaida ya baba Omari akiishiwa na hela kuzichukuwa ki nguvu pesa za mkewe katika biashara yake.
“Atakuwa anadaiwa huyo huko bar…” alisikika mama Omari akijisemea
Omari kwa kuwa alikuwepo jirani alisikia mazungumzo yote, na haikuwa kawaida yake kuingilia ugomvi wa baba yake na mama yake kwani kuna siku ‘alilapuliwa’ na ‘mkanda’ na kusababishiwa maumivu makubwa ambayo yalimuachia alama mwilini.
Lakini siku hiyo Omari akamuambia mama yake, ngoja nimfuate baba huko huko bar, si anakunywaga ile bar ya pale ‘Jamborii’, akaondoka fasta.
Dakika chache baadaye akafika kwenye ile bar, tayari alikuwa ameshatenga noti mbili za elfu 10 ili ampatie baba yake.
Baba yake wakati huo alikuwa amejiinamia kwa ulevi na mawazo wala hakumuona mwanawe wa pekee Omari alipofika karibu naye.
Omari alichuchumaa na kumnong’oneza baba yake sikioni huku akimshikisha zile hela mkononi. Baba Omari alipohisi kitu kama hela hivi, akainua shingo na kuangalia vizuri. Akamuona mwanae na kupigwa na mshangao...
“Ahsante sana Omari, umeniokoa…” alisema kwa kifupi kisha akainuka kuelekea Kaunta na Omari aliondoka haraka maeneo yale kwa kuchelea aibu za baba yake.
Nyumbani alikuta mama yake ameshafunga genge na anaendelea na kuandaa chakula cha jioni.
“Nimerudi mama, nimemkuta baba pale bar na nimempatia elfu ishirini…” alisema Omari.
“Elfu ishirini? Umezipatia wapi…!?” aliuliza kwa mshangao mama Omari.
Wakati Omari akiwa anazunguka na daladala ilikuwa ni kawaida sana kurudi nyumbani hadi na shilingi elfu hamsini, lakini alipoanza kupiga debe pato lilishuka hadi akawa anarudi na elfu tatu, siku nyingine nne, na ikizidi sana elfu sita. Lakini alipoanza shughuli za ufukweni ndio aliweza kufikisha elfu kumi wakati mwingine elfu kumi na tano kwa siku.
“Ndiyo maana nimekuambia leo nina habari mbili njema mama…” Omari alitabasamu huku akimuangalia mama yake kwa bashasha.
“Halafu leo, kapu lako naliona unapoliwekaga, hukwenda ‘pwani leo’? “ alisema mama Omari akimaanisha ufukweni.
“Ndiyo mama, leo sikwenda…”, alisema kisha Omari akakaa kitako kwenye kigoda kilichopo eneo la jikoni pembeni ya mama yake aliyekuwa akiandaa mboga za jioni.
Omari akaanza kumsimulia mama yake kisa kizima cha chupa aliyoiokota baharini na habari zake zote hadi muda huo…
“Hivyo mama hapa nina furaha ya kupata milioni moja na kuna ofa ya kusafiri kusikojulikana na kufaidi ya huko…” alihitimisha kwa kutotaja kiasi halisi cha fedha alichonacho.
Omari akatoa nakala ya ile karatasi aliyokuwa nayo mfukoni na kumpatia mama yake.
“Mmmh, si kizungu hiki, haya mie na kizungu wapi na wapi…” aling’aka mama Omari.
“Ipo hii tafsiri yake…” kisha akampatia ile karatasi aliyoandikiwa na Frank.
Mama yake akaisoma na kuirudia na kuirudia kisha akasema…
“Alhamdulillah, Mungu ametuhifadhi, sasa mwanangu usimwambie baba yako…”
Baada ya mazungumzo marefu pale, mama Omari alihitimisha kuwa mwanawe atumie tu zile hela kujianzishia biashara na wala asifikirie kusafiri kwenda huko ughaibuni isije ikawa mtego wa kuishia kwa maharamia, wakamdhuru mwanawe.
“Usije ukaenda huko ukaishia kuwa mtumwa, ama kunyofolewa figo zako ama kudhuriwa kwa namna yoyote ile, baki hapa hapa, tafuta biashara nyingine nipatie na mie niongezee mtaji wa genge langu maana hali halisi ya nyumbani si unaiona?!”
Omari akajibu…
Sawa mama, nimekusikia, ngoja nitafakari kwanza.
Itaendelea...